Saturday, 20 April 2013

Nilialikwa kuapishwa Uhuru Kenyatta

Naona yule anacheka akidhani ni kamba. Soma ujue ilikuwaje. Kuarikwa Kenya unastuka ingekuwa kwa Obama si ungekata roho! Kenya ukiuliza imekuwaje, wanajibu ishakua. Seriously, nilialikwa na kushiriki kuapishwa rais wa mpya ambaye si mpya wa Kenya Uhuru Kenyatta.
Wengi hawajui uhusiano wangu na Kenyatta wala Moi Kibaki. Hiyo siri yangu na personal issue.
Wengi walishangaa kusikia nikitambulishwa kabla ya marais waliohudhuria. MC, kwa manjonjo, alisema, “Namleta kwenu rais asiyetambulika na kukubalika wa walevi wote duniani mstahiki mtukufu Nkwazi Mhango. Wengi walipigwa na kihoro wasijue nami ni rais tena ninayejulikana.
Ghafla Kenyatta alinitania akisema, “Wali ku mutongolya wa njohi, yaani ulikuwa wapi kiongozi wa pombe?” Bila kujivunga nilimjibu, “Lehe kanjohi ka uthamaki wa forori ya Muratina na Mwomboko.”
Nilimtania kuwa urais umevuka tena mto Chania na kurejea Kiambuu toka Nyeri. Alicheka sana na kushangaa ninavyojua utani wao wa asili baina ya watu wa Kiambuu, Kiambaa, Gatundu na hata Kangema na wa Nyeri, Othaya, Tetu, Githakwa na Ithekahuno.
Muda ulikuwa hautoshi. Aliniomba niwe mshauri wake mkuu kuhusiana na kilevi. Sikukubali wala kukataa. Nilimwambia kuwa nitafikiria. Siwezi kukueleza yote tuliyoongea.
Maana mambo mengine ni yetu wakubwa si makapuku wala walevi wa kawaida kama wewe msomaji wangu.
Tulicheka sana na kukumbatiana kwa furaha hasa baada ya kutoonana kwa muda mrefu. Mara ya kwanza tulionana nchini kwa Joji Kichaka akisoma wakati ule nikiwa visiting professor wa falsafa. Nilimsaidia sana huyu dogo kiasi kwamba hawezi kunisahau. Mara ya mwisho tulionana mitaa ya Muthangari na Gigiri tulipokuwa tukipata kanywaji pamoja na washirika zetu wengine ambao nisingependa niwataje hapa. Dogo alishangaa kufahamu kuwa nafahamiana na jaji mkuu aliyemwapisha Dk. Willy Mutunga. Hayo tuyaache.
Hakuna kilichonivutia kama ahadi ya Uhuru Kenyatta ya kulinda raslimali, mazingira na maslahi ya Kenya. Dogo alisema bila kumung’unya kuwa atahakikisha analinda raslimali za Kenya na mazingira kwa ajili ya vizazi vijavyo
Pia aliahidi pesa yote itakayopatikana toka kwenye raslimali husika itatumiwa kwa adabu na nidhamu
Maneno ya Kenyatta yaliniacha na maumivu sana kuona Tanzanite inavyoibiwa huku wachukuaji wakija na kuchimba madini na kujiondokea na mifweza huku wakituachia mishimo na mabalaa ya kimazingira. Hivi nani alituroga yarabi?
Hakuna aliponiacha hoi kama pale aliposema kuwa atahakikisha uhusiano na majirani zake hasa Bongolalaland unadumu ili aweze kujipatia ardhi aongezee kwenye ile aliyo nayo ambayo ina ukubwa sawa na mkoa wa Arusha. Pia alisema atahakikisha anaunganisha Kenya na nchi jirani ili kuwawezesha watu wake wasio na ardhi waende kule na kujitwalia ardhi madini na raslimali kutokana na wajinga fulani kuchezea vitu hivi.
Kwa tunaomjua alikuwa akirusha kijembe kwa majuha wanaochezea raslimali na uchumi wa mataifa yao. Aliporusha hili dongo nilimuona jamaa yangu mmoja toka Bongo ambaye kwa leo simtaji akikenua meno wakati roho ikimuuma. Nilijisemea moyoni kuwa kumbe kimwana cia Kamau wa Ngengi ni noma!
Baada ya kuongea na Uhuru nilikwenda kuongea na mzee Daniel arap Mwai ambaye alifurahi sana na kuniambia kwa Kiswahili chake kibovu, “My friend ukuje tubulahi pamoja my project has won at last.” Baada ya kukumbatiana na kuamkuana na mzee Nyayo niliamua kumuasa amwambie dogo abadili baadhi ya ahadi zake.
Kwa mfano aliahidi kutoa laptop kwa kila mwanafunzi wa shule ya msingi bila kujua kuwa Kenya yote haina umeme na kwamba watoto wa maskwata hawana chakula wala viatu.
Hivyo laptops alizoahidi wangeziuza kwa watoto wa mafisadi kwenda kununua unga. Tulikubaliana na kuagana ndipo nikajikunja kwenye laptop yangu kumwandikia email agwambo Raila Odinga ambaye alikuwa Sauzi kumjulia hali Mandela na kuepuka kukirihishwa kushuhudia ulaji wake akipewa mtu mwingine.
Alinijibu haraka kuwa kwake Mandela was better than anything except God alone. Nilimpa pole ya kuzidiwa kete kwenye kile alichoona ni uchakachuaji na uchafuzi wa uchaguzi. Anyways, siasa wakati mwingine ni mchezo mchafu.
Hakuna mtu alitia aibu na kuchefua watu kama jamaa yangu M7 aliyechemsha kwa kuishambulia ICC akidhani anamsaidia dogo. Alijigamba kuwa anachukua ufisadi wakati ndicho chakula na hewa yake. Nilitaka niamke nimzabe mabao ila niliacha kwa vile bodigadi wake wakijitia kujua nkawaumiza.
Mna habari kuwa nilitambulishwa kwa habithi wa Sudan anayejiita mwarabu wakati ni mmakonde tena mwenye machale nikakataa? Mie sio kama wajinga wanjinga wanaoendekeza nakuchekacheka na kushikana mikono na maadui na kila habithi kwa vile nao wameficha uhabithi wao.
Wajua kuwa baada ya sherehe ya kuapa nilifanya kitu ambacho kililetea kaya yangu heshima kubwa? Ilikuwa ni pale makamu wa Kenyatta alipopotosha historian a ukweli kusema eti mabaki ya mtu wa kwanza yaligunduliwa Kenya wakati ni Bongo tena Odivai Gorge. Niliudhika nusu ya kunasa mtu mabao hadi Kenyatta akashangaa.
Hata hivyo Rutuo aliniandikia SMS akiniomba msamaha kwa vile alisema kuwa alikuwa amehemkwa nilimsamehe na kuelekeza hasira zangu kwa majuha walioshindwa kuitetea Bongolalaland yangu. Nilishangaa kuona ujumbe wa Bongolalaland ukikenua macho badala ya kudai afute kauli yake maana hii ilikuwa ni kutuibia haki yetu ukiachia mbali kutudhalilisha.
Hii imenikumbusha kisa ambapo mzee Mchonga alitaka kufungulia jeshi baada ya hawa jamaa kudai mlima Kilimanjaro uko kwao. Baada ya hapo wanadai karibu kila kitu kuanzia Kiswahili, Serengeti hata Tanzanite viko kwao huku jamaa zangu wanaopaswa kuwatolea uvivu wakichekelea kama vile hawana akili! Hayo tuyaache.
Baada ya kumaliza shughuli nilianza kuwaza mantiki ya kumzawadia Moi Kibaki jumba la mabilioni ya shilingi na mshahara na marupurupu bila kufanya kazi ni nini kama si wizi wa siasa za kijambazi za Kiswahili za kuwaibia makapuku.
Jitu lina mijumba kama serikali halafu linaongezwa mengine wakati wananchi wakilala njaa! Nilijionea huruma. Nikistaafu urais wa walevi nitapewa michupa ya gongo na misokoto ya bangi. Kweli wanajua kututenda!
By the way, if I attended the inauguration or not, if I was invited or not and if what I’ve said is true or not what’s it to do with you? Think twice. Again, I’m just kidding. Tafsiri nyepesi:Kama nilihudhuria kuapishwa huko au la, kama nilialikwa au la na ni vipi kama nilichosema ni kweli au siyo, inakuhusu? Fikiria mara mbili. Ninatania
Walevi wa Roundabout shule ya Uhuru mpo! Smile!
Chanzo: Nipashe Jumamosi Aprili 20, 2013.

No comments: