The Chant of Savant

Wednesday 16 September 2015

Kijiwe chamshauri Gwaijumaa aanzishe chama

          Baada ya mchunaji, sorry, mchungaji wa kujipachia uaskofu aitwaye Jose Gwaijumaa kuwafunika wanasiasa kwenye siasa, kijiwe kinahoji anafanya hivyo kama nani wakati kayani kwetu kuna utaratibu wa kutenganisha siasa na dini au anahubiri duni?
          Mpemba anaingia akiwa anavuta tasbih yake na kusema, “Wallahi mie nshangaa sana hawa UKAUA. Yaani pamoja na kumuua Pumba na Silaha bado waendelea kujiua kwa kuhubiri udini?”
          Mgosi Machungi anamchomekea Mpemba, “Hebu Ami tieeze vizui tikikueewe. Unamaanisha nini unaposema eti UKAUA wanahubii udini?”
          Mpemba anajibu, “Ami hujamsikia huyu nchunaji Jose Gwaijumaa aiyejipachia uaskofu na upupu anaomwaga ukiachia mbali madai ya ajabu aniyotoa?"
          “Ahaa unaongelea huyu msanii na mshenga wa Luwasa siyo! Nadhani anafaa sana kuvaa gwanda na si joho. Sioni tofauti yake na yule kidhabu wa nambari wani aitwaje Livingjiwe Lushindo. Hata hivyo, sishangai, msimu wa kutafunana, kuhadaana, kuuzana, kuchuuzana na kutapeliana ndiyo huu. Kimsingi, huyu Gwaijumaa alipaswa achunguzwe ukwasi wake kabla ya kujitiatia anajua siasa wakati si cha dini wala siasa ajuacho.” Anajibu Msomi Mkatatamaa.
          “Nadhani huyu msakatonge mnamuonea bure. Mshaambiwa ni mshenga. Sasa mnataka afanye kazi gani zaidi ya upambe. Je mnajua analipwa au ameahidiwa kiasi gani?” anajibu Mijjinga huku akibusu kikombe chake cha kahawa.
          Kapende anaamua kutia timu, “Nyie hamumjui huyu. Huyu ni wale wanaotumia majoho kujitajirisha. Yuko tayari kuingia kitandani na yeyote ilmradi mkono uende kinywani. Hata hivyo, siwalaumu hawa wasanii kutokana na kaya yetu kugeuzwa ya wasanii. Huoni anavyomlaumu Dk Silaha kuwa anatumiwa wakati yeye alianza zamani kutumiwa siyo kutumika?”
          Mipawa hataki aachwe nyuma. Anakwanyua mic, “Dokta Kapende nakuunga mkono na mguu. Usemayo yana maana sana. Tokana na mfumo wa kisanii, sasa hivi tuna hata wauza bwibwi wanaojiita wachungaji hata maaskofu. Ama kweli kaya imeingiliwa na mdudu huyu wa ufisadi na ulafi. Gwaijumaa akitumika basi kila mmoja anaona anatumika kama yeye!”
          Sofia Lion aka Kanungaembe anakwanyua mic, “Japo kaka zangu huwa natofautiana nanyi mara nyingi. Kwa hili mmenipata kweli kweli.”
          Kabla ya kuendelea, Mbwamwitu anamchokea Sofi na kusema, “Hebu tueleze vizuri nasi tukupate. Wamekupataje?”
          Huku akiwa anatabasamu Sofi anajibu, “Usipate tabu hata nawe utanipata tu. Kusema ukweli huyu kidhabu anatia kinyaa kiasi cha hata kuamsha hisia za udini. Tuliwaonya siku nyingi kuwatahadhari hawa wapingaji wa kila kitu. Sasa nadhani mnaanza kutuelewa hatimaye. Hawa ni waharibifu wala hawana lolote.”
          “Da Sofi mie nimekupata japo sivyo unavyotegemea. Yapo mambo nakubaliana nawe na yapo mengine sikubaliani nawe katu. Nadhani kama alivyosema Dk Silaha, kinyesi ni kinyesi hata kiwe chooni au chumbani. Hivyo, kwangu huyu mchunaji wala hanishangazi anachofanya. Hivi kweli kiongozi wa kiroho anaweza kuwa yule? Mmewahi kusikia lugha ya wapiga debe anayotumia? Sijui kwanini asingejiendea shule lau kujipatia elimu kuliko kuendekeza njaa! Hata hivyo, tuwalaumu hawa waliotawala kaya miaka yote kwa kulea uoza kama huu ambapo kila tapeli anawatapeli wachovu. Huyu ametumia vyote siasa na dini.”
          Kanji naye anaamua kula mic, “Mimi sangaa sana ona hii chunaji nasema ongo mingi. Mimi ona kwa TV. Eti sema bibi ya Silaa nakataza yeye siasa. Sasa veve mambo ya tandani ya Silaa sisi nahusu nini dugu yangu Jimaa?”
          Msomi anarejea, “Kuna jambo mnapaswa muelewe. Nadhani jamaa wanamng’ang’ania Dk Silaha ili waepushwe kung’ang’aniwa wao. Ukitaka kuwakwepa mbwa watupia mifupa. Kwa watu wasomi na ambao wako serious kutaka kuchukua kaya, wangejikita kuichapa nambari wani. Pia kwa watu waliopiga shule na kujua mikakati ya kisiasa wasingeruhusu wahuni na majuha kusimama majukwaani na kujadili mambo mazito wasiyo nayo ujuzi. Huyu Gwajumaa ana madhambi mengi ambayo yakiwekwa wazi kama si kukimbia kaya anaweza kuishia lupango kama si kujinyonga. Nadhani wanaojenga hisia za udini hawakosei.”
          Mzee Maneno anakula mic, “Nasikia hata hii chopa wanayoita ya Gwaijumaa kumbe si yake bali ya Luwasa anayemtumia huyu mchunaji. Hata hivyo, nawalaumi nambari wani kwa kutengeneza mazingira ya baadhi ya matapeli kuwaibia wachovu kutumia dini wakitangaza kufanya miujiza wakati miujiza yenyewe ni kuwatoa mshiko na si zaidi. Huyu Gwajumaa anapaswa achunguzwe kama kweli ni askofu, ukwasi wake na kama ana sifa anazodai anazo.”
          “Mzee Maneno maneno yako mazito sana. Nimependa pendekezo lako la kuchunguzwa akili na ukwasi wa mhusika. Kwa mtu kama yeye angefanya kama akina Rugemalayer na Singasinga wa escrow, kunyamaza akiomba Mungu itokee miujiza asinyee debe ingawa hili hawataliepuka siku moja iwe ni hapa duniani au mbinguni,” Kapende anazoza.
          “Yakhe mie nshawaambia tuunde chama vinginevyo twaweza kuwa kitu cha kupokezana baina ya matapeli wa kisiasa.” Mpemba anaonya.
          Mgosi hangoji Ami amalize. Anachomekea, “Nadhani hapa wa kuanzisha chama siyo si bai Gwaijumaa ili ahubii vizui siasa badaaa ya dini.”
          Kijiwe kikiwa kinanoga si likapita shangingi la Gwajumaa. Tulilikimbiza likatuacha. Vinginevyo tulitaka tunkamate na kutia adabu halafu tumvue majoho na kumvisha magwanda.
Chanzo: Tanzania Daima Sept., 16, 2015.

7 comments:

Anonymous said...

Gwajiomo haitaji chama yeye tayari ana-ulaji wake, isipokuwa ukimshirikisha katika kuleta porojo za kinafiki lazima atakuumbua, maaana hivi karibuni tulimkaribisha kijiweni alipopata urabu wacha amuumbue mnafiki mmmoja ambaye alikuwa huko dhehebu kubwa na likamshinda...Sasa hapa kijiwe cha walevi hatumwitaji tena tutamfurumisha kwa madongo ya madigrii akirudia tena kuleta porojo katika mambo makini.Iwapo huyu Silaha ameahamua kuja huku kijiwe cha walevi anatakiwa kuja kujifunza ulevi na matumizi ya ulevi katika kulinda uzalendo na siyo vinginevyo.

Anonymous said...

Silaha na Mishombobuko tupo zetu nchi ya ahadi tunakula bata tena kwa raha zetu za kukosa uzalendo kwa kuchukua mkwanja na kuleta porojo kama Mwenzangu Profisi Mapepe naye kajichukulia chake huyo na kwenda nchi jirani kisizingizio cha utafiti.

Anonymous said...

alamu Mwalimu Mhango,
Inapotokea katika nchi viongozi wa kisiasa wanapofungua hutuba zao kwa kuwaamkia wananchi ASSALAMU ALAYKUM na ASIFIWE BWANA!kana kwamba utadhani wanasisasa hao wamekuwa wanahutubia misikitini au makanisani hali hii haibashiri heri kabisa katika nchi yetu.Kama alivyosema Mwalimu Nyerere msemo wake maarufu amabao sio mapadri wala masheikh au wananchi waliuelewa msemo huo kwamba "Watanzania wana dini lakini serikali haina DINI"na kutoelekwa kwa msemo huo ilibidi akahutubie kule Zanzibar kuwafafanulia mapadri,masheikh na wananchi kuhusu msemo huo.Mwalimu Nyerere aliiona hatari ya udini na ukabila unavyohatarisha usalama wa nchi na wananchi wake,Lakini hadi hii leo hatukuchukulia maanani wala kuhofu hatari hiyo kwa kuzuka wanasiasa mabao wanataka kupata umaarufu rahisi wa kisiasa na kuzingatiwa kama wanasiasa ambao wanaipenda dini yao,hapa Rais mstaafu Mwinyi ni mfano hai katika hili na ni mwanasiasa amabe alikuja na utaratibu huu wa kuwaamkia wananchi katika hutuba zake kwa BISMILLAHI na Assalaamu alaykum.Kwa hiyo msataafu Mwinyi ndio alieukoka moto huu wa wanansiasa kuitumia dini kwa masilahi yao ya kisiasa na kuanzia hapo wakazuka viongozi wa kidini za kiislamu na kikrristo wakaja kwa kasi kubwa sana kujiingiza katika siasa na kuhubiri siasa na dini kwa wakati mmoja na kujiingiza hata serikalini aidha kwa upande mmoja au mwingine na kusahau majukumu yao ya kuwaongoza waumini wao makanisani na misikitini.
Mwalimu Mhango,hivi kweli sisi wafrika hatujajifunza historia ya uovu wa dini hizi mbili katika dunia?Dini hizi mbili hazina historia nzuri kabisa kwa kule zilipoanzika hadi kule walipozipeleka.Je somo la bara la ulaya katika karne ya 15 kuligeukia kanisa na kuliondoa katika maisha ya kisiasa,sayansi na tekinolojia kwetu sisi halina maana yoyote ile?Leo hii wanansiasa wetu wanalala kitanda kimoja na viongozi wa kidini ili wauendeleze ujinga,umasikini na kuwagandisha akili wananchi wao na waumini wao kwa masilahi yao binafsi?
Inaendelea........

Anonymous said...

Naam,Mwalimu Mhango kwa Bara la Ulaya kuliondoa kanisa katika maisha ya kijamii(isipokuwa kiroho tu)kanisa hilo limezigeukia nchi za ulimwengu wa tatu na kutuzamisha katika ujinga wa kumpenda adui yako asipokutendea uadilifu au kukupa haki yako akikunyang'anya utambulisho wako,na ndivyo hivyo hivyo walivyofanya waarabu walioleta dini ya kiisilamu kwa kutuingiza utumwani wa kiwiwili na kiakili na athari zake tunaishi nazo hadi hii leo.
Mwalimu Mhango,wananchi wanapokuwa na umasikini wa kunuka na umasikini huo unasababishwa na wanasiasa wao, wananchi hao wanakuwa hawana badala nyingine isipokuwa kuikimbilia na kuikumbatia DINI.Je umeliona wimbi lisilokupwa la wananchi hao kujaa makanisani na misikitini?je unadhani ni kweli kwamba wanampenda sana Mungu au ni kujipiga tu sindano ya ganzi ili kukumbia ukweli mchungu ambao hawana ufumbuzi nao na kuishi na matumaini ya kuingia peponi au katika ufalme wa Mungu mbiguni?Wakati ule wa utawala wa Mwalimu Nyerere katika miaka ya 60 hadi mwanzoni mwa 80 wakati ule kulikuwepo na ajira za kumwaga kwa wananchi na hususa vijana hatukuliona wimbi hili la wananchi kukimbila makanisani na misikitini waumini waliokuwa wakihudhuria nyumba zao za ibada kwa moyo safi na bila ya unafiki wa kijamii na ni kweli walikuwa wanampenda Mungu wao na kutafuta utulivu wa kiroho ambao hakuwa na msharti yoyote kama tuonavyo hivi leo.
Sasa inapotokea katika karne hii ya 21 muhubiri wa kidini anadai kwamba ana uwezo wa kumtibia mtu kwa kutumia simu tu akiwa ughaibuni na mgojwa huyo akapona na pepo zikatulia je si kutiana ujinga huko?Hivi leo wananchi na wansiasa wetu kila mtu anataka kuombewa kusomewa na kutafuta kinga kwa mapadri na masheikh na kuwalipa kwa vyovyote vile kulingana na kila kundi na uwezo wake wa kiuchumi unategemea nini katika nchi kama hiyo?Vyovyote vile tutakavyoongea kama hali itaendelea hivi tunakoelekea ni kubaya wanasiasa wachache na viongozi wa kidini watazidi kuendelea kutuparamia na kutuona ni mabuzi wao wa kutuchuna tu.Mimi nadhani kwa kiongozi kama Mwalimu Nyerere amezaliwa sehemu sio na wakati sio na ndio mana hatukumuelewa kwa wakati wake na hatutomuelewa baada ya kuondoka kwake.Sasa nawakumbusha tu wanasiasa kwamba nchi ya Tanzania wenye dini sio waisilamu na wakristo tu peke yao kuna wananchi ambao wanaofuata dini za mababu zetu kwa hiyo na wao hawa wawatafutie maamkizi ya kuwaamkia wakiwatubia wananchi.Na ibaki tu Tanzania kwa watanzania wote na zirudi dini na kubaki katika makanisa na misikitini kwani dini ni uhusiano wa mtu binafsi na kile anachokiabudu wengine haituhusu chochote dini yako hiyo.

Ndugu Nkwazi N Mhango said...

Anon karibu tena na asante kwa mchango wako hasa kukemea huu udini uchwara ambao mimi hupenda kuuita uduni. Kimsingi, kinachofanyika kwa sasa ni wanasiasa na wachunaji wanaojiita wachungaji au maaskofu wa kujipachika kama Gwajima kuwaibia wananchi. Ni kweli watanzania wana dini lakini serikali haipaswi kuwa na dini. Wanatumia salamu za kitumwa kana kwamba dini nchini mbili tu yaani ukristo na uislam wakati kuna dini nyingi tu za asili ambazo waliziua kwa ujinga na ulimbukeni wao.
Kimsingi ulichosema ni cha msingi sana kuwa watu wanaingia makanisani na misikitini kwa wingi kukimbia umasikini wakitegemea kupata ima fedha toka ulaya au uarabuni. Umenikumbusha jambo moja kuu kuwa wanasumbuliwa na ganzi na ujinga. Katika kitabu changu ninachotegemea kutoka hivi karibuni kiitwacho SONG OF SHEEP nauliza swali dogo kwa waswahili kuwa ni kwanini mlikutwa kwenye pepo yenu mkaitoa baada ya kuahidiwa pepo za ndotoni wakati wao ndiyo walisema kuwa binadamu wa kwanza alikuwa hapa Afrika? Upuuzi kusema ukweli ni mwingi. Unashangaa kusikia tapeli kama Gwajima au Kakobe, Rwakatare, Gamanywa na wengine wengi kuitwa eti kiongozi wa kiroho wakati wnaongoza katika uroho na kuwatapeli watu maskini na wajinga kwa kuwaahidi miujiza ambao kimsingi si chochote wala lolote bali utapeli mtupu. Hata kama waliaminishwa kuwa Yesu alimfufua mtu, je nani anahitaji hiyo sayansi wakati huu? Nadhani kama Yesu au Muhamad wangekuja leo wakaona internet na midege iendayo kwa kasi haraka na wakaambiwa kuwa hii ni kazi ya Mungu wa waliovitengeneza vitu hivi wangeweza kuacha imani zao na kufuata hizi nyingine. Ni aibu kwa watu wa karne ya 21 kuendeshwa na mawazo ya karne ya kwanza. Maana yake ni kwamba hawafikirii wala hawana uwezo wa kuhoji. Kwangu ndini ni bangi ya kawaida inayolenga kumtisha na kupumbaza mtu ili imnyonye. Hujasikia watu wakifia dini ya mwenyezi Mungu? Kwanini binadamu anayekufa afie dini ya Mungu asiyekufa kama kweli yupo na hafi? Mungu gani anategemea nguvu dhaifu na ya hovyo ya binadamu?

Anonymous said...

Mwalimu Mhango tupo katika jamii iliyokata tamaa na kukosa ubunifu na kutumia njia za mkato kupato vipato. Kimsing bara la afrika nikijumisha Tanzania hiyo ganzi imejishika kweli ya uduni(Udini). Hivi katika karne hii jamii ya kitanzania inachagua dhambi na uvunjaji wa sheria kwa kuleta porojo na upuuzi. Mfano ni jamii hii inayosema ina imani ya kidini ndiyo inayowinda albino kama swala porini, jamii hii ndiyo inayouwa vikongwe, jamii hii ndiyo inayokwenda kwa waganga wa kienyeji ili wafaulu mitihani ya kielemu na maarifa, kupatiwa viza za kwenda kuishi ughaibuni, hata hivi karibuni nimeona Tangazo la dawa ya kuondoa mgao wa umeme kutoka kwa mganga kienyeji, wanasiasa na viongozi wote ni wateja wakubwa wa mtazamo huo huo. Hayo yote yanathibitisha kwa kupoteza mwelekeo wa kimtazamo na maendeleo kwa ujumla katika dunia ya karne hi ya ishirini na amoja katika jamii yetu wanaojazana katika hizo wanazoita nyumba za imani.

Ndugu Nkwazi N Mhango said...

Anon umeniacha hoi, eti dawa ya kuondoa mgao siyo! Sishangai hasa nikizingatia kuwa waganga njaa wa kienyeji na matapeli wa kidini wanavyokuwa matajiri kwa kuwaibia wapumbavu waliokata tamaa. Nchi yetu imegeuka ya usanii kiasi cha wasanii sasa kuanza kuvamia siasa na kuzidi kutajirika. Hebu jiulize. Magazeti ya udaku ya Shigongo yanauza maelfu ya nakala wakati magazeti ya habari yanadoda. Hii maana yake ni kwamba watu wetu walio wengi ni wadaku na wapenzi wa masihara na wasiopenda kuumiza vichwa kutafuta majibu ya matatizo yao. Hata hizi siasa za kitapeli zinareflect hali halisi ya watu wetu japo si wote ingawa ni wengi. Eti kuna dawa za kufanya watu waishi ughaibuni? Basi nadhani waje kwangu niwatibie nitajirike haraka bila kutumia hata akili.