The Chant of Savant

Saturday 28 March 2015

'Nawapongeza waishiwa kwa utoro mjengoni'

Taarifa nilizo nazo ni kwamba waishiwa ni mabingwa wa kutoroka mjengoni hasa wakati wa mijadala inayohitaji kutumia bongo. Nani anapenda kuumiza bongo lake wakati anaweza kuchepuka mijadala ya kuboa ikaisha akacha akazoa uchache na kwenda kujinoma? Je namna hii mnamkomoa nani zaidi ya kaya wajameni? Hata hivyo, tangu kaya igeuzwe No Man’s Land aka Shamba la Bibi nani anajali?
Hata hivyo, kwa kuelewa umuhimu wa chata la Mzee Jose Walioboa walilonyonga wakota kwa kutaka kuzuia ufisadi wao, msishangae kusikia wahishimiwa waishiwa wakifanya utoro.  Wamekuwa wakifanya hivyo hata wengine kuuchapa mjengoni huku wakianikwa na vyombo vya umbea udenda ukiwatoka na wengine kukoroma na kushua kwa kisambaa yaani kutoa hewa mbaya.  Bila kuua ili chata mbona wengi wangekoma na kukomaa. Kama wanakaya walitaka kuwatimua hata kabla ya msimu wao wa uishiwa haujaisha wanapoboronga viherehere wakawakingia kifua unategemea nini? Hivyo, haka kamchezo ka kukacha mjengo au kukaa mle kama masanamu bila kuchangia kataendelea. It is a lucrative business of siphoning boozers’ dosh. Acha niseme kimombo kidogo kuonyesha kuwa sikughushi wala kupewa ya dezo kama jamaa zangu madaktari na maporofwesa wa urongo na ukweli. Jei nonihino upo mpenda sifa?
Kwa vile waishiwa wanapotoroka mjengoni wanaishia kwenye mabaa na majumba ya kulala wageni kufanya vitu vyao, lazima niwapongeze kwa kupata kanywaji na starehe au vipi? Naona yule anasoma na kutikisa kichwa. Yule muishiwa naona anaanza kuchukua notebook ili aende kuchongea gazeti hili kwa kuwapa vipande vyao. Usijihangaishe. Ninaposema wanakwenda kwenye nyumba za wageni simaanishi wanakwenda kufanya majamboz zaidi ya kuuchapa usingizi. Hivyo, huna haja ya kupandwa na presha bure kuwa nimetukana au kugusa pasipoguswa. Waende huko wafanya majamboz au inanihusu nini wakati miwaya ipo inawangoja? Wakitaka waende au waache shauri yao. Kinachonihangaisha ni huu wizi wa mchana watoto hawa wanaofanya. Kama wamechoka uishiwa si waache kuliko kutelekeza majimbo yao? Walichaguliwa kuwakilisha walevi siyo kwenda kufanya ulevi na utoro ati.
Nawapongeza waishiwa si kwa kuibia walevi wala kujiweka hatarini kuukosa ulaji kwenye uchaguzi ujao hasa baada ya kufichuka uhovyo wao kuwa kumbe hawawakilishi walevi bali kwenda kujifanyia mambo yao huku wakizoa mshiko! Nawapongeza kwa vile wamenusurika na bonge ya zali kama si sanga au vipi? Hata hivyo, you are not out of woods yet folks.  Hili nadhani kwa walevi halivumiliki. Lazima kwenye uchaguzi ujao mwezi wa kumi wapige watu chini tena kwa kishindo cha ki-Tsunami. Najua wengi wanajipa moyo kuwa watachakachua kama walivyofanya mwaka 2010. Thubutu, mkijaribu kitaumana kiasi cha kuchimbika bila jembe. Patakuwa hapatoshi maana walevi wameishachoshwa na mchezo huu wa kichovu mchafu.
Kama si mama kipaza sauti kuwakingia kifua chake, ningewalima barua waandike maelezo juu ya kwanza, walipokuwa, walichokuwa wakifanya na kwanini wasipigwe bakora au mambo yao kuweka hadharani ili umma uwajue walivyo wa hovyo.
Pili, ningeamuru mshiko wote waliokwishazoa warejeshe tena kwa kulipa na interests kwa muda waliokaa nao. Ambao wangeleta gozigozi ningeamuru mashangingi yao yakamatwe na kupigwa mnada hapo hapo bila kuwapa muda. Hata hivyo, ni ngedere gani anaweza kumfanyia kweli nyani wakati wote lao moja yaani kuiba mahindi?
Tatu, ningeandika barua ya onyo na kwa watoro ili iwe kwenye kumbukumbu za mjengo kuwa walitenda jinai hii.
Nne, ningesambaza waraka kwenye majimbo yao kuwataarifu wenye jimbo kuwa hawana mwakilishi bali mtoro wa kawaida anayetumia muda na dhamana yao kufanya mambo yasiyo na maana.
Tano, ningehakikisha vyombo vya habari vinapewa orodha yao na picha zao ili vichapishe walevi wawajue na kuwatahadhari kwenye uchaguzi ujao.
Kwa vile yote haya hayakufanyika, kwanini nisiwapongeze waishiwa kunusurika kupatikana hata kuutema ulaji kama yule jamaa yangu Mzito Kabwela aliyejitiatia akaishia kupigwa kadi nyekundu na kuuacha ulaji wakati akiuhitaji.
Lo! Nilitaka kusahau kuwapa inshu. Mna habari kuwa waishiwa wanaosemekana walitoroka mjengoni kwa wingi walikuwa wapi? Kuna shushushu amenitonya kuwa walikuwa wamekwenda kwenye maadamano ya kumtaka fisadi fulani agombee ukuu ili awabamize mkenge walevi kama hana akili nzuri. Kwa vile waliamini kuwa jinai yao ya kutubambika mkenge mwingine inaweza kupita, walijiamini kwenda wakijua mkuu mpya atawakumbuka wale watakaotoswa na walevi kutokana na kuwa na nafasi bwerere za kujaza kama vile ukuu wa wilaya na mikoa, ubalozi, uwaziri ambavyo vimegeuka uchochoro wa kupachikia washikaji zao. Hata hivyo, lazima niseme wazi. Kama fisadi huyu atafanikiwa kugombea na baadaye akaupata ukuu basi mwenzenu nitajinyotoa roho kabla ya kuishi chini ya kidhabu huyu. Uchafu wa kisiasa, sanaa, ujambazi na uchangudoa wa kila aina vimenitosha. Lazima nijiondokee mapema kama mzee Mchonga ili nisishuhudie makufuru yanayoweza kuniua kwa sononi.
Ngoja. Naona yule muishiwa anaruka ukuta wa mjengo kuelekea Short time Nyumba ya wageni. Naona na yule mwingine anakata mbuga kuelekea baa ya Mama Coltide akastue kidogo. Naona yule naye ana msokoto wake wa ganja anakwenda uchochoroni kupata stimu kama alivyowahi kusema brother Jobless Nduguy kuwa waishiwa wanavuta mibangi na kubwia miunga nao wasikanushe.
Hakika kuna haja ya kuwapongeza wahishimiwa waishiwa kwa kuonyesha sura na nia zao halisi. Kazi kwa walevi kutafakari kuwa wenzenu wanakwenda kule kujiwakilisha na si kuwawakilisha. Hivyo, ufikapo mwezi wa kumi lazima muachane na ulevi na mibangi. Badala yake mchunguze nani anaweza kuwawakilisha mjengoni bila kutoroka, kuupiga usingizi, kukoroma, kushua, kutchangia hoja au kutoa upupu anapopata nafasi ya kuchangia.
Chanzo: Nipashe Machi 28, 2015.

No comments: