The Chant of Savant

Tuesday 24 March 2015

Mauaji walemavu wa ngozi yatosha

          Kumekuwapo na mikakati, harakati na juhudi za kisiasa na maneno matamu kuhusiana kadhia hii. Vitendo ni haba tokana na uoza wa kimfumo unaoruhusu watu kutajirika bila kutaja walivyochuma wala kupata hizo mali. Ingawa tunaweza kuhanikiza kwenye majukwaa ya kisiasa kuwa tutapambana na kadhia hii, bila kushughulikia chanzo cha kadhia hii tunapoteza muda. Wengi watauawa kama ambavyo ilitokea hivi karibuni baada ya rais kufanya mkutano na walemavu wa ngozi. Huu ni ushahidi tosha kuwa mbinu na mikakati tunayotumia ni vya mdomoni tu na si vya moyoni wala vitendo. Inashangaza kwenye taifa ambalo limekuwa huru kwa zaidi ya miaka 50; lenye vyombo vyote vya usalama na upelelezi kushindwa kutatua tatizo hili.
          Inakuwaje tunapata mshipa na nguvu ya kuwalinda wanyama pori walioko kwenye hatari ya kutoweka lakini tunashindwa kuwalinda wanadamu wenzetu? Jibu ni rahisi kuwa tangu maadili yauawe na nafasi yake kuchukuliwa na uroho, roho mbaya, wizi, ufisadi na ujambazi, kila mtu anataka kuukata kwa njia yoyote iwe halali au haramu. Kimsingi, chanzo cha mauaji ya watu wenye ulemavu wa ngozi ni ya kimfumo. Tuna mfumo mbaya wa kujitajirisha bila kutoa jasho wala kukfauta utaratibu na kanuni ambavyo ni kufanya kazi halali kwa kujituma.
          Si uzushi kusema kuwa mamlaka zetu zinashiriki wazi kwenye mauaji ya ndugu zetu hawa. Haiwezekani taifa lenye kujitambua, kutambua na kujali utu wa watu wake likaruhusu au kushindwa kupamana na jinai na dhambi hii. Bila kukata mzizi wa kadhia hii ambao ni mfumo fisadi, wengi wataangamia bure. Sababu nyingine ni ujinga na imani za kishirikina. Hivi mnategemea nini kama mnaruhusu kila matapeli kutangaza biashara yao haramu kama uganga njaa na wa kienyeji au mahubiri ya kishrikina ya dini ambapo wahusika  huwahadaa watu maskini na waroho kuwa wanweza kutatua matatizo yao wakati wao  wana yao?
          Japo rais – kwa kukutana na walemavu wa ngozi –anaweza kutuaminisha kuwa atapambana na kadhia hii, yote ni bure bila kubadili mfumo wa sasa wa kijambazi. Turejeshe kanuni, sheria na miiko ya maadili uone. Mauaji ya wenye ulemavu wa ngozi na vikongwe –hata ya wanyama –yatatoweka yenyewe. Maana bila kuwakatisha tamaa washirikina na wajinga wanaosaka utajiri kipumbavu na kikatili, wataendelea kuua ndugu zetu bila sababu na utajiri wenyewe wasiupate.
          Huwa siachi kujiuliza; Hivi kweli haya mauaji ya walemavu wa ngozi yangekuwa yanawalenga matajiri au wanasiasa yangeendelea hivi kama ilivyo sasa ambabo kuzaliwa au kuzaa mtu mwenye ulemavu wa ngozi imekuwa ni kama laana? Pamoja na kwamba tumegeuka wanyama na wapumbavu kuhalalisha uroho, ufisadi na wizi, tunapaswa kujisuta kama taifa na jamii ya watu wenye akili na hisia. Sidhani kama rais angekuwa na mtoto mwenye ulemavu wa ngozi angeruhusu hali hii iendelee. Kama mzazi bila shaka angechukua hatua kwa kujua thamani ni mtoto wake. Hawa wazazi maskini wanaopoteza watoto wao au watu wanaopoteza ndugu zao wana hisia na uchungu kama binadamu yoyote. Inakuwa vigumu kuamini kama walemavu wa ngozi wanajivunia kuwa watanzania wakati wanaishi kwa kuwindwa na kuuawa kama wanyama wasio na thamani wala mlinzi. Kwao serikali ni genge la mauaji linaloshabikia maangamizi yao. Bila kuchukua hatua, hata tukiandika mabango ya “yatosha” bila kuchukua hatua mujarabu ni bure. Tuache kufanya mazingaombwe na mchezo na maisha ya binadamu wenzetu tena katika nchi yao inayopaswa kuwalinda na kuwatendea haki. Uhai ni haki ya kwanza na kubwa kuliko zote ya binadamu yoyote.
          Pamoja na kupambana na vyanzo vya mauaji ya walemavu wa ngozi ambavyo ni mfumo fisadi na jambazi, serikali inapaswa kutoa ulinzi na kuanzisha operesheni ya kupambana na wauaji hawa katili na wanyama wa walemavu wa ngozi. Umma unapaswa kuelimisha na kushirikishwa katika vita hii. Kimsingi, kama kutakuwapo na juhudi na utashi wa kweli wa kisiasa, tatizo hili ni dogo tu. Hivi kweli, hawa wanaoua ndugu zetu wangekuwa ni wavamizi wanaotaka kuchukua ardhi tena ya jangwa ya taifa letu tungewaangalia tu na kutoa matamko na ahadi hewa za kisiasa? Hivi kweli haya ndiyo maisha bora aliyowaahidi watanzania wote rais Kikwete wakati wa kampeni zilizomuingiza madarakani? Wakati tukipiga siasa na kutoa ahadi tamu lukuki wenzetu wanateketea. Sasa waende wapi kama serikali waliyoamini ina jukumu na uwezo wa kuwalinda imewatelekeza na kuwasaliti hivi? Ina maana wauaji wa wenye ulemavu wa ngozi hawafahamiki? Bila shaka wanafahamika. Je utawajuaje?  Huwezi kuacha nchi ijiendeshe kwenye autopilot ukategemea kadhia kama hii ijiondoe yenyewe. Pambaneni na ufisadi, wizi, ukosefu wa maadili na utajirisho wa haraka bila kutoa maelezo muone. Bila kubadili mfumo, mabango ya “yatosha’ na ahadi za kisiasa za midomoni majukwaani havitasaidia. Ifikie mahali tuseme kama taifa na jamii ya watu YATOSHA NA ITOSHE KWELI. Walemavu wa ngozi wasihofie kutembea wala kuishi kwa kujificha au kufichwa. Hii ni nchi yao sawa na wasio walemavu wa ngozi. Tuanze sasa kupambana na mauaji ya wenye ulemavu wa ngozi. YATOSHA, YATOSHA, YATOSHA.
Chanzo: Dira ya Mtanzania

No comments: