Sunday, 14 April 2013

Eti anatafuta mchinjaji wa kitimoto!


Kuna watu wachokozi na wabishi duniani sina mfano! Hayo hapo juu si maneno yangu bali mlevi mmoja anayejiita mwana falsafa wa kizazi hiki. Bwana huyu, licha ya kuwa mlevi, huibua hoja zenye kufikirisha hata wakati mwingine kukera. Naamua kuwasilisha ‘vitu vyake’ kama vilivyo---bila kuyachuja wala kuchakachua. Sina tabia ya kuzuia watu kufikiri hata kama wanavyofikiri vinaweza kuwa kero. Hata hivyo, ukitaka kuepuka kero duniani, jifanye kama haupo wala huna thamani kuliko wengine. Ukijitia kimbelembele cha kujiona ni bora na sahihi kuliko wengine, hao wengine watakuudhi utamani kujinyotoa roho. Mie humo simo wala sitakuwamo. Mie si fala hivyo ati!
Kwanza, niseme mapema ili tusijelaumiana bila sababu ya msingi. Sina dini zaidi ya ulabu. Seriously, wakati wengine wakiapa kwa misahafu yao mie naapa na chupa ya gongo na msokoto wa ganja. Kwani dini ni nini zaidi ya imani? Hakuna imani inayoweza kushinda imani nyingine kama tutaondoa mawenge na makengeza. Hakuna imani inayoweza kukuonyesha kitu kwa uhalisia wake zaidi ya kutumia mifano na hadithi, ngano visa na heakaya. Hayo tuyaache.  Naheshimu dini zote kwa sharti kwamba ziheshimu dini yangu. Kama dini yako inapiga vita ulabu ujue unavunja na kupinga sheria za walevi.
Juzi kwenye kikao chetu tukikamata kanywaji ilitokea mpya. Baada ya mlevi mmoja kusikia habari za ugomvi juu ya nani achinje au kutochinja, alikuja na mpya. Alidai eti ana nguruwe wake na angependa yeyote mwenye kuruhusiwa kuchinja akamchijie ili kuepuka kuingia mtafaruko. Wakati jamaa akisema haya kulikuwa kumetokea mapambano na minyukano huko Mwanza na Tunduma wakigombea kuchinja.  Hii ilitokea wakati tukishangaa: Inakuwaje watu wagombee vitu vidogo na vya kibinafsi hivi kana kwamba hawana vitu vya maana vya kufanya?
Baada ya mlevi kuja na hoja yake, nilimpa laivu kuwa sina ugomvi na hilo. Akichinja mchinjaji au asiyemchinjaji mie natwanga tu. Mie hata ukitwanga nyundo au kunyonga naramba tu. Kwani tumboni kuna sheria zaidi ya njaa? Ukila haramu halali kibudu au whatever mwisho wa yote unaishia kudownload chooni. Ingekuwa amri yangu kuna vyakula hasa aina ya samaki ningeharamisha. Maana kuna mifish ina sura mbaya sina mfano. Mingine inanuka sina mfano! Anyways hayo tuyaache.
Pia nilimuonya mlevi kuwa atajiingiza kwenye mzozo na mjadala wa kipuuzi wa nani achinje na nani asichinje. Msimamo wangu simpo. Kama mzee Ruksa, kula kitu roho inataka ilmradi kisinitapishe wala kuniletea madhara. Kwangu, ugomvi ungekuwa kwenye uhalali na uharamu wa nani kafuga lakini si nani achinje ingeniingia akilini hata kama nafikiri kilevi.
Sasa nisaidie nimsaidie mlevi mwenzangu.  Anasema alipewa zawadi ya kitomoto na wakwe zake na ana usongo na kitu ile. Anasema,hachagui dini bali usongo wake ni kutaka kutafuna kitu ile. Je amuite nani amchinjie kitu hii? Maana, sisi walevi hatutaki shari na yeyote.  We are the bin-Adams of peace and only peace. So whenever you read this, please take seriously and sincerely. Lo! Ulabu nao! Yaani sijavuta bangi zangu naongea kikameruni hivi. Je nikishaliweka itakuwa mbwai? Forgive me for my ukameruni.
Tuache utani. Kumbe kila kitu duniani ni darasa. Kabla ya mlevi kuja na wazo la kutafuta mchinjaji wa kitimoto yake sikuwa nimeangalia utata huu. Naona utata ambao unahitaji wana falsafa kama mimi kuutatua.  Naona hatari mbele ya safari. Kuna siku watataokea watu kutupangia nini tule, tupike, tunywe hata wapi tutembelee na kutembea kwa staili ipi. Hivyo, kwa sisi walevi kuona hatari hii, tunaamua kutoa mapwenti na mawazo ya kuwasaidia wachovu waepuke kuingia mkenge huu. Nadhani tangu tuliponyaka Uhuru wetu wa hovyo, tulikubaliana kuwa kila mtu ana uhuru wa kufanya atakavyo ilmradi asivunje sheria.
Juzi nilisoma sehemu kuwa katika kaya hii hakuna sheria inayomzuia au kumruhusu mtu kuchinja. Kila mmoja anaweza kuchinja ilmradi asimchinje binadamu mwenzake kama wale washenzi wanaochinja na kuua mazeruzeru. Nakubaliana na busara hii ikizingatiwa kuwa kuchinja si kazi sawa na kufuga au kununua hicho kichinjwacho. Haiingii akilini nifuge au kununua mnyama wangu halafu mtu baki eti anipangie jinsi ya kumchinja. Huu ni ukoloni tena ubeberu so to speak. Kama dini, ni suala la mtu binafsi ati.
Hebu niwamegee kidogo mjadala wa kuchinja ulivyokuwa. Alikuja mlevi mmoja aitwaye Shebby Machungi. Huyu bwana anasifika kwa kupenda sana nyama. Machungi ni mwenyeji wa Mashindei, Lushoto. Yeye huiita Ushoto. Kwanza, alipokuja alikuwa na mpango wa kunifundisha ngoma za kwao ili nikiwa narejea kutoka kupiga ulabu nijiimbie. Badala ya kuendelea na kufundishana ngoma alileta wazo la kimasaburi la kugombea kuchinja.
Siku moja kabla tulikuwa tukiongolea ngoma ya Kidembwa na mdumange ambazo nilitokea kuzizimia. Hii ilitokea baada ya kumsimulia safari yangu ‘nchini’ mwake ambapo nilitembelea maeneo kama Nyasa, Kwembago, Shashui, Magira, Mbelei,Kwesime, Baga,Mgwashi,Kongoi, Bumbui, Mazumbai, Malimbwi, Kwemakame, Kwekanga, Kwai (msichanganye na River Kwai kule Uthailandini), Kwenkwazi, Kwenkuzi, Lukozi, Kongei, Kizelui, Kweshashi, Kwenesaa na Kwemachungi, Kwemlazi,Kwemtonto, Kwezumi,Kwemdoe, Kishewa,Kwemtonga, Kwekitui, Makanka.  Ukiondoa KweNkwazi na KweNkuzi yaliyobaki majina ya ajabu ajabu kama dawa za kienyeji!
Kilichomuua Machungi ni kugundua kuwa nayanyaka majina yote hapo juu kichwani tu bila kusoma popote. Alishangaa kipaji hiki. Nilimwambia kuwa hayo ni madogo. Maana ninajua karibu majina ya nusu ya miji yote duniani bila kutazama kwenye kitabu. Hayo tuyaache.
Kuhusu nani achinje, kesho utasikia ndugu zangu akina njomba nao wakiuliza nani anaruhusiwa kunchinja chamaki nchanga. Nashukuru: Kule kwa akina Mwauka bwanji na muli bwanji hakuna kamchezo haka ka kugombea kuchinja. Maana wanavyochinja mbewa na kugombea mbewa zanga ingekuwa noma kama siyo so. Kwa wasiojua nimaanishacho ni kwamba ukivuka mpaka wa Kasumulu pale Mbeya ukaingia nchi ya Maravi usishangae kuona panya wamebanikwa na kutembezwa mitaani kama pweza na ngisi. Kwa ufupi ni kwamba hawa jamaa wakiamua kugombea kuchinja, sijui nani atakuwa tayari kuwachinja hawa jamaa wapenda karanga? It is indeed a challenge and wakeup call that not all that grimmer are diamond. Wakati mwingine tunaweza kugombea vitu tusivyojua au tukivijua vikazuka ambavyo hatukutegemea.
Du yule manzi ana masaburi makubwa hayo! Sijui huyu naye anapaswa kuchinja. Sorry, nilipotea mawazo kiasi cha kubwabwaja. Hi kwa walevi wasomaji wangu wote popote mlipo.
Khalas kweisi.
Chanzo: Nipashe Jumamosi April 13.2013.

No comments: