Saturday, 7 March 2015

Mwaadhimisha kuzaliwa CcM au njaa zenu?


          Baada ya Mlevi kubadili jina na kujiita Ml JK ambayo wengi hudhani ni Mteule Jaa Kaya au Riz, mambo yameanza kujipa. Juzi nikiwa zangu kwa Joji Kichaka nilipokwenda kumpa somo la kuchora picha si niliangukia kama wasemavyo ndugu zetu wa kaya ya Nyayo. Kwa wabongo unaweza kusema nilibamba ua vipi?
          Baada ya kutoka zangu Texas kwa Kichaka nilijitoma kwenye ubalozi wetu unaosifika kuwa kituo kikuu cha wasanii. Nilipata picha na wahusika pale na kupewa mwaliko wa kushiriki maadhimisho ya kuzaliwa chata la ulaji yaani Chama cha Maulaji (CcM). Lahaula! Waandaaji ambao –kimsingi si wakereketwa wa chama wala nini bali njaa zao – walistuka waliponiona. Walitikisa vichwa na wengine kutishia kuniramba vibao. Baada ya kusimama kwenye mkao wangu wa karate na kung fu mbona walinywea wakaanza kujichekesha na kukubali yaishe.
          Niliwatolea uvivu kwa kuwaambia kuwa kama wanawatapeli wengine ambao nao huwatapeli walevi, kwanini nao wasitapeliwe na kukubali kuwa ngoma ni droo? Waliridhika hasa baada ya kugundua kuwa nina mikanda yote ya karate na judo. Hivyo, hawakuwa na kidume cha kunishikisha adabu. Hayo tuyaache.
          Kama nilivyosema, kubadili jina na kubeba jina kuu kumelipa. Nilishiriki mauzauza haya yanayoitwa maadhimisho ya kuzaliwa kwa CcM. Hapakuwapo cha maana zaidi ya makulaji dhaifu na kanywaji kidogo na watu kuchonga misheni ya kuondolea aibu na kurejea Bongo baada ya kupigika ughaibuni.
          Baada ya kupata ulabu na kutoka nje na kupata bangi kidogo si Mwenembago wa kupayuka akapanda. Mtoto wa bosi mwenye chata lake alikuwapo amejaa tele kama pishi la mchele akichekacheka kama dingi wake ingawa inavyoonekana atazeeka haraka kuliko dingi wake. Maana nilipomkaribia nikagundua kuwa kipara kimeanza tofauti na mimi njemba ya miaka zaidi ya 50 ambaye bado nadai kuliko yeye kinda la jana. Sijui anazeeshwa na ulaji au fikra za jinsi atakavyoishi baada ya dingi kukabidhi mikoba.
          Niliporudi ndani ya kijiukumbi yalipokuwa yameandaliwa mauzauza wenyeji wangu waliniomba nitoa nasaha zangu kuhusiana na jinsi ya kuendeleza chata nje ya kaya. Si unajua mibangi tena? Ulimi nao hauna mfupa. Badala ya kusifia usanii huu si niliuponda. Mara nilianza kuzoboka. Nilikohoa kidogo na kupiga chafya kuonyesha kuwa niliyolenga kusema yasingempendeza mtu bali kumuudhi.
Nilisogeza mic karibu na kinywa changu na kusema,  ni jambo jema kupenda kitu. Lakini mapenzi haya lazima yawe ya dhati. Tofauti na hivyo huku si kupenda bali kuponda. Niligeuka huku na huku na kusema, mmefanya jambo jema sana ingawa kuna wanafiki wanajifanya wanaipenda kaya yao na chata letu. Huwa najiuliza: Nyinyi mmeonyesha mapenzi ya dhati kwa kuandaa kumbukizi hili adhimu. Niligeuka na kumwangalia mwana wa mfalme ambaye wao walidhani ni mteule kiasi cha kuingia mkenge wakanikaribisha wasijue nuksi. Nilikohoa tena na kusema, walaaniwe wanaokaa ughaibuni na kujifanya wanapenda chata lakini hawafanyi maadhimisho ya kuzaliwa kwake. Kama hawa wanaojifanya wanaipenda CcM bila kufanya maadhimisho ya kuzaliwa kwake basi warejee  kayani lau waijenge badala ya kudanganya wanaipenda wakati wanatafuta gea ya kurejerea baada ya mambo kuwashinda ughaibuni.  Hivi wanaweza kunieleza ni kwanini wameshindwa kuandaa party la nguvu na kutuita magwiji na wateule kuwahutubia na kubarika mambo yao? Hawajui wenye kaya nini?
Nilikohoa tena kutokana  na kijibaridi cha kipupwe au winter. Niliendelea kumwaga sera. Nauliza. Hivi hawa wangekuwa wanapenda chata letu CcM mngekimbia utawala wake na kukaa ughaibuni bila kuonyesha mapenzi ya dhati kwa kufanya maadhimisho ya kuzaliwa kwake? Ghalfa nikasema. I don't pay a hoot. Nitasema na nina hakika hakuna awezaye kunidhuduru. Najua wenzetu wanaojifanya wanapenda chata letu hawatapenda manaeno yangu. Wengine walishawahi kunitishia maisha wasijue siogopi kifo. Siasa za kijambazi zimepitwa na wakati. Lazima tuwaambie hata kama hawapendi kuwa hawana sera bali njaa na usanii. Huku ughaibuni kuna vyuo bwerere. Nawambia wazi wazi. Nendeni mkasome na kujikomboa badala ya kuendekeza kujikomba kwa vinyamkera na mafisadi wanaoitwa wapingaji wa chata letu tukutu.
Ghafla niliona kila mtu anakunja uso wakidhani nilikuwa nawapasha walioko juu ili walioko chini wapashike. Mara walianza kunong’onenezana. MC alikuja na kuninong’oneza sikioni akisema, “Wewe bwana unaogea sana kiasi cha kutoka kwenye point. Tafadhali malizia hotuba yako vinginevyo tutakutoa nje.”
Utadhani alikuwa amechokoza nyuki. Bangi na ulabu vilipanda nikaanza kuhema kwa nguvu na kupayuka zaidi. Nilisema kwa sauti ya juu kama wale wasanii wanaohubiri neno wakati wakificha meno ya kutaka njuluku. Nilisema. Nimefurahi kuwa ujumbe umefika. Kimsingi, ninaowaambia si wengine bali wasanii nyinyi mnaojigonga na kujikomba kwa dingi na hata vitegemezi vyake ilimpate gea ya kurejea baada ya mambo kuwashinda hapa ughaibuni. Rejeeni nyumbani mkachangamkie ulaji badala ya kuja na usanii wa kitoto. Siogopi ngurumbili. Mwenye ubavu wa kunivaa ajitokeze nimuache vipande vipande bila kujali nini wala nini. You are a bunch of criminals and con men and women hell bent to reap where you didn’t sow. Shame on you!
Baada ya jamaa kuona vimondo vyagu vikwachoma si walitishia kuniitia FBI baada ya vibaunsa vyao kunigwaya. Niliwapa live kuwa mimi mwenyewe FBI.  Pia niliwaonya kuwa wakiwaita FBI wenye makaratasi nao wataondoka name. baada ya kuona nimeshatoa dozi ya kutosha niliamua kujiondokea kwenda kuchonga na mzee Brack Obamiza mipango ya maana.

Tuache utani. Kujigonga kwa CcM kumegeuka aina mpya ya dili kwa wachovu waliokwama ughaibuni kutafutia gea ya kurejerea kayani lau watupiwe makombo. Ni bahati mbaya kuwa wanapotapeli chata nalo linawatapeli kwa vile linajua fika walivyokimbia sera zake sikinishi na fisadi. Hilo ndilo zali lililonipata kwenye kaya ya Joji Kichaka.
Chanzo: Nipashe Feb., 7, 2015. 

2 comments:

Anonymous said...

pengine humo hana maji wala nini ana act tuu anatafuta sifa alokuwa hanazo

NN Mhango said...

CCM wameishiwa sanaa na sera si akauze maji mjini badala ya kutupotezea muda.