Tuesday, 17 March 2015

Kikwete: Suluhu ni bora kuliko rambirambi

  • ... RAIS KIKWETE AWAFARIJI WALIO PATWA NA MAAFA YA MVUA YA MAWE KAHAMA LEO
          Vifo vya mara kwa mara vya watanzania ambavyo vingeweza kuzoeleka kutokana na ajali za mara kwa mara vimeanza kuzoeleka. Hii ni bahati mbaya sana. Yamekuwa mazoea kusoma taarifa za salamu za rambirambi za rais Jakaya Kikwete kwa familia za wahanga wa vifo vitokanavyo na uzembe wa watendaji wake. Japo si jambo baya kwa wafiwa je rambirambi badala ya kushughulikia vyanzo ambavyo viko chini ya rais si bora kuliko rambirambi? Mfano wa karibuni ni ajali mbaya iliyotekea Mafinga ikuhusisha basi la abiria la Majinga Express na roli lilokuwa limebeba kontena. Vyombo vya habari vilikaririwa vikesema chanzo cha ajali hii iliyogharimu maisha ya watu zaidi 30 ni kutaka kukwepa shimo kubwa katikati ya barabara. Je hili shimo lingezibwa mapema maisha ya wahanga yasingeokolewa? Je mamlaka zinazoshughulika na miundombinu zinaweza kutoa maelezo gani ya kina? Je kwanini rais – badala ya kupoteza muda mwingi kwenye rambirambi – kwanini asikae kimya akawashughulikia wahusika na kutoa taarifa ili lau kuwapoza nyoyo wahanga badala ya kutoa salamu za rambirambi ukawa mwisho wa kila kitu? Je inaingia akilini kwa rais ambaye serikali yake inahusika na vifo hivyo kutoa salamu za rambirambi badala ya kushughulikia watendaji wake wabovu na wauaji?
          Wengi wanaweza kujiuliza hapa rais anaingiaje kwenye ajali ya barabarani? Ni rahisi kumuunganisha rais na kadhia hii. Kwanza, kama mkuu wa nchi anabeba lawama kwa kutopambana na rushwa na ufisadi ambavyo ndivyo vyanzo vikubwa vya miundo mbinu mibovu ima tokana na kujengwa chini ya kiwango au kutohudumiwa ingawa bunge linatenga fedha kwa ajili yake kila bajeti. Kwa kumbukumbu hata vyombo vya habari –kwa mfano – viliporipoti aina mpya ya ufisadi ambapo ukubwa wa barabara unapunguzwa hadi kwa upana wa meta moja, sikusikia serikali ikitoa maelezo wala kushughulikia jinai hii. Nahisi rais anayeshughulikia vyanzo vya maafa kama haya ya barabarani yanayoweza kuepukika ni bora kuliko anayeshughulishwa na salamu za rambirambi.   Pili, kama sheria za uongozi bora zingefuatwa, waliosababisha kutozibwa shimo husika wangefikishwa mahakamani na kupewa adhabu baada ya kukabiliwa na mashtaka ya kuua hata kama bila kukusudia jambo ambalo rais alipasa kulitolea maelezo jinsi atakavyolishughulikia kwa ama kuwawajibisha wahusika au kuwafikisha mahakamani au vyote kwa pamoja.
          Tatu, rais kuonyesha uchungu kwa kutoa rambirambi badala ya kubuni mipango ya kupunguza au kuzuia ajali inafanya wengi kujiuliza ni kipi kinapaswa kupewa kipaumbele na rais hapa. Hata hivyo, kwa rais ambaye habanwi na sheria wala asiyetumia barabara mara kwa mara, hili haliwezi kumhangaisha hasa ikizingatiwa kuwa yanapotokea mauji kama haya serikali yake haibanwi na sheria kulipa lau fidia au kutoa maelezo au hata kutumliwa madarakani kama kwenye mataifa ya wenzetu wa magharibi. Utashangaa, hata mawaziri wa Uchukuzi na Ujenzi hawataguswa zaidi ya kumsingizia Mungu kuwa ni mapenzi yake wakati ni uzembe na ubovu wa kimfumo kuanzia juu hadi chini.
          Nne, rais  kama kiongozi  wa nchi kutuma rambirambi kwa wakuu wa mikoa ambao kimsingi ni wawakilishi wake ni kama kutaka aonekane anajali hasa kazi za wakuu wa mikoa na wilaya ni kumwakilisha rais.  Hapa ni kama rais anajitumia salamu. Kimsingi, sielewi mantiki ya utaratibu huu na jinsi unavyosaidi kwenye kutatua matatizo husika.  Nadhani ingeingia akilini kama rais angetoa huduma kwa waathirika na waliowaacha nyuma badala ya maneno matamu. Mzazi – kwa mfano anapokufa ghafla kama hivi – wanaoathirika kwanza ni familia yake. Nadhani kwa anayemjali marehemu na familia yake –kwa siri au wazi wazi – angehangaishwa na kutathmini mahitaji ya waliobaki ili kuona asaidie wapi badala ya mashairi na ngojera. Hili lipo chini ya uwezo wa rais hasa ikizingatiwa kuwa ofisi yake licha ya kuwa na kitengo cha maafa ina fedha ambazo zinatumika bila ulazima ambazo zingeelekezwa kuwasaidia wahanga wa sera na usimamizi mbovu wa serikali. Hivi –wa mfano –rais akiamua kuacha ziara moja isiyo ya lazima ughaibuni akaelekeza fedha zake kwa wahanga ataokoa maisha ya waathirika wangapi ukiachia mbali kuchangia kwenye maendeleo yao na ya taifa badala ya kutuma rambirambi? Nani anaweza kula salamu za rambirambi? Salamu za rais haziwezi kumpeleka yatima shule wala kumpa kibarua mama aliyekuwa akimtegemea mumewe aliyeuawa na mfumo wa kizembe na wa kifisadi kama miundombinu mibovu kama kwenye ajali tajwa. Nafahamu ninayosema hafurahishi kwa wakubwa. Ila kwa waathirika nadhani ni ushauri mzuri kwa wakubwa kama kweli wanawajali kama wanavyoonyesha kwenye salamu zao. Huwezi kula wala kuvaa salamu za rambirambi jamani kama tutakuwa wakweli kwa nafsi zetu wenyewe tukaweka siasa pembeni na sifa rahisi.
          Tumalize kwa kushauri kuwa tufikie mahali tufanye vitu kama watu wenye akili na utu badala ya kufanya mchezo na uhai wa wenzetu. Vifo vitokanavyo na ajali za barabarani –hata kama si vyote – vinazuilika kama serikali itaacha uzembe, ubabaishaji na ufisadi, kulindana na kushughulika na mambo yasiyo muhimu huku ikiacha ya muhimu. Kikwete, suluhu ni bora kuliko rambirambi.
Chanzo: Tanzania Daima Machi 18, 2015.

2 comments:

Anonymous said...

hongera rais wetu umefanya jambo zuri sana bora mkate nusu kuliko kukosa kabisa wewe ndio kiongozi bora katika africa nzima sijuwi ukiondaka wewe tanzania itakuwa vp
tuombe mungu tanzania ni nchi pekee yenye amani na au kuna anayebisha hilo

NN Mhango said...

Anon usemayo ni kweli. Kama ukiwa na mtazamo wa karibu unaweza kuona anachofanya rais ni cha maana wakati si kweli. Kinachotakiwa hapa ni kuwa na mipango madhubuti ya kupambana na maafa. Pia kupambana na umaskini. Maana wahanga wangekuwa wamejenga nyumba bora madahara yasingekuwa makubwa kiasi hicho. Je kwenda kwa rais kuwajulia hali kumeondoa tatizo wakati juzi tumeona wakifunga barabara baada ya kusahaulika?