Tanzia, tanzia nakuhofu kwa moyo wote,
Niamkapo nakuhofu wewe,
Nilalapo ni shari yenyewe,
Jina lako ni hofu tupu,
Tanzia, tanzia nakuhofu kwa nguvu zote.
Niendapo kwa majirani,
Huning’ong’a mimi,
Hushangaa ukapuku wangu,
Wakati nina mali kibao,
Hushangaa utaahira wangu,
Niruhusuvyoo majizi kuiba,
Huu si mzuri. Niwaza.
Hizi bangi na gongo vitanisababishia kulala lupango na ku-download kwenye debe! Nina hasira, huzuni, usongo na ngoa.
Baada ya kupata kinywaji na simulizi za `wachovu’ walivyokufa vifo vya kutisha, nimepandwa na Mwenembago. Nabwabwaja.
Sina akili nzuri. Kweli sina akili nzuri. Usiombe mlevi akashuhudia tukio kama lile. Kuna mlevi alisimulia alivyoona miili mamia yasiyohesabika. Akisimulia majonzi ya mkuu na `kidosho’ chake, utacheka hata kama hili si la kuchekesha.
Hamkumuona jamaa akijitia kuwa na huruma kwa kupiga kambi pale wakati kamba tu? Angekuwa sincere, angekwenda zake mapumziko mbugani? Bila shaka ana roho ngumu kwenda ‘kutanua’, wakati `wachovu’ wakiuawa kwa uzembe wa watendaji katika `sirikali’ yake.
How could a sane person go to enjoy while the kifusi had killed people a day before? Jamani, msidhani nawanga. Baada ya kushuhudia balaa la juzi jengo lilipopatwa usingizi na kuanguka, nimejihisi kuchanganyikwa.
Nikilala naota ubavu wangu wa mbwa ukianguka na kunyotoa roho. Nikibadili ndoto naona ghorofa ikinikimbiza iniangukie. Njiani kwenda kwa mama muuza ‘msosi’, kuna kijighorofa cha Mpemba.
Ninakiogopa kuliko ukoma, sorry to speak. Imefikia mahali mtoto akilia ukimwambia: Nitakupeleka maghorofani, ananyamaza haraka.
Tuache utani. Tubadili jina la kaya iwe Tanzia na mji mkuu uitwe Dar- es- Zahama. Sababu? Mosi, kwanini tujidanganye na bandari salama wakati bandarini kwenyewe wizi na udokozi mtupu?
Kwanini kujipa imani kuwa ni kaya ya salama na amani, wakati hakuna hata chembe ya vitu hivi? Hawa wanaokufa kutokana na wakubwa kula rushwa, wakiruhusu ujenzi wa kipuuzi, wana salama na amani?
Hivi jijini Dar -es- Zahama kuna amani? Jiji gani chafu, hovyo, hatari, lisilo na maji, mitaro ya maji machafu, mpangilio na hata maana? Ikinyesha mvua kidogo, linafurika vinyesi, huku watu wakifa kwa kiu ya kukosa maji safi.
Mabomba, badala ya kutoa maji, yanatoa bill. Bado mgao na ulanguzi wa umeme, misongamano barabarani na majumbani. Pamoja na yote haya, bado watu walalamika, badala ya kuchukua hatua!
Hili nalo lahitaji wafadhili wa kuwakomboa? Shame on you! Yaani aibu iwe juu yenu.
Heri kaya iitwe Tanzia. Sababu? Imejaa tanzia. Jumba limeporomoka likanyonga. Kifusi kule Moshono kimenyonga. Trafiki kasimamisha magari manne kwa mpigo, yamegongana.
Kila siku tunapata taarifa za kuuawa mazeruzeru, ndata kuua, waandishi wa umbea kama Absalom Kibanda, matabibu kama Ulimboka wanaotekwa na kuteswa, wakifanyiwa `kitu mbaya’, ufisadi, ubabaishaji, usanii, ufujaji, uzuruaji wa wakubwa na kila upuuzi.
Mara kwa mara meli zilizojazwa kupitia uwezo na zisizokidhi viwango zinaua, madawa `feki’, umasikini wa kujitakia na kila upuuzi vinaua.
Nani anajali? Uwanja wa ndege wanachana mabegi. Sum all of them up. Nini matokeo? Misiba, misiba, misiba…ad infinitum. Wasiojua kilatini, maana yake ni bila ukomo.
Nina usongo na ule `mkampuni’ wa ujenzi wa maghorofa ya mauaji wa Ladha. Hata kama ni mali ya diwani, nitamfanyia `kitu mbaya’ kwa mujibu wa sheria za nchi.
Je, wajua kuwa ghorofa zinazojengwa tulipoanza sera za uholela na uhujumaa na kujimegea, ni mabomu yanayongoja kuua?
Je, wajua: Majengo yote yaliyojengwa baada ya kuhalalisha rushwa, kitu ya kitu kidogo na kitu kikubwa ni balaa kuliko hata tsunami?
Japo naongea kilevi, huo ndio ukweli mtupu? Hii haitokani na huzuni na kukata tama, bali utafiti niliofanya kwa walevi wasomi ninaokamata nao `ulabu’.
Tumegundua kumbe ‘watuwala’ wetu si wa kujifunza. Kuna mlevi aliyetufunga kamba kuwa amewahi kufanya kazi Ikulu.
Akasema eti watu wetu waendapo `majuu’ ima huwa wanatembea usiku au kuupiga kiasi cha kushidwa kujifunza mazuri, kama vile majengo imara na mazuri, madaraja na hata barabara.
Hebu fikiri ni barabara ngapi zinajengwa na kubomoka kabla ya kuzinduliwa. Tumeshindwa hata na jamaa tuliozoea kuwaita `manyang’au’.
Wamejenga Thika hata kama wanachaguana kikabila na `kudedishana’ wakigombea matokeo!
Wao walichinjana kikabila. Wana sababu za `kijinga’ sisi za `kipumbavu’. Ajabu bado tunawacheka wakati wanapaswa kutucheka hasa ikizingatiwa urithi wetu! Tunauzana na kunyongana kifisadi. Mechi droo!
Sina imani na kaya hii hata kwa viboko. Hata huo `mdaraja’ wa Kagamboni sina imani nao.
Kama utasimamiwa kama hii `mighorofa’ ya wachukuaji wa `Kigabacholi’, amini usiamini utaua siku moja.
Wanajali nini iwapo hawataishi huko? Hamkusikia kuwa yule mchukuaji aliyekuwa akijenga ghorofa ‘lililonyonga’, alikamatwa uwanja wa ndege akielekea zake kwao?
Alijua alichofanya. Angekuwa mlevi angekimbia aende wapi? Bado hatujifunzi! Mbona Chavda alitusaidia alipotuibia akikimbilia zake India, hatukujifunza?
Kaya imegeuka kama choo! Kila mtu ana-download `saizi’ yake kwa `staili’ yake. Hata chooni kuna nafuu maana kuna ustaarabu wake na si kama kaya hii inayochezewa na kila kibaka.
Ili walevi waishi kwa amani na salama maghorofani, napendekeza: Nichagueni kuwa kiongozi wenu muone.
Nitahakikisha hakuna anayejenga nyumba bila kueleza alivyopata fedha zake. Japo ni mlevi, nina mawazo ya maana. Nitabomoa nyumba hata miji yote iliyojengwa kiholela.
Nitawafunga wote walioshiriki kwa njia yoyote katika uwepo wa majengo na miji isiyo na mpangilio wala usalama.
Nitapiga marufuku NHC kuuza viwanja vya umma kifisadi kama ilivyokuwa kwenye uchafu huu. Hata kama hawakiri, `mghorofa’ ulioua ni `dili’ lenye kila harufu ya ufisadi.
Nitapeleka muswada bungeni wa sheria ya kunyonga na kufilisi wanaojenga nyumba za mauaji.
Nitaikalia kooni Karikoo iache kuendelea kutukalia kooni na kuua walevi wetu. Pia nita-post maangamizi yangu ya kisheria Posta ili nako kuwe salama.
Hata ile minara miwili ya Band of Thieves (BoT) inayoajiri watoto wa `vigogo’ nitaangusha ijengwe upya maana siielewi elewi.
Nitapiga vita wepesi wa kuwahi kwenye misiba badala ya kuwahi kutafuta majibu ya matatizo yetu. Nitapitia upya vibali vyote vya ujenzi.
Saleh as Sagaf na Shed Mijinga take care.
Chanzo: Nipashe Jumamosi Aprili 6, 2013.
No comments:
Post a Comment