Saturday, 21 March 2015

Mlevi amlilia 1st Leidi kutupwa lupango

          Nadhani wengi mnamkumbuka bi Mkubwa Daktari Simone Gbagbo mama wa kwanza aka First Lady wa kaya ya Kodivaa au Cote d’Ivoire, mke wa rais Profesa Laurent Gbagbo ambaye walevi walipenda kumuita Badboy.  Aliitwa iron lady au bibi wa shaba kabla ya kuporomoka na kugeuka soil lady au bibi wa dongo tena tope. Si juzi akanyeshewa mvua 20 akanonihino lupango badala ya kula mikuku. Kama haitoshi –mzee Gbagbo – tangu mwaka 2011 yumo korokoroni akinonihino kwenye debe kule The Hague akingojea pilato aamue majaliwa yake.  “Hujafa hujaumbika” waweza kuumbuka. Nani alijua kuwa huyu mama bingwa wa nyodo za kufuja ulaji wa mumewe –kwa vile walilala kitanda kimoja –angeanguka kuumbuka na kufungika? Cheo ni dhamana na aliyeko juu mngoje chini waliona mbali.
          Profesa Gbagbo –japo tulikuwa faculty tofauti, tulifundisha pamoja kule Paris – wao huita Parie –Ufransee jiji la maraha na fasheni ambao wakubwa huenda kujinoma kabla hajaukata japo baadaye ulimkata akaishia kuadhirika na kunonihino debe.  Tulifundisha nini? I think haikuhusu hasa ikizingatiwa elimu ya Bongo ni kwa kiswa. Hata nikiyataja itakuwa vigumu kuyamanya. Est-ce-que connaissez vous qui anglais est langue comment les autre langues internationale?  Lol! Samahani nimechanganya kemiko. Hata hivyo tafsiri ya ufransee wangu ni kwamba ulijua kuwa ufransee ni lugha kama lugha nyingine za kimataifa? Je kimakonde kina ubavu wa ku-compete na lugha hizi kongwe na koloni? Hayo tuyaache.
          GbagobAlikuwa profesa wa kweli; si wa kuzawadiwa wala kilaza –japo baadaye –alifanya mambo kama kihiyo hadi akaishia pabaya. Pamoja na kisomo kikubwa –akina Gbagbo –walishindwa kusoma alama za wakati. Kama kuna jambo linawapiga chenga wengi si jingine bali hili. Unakuta jitu zuzu, shamba, kihiyo, bunga na kila kitu, baada ya kuukwaa ukubwa linajisahau. Hivi unategemea jitu lililokuwa ticha wa vidudu – kwa mfano – ligeuke profesa kweli hata kama uprofesa siku hizi unagawiwa kama pipi ukiachia mbali maprofedheha wenyewe kuwa vihiyo isivyotegemea kama ilivyotokea kwa wawili waliomwagwa maji hivi karibuni kwenye ulaji kayani?  Hii imenikumbusha fest leidi fulani ambaye akiandikiwa kimombo asome kwenye kuzurura kwake hutokwa jasho utadhani atanyauka na kudondoka. Si uende ukasome badala ya kuungaunga na kupaniki utadhani kuongea kimombo ni kumeze misumari wakati ni lugha kama nyingine?
          Turejee kwa 1st leidi. Baada ya kulewa ulaji aliona ni jambo jema kufia kwenye jungu akihomola asijue wapo wengine wanaongojea kwa hamu na ghamu! Hapa ndipo raha au karaha ya ulevi ilipo.  Nakumbuka alipopigwa chini na Alassane Outtara nilikwenda kule kumpa tafu nikasihi aachie ngazi kabla mambo hayajawa mambo. Tulikubaliana kisomi: Afanye hivyo haraka. Hata hivyo, punde si punde bi mkubwa Simone alipiga sindano za sikioni akamwamuru asiachie ulaji! Na kweli –wa muda mfupi – walionekana kushinda na kubaki kwenye ulaji wasijue ndiyo mambo yalikuwa yanaanza. Guess what. Walipolazimisha kukaa kwenye ulaji kwa muda wakajiridhisha, wapinzani wakaamua kuchukua zana kupambana nao. Kila mtu anajua aibu na ghadhabu iliyowapata wakubwa hawa vipofu waliochimbuliwa kwenye shimo la nguchiro utadhani Saddam Hussein.  Hii ndiyo tabu ya ulabu ndugu zanguni. Ukiisha uchapa uwe mma au makulaji basi unajisahau na kujiona wewe ni wewe usijue avumaye baharini pweza.
          Japo Simone anaweza kulaumiwa kwa vile yamempata. Je yuko peke yake? Siku hizi ufesti ledi umegeuzwa urais tosha.  Kwani mafesti leidi tena uchwara wanapigiwa saluti. Wakisafiri wanapokelewa na wakubwa wa kisiasa na kutoa kauli kama wanasiasa. Mchezo mchafu hauishii hapo.Wanaanzisha kampuni zao na kuziita NGOs na kuzichanga njuluku kama hawana akili. Wanajenga mashule binafsi na kujifanya ni mchango kwa jamii wakati ni vitega uchumi vyao. Kwanini mambo mazuri yote yatokanayo na biashara hii ya kichovu yapelekwe kwenye eneo alikozaliwa mhusika kama si biashara na kutaka kutumia hii kama mtaji wa kisiasa baadaye? Hii ni hongo hasa mhusika anapolenga kujiingiz akwenye siasa baada ya kutoka ikulu. Kwani hatuoni wala kujua?
          Kwenye kaya nyingine fisadi, chafu na chovu mafesti leidi wamewabana waume zao hadi wakawateua kuwa mawaziri au maafisa na wajumbe wa siasa kwenye vyama vya waume zao. Wawakatalie waone.  Mnajua wanawapa nini hadi wanalewa kiasi hicho. Sitaki mseme ni limbwata hata kama ni hivyo. Wamewanasa na wanatanua kama hawana akili nzuri kusema ule ukweli. Bila kujipendekeza kwa bi wakubwa hakifanyiki kitu. Hivyo, si vibaya wala bangi na ulabu kusema kuwa hawa mafesti leidi wanasiasa na wafanyabiashara wakati mwingine wanafaidi urais kuliko waume zao ambao wakiboronga wanalaumiwa kwa vile walichaguliwa na kuapishwa wao. Ila hii ya kutupwa lupango kwa Simone imeanza kubadili mchezo tahadhalini wahusika.
          Baada ya Simone kutupwa lupango nimekundua kitu kimoja. Kama dingi atakuwa kipofu kama festi nonihino wake wote wanaishia kunyea sorry kunonihino debe. Hakuna sehemu marais hawa wa bedroom waliponiacha hoi kama kuwawezesha mashoga, watoto, ndugu ya jamaa zao kuula kwenye sirikali za warume wao baada ya kuwa-corner huko kwenye bedrooms zao.
          Baada ya Simone kuvunja ndoa yake kwa kumshauri vibaya mumewe na kung’ang’ania madaraka, sasa amepigwa mvua 20lupango. Akitoka atakuwa kibibi cha miaka zaidi ya 85 akijjaliwa kutoka. Laiti angetumia akili za kawaida yaani common sense badala ya tumbo kujua kuwa ulafi mwisho wake si mzuri. Angajua tamaa ya madaraka ili kula bure wakati mwingine hugeuka kuwa chambo kwa fish ambaye huishia kunaswa akaliwa mzima mzima kama Simone. Je kuna Simone wangapi kwenye bara letu la mwanga kwa sasa?  Najikuta nikimlilia 1st leidi kwa kicheko badala ya kilio!
Chanzo: Nipashe Machi 21, 2015.

No comments: