The Chant of Savant

Tuesday 31 March 2015

Serikali inawapa wanachi ardhi au kampeni?


        Hivi karibuni rais Jakaya Kikwete alimfutia hati ya umilki mwekezaji ambaye hakutajwa jina aliyekuwa akimilki shamba la Kampuni ya Galapo Ufyomi Estate lenye ukubwa wa Heka 1,220. Shamba hili liko Kata ya Galapo, wilayani Babati mkoani Manyara. Ni bahati mbaya kuwa wahusika hawakueleza sababu za kuchukua hatua hii na namna mhusika alivyopata ardhi kubwa kiasi hiki na alikaa nayo kwa muda gani. Hili ni muhimu ili mhusika alipe fidia ya kumilki ardhi visivyostahiki kwa muda aliomilki ardhi husika.
 Wengi walishangaa kusikia habari hii hasa ikizingatiwa kuwa haijulikani huyu mwekezaji alilipataje shamba hilo na rais alitumia sheria gani kuchukua hatua husika. Wapo wanaoshangaa haya “mapenzi mapya” ya rais Kikwete kwa wananchi tofauti na ilivyozoeleka kuwatetea na kuwalinda wawekezaji kama ilivyotokea hivi karibuni kwenye sakata la escrow ambapo rais alikuwa tayari kuwatosa mawaziri wake huku akiwaacha watuhumiwa wakuu mitaani wakitanua ukiachia mbali kwenda mbele zaidi na kusema kuwe hiyo pesa ya escrow ni halali yao.  Kuepuka malalamiko na hasara baadaye – kama ilivyotokea kwenye sakata la Tanesco na IPTL – rais anapaswa kueleza kwa kinagaubaga sheria iliyompa mamlaka ya kuchukua hatua hii ili kuondoa wasi wasi wa mhusika kwenda mahakamani akajishindia fidia ya mabilioni ambayo – kimsingi – hulipwa kutoka kwenye kodi za wananchi hawa hawa wanaosemekana watapewa ardhi bila kuweka utaratibu wa wazi na unaoeleweka na kukubalika. Kuna haja ya kuchunguza suala hili kwa undani na makini zaidi. Upinzani unapaswa kutuletea majibu na taarifa zake kuhusiana na hatua hii.
Kwa upande mwingine, wapo wanaoona kama kitendo cha rais kina weza kutafsiriwa kama kinalenga kuwavutia wapiga kura na kuonyesha kuwa serikali yake chini ya chake cha Chama Cha Mapinduzi (CCM) vinawajali wananchi wakati siyo. Maana swali kuu hapa ni: Ilikuwaje mwekezaji mmoja akamilki ardhi kubwa kiasi hiki huku wananchi walio wengi wakiishi bila ardhi. Huyu atozwe fidia ya kukaa na ardhi kinyume cha sheria na bila kuiendeleza na fidia hiyo wapewe wananchi ili uwe mtaji wao wa kuanza kuendeleza ardhi hiyo.
Pia wapo wanaoshangaa na kuhoji kama rais hajavunja sheria na kama amefanya hivyo kwa kuwapa wananchi ardhi iliyouzwa kwa muda mrefu ili baada ya uchaguzi mahakama iirejeshe hiyo ardhi au kuamuru serikali iwalipe wenye ardhi iliyotwaliwa. Kwanini wakati huu kuelekea uchaguzi kama hakuna namna? Muda wote rais alikuwa wapi na je ni jibu kwa watanzania wote wenye matatizo ya ardhi yaliyotokana na mfumo na utawala mbovu? 
 Wapo wanaodhani kuwa rais anaweza kutoa ardhi husika akilenga kupata kura kwenye uchaguzi huku akijua fika kuwa mahakama itaamuru serikali iirejeshe kwa mhusika au kumlipa fidia. Kimsingi wanachofanya hapa ni kutumia kodi za wananchi kununua mashamba husika ili wapewe kura kwenye uchaguzi. Ngojeni mtaniambia siku moja. Kwani nani aliwauzia hao wawekezaji hiyo ardhi? Haya yangefanywa na serikali mpya nadhani yangeingia akilini.
Naye waziri wa ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi William Lukuvi alikaririwa akisema. “Baada ya Rais kufuta hati ya shamba hilo, sasa viongozi wa mkoa na wilaya hakikisheni mtu ambaye anahodhi eneo kubwa bila kuliendeleza, ananyang’anywa na kupatiwa wananchi, mtakaposhindwa tuleteeni juu.” Ina maana kuwa zoezi hili linaendelea? Kama ni kweli, kwanini waziri anatoa amri kisiasa badala ya kisheria kama kweli hakuna namna ya kuwaingiza mkenge wananchi.
Katibu Tawala wa Mkoa wa Manyara, Mhandisi Omari Chambo alikaririwa akisema, “Mashamba hayo ni ya Endanahai Estate (Kiru Valey), lenye ukubwa wa heka 2,930, Kiru Plantation lenye ukubwa wa heka 1,536 na shamba la Unit 18 lenye ukubwa wa heka 2,390. Mashamba haya yatagawiwa kwa wananchi.” Pamoja na “nia” njema ya rais kufuta hati na kuamuru ardhi husika wagawiwe wananchi, je ni vigezo na sifa zipi na utaratibu upi utatumika kugawa ardhi husika? Kuna haja ya mamlaka kuweka wazi vitu hivi ili kuepuka ardhi husika kuishia kwenye mikono ya wanyakuzi wa ardhi au kugawiwa kirushwa na kiupendeleo kwa kufuata itikadi za kisiasa kwa faida ya chama tawala.
Tungeshauri uwekwe utaratibu wa kutangaza majina ya wanufaika (baada ya kuyahakiki) kwenye vyombo vya habari ili wananchi waone na kujiridhisha kuwa zoezi hili halitaishia kuwa la kuwanyang’anya ardhi wanyakuzi waitwao wawekezaji na kuwapa wanyakuzi wa kisiasa au ndugu na jamaa na marafiki zao kupitia rushwa, ufisadi a upendeleo.  Pia uwekaji wazi majina ya wanufaika, vigezo na sifa vilivyotumika utaepusha ardhi yetu kuishia kwenye mikono ya wageni hasa ukizingatia kuwa ardhi hiyo iko kwenye mkoa wa mpakani ambapo Tanzania siku hizi imegeuzwa shamba la bibi ambapo tunaambiwa kuwa wageni wamejiandikisha na kujipatia vitambulisho vya uraia wakati si raia. Inapokuja kwenye ardhi tena ya bure, ushawishi ni mkubwa kupita kiasi. Pia watakaosimamia zoezi hilo watajwe na ielezwe wamepatikana kwa vigezo vipi ili kuepuka wahusika kuishia kujigawia ardhi husika huku wananchi wakitumika kama mhuri tu kama ilivyozoeleka kwenye mambo mengi nchini.Huwezi kugawa ardhi kama pipi bila kuweka utaratibu unaofahamika kisheria kwa kila mwananchi.
Chanzo: Tanzania Daima Machi 31, 2015.

No comments: