Saturday, 14 March 2015

'Porofweza' Nshomile na mboga ya milioni 10!

Iwe bojo wakati  mwingine inakuwa vigumu kuelewa busara ya baadhi ya walevi. Inakuwa kazi  hasa unapokuta mlevi anayechukuliwa kama msomi wa kupigiwa mfano akifanya vitu ambavyo hata mjinga wa kawaida hawezi kufanya. Hivi karibuni waziri wa zamani wa Udongo, Mbavu na Maangamizi ya Nyumba za umma profesa  NshomileTibakumbuka alitoa mpya kiasi cha kuacha wavuta bangi na walevi wakishangaa hata huo ubukuzi na busara yake. 
 Porofweza Nshomile alikaririwa na vyombo vya habari akisema, “Nilitoa Shilingi milioni 10 kununua mboga, kwani kuna kosa gani.” Hapa anachomaanisha Nshomile ni shilingi za kibongo milioni kumi. Hata kama alikusudia kitu kingine, kwa mtu msomi ngazi ya Nshomile alipaswa kujua madhara ya kauli kama hii ambayo Waingereza huita irresponsible. 
 Huwezi kuita milioni 10 pesa ya mboga wakati walevi wengine maskini wanakufa bila kupata hata alfu  10, jamani milioni 10  ni fedha ya mboga huku watu wanalala njaa kwa kukosa 1,000. Kwa lugha rahisi ni kwamba Nshomile alijitahidi kuonyesha alivyo tajiri anayeweza kutumia mamilioni ya fedha kwa ajili ya kununulia mboga.  
Sijui hiyo mboga ni ya aina gani? Bila shaka ina viungo vya almas, dhahabu, bangi na rubi.Hata hivyo, kutoa nyodo kama hizi ni kuwakera walevi. Nani mara hii kasahau jinsi mwenzie ‘Mtemi’  alivyoita dola za ki-jiji Kichaka alizosemekana kupokea kama rushwa na kuzificha kwenye visiwa vya Jersey huko Uingereza kuwa ni  vijisenti? Kama haitoshi, bingwa wa kuhonga na mtuhumiwa mkuu wa wizi wa ‘escroew Jammy Rugemalayer aliita Dola milioni 75 vijisenti vya ugoro. Sijui ni aina gani hii ya ugoro anaobwia Rugema. Kimsingi, wahusika waliamua –bila huruma wala aibu –kuwakoga walevi maskini waliowaamini ofisi zao wakazitumia kama vijiko vya kuchotea utajiri. Ajabu ya maajabu, mzee wa vijisenti na mama wa mboga bado ni waishiwa mnjengoni! Mwe!  Tumekwisha! Je hawa wanafanana na walevi? Naona kama hawafai kumwakilisha yeyote mnjengoni zaidi ya matumbo yao. Wanakwenda kupiga dili na kuzika maadili utu na huruma ukiachia mbali kushiba hadi wakalewa na kuondokewa busara. 
Ukiangalia tambo za kijinga za namna hii unagundua kitu kimoja. Wanatoa motisha kwa maskini kutafuta fedha kwa njia yoyote ile ili mradi nao waukate kama wakubwa hawa mabingwa wa kusema bila kufikiri wala kuchelea nini inaweza kuwa tafsiri ya kufuru zao. Unashangaa mantiki ya mtu kama mzee wa vijisenti kuwa mwanasheria mwenye shahada ya uzamili lakini akatenda kama mtoto wa darasa la tatu. 
Kimsingi, kaya inatawaliwa na watu wasio na utu wala huruma; waroho na wenye roho mbaya wasiowajali wenzao. Sidhani kama Wamarekani wanaosifika kwa utajiri wanaweza kusema maneno kama haya tena mbele ya vyombo vya habari.  
Kilichofanywa na wajivuni hawa ni kuonyesha kuwa tumegeuka kaya ya kifisadi na kijivuni ambapo kila mlevi anaweza kujipayukia atakavyo ilmradi afurahishe roho yake kama alivyowahi kusema mkulu Njaa Kaya kuwa furaha ujipe mwenyewe usingoje kupewa. 
Hata hivyo, ni kuumiza wengine kwa kujipa furaha kwa kuwaibia au kuwaudhi wengine. 
Ukifuatilia matamshi ya wanene wetu, unabaki kuhuzunika. Nani amesahau maneno ya Mkulu kuwa wasichana wa shule za msingi na sekondari wanapata mimba kwa kiherehere chao bila kuangalia chanzo hasa cha jinai hii ambayo imetokana na kukithiri kwa ufisadi na wizi kiasi cha wenye fedha kuzitumia kuwahonga watoto wa shule na mahakimu wanapofikishwa mahakamani? 
Hivi shilingi milioni 10 ni mshahara wa miaka mingapi wa ticha, karani au muuguzi wa Namanyere? Hata hao matajiri wenye biashara zao–tena halali –hawawezi kuita fweza hizo za mboga. Hata hivyo, Nshomile alikuwa na uchungu gani na fedha husika kama anaweza kutumiwa mabilioni bila kueleza alichofanya? Sijui kama huyu analipa kodi vilivyo. 
 Na ni ajabu kuwa pamoja na kuonyesha jeuri ya utajiri sirikali haijambana arejeshe njuluku hiyo kwa vile hawezi kuitolea maelezo ya ni kwanini alilipwa na kama alilipwa ni kwa kazi ipi wakati alikuwa mtumishi wa umma! Je mamlaka zinashindwa kuwashughulikia wajivuni kama hawa kutokana na kufanana na wakubwa wake wengi waliojificha nyuma ya ulaji? 
Nyodo hizi zinanikumbusha Giriki aliyewahi kudai kuwa alikuwa ameiweka serikali ya awamu ya kwanza mfukoni mwake.  Mzee Mchonga aliposikia kufuru hizi aling’aka, “Hilo fuko linaloweza kuweka serikalina ukubwa kiasi gani?”  Punde si punde, Mchonga alimtimua mjivuni huyu bila kujali nini wala nini. 
Huu ndiyo uongozi wenye kuona mbali na uliotukuka. Kwani mzee Mchonga alijua madhara ya kauli ile kama asingechukua hatua haraka. Baada ya madaraka kuwa ulaji wa dezo na wa kifisi, nani anakerwa na kauli kama hizi ambazo ni maudhi kwa walevi? Nani amshughulikie nani wakati wote ni kambale wenye sharubu? 
 Kwa jinsi mamlaka zinavyowaendekeza, kuwalea na kuwagwaya mafisadi na wezi wakubwa kwa vile wana fedha ya kuhonga, si vibaya kujenga dhana kuwa siri-kali yote inaundwa na wale wale wanaoweza kujipayukia bila vinywa vyao kuwasiliana na ubongo. Ni balaa kiasi gani kwa taifa? 
Tumalizie kwa kumpinga Nshomile kuwa hata huko Marekani wanene wanakokesha wakijigonga na kutembeza bakuli bado hiyo njuluku hawezi kuwa ya mboga. Yatosha kusema kuwa maneno ya Nshomile ni ushahidi kuwa sifa zake zina mshikeli. Mlevi anayetumia milioni 10 kwa mboga ahitaji kazi toka kwa umma wala hafai. Hivyo, sitegemei kama Nshomile atapitishwa na chama chake kugombea tena uhishimiwa. Ili kutaka nini na kufanya nini wakati ameishajilipa?
Chanzo: Nipashe Machi 14, 2015.

No comments: