Tuesday, 24 March 2015

Kijiwe chalaani na kutaka mauaji ya albino yakomeshwe


          Baada ya kutoridhishwa na sanaa na ubabaishaji unaofanyika dhidi ya maisha ya ndugu zetu wenye ulemavu wa ngozi, kama Kijiwe, tumekaa kama kamati kulaani na kushinikiza mauaji haya ya kishenzi yakomeshwe.
          Mpemba leo ndiye anaanzisha mjadala. Anakula mic baada ya kubwia kahawa yake, “Yakhe mmeshuhudia jinsi rahisi alivokutana na uongozi wa watu wenye ulemavu wa ngozi? Je mmepata somo gani hapa?”
          Msomi Mkatatamaa anaonyesha kukerwa na kadhia hii wazi wazi. Anakwanyua mic, “Japo somo tulilopata ni la hovyo, ni kwamba ndugu zetu hawa wenye ulemavu wa ngozi watauawa sana hasa kutokana na siasa na usanii vinavyofanywa kwenye kadhia hii. Kwangu rais kukutana nao na kupiga picha si jambo la msingi kama kufumua mfumo unaochochea mauaji haya.”
          Kabla ya kuendelea, Sofia Lion aka Kanungaembe anamchomekea Msomi akisema, “Sasa hapa mfumo unaingiaje na kukosekana kwa maana kwa mtukufu rahisi kukutana na walemavu wa ngovi vinatoka wapi kama siyo kutafuta kumtwisha mtukufu zigo bila sababu?”
          Msomi anakwanyua mic, “Umeuliza swali zuri da Sofi. Ina maana hujui kuwa haya mauaji ya kinyama na kishenzi yamechochewa na kuridhia na kulinda ufisadi?” Anamkazia macho Sofi na kuendelea, “Je wewe kwa uzoefu wako hata kama ni mdogo, unadhani nini kinafanya haya mauaji ya kipuuzi na kipumbavu yaendelee kama si kutawaliwa na mfumo wa kifisadi unaofumbia macho wahalifu wanaotaka utajiri wa haraka? Mtaua wote na baada ya hapo mtafanya nini kama si upuuzi na upumbavu wa mchana? Hawa ni watu sawa na wengine wanaopaswa kulindwa na kaya yao. Vinginevyo lisirikali halina uhalali wa kuendelea kuwa kwenye maulaji kama haliwezi kuhakikisha ulinzi na usalama kwa wanakaya wake.”
          “Una maanisha nini? Mbona sijakuelewa hapa?” Sofi anajibu kwa kujitetea.
          “Usiwe na shaka utanielewa na nitakutosheleza kwa kukupa dozi ya kutosha.” Msomi anajibu.
          Kabla ya kuendelea, Mbwamwitu anadakia, “Unamtosheleza vipi na katika nini na kwa dozi ya nini? Msomi mbona umeniacha hoi?”
          Msomi anakwanyua mic na kujibu, “Usipate taabu. Hata wewe nitakutosheleza tu. Utajua ninamaanishacho punde.  Hebu tujiulize kama watu wenye akili na mapenzi mema kwa kaya. Hivi, bila kuwa na ukosefu wa maadili na badala yake kukawapo madili unadhani hawa wanaoua wenzao kwa tamaa za utajiri kama wangekuwa wanabanwa na sheria kueleza walivyopata utajiri wao kweli wangepata motisha wa kutenda jinai hii?”
          Mbwamwitu anajitetea,”Msomi nakuheshimu sana. Tuheshimiane  na kama ni dozi basi kampe Sofi siyo mimi.”
          Anamkazia macho Mbwamwitu na kuendelea, “Japo ni matokeo ya ujinga na ushirikina, ukweli ni kwamba hawa wanaoua ndugu zetu wanadanganywa na matapeli wanaojiita waganga waliotamalaki kila sehemu kuwa viungo vya ndugu zetu wenye ulemavu wa ngozi vikichanganywa na dawa vinaweza kuwafanya wawe matajiri wakati ni ujinga na upumbavu. Bila kuchapa kazi kwa juhudi na maarifa yote ni bure mtaendelea kuwa maskini tu.”
          Mijjinga anachomekea, “Unamaanisha kama yule mwenye kibao kinachosema “Njoo nikusafishie nyota na kukupa dawa ya utajiri”? Ananyooshea kidole bango la mganga wa kienyeji lililoko mtaani karibu na kijiwe.
          Kapende ambaye leo kauramba kweli kweli anatia guu, “Tuache uvivu wa kufikiri kama mzee Ben. Kwanini baada ya mjadala huu tusiporomoshe haya mabango angalau hapa mtaani?”
          Mipawa anakwanyua mic, “Kapende umenena. Lazima leo tufanye kweli.”
          Mpemba anachomekea, “Wallahi nami naunga nkono hii hatua ya kimapinduzi na kishujaa. Lazimu tufanye kweli ati.”
          Kanji naye hajivungi, “Hata mimi unga kono na guu. Veve nasema kweli kabisa dugu yangu. Sisi kama nakwenda angusha bango jua fika kuu naye tia akilini.” Anamalizia huku akimtaza Sofi ambaye huwa hapendi mkuu kuguswa vibaya.
Mheshimiwa Bwege anaamua kujinoma, “Waheshimiwa msemayo ni kweli tupu. Tumegeuka kaya ya washirikina kutokana na kutawaliwa na wasanii na washirikina wasioona mbele zaidi ya usawa wa pua zao. Ningekuwa mkuu haya mauaji yangekoma ndani ya masaa 24. Kwanza, ningeamuru waganga wote wa kienyeji waswekwe lupango mara moja. Pili, badala ya kutumia ndata kuua waandamanaji, ningetoa amri kila ndata aje na mhalifu mmoja ndani ya wiki moja.”
“Huna haja ya kuanzisha udikteta na matumizi ya nguvu. Ukifanya hivyo, usishangae ndata kuwabambikizia kesi wabaya wao au wanaowanyima rushwa. Dawa ni ndogo tu. Rejesha maadili kwa kaya nzima bila kujali kazi wala cheo cha mtu. Taja mali zako na halafu waambie wanakaya wote kufuata mfano. It is as simple as that so to speak.”
Mipawa anakwanyua mic, “Nkwingwa hoja yako ina mashiko. Naona hili unalopendekeza linaingia akilini kuliko kukutana na wahanga na kupiga picha nao kwa ajili ya kutafuta ujiko wa shilingi mbili.”
“Kwa vie muda unakwenda, kwanini tisiende kuangusha yae mabango hapa kwanza ili iwe saamu tosha kwa mkuu? Azima tiwaonyesha mfano tena hapa hapa na humu humu au vipi?”
Baada ya kuona muda unayoyoma, tuliamua kwenda kuangusha mabongo ya waganga njaa kama onyo kwa wote wanaocheza makidamakida na maisha ya ndugu zetu wenye ulemavu wa ngozi. Ole wao watakaoendelea kufanya usanii na maisha ya ndugu zetu!
Chanzo: Tanzania Daima Machi 25, 2015.

No comments: