Saturday, 21 March 2015

Hawa mashehe au mashena ya njaa?

Njaa kitu kibaya! Humdhalilisha mja hadi akajigeuza taulo au nepi. Hawa wamesikinishwana sera mbovu na ufisadi wa hawa wanaowaomba wagombee ili wawaumize zaidi. Kweli kuna haja ya kuelimisha watu wetu waachane na kugeuka kikwazo chao wenyewe kutokana na kufikiri kwa matumbo badala ya vichwa. Lowassa ana jipya gani zaidi ya kuwa shehe yule yule japo kanzu mpya? Inahuzunisha na kuamsha hasira.
Wanaodaiwa kuwa mashehe kutoka Bagamoyo eti wakimshawishi Edward Lowassa waziri mkuu aliyetimuliwa kwa kashfa ya Richmond agombee urais kana kwamba ana sifa. Sijui tangu lini profesa Kapuya akawa shehe wa Bagamoyo au ni mchezo wa Kikwete kumpigia ndogondogo rafiki na mshirika wake? Hatuhitaji rais wa kushawishiwa bali mwenye ushawishi na udhu kwa watanzania. Lowassa anapoteza muda wake ingawa ni haki ya kila mtanzania kuwania cheo chochote. Laiti angejibu tuhuma za ufisadi dhidi yake tangia zile zilizorushwa na Mwalimu Nyerere angeeleweka.

4 comments:

Anonymous said...

Ulichoeleza kinaweka wazi uwezo wetu kama taifa kwenye kufikiria. Ni busara ndogo tu inayoweza kukuaminisha kuwa, mbali na tofauti zao za hapa na pale, hawa waliokusanywa kama nyanya toka Matombo Moro na kusafiri hadi Dodoma ni kijikundi cha wenye kutafuta 'sukari' na hata hawana hakika ya kuni za kuchemsha chai hiyo. Tungali na safari ndefu sana kama taifa, maana watu wachache, ambao kwa uelewa wao mdogo ndiyo wamekua vinara wa kuburuza wababa wazima kama hawa na kuwa kama watoto wa shule za vidudu. Hata mikakati yao yatia shaka, ati tukamuombe agombee! Alipolazimishwa kuachia uwaziri mkuu alidai 'analinda heshima ya chama na serikali yao ya wezi', sasa leo huyo wa nini kwa Tanzania yetu?

NN Mhango said...

Anon nakushukuru kwa kuliona hili. Maana nilipata mstuko si kawaida. Hata hivyo, Lowassa naye anaonekana kuishiwa mbinu ya kujitangaza. Mbinu anazotumia zinamuonyesha kama mtu wa hovyo na hatari zaidi ya tuliyemjua. Naamini mbinu zake zitaishia kuwa counterproductive kwenye safari yake isiyo na matumaini japo anaiita ya matumaini.

Mbele said...

Napenda kuongelea hiyo picha inayoonyesha makabidhiano. Nilipoiangalia, niliona uso wa Profesa Kapuya. Namkumbuka vizuri, kwani tulifundisha wote Chuo Kikuu Dar. Ulivyomtaja ni kama umenithibitishia. Sijui ni lini Profesa Kapuya kawa shekhe mojawapo wa Bagamoyo. Au ndio ubunifu wa waandishi wa habari?

NN Mhango said...

Kaka Mbele lazima ushangae hasa ukizingatia kuwa Kapuya kwa usomi wake alipaswa kuwa nuru ya kuwafumbua wengine wasifakamie ujinga na njaa kama wanavyofanya. Anachofanya Kapuya ni kutuaibisha walimu. Kama ni ubunifu basi lazima mwisho wa siku uishie kuwa counterproductive- sina neno zuri la kiswahili kwa hili. Ila inaudhi na kusikitisha sina mfano