Friday, 14 November 2014

Nape sera za wapinzani zinakuhusu nini?

Katibu wa Itikadi na Uenezi wa CCM, Nape Nnauye ni kijana anayefikiria kikale. Siwezi kusema anafikiria kizee hasa ikizingatiwa kuwa kuna wazee wenye akili zinazochemka kuliko vijana tena wanaojiita wasomi wakati siyo. Hivi karibuni Nnauye alikaririwa akisema, “Ukawa ni bomu ambalo litawalipukia na kwangu sijaona jambo jema kwa ushirikiano huo.” Kama kawaida yake, Nnauye huwa haishiwi vituko hasa kusema bila kufikiri. Kama tutaangalia ukweli wa mambo na mparaganyiko wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), ukosefu wa dira na uongozi wenye visheni, nani ni bomu haswa?
Kwa wanaojua hasira za wananchi baada ya CCM kuchakachua rasimu ya Jaji Joseph Warioba, anashangaa Nape anaishi dunia gani. Je Nape ambaye anajulikana kwa mipayuko ili kuwaridhisha wakubwa zake anasema asemayo kutokana na kutojua au ni ile tabia yake ya kujisemea. Nani amesahau jinsi Nape alivyowahi kudai kuwa baraza la mawaziri la rais Jakaya Kikwete limejaa mawaziri mizigo? Je Kikwete alipompuuzia na kumdharau Nape alifanya nini zaidi ya kufyata mkia? Kwa wanaojua na kuona uoza hasa ufisadi uliotamalaki kwenye CCM wanashangaa uwezo wa Nape wa kufikiri. Huyu ndiye tunaambiwa ana shahada ya uzamili. Mbona haonyeshi usomi huu kwenye matendo na matamshi yake? Inakuwaje Nape aone ya wenzie wakati yake yanamshinda? Je Nape anadhani kuwa maneno yake yatawakatisha tamaa Umoja wa Katiba ya Wananchi (UKAWA)? Ama kweli mkataa wengi ni mchawi!
Nape aliendelea kufichua ujinga wake kwa kusema, “Ukiangalia Chadema wao itikadi yao ni ya kibepari, CUF ni kiliberali na NCCR-Mageuzi ni ujamaa, sasa wakiunda serikali itakuwa ya itikadi gani? Hili ni jambo la kujiuliza.” Angalau UKAWA wana sera zinazojulikana ikilinganishwa na CCM ambayo sera yake ni ufisadi.  Anashangaa eti UKAWA wakiunda serikali itakuwa na sera gani. Kwa waliosoma siasa hasa wakati huu wa mfumo wa vyama vingi, vyama kuunda serikali ya umoja si jambo geni wala lenye utata. Nadhani kama Nape hajui serikali itakuwaje chini ya vyama vyenye sera na mirengo tofauti, ajiulize: CCM ilipounda serikali ya umoja na CUF kule Visiwani serikali husika ilikuwa na itikadi gani. Hili ni jambo jepesi ambalo Nape alipaswa kulijua hata bila kuwa na shahada ya uzamili. Nadhani tatizo la taifa letu kwa sasa si itikadi bali kupatikana serikali yenye udhu na nia ya kusafisha takataka za CCM iliyokumbatia wizi wa fedha za umma, ufisadi na majungu badala ya kuchapa kazi. Nilidhani Nape angejibu hoja wanazotoa UKAWA hasa kuhusiana na kuchakachuliwa kwa katiba na ufisadi.
Kwa wanaojua umuhimu na dhima ya nafasi ya katibu wa Unezi na Itikadi wanashangaa jinsi Kikwete alivyoweza kumteua mtu kihiyo kwenye nafasi hii nyeti. Hata hivyo, kwa vile Kikwete ameambiwa mara nyingi jinsi ya mtu wake, bingwa wa kuona mizigo mingine wakati naye ni mzigo, amuwajibishe bila kufanya hivyo. Heri Kikwete angezingatia wosia wa wahenga kuwa ukicheza na nyani unaishia kula mabua.
          Japo CCM imeishaanza kujifia, Nape ni miongino mwa waliofikisha hapo ilipo kutokana na kutokuwa na visheni wala busara katika matamshi na matendo yake. Bila hata kufikiri Nape anasema kuwa muungano wa vyama vya upinzani ni kaburi la vyama hivyo. Kama kuungana ni kaburi basi Tanzania nzima ni kaburi baada ya Tanganyika kuungana na Zanzibar. Eti hawa ndiyo wanaosema wanaweza kuboresha na kudumisha muungano. Midomoni wanaweza kufanya hivyo ingawa kimatendo ni wauaji wazuri wa muungano.
Hata hivo, UKAWA walishatambua hila za CCM za kutaka kuwaganya kama anavyojaribu kufanya Nape bila mafanikio. Kwani walikaririwa hivi karibuni wakisema, “Tunafahamu na tunatambua wapo watu ambao walijitahidi sana kutugawa na kutugombanisha, lakini naomba Watanzania watambue kwamba katika hatua hii hatutakubali kugawanyika tena wala kugombana tena.” Kinachowasumbua CCM licha ya kuwa homa na woga wa upinzani imara ulioungana, ni kusikiliza ushauri na maneno ya wapiga ramli kama Nape na wengine wanaojitambulisha kama wasomi lakini wakatumiwa na CCM kama nepi. Mmojawapo wa hawa si mwingine bali Dk Benson Bana anayejulikana kuwa kibaraka wa CCM.
Bana alikaririwa akisema, “Hamuwezi kuungana kwa sababu ya kwenda Ikulu. Tunahitaji wawe na itikadi ya aina moja na sera za mbadala ingekuwa ni jambo jema zaidi.” Huyu bwana anachekesha. Eti anasema hawawezi kuungana kwenda ikulu. Alitaka waungane kwenda sokoni siyo? Kwa chama chochote cha siasa, lengo kuu na maalum ni kushida dola na huwezi kushika dola ukiwa nje ya ikulu. Sijui kwanini daktari huyu anashindwa kuelewa kitu rahisi kama hiki au ni wale madaktari waliosoma wakati wa ukomunisti wakipewa diploma wao wakazigeuza PhD? Bana anaongeza kuwa, “Wakubaliane sera za mambo mbalimbali ambayo yataweza kuing’oa CCM na si kujiwekea mkakati wa kugawana madaraka.” Ukimuuliza sera ya CCM ni ipi sijui kama atakupa jibu linaloingia akilini. Katika kuendesha nchi unaweza kuamua kuanza na sera au kuweka misingi ya kugawana madaraka.  Kama Kikwete aliweza kuingia bila sera na akatawala miaka kumi kwanini wapinzani washindwe?
Tumalizie kwa kuwataka CCM na vibaraka wake watangaze sera zao na kuwaacha wapinzani na mipango yao. Kwani watakaoamua si wao bali wapiga kura. Waache ujinga kama ule wa wachochezi wa kidini ambapo wahubiri wengi wa dini fulani huwa hawajui hata mstari mmoja wa kitabu chao lakini hujionyesha kama mabingwa na wakosoaji wa dini nyingine. Huu, licha ya kuwa ujinga,  ni upogo na udandiaji unaoficha uoza wa wahusika ambao mara nyingi huwa ni vihiyo. Pilipili usiyokula yakuwashani?
Chanzo: Dira ya Mtanzania

2 comments:

Anonymous said...

Muungano wa vyama upo nchi nyingi tu duniani
CCM hamna tija kwa hili
Ujerumani , England, Norwary nk
Wameunda serikali za muungano, tatizo la CCM ni ufisadi na kuogopa hili Kwani wengi waliopo madarakani wamepachikwa tu

NN Mhango said...

Anon umesema vyema. Ni jukumu la wananchi kupembua pumba na nafaka.