The Chant of Savant

Tuesday 24 March 2015

Kikwete anawaonea wakuu wa wilaya walevi

JK apokea vitabu vya sayansi kwa shule za Sekondari vilivyochapishwa ...
 
Hivi karibuni rais Jakaya Kikwete alisikika akilalamikia wakuu wa wilaya walevi ambao ulevi wao ulimlazimisha kuwatimua kazi. Alikaririwa na vyombo vya habari akisema, “Pale ulipo ni role model (mfano wa kuigwa), lazima uwe na tabia njema kwa kauli, matendo, nidhamu na uadilifu usiotiliwa shaka.” Hivi Kikwete anaishi dunia gani kuongelea uadilifu ambaye yeye hana ila anataka wenzake wawe nao? Mara hii amesahau alivyoshindwa kutoa maelezo baada ya kutuhumiwa kushiriki wizi wa EPA ambapo mabilioni ya shilingi yaliibiwa toka Benki Kuu kwenda kufadhili mradi wake wa kuingia madarakani? Mara hii Kikwete amesahau kuwa alikataa kutaja mali zake na kama alishafanya hivyo ilikuwa ni baada ya mbinde? Anataka hao wakuu wa wilaya waige uadilifu toka kwa nani wakati taifa kwa sasa linaendeshwa kwa uhalifu na ufisadi?
Je nani aliwatuea watu walevi na wasio makini zaidi ya rais mwenyewe ambaye kwa kufanya hivyo ni ushahidi tosha kuwa hakuwa makini? Je kama si kuendelea kulindana au kuwasingizia, kwanini rais hakuwataja kwa majina lao umma uwajue? Je katika hawa aliowateua kiasi cha kuzusha malalamiko toka kwa wananchi hakuna walevi na watu wasiojua hata umuhimu wa nafasi zao ukiachia mbali kutofaa kabisa? Rejea uteuzi wa hivi karibuni ambapo watu vihiyo, wahuni na wababaishaji hata wasaliti kupewa ukuu wa wilaya.
Kukiri kwa rais ni ushahidi tosha na matokeo ya kupeana vyeo ima kwa kujuana, kulindana, kulipana na fadhila na kuzawadiana bila kujali sifa za mhusika. Si chuku wala uzushi kusema kuwa wateule wabovu wako karibu kila mahali kwenye serikali ya Kikwete. Si kwenye ukuu wa wilaya wala mikoa bali hata kwenye baraza la mawaziri, kumejazwa watu wa kutia shaka ambao kimsingi hawalisaidii taifa bali kuwa mizigo kama makada wenzake wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) walivyowahi kudai akawapuuza kulinda urafiki na kujuana kwake na mizigo yake ambayo inaendelea kuwa mizigo kweli kwa taifa. Tuna viongozi wa hovyo wanaozurura kama ambavyo katibu mkuu wa CCM Abdulrahaman Kinana alivyosema kuhusiana na waziri Lazaro Nyarandu aliyemtuhumu kwa uzururaji japo naye Kinana ni mzururaji mzuri tu. Ama kweli nyani haoni kundule!
Kama tutakuwa wakweli, baadhi ya tabia ambazo Kikwete amewatuhumu wenzake wamezipata toka kwake. Mfano, tabia ya baadhi ya wakuu wa wilaya kukopa hata pombe kwenye mabaa. Kwani hii ina tofauti gani na tabia ya Kikwete ya kukopa kopa na kutumia hovyo kiasi cha deni la taifa kuongezeka bila ulazima? Rais anayekopakopa huku serikali yake ikisifika kutoa misamaha kwa wezi wakubwa wanaoshirikiana na wakubwa au kuacha mafisadi na majizi wajiibie fedha ya umma kama watakavyo kama kwenye kashfa ya escrow, hakuna tofauti na kule kulikokuwa kukifanywa na wakuu wa wilaya anaowalalamikia Kikwete.  Kikwete anawataka wawe role model (kioo). Je yeye ni kioo pamoja na madudu yote ambayo amekuwa akiyafanya tangu aingie madarakani? Mbona hatukuona uoza huu wakati wa awamu ya kwanza ambapo kuteuliwa kuliendana na sifa kemkem za mhusika tena baada ya kuchunguzwa kwa muda mrefu? Watashindwa nini kulewa wakati nchi inaendeshwa kwa misingi ya kupiga dili badala ya maadili, kujuana, kulipana fadhila na usanii kila aina.
Kuna usemi kuwa jogoo aliwafundisha vifaranga kunya ndani baada ya kumuona akifanya hivyo.  Nadhani wahusika waliweza kufanya madudu waliyofanya kwa kujua kuwa waliowateua hawajali na hawana muda wa kuwashughulikia kutokana na kuwa bize na matanuzi na mambo ya hovyo kama hayo. Bila shaka mkuu wa wilaya anayepoteza muda kwenye mabaa ni wa hovyo kama rais anayetumia muda mwingi kwenye kuzurura akiomba na kukopakopa ughaibuni. Kama tutakuwa wakweli, tangu aingie madarakani, Kikwete ametumia muda mwingi nje kuliko kwenye ofisi yake alikopaswa kuwa akitatua matatizo ya taifa. Tumeona marais wa nchi jirani. Hawazururi kama Kikwete.
 Hata baba nyumbani ukiwa bingwa wa kurudi nyumbani usiku wa manane usitegemee watoto wako warudi mapema wakati wanajua hakuna mtu wa kuwabaini wala kuwaadhibu wanapochelewa kufanya hivyo. Kikwete anaweza kujiridhisha kuwa “amewashushua” wakuu wa wilaya walevi waliokuwa wakitumikia serikali ya kilevi. Kimsingi, alichofanya Kikwete ni kama kujisuata. Heri angejinyamazia kama alivyofanya kwenye kashfa ya EPA na kutaja mali zake.
Kama anenona nuru japo amechelewa kutokana na ukweli kuwa siku zake za kuwa madarakani zinahesabika, basi awawajibishe marafiki zake waliojazana kwenye baraza la mawaziri walevi na wanaolala hata bungeni. Vinginevyo inaweza kujengeka dhana kuwa wakuu wa wilaya walevi wameonewa hasa ikizingatiwa kuwa kwa sasa ulevi uwe wa madaraka, mihadarati na pombe umehalalishwa. Rejea jinsi naibu spika wa Bunge Job Ndugai alivyowahi kudai kuwa kuna wabunge wanaotumia madawa ya kulevya na hakuna aliyempinga wala kutaka atoe ushahidi.  Kikwete amewaumbua wakuu wa wilaya. Mbona amewahifadhi wakuu wa mikoa ambao wapo wengi wanaotia shaka kama mmoja aliyekuwa mkuu wa mkoa wa Arusha ambaye alionyesha wendawazimu wazi wazi na Kikwete wala hakumchukulia hatua? Leo tuna mawaziri wanaosifika kwa kutalii nje na mabinti na hata maanti wakati wizara zao zikifanya madudu na hawawajibishwi. Unategemea nini unapoteau watu kwa vile ni marafiki zako au marafiki na mashoga za mkeo au watu waliofanya kazi chafu ya kuchafua wenzao wakati wa kampeni? Unategemea nini unapoteua wakuu wa wilaya ambao sifa yao kuu ya kuwateua ni kuwafanyia uhuni maadui zako?
Ukipanda mbigiri shurti uvune mbigiri. Hivyo, Kikwete hana haja ya kulalamika wala kuamini kuwa kuna jipya kwenye tuhuma zake kwa wakuu wa wilaya walevi.
Chanzo: Tanzania Daima Machi 25, 2015.

No comments: