Friday, 26 April 2013

Tunaadhimisha siku ya kuzaliwa Muungano au Mgongano?


Imetimu miaka 49 tangu mataifa ya Tanganyika na Zanzibar kuungana na kuzaa Tanzania. Hakika miaka 49 si haba. Je tunasherehekea Muungano au Mgongano? Je watanzania bado wana hamu na hamasa na Muungano? Je nani anafaidi Muungano ukiondoa watawala wa pande zote mbili? Maana ukisikia manung'uniko toka pande zote unashangaa mantiki ya kuendelea na kuwa na Muungano wenye kila aina ya migongano miongoni mwa wananchi wa pande mbili. Ilifikia mahali watu wa visiwani wakahisi kama watu wa bara wanawanyonya ingawa hawana cha kunyonya. Ilifikia mahali tukaanza kuitana majina ya machogo na upuuzi mwingine hata kusingiziana jinai.Kwa vile watanzania wanaanza kujitambua, kuna haja ya kuwasihi wauangalie upya Muungano ambao umegeuka kero. Blog hii ni shabiki wa umoja wa Afrika. Tofauti ni kwamba Umoja huu ujengwe na waafrika wenyewe badala ya watawala. Huwa nashangaa kuona Tanzania inavyopoteza muda na raslimali kujiingiza kwenye Jumuia ya Afrika Mashariki wakati huo huo ikishindwa kutatua kero za Muungano wake. Je watanzania tutaendelea kufanyiwa majaribio hadi lini? Wakati tukitafakari hali ya Muungano wetu, majibu tutakayopata yatusaidie kupinga kuingia kichwa kichwa kwenye Jumuia hasara ya Afrika Mashariki ambayo inatumiwa na nchi wanachama kutaka kutuibia ardhi na raslimali zetu. Haiingii akilini kwa nchi yenye ardhi nzuri na kubwa na raslimali kuungana na vijiinchi visivyo na lolote bali mzigo wa ongozeko la watu na watu wasio na ardhi.
KILA LA HERI NA TAFAKARINI.

7 comments:

mtwangio said...

Kwa maoni yangu nami nakubaliana kabisa nawe kwamba uliposema"tofauti ni kwamba umoja huu ujengwe na waafrika wenyewe badala ya watawala"
Nadhani utakubaliana na mimi kwamba muungano wa Tanganyika na Zanzibar ni matokeo ya Cold War na bila muungano huo nadhani Zanzibar pengekua aidha satellite ya nguvu ya kambi ya mashariki au kukosa utulivu wa mapinduzi kutokana kwa waliopinduliwa.
Kwa maana hiyo basi viongozi waliona haja ya kulinda mapinduzi na kuondoa kero la joto la Cold War.kwa maana hiyo hatukushauriwa wananchi wa pande zote mbili kutoa maamuzi yetu kuhusu muungano huo.kwa hiyo viongozi wetu ni sawa na baba ambaye wanaangalia masilahi na kulinda afya na usalama wa watoto wao.Sasa wakati umeshafika kwamba sababu zote za kuwepo kwa muungano huo haupo tena,kama watoto wameshakuwa na wanjua wenyewe masilahi yao na kama Cold War imeshakwisha sasa kuna sababu gani nyingine ya kimsingi ya kuwepo kwa muungano huo?

mtwangio said...

Wazanzibar wamekuwa wakipiga sana makelele ya kuonewa kudhulumiwa na hata kunyonywa kama ulivyagusia pia naam nami naona hivyo ukianagalia jinsi gani kero za muungano huo ulivyo au unavyoendesha hili halina shaka kabisa!Na wana haki ya kupiga makelele hayo lakini cha ajabu na kushangaza wananchi wa tanganyika hawasiriki kikamilifu katika kuungalia muungano huo kwa kujiuliza kama tanganyika inafaidika nini na muungano huo,mimi kama mtanganyika sioni faida yoyote ambayo Tanganyika au watanganyika wanafaidika na muungano huo na kama kuna faida hiyo kwa tanganyika na watanganyika ningeomba niwekewe ubaoni.Wakati mchunganji Mtikila alipokuja kuwatikisa watanganyika na wazanzibari kuhusu muungano viongozi wa pande mbili zote walimuona kama ni nuksi na nahatarisha usalama wa muungano huo na wakamzima!

Kwa hiyo wakati umeshafika wa kuvunjwa kwa muungano huo na kuungana tena basi tuungani kwa ridhaa ya wananchi wa pande zote mbili baada ya kuangalia masilahi ya nchi zote mbili na wananchi wake.

Mimi siungi mkono hoja ya tuungoleee kero za muungano mimi ni katika wale watanganyika ambao wanasema muungano uvunjwe na hauna faida hata kidogo na Tanganyika na wananchi wake na kila nchi ingalie masilahi yake na ya wananch wake na hata kama kutakuwa na fikra ya kuungana tena bado naona wakati huo haujafika bado,na hapa ndipo napotaka kuungana mkono nawe kuhusu hili shirikisho la Afrika Mashariki je kwa nini viongozi wetu hawaipendelei kheri nchi ya Tanganyika na wananchi wake kama alivyokua Baba wa taifa hilo Mwalimi Nyerere amabye eti hii leo kuna kampeni za kila aina Tanganyika na Zanzibar za kuwa eti yeye ndie aliyesababisha mabalaa yote ya nchi yetu?!!!!

mtwangio said...

Wananchi wa Tanganyika bado tumelala kama ulivyoliweka jina mahala pake "Bongolalaland"na kulala hko ni kutojua thamani ya ardhi na kutojua thamani ya ardhi kwamba historia ni ardhi bila ya ardhi tusiandika historia,vita ni ardhi bila ya ardhi kusingekuwa na vita haslan!

Baba wa taifa la Tanganyika alilitambua jambo hilo na ndiyo maana aliilinda ardhi ya Tanganyika na utajiri wake kutokuwa mikononi mwa watu wachache au watu wachache wajilimbikizie ardhi kwa kadri wanavyotaka wao kulingana na uwezo wao wa kiuchumi.Na kama hali itaendelea kama ilivyo hivi sasa kuanzia awamu ya pili ya utawala mpaka tukiyokuwa nayo leo basi tahadhari ni kwamba itafika wakati Mtanganyika atakuwa mtumwa katika nchi yake mwenyewe.Kwani na tuangalie nchi zote za jirani ambazo tulioungana nao katika shirikisho la Afrika mashariki amabao kuanzia mwananchi wa kawaida mpaka waliokuwepo sereikalini wanavyojua thamani ya ardhi na wakati wao chi zao wameshamaliza ardhi kwa siasa ya ubebari kwa kumilikiwa kwa ardhi na watu wachache je kwao wao hiyo si nafasi ambayo tunawakabidhi katika sahani ya dhahabu kuchukua sehemu kubwa ya ardhi ya wananchi waliolala na masikini wa Tanganyika?!!!!

NN Mhango said...

Kweli wewe ni Mtwangio. Maana unavyotwanga wala sina la kuongeza. Nakubaliana nawe kuwa Wadanganyika aka Bongolalalanders wamelala. Hakuna uliponiacha hoi kama ulivyo-coin joto la Cold War yaani joto la vita baridi. Kwa vile wadanganyika tumeanza kuamka nadhani kitaeleweka. Nakushukuru sana kwa mchango wako na fursa na wasaa uliotumia kukoleza jungu. Kila la heri na karibu tena uzidi kupitia uga huu ambao kimsingi ni wenu na si wangu.

mtwangio said...

Ilitokea tu nilipokuwa najaribu kuielezea hali halisi ya nchi yetu,hofu zangu na kukatishwa tamaa kwangu na viongozi wetu kwa watanzania wenzangu ndipo mmoja wao akanitabahisha kuhusu hii Blog yako tukufu akisema kwamba "kama watanzania wa kawaida wangekuwa na access ya internet na wakawa wanamsoma Mhango basi watanzania tusingeweza kulala tena kama tulivyo lala sasa hivi.Na hapo ndipo nilipoanza kuisoma Blog yako hii tukufu,ukweli vyovyote vile nitakavyokupongeza kwa ushujaa wako,kazi yako na kuipendada nchi yako na bara lako siwezi kupata neno hasa linalolingana na sifa za hapo nyuma.Nililoliona wakati nasoma topics nyingi ambazo ni muhimu sana na sensitive sana kwa nchi yako hasa na nchi jiranani kwa ujumla,nimehuzunishwa sana kwa kukosa kusoma maoni mabali mbali ya wananchi hususa watanzania ambao unatufungua macho na kutupigia makelele kila siku tujue wapi tulipotoka,wapi tulipo na wapi tunapoelekea lakini sijaona ushirikianaji wa kutosha kutokan na majuhudi yako yote haya,lakini ni imani yangu na kama ninavyoaamini kwamba kupayuka kwa maandishi ni bora zaidi kuliko kupayuka kwa sauti kwani maandishi yanabaki daima kwa faida ya kizazi hiki ambacho bado kinasuasua kuchukua maamuzi busara ya kuwang'oa viongozi wetu hawa ambao wala hawastahiki kuitwa viongozi na yatabaki kama ufunuo na mwongozo kwa kizazi kijacho.Bwana Mola akulinde,akupe afya njema na kukupa ilhamu zaidi ya kuendelea na huu unabii.Ningependa tu unielimisha jinsi gani ya kuvinunua vitabu vyako,baki salama na kila la kheri

Jaribu said...

Mhango, nafurahi kuona wanaongezeka watoa maoni.

NN Mhango said...

Mtwangio na Jaribu nami sina jinsi ya kuwashukuru,.Siku zote yangu imekuwa ni sauti ya mtu aliyeko nyikani. Huwa naamini kuwa kuna siku nitasikika na wenye kujua unabii wataitikia na kuamini kuwa saa ya ukombozi imetimia. Hakina Mtwangio kati ya vitabu hivyo kimoja ndicho kimechapishwa cha SAA YA UKOMBOZI kama uko Dar nadhani unaweza kuulizia kwenye maduka ya vitabu pale. Kwa Arusha unaweza kuvipata Kasa bookshop. Yote natoa maelekezo sina uhakika kwa vile tangu kitoke sijakanyaga huko. Nimeajaribu kuwasiliana na wachapishaji hapo nyumbani lakini wengi wameonyesha ima kuwa woga na wababaishaji. Inasikitisha kuona kuwa Uganda na Kenya wanazalisha kazi nyingi za kisanii tena kwa kiswahili wakati Tanzania wauzaji na wachapishaji wanakufa kwa kukosa soko. Nchi yetu imegeuka makao makuu ya ujinga na ufisadi duniani. Uzuri wake unaanza kumezwa na ubaya utokanao na jinai ya roho mbaya uchoyo ufisadi na ufisi vilivyotamalaki kila mahali, Napata simulizi za kutisha kiasi cha kuogopa hata kuja kutembea. Kila mtu anafikiri amlize nani ili kieleweke. Naona niishie hapa kwa leo.