Tuesday, 31 March 2015

Kijiwe kuandamana kumshawishi Lowassa asigombee


          Baada ya kushuhudia aina mpya ya usanii ambapo wagombea urais hwapa watu hongo kidogo ili wajifanye wanakwenda kuwashawishi wagombee, Kijiwe kimeamua kuja na mpango tofauti ambapo kitakuwa kikiandamana kupinga wale wanaokuwa wameshawishiwa.
Mpemba anaingia huku akiwa anavuta uradi na kula mic, “Yakhe leo sinywi kahawa mpaka mnshawishi kama wale wanaotaka washawishiwe ndo wagombee urais utadhani hawautaki. Nshawishini basi.”
Kiiwe hakina mbavu jinsi Mpemba anavyotoa mikono akitaka ashawishiwe asijue ushawishi mwingine ni hatari hasa unapoinga kwenye siasa.
Mgosi Machungi anaamua kumnyang’anya mic, “Tikishawishi bue bue bia kutupa chochote kama wale wanavyohonga wasaka tonge kama aivvyosema mwanangu Jan Makambale? Siku hizi dunia imeahaibika kwei kwei. Hata mashehe wanahongwa upuuzi!”
“Yakhe mie nsema, wale si mashehee bali masheena. Mie hapa shehe nani awezakuja nambia eti anipe mapupu, utumbo, rushua ndogo ndogo na ujinga mwingine eti nende kumshawishi.  Kwani yeye binti anotaka wa kumuooa?” mpemba anaamua kuzoza.
“Du hii kali. Tukiwa wakweli ukweli ni kwamba anayeshawishiwa ni mchumba na si vinginevyo. Du wapinzani wakiipata hii jamaa ataipata kweli kweli!” Mipawa anajibu. 
“Tuache utani jamani. Mie nadhani kuwasaidia hawa wanaodhani kuwa wote tuna njaa kiasi cha kutumia matumbo au tu wepesi wa kusahau kama panya waache matusi ya nguoni. Tunapaswa kuanza kuandamana kila wanapotokea wasanii hawa uchwara na wala makombo wao wakashawishiana.” Anachomekea Mijjinga.
Kapende anadakia, “Kweli hapa umetoa bonge la pwenti. Kama wao wanafurahia kushawishiwa kama haki yao ya kidemokrasia, kwanini nasi tusifurahie kuwashawishi wasigombee hadi watimize mambo fulani fulani?”
Mipawa anakatua mic, “Yes, itakuwa bomba kama tutaandamana kumshawishi Lowassa asigombee hadi atoe maelezo dhidi ya tuhuma ambazo zimekuwa zikimkabili tangu enzi za mzee Mchonga. Pia tumshawishi asigombee kwa sababu alishapewa nafasi ya juu ya uongozi akaifuja. Hivyo, tumshauri aache wenye sifa safi wagombee wenyewe tena si kwa kushawishiwa.”
Msomi Mkatatamaa anaamua kutia guu tena mapema. “Hebu tuwe serious kidogo, mnadhani hiki kinachoitwa kushawishiwa ni kushawishiwa kweli au kuishiwa? Nadhani mgombea urais anayesema ameshawishiwa wakati alishatangaza miaka mingi iliyopita hadi akapewa adhabu anatugeuza wote majuha na pia kuna kitu anachoficha. Kwani lazima yeye?”
“Usemayo kweli Msomi. Kwani lazima yeye au ana lake? Nadhani kwa kitendo cha kuwakusanya wachovu na kuwadhalilisha kwa kuwapa vijifedha mapupu pombe na tende kinatosha kutuonyesha mtu wetu alivyo wa hovyo.” Anachomekea Mzee Maneno.
Msomi anaendelea, “Kimsingi anachofanya huyu bwana ni kutoa hongo hadharani tena kwa halaiki ambalo ni kosa kubwa sana tu kisheria. Huoni hata chama chake kilivyompiga stop baada ya kugundua anavyovunja sheria na kuzidi kukipaka mavi wakati matope kilicho nayo yanatosha?”
Sofia aka Kanungaembe anaamua kuingilia, “Hivi jamani rushwa gani hii ambayo inatolewa hadharani? Si mseme mnamchukia baba watu tena mtu mzuri tu.”
Mbwamwitu anamchomekea Sofi na kusema, “Mtu mzuri siyo? Mkewe akikusikia utatafuta ba kujificha mwenyewe.”
Mheshimwa Bwege aliyekuwa akivuta sigara kali yake, anatupa kipisi na kumpoka mic Sofi, “Sofi dada yangu kwanza nikuonye. Haya mambo ya kusifia waume za watu hayatusaidii. Kama unamtaka si umfuate ukamshawishi nawe? Nadhani huyu jamaa kaja na mkakati wa kujimaliza. Hivi unapochukua mashehena ukayaita mashehe sie mashehe wa kweli tutakuelewa? Aache kudhalilisha watu kwa tamaa zao na zake. Sasa namtumia salamu kabla ya kuandamana kumshawishi asigombee. Hata angeshawishiwa na malaika na watakatifu hapati kitu, hafai hafai hafai hafai ad infinitum.”
Msomi anakwanyua mic, “Mheshimiwa Bwege umeniacha hoi. Eti hata kama Lowassa atashawishiwa na malaika na watakatifu hafai? Hapana, kufaa au kutofaa sisi hakutuhusu. Kinachotuhangaisha ni kutaka atutendee haki lau atupe maelezo au kujibu tuhuma dhidi yake. Najua anaweza kusema hajashitakiwa. Ila ajue mahakama ya kisiasa ni wananchi na si mahakama za kiserikali kama baadhi ya watu aliwaoliwapa kumtetea wanavyodhani.”
Sofia anamchomekea Msomi, “Nasema jamaa ni safi na wanaomtuhumu wanahangaishwa na chuki binafsi.”
Kapende aliyekuwa akisoma gazeti ameamua kurejea, “Sofia acha utani. Hivi umeingiliwa na nini au nawe unataka ushawishiwe uache imani hizi. Unataka kuniambia kuwa hata baba wa taifa alikuwa na chuki binafsi siyo?”
Maneno ya Sofi yamewaudhi wangi, Mpemba anakula mic, “Yakhe huyu dadaetu aonekana ana mapenzi ya kibubusa. Hata hivo tumwambie, ka antaka huyo mtu wake si ende washawishiane huko?
Kanji haridhiki, “Pemba hapa sambulia sofi. Hapa sema sawisi Lowassa. Tafunja doa yake na bi kuba taumiza Sofi yetu hiii hiii mimi lilia sana Sofi.”
Baada ya Msomi kugundua kuwa kumbe utani unaanza kuingilia mjadala anaamua kuingiza pwenti nyingine. Anakula mic, “Mnaonaje tukapanga siku ya kwenda kumshawishia jamaa asigombee na badala yake aende kujisafisha kuhusiana na tuhuma zinazomkabili? Pia tukienda tumshauri afanye vitu vinavyowezekana badala ya maigizo ambayo mwisho wake si mzuri.”

Kijiwe kikiwa ndo kinanoga si wakatokeza wale mashehena walionunuliwa na kuhongwa upuuzi kiasi cha kutudharaulisha na kutudhalilisha sisi mashehe wa kweli. Acha tuwakimbize lau tuwarambe bakora watie akilini!
Chanzo: Tanzania Daima Machi 31, 2015.

No comments: