Monday, 17 November 2014

Uhuni dhidi ya Warioba mbona ikulu inajichanganya?

 
          Taarifa iliyotolewa na ikulu baada ya kuchelewa muda mrefu kuhusiana na sakata la kuvamiwa na kutaka kupigwa kwa waziri mkuu wa zamani Jaji Joseph Warioba, zinachekesha. Hivi Katibu Mkuu Kiongozi, Ombeni Sefue, alikaririwa akisema, “Tumekerwa sana na tukio lile, halikutufurahisha hata kidogo kama Serikali kwa kuwa limemvunjia heshima Mzee Warioba, yule ni mzee wetu, anahitaji heshima, kwanza heshima yake na ulinzi.”
Je ni machozi ya mamba? Inakuwaje ikulu itoe tamko, kwanza ikiwa imechelewa? Na pili, baada ya mkuu wa ikulu yaani rais kutoa tamko akionyesha wazi kufurahishwa na yaliyomsibu Warioba? Je ikulu inamsemea nani wakati mwenye ikulu ameishajisemea. Kikwete alikaririwa akisema, “Nadhani na mimi nitakavyokuwa napiga kampeni hayatatokea yale ya jana (juzi), maana mie sioni haya kuipigia kampeni kama wale wenzetu ambao wanataka isipite.” Haya si maneno ya busara kwa kiongozi wa nchi tena akiongelea tukio la kupigwa kiongozi mwenzake tena mwenye uzalendo kuliko hata huo wake. Je maneno ya Kikwete hayaonyeshi kufurahia na kuridhishwa na uhuni aliofanyiwa Warioba. Je Kikwete alishindwa nini hata kumpa pole mzee Warioba hata kama ni kwa kuondoa laawama? Kitu kizuri alichofanya Kikwete ni ile hali ya kushindwa kuficha chuki yake dhidi ya Warioba na furaha yake kwa uhuni aliotendewa Warioba.
Tujalie kuwa kweli Ikulu imeudhiwa na kukerwa na yaliyomkuta mzee Warioba. Je nani mkweli kati ya Sefua na Kikwete kuhusiana na sakata hili? Je kwanini ikulu ilichelewa kutoa tamko kama hakuna namna? Je ikulu inadhani kuwa mzee Warioba na watanzania ni wajinga kiasi hiki na wasahaulifu kushindwa kupembua pumba na mbegu? Je jibu ni “kufedheheshwa’ au kuwachukulia hatua wahuni na wahalifu waliotaka kumzuru Warioba? Je ni wangapi wameishakamatwa? Je vurugu na udhalilishaji aliofanyiwa Warioba angefanyiwa Kikwete polisi wangekuwa bado wanasuasua?
Sefua alijinanga zaidi pale aliposema, “Najua si jambo zuri, iliwahi kutokea pia kwa Mzee (Ali Hassan) Mwinyi, alipigwa kibao... sasa kingine ni mazingira yanapotokea matukio haya, wakati mwingine ni ngumu.” Mbona kwenye sakata la kupigwa kibao mzee Mwinyi mhusika alikamatwa pale pale na kufikishwa kwenye vyombo vya dola? Je polisi wanaopaswa kuwalinda watanzania walikuwa wapi kama hakuna namna?
Kimsingi, watu kama Sefue na Mkurungezi wa Mawasiliano Ikulu, Salva Rweyemamu walipaswa kuwajibishwa mara moja kwa kuonyesha kunyamazia uovu wakionyesha chuki na upendeleo vya wazi. Sijui tunajifunza nini kwenye matumizi ya upendeleo kisheria? Ndiyo ni upendeleo. Kwanini wahuni waliotaka kumdhuru Warioba hawakukamatwa siku hiyo na kufikishwa kwenye vyombo vya dola? Je hawa polisi ni wa nini wanaolipwa kodi zetu lakini wakatumia madaraka yao kwa upendeleo kwa Chama Cha Mapinduzi (CCM) na uonevu dhidi ya wale wasiokubaliana nacho kama mzee Warioba na wapinzani kwa ujumla?
Hii inakumbusha sakata lilolotekea siku chache kabla ya hili la kufanyiwa fujo mzee Warioba ambapo mwenyekiti wa Baraza la Wanawake la CHADEMA (BAWACHA) Halima Mdee alitupwa korokoroni na kucheleweshewa kupewa dhamana ambayo ni haki yake kisheria wakati watuhumiwa wa makosa mbali mbali kama vile kusambaza na kuuza madawa feki yanayowakabili akina Ramadhani Madabida mwenyekiti wa CCM wakifumbiwa macho.
Polisi, ikulu na CCM hawawezi kukwepa lawama kwenye uhuni huu. Mbona polisi hao hao waliweza kwenda kwenye makazi ya mtu saa saba usiku huko Kyerwa kuzuia kufanyika mkutano wa CHADEMA uliokuwa umeishakubaliwa siku chache kabla ya kuja na tamko hili lenye kuonyesha machozi ya mamba ya wazi? Hapa lazima kuna namna na wananchi wasipoamka na kuchukua hatua, wataendelea kuumia na kuumizwa huku wakidhulumiwa haki zao kwenye nchi yao na kuishi kama wakimbizi kwenye nchi yao. Hii nchi ni yetu sote bila kujali itikadi wala mafungamano ya mtu. Kufungamana au kutofautiana na chama chochote ni haki ya watanzania kikatiba.
Kitendo cha ikulu ambayo siku chache kabla ya kuja na mazingaombwe ya  “kukerwa’ na uhuni aliofanyiwa Warioba iliwezaje kupata muda wa kutangaza kutenga mabilioni ya shilingi kwa ajili ya kupigia kampeni katiba anayopinga Warioba kabla ya kutoa tamko? Kama kweli katiba inayofanya watu wadhalilishwe ni bora kama anavyosema Kikwete, mbona wanaoipinga wanafanyiwa uhuni na kuonekana kama hawana haki na uhuru wa kuipinga kama raia wengine?
Japo wanaofanya ujinga huu wa kushabikia uhuni wanaweza kudhani wanaawakomoa akina Warioba na wote wanaopinga katiba yao kiini macho, wafahamu. Wanamdhalilisha rais wao ambaye naye ameamua kujiingiza kwenye mambo yasiyolingana na hadhi yake. Huwezi kusema, “Nadhani na mimi nitakavyokuwa napiga kampeni hayatatokea yale ya jana” ukaeleweka wala kutenganishwa na watu wanaofurahia upuuzi huu. Nadhani kitu ambacho ikulu inaweza kufanya na kueleweka ni kukiri kuwa ilifurahia masahibu ya Warioba. Hivyo, imuombe yeye na umma wa watanzania msamaha kwa hili tuendelee na mambo mengine. Hebu tutoe mfano wa hivi karibuni. Rais Kikwete amefanyiwa operesheni ya tezi dume hivi karibuni huko Marekani. Hivi akitokea mtu akasema “natamani hili lisinikute’ wakati akiongelea afya ya rais mtamuelewaje? Tujalie Warioba au kiongozi yeyote wa upinzania aseme hivyo ikulu itamchukuliaje? Kwanini mkuki unakuwa halali kwa nguruwe na kwa binadamu mchungu? Unafiki ni wa nini katika shughuli za umma? Nani atakaa madarakani milele? Mbona mzee Mwinyi alifanyiwa uhuni na watu hawataki kujifunza? Ampigaye mzaziwe naye atapigwa na amkiaye mabaya mwenzie naye yatamkuta tena makubwa kuliko hayo.
Chanzo: Dira ya Mtanzania.

2 comments:

Anonymous said...

CCM hiyo proganda zao, kama wapinzani wakijipanga vizuri , bila ya kurubuniwa na CCM , 1000000% watashinda , waungane watukomboe Watanzania , leo wachina wanashikwa kenya kwa kutoroka na pembe za ndovu Tanzania , inatisha na inashangaza sana, watanzania amkeni, wazungu nawapenda sana kwani kura yao ni Mali kwa serikali , bongo utasikia Oo mpeni amalizie alichoanza, miaka zaid ya 50 hawajamalizia tuu, kama si wizi, haya kafurira alitwa tumbuli na hili jinga lisilojuwa sheria sijui alisoma wapi huyu mwana sheria wa serikali hajui hata maadili, ona sasa yamewakuta ukweli huo, pesa ni za umma. Lakini hatofukuzwa ngo kama mzee wa vijisenti anapeta,
Licha ya skendo zote, kauwa akiendiesha gari kalewa Kesi imeishiya wapi
Mungu ibariki Tanzania

NN Mhango said...

Anon nakuunga mkono. CCM imechoka na kuchosha. Hivyo inapaswa kupigwa chini. Hata hivyo, si jukumu la CCM kujipiga chini bali watanzania wadanganyika kufanya hivyo kwenye uchaguzi ujao.