The Chant of Savant

Tuesday 2 April 2013



LEO nakuandikia rafiki yangu Absalom Kibanda ambaye ulitolewa kafara siku za hivi karibuni. Yesu angekuwapo leo angekula Pasaka nawe.
Kwani umebebeshwa mzigo wa dhambi za taaluma yetu. Ni bahati mbaya kuwa waliokusulubu ni wale wale kina Yuda na walinzi wa Kaisari na Herode mwenyewe.
Nawashitaki wenye mamlaka kwa kuyatumia vibaya kuzima na kuumiza sauti ya umma. Je, wanadhani tumesahau udhalimu wao? Katu hatujasahau. Hatujasahau mateso na unyama aliofanyiwa Dk. Steven Ulimboka wala kifo cha kinyama cha Daudi Mwangosi. Katu hatutasahau wala kusamehe ushenzi na unyama huu.
Watesi wako wanajulikana kwa sura na hata sauti na vyeo. Unawajua tunawajua. Hukumsikia Dk. Ulimboka akiwataja Usalama wa Taifa wakati ni Uhasama wa Taifa kama si Zahama ya Taifa? Hukusikia akisema kuwa wapo waliokuwa wametokea kukuu na hakuna aliyekanushwa wala kushughulikia tuhuma hizi?
Taifa gani liko salama wakati watu wanateswa hata kuuawa kinyama kila uchao? Usalama huu ni wa nani? Mungu awalaani.
Rafiki yangu Kibanda, ujumbe huu ni wako. Najua unaugulia kwa maumivu na mateso kwenye kitanda hospitalini ughaibuni. Namshukuru Mungu siandiki tanzia yako bali dokezo.
Najua unanisoma kwa taabu. Hata hivyo, nasema: Usilie rafiki yangu. Usijililie bali lilia nchi yako. Usijililie ndugu yangu. Mungu si Nkwazi. Nina hakika atawalipa watesi wako kwa kadiri ya stahiki yao.
Wajua ndugu yangu? Hawa kwa Kireno huitwa Puta, yaani wanaume ambao si riziki na woga. Wangekuwa wanaume kweli wangekuvamia usiku wakijificha nyuma ya giza? Wasen--- wakubwa hao. Wanatumiwa kama nepi na mabwana zao wanaowalipa kutekeleza kazi chafu.
Wangekuwa wanaume kweli wangekukabili mchana kila mtu akiona. Hata wanaowatuma ni hao hao watoto si riziki. Wanaume gani wanaweza kufanya mambo ya kipuuzi na kinyama tena kwa watu wasio na hatia hivi?
Rafiki yangu Kibanda, nakupa wosia wangu. Naomba uushike wosia huu. Usidanganywe na machozi ya mamba na maneno matamu. Usileweshwe na laghba na hadaa za wanafiki waliojihimu kuja Afrika Kusini kukusanifu wakijidai wanakujulia hali.
Hao ni wanafiki. Ni fisi kwenye ngozi ya kondoo. Dharau, tabasamu na maneno yao ya upole hata viapo kuwa watawasaka waliokufanyia unyama na ushenzi, lao ni moja. Usidanganywe na sentensi kama pole sana-bwana-Kibanda na nyimbo nyingine za sifa.
Laiti ningekuwa wewe hata nisingewaruhusu kuingia chumbani kwangu. Kwani huwajui wachawi na wanafiki? Wauapo au kudhuru huangusha kilio kuliko hata wafiwa.
Hizo ndizo alama zao. Watajifanya wanakujulia hali na kukuombea upone haraka. Haya ni maneno midomoni. Mioyoni wanajilaumu kwanini hukufa. Kwani hilo ndilo lilikuwa lengo lao kwako. Hiyo ndiyo mbinu yao chafu ya kupambana na wakosoaji.
Rafiki yangu Kibanda, usilie bali omba Mungu kibao kiwageukie siku moja wajikute wakilipa mara mia ya maovu waliyokutenda.
Wanaweza kutuhadaa hata sisi lakini hawatamuhadaa Mungu. Ipo siku atawaumbua tena hapa hapa duniani. Hata hivyo, nyoyo zao zinawasonga. Hawana raha duniani hata wakionesha nyuso za furaha.
Ndugu yangu Kibanda, nasema usililie jicho lako uliloibiwa. Ililie nchi yetu iliyokumbwa na uharamia na unyama. Ililie nchi inayoficha wahalifu na kuwazawadia. Ililie nchi inayopenda uchafu ikachukia usafi. Usililie jicho lako. Kwani huo ni mchango wako wa aina yake kwa taifa lako.
Usilie rafiki yangu. Omba Mungu akulipie. Omba Mungu akulipe na kukufariji. Hujafa hujaumbika. Hata waliokutendea huo unyama hawajui mwisho wao. Badala ya kulia omba. Omba tupate mwanga na ukombozi. Omba umma ujitambue na kukataa huu utwana na ushenzi wa mchana kweupe.
Omba umma uwawajibishe wasiowajibika. Omba umma usimame na kupinga huu ushenzi, ufisadi na unyang’au unaotendwa na wenye mamlaka.
Ndugu yangu Kibanda usilie, lilia taaluma yako. Lia na kuomboleza ukisikia mwandishi mwingine ameuawa, kununuliwa, kunyamazishwa, kutumiwa, kujikomba hata kujituma kuwatumikia waovu na mafisadi. Lilia wasio na sauti wala mtetezi. Ni wengi yanawakuta yaliyokukuta, tena wasisikike wala kupelekwa nje kutibiwa.
Wapo wanaopigwa risasi kama swala. Wapo wanaopotezwa. Wapo wanaofungwa tena kwa kesi za kubambikiziwa. Lia ili machozi yako yawe kichocheo na zana adhimu ya ukombozi muhimu kwa taifa.
Rafiki yangu Kibanda, ingawa watesi wako wanadhani hawajulikani, hata ndege wanawajua. Kila mmoja anajua kuwa kuna siku uovu wao utawarudia na mchezo wao mchafu utafikia tamati.
Watesi wako wanajulikana, sema wamekuwa shirika na wale wanaopaswa kuwafikisha mahakamani. Nani wa kuwakamata? Wanaogopa wakiwakamata watamwaga mtama kwenye kuku wengi ili usiowategemea waumbuke na kuumbuliwa.
Tunawajua wamekodishwa. ni wauaji wa kukodishwa wanaoweza kuwadhuru hata mama zao ilmradi wamelipwa kufanya hivyo. Ni viumbe wa hovyo wasiopaswa kuishi hata kwa sekunde.
Wanaharamu hawa majinuni na habithi twawajua hata wanaowalipa watuumize na kutuua au kutunyamazisha. Je, tutanyamaza? Hasha! Kwani nani hatakufa huyo tumuone akiua wenzake?
Je, wanadhani watashinda siku zote? Ipo siku ya siku arobaini yao itafika kama ilivyowafikia wenzao waliotangulia. Nani alijua kuwa watu majinuni na wajivuni kama Muamar Gaddafi, Hosni Mubarak, Sadam Hussein na wengine wangekufa vifo vya aibu au kudondoshwa kama ubua?
Rafiki na ndugu yangu Kibanda, acha nimalizie kwa kukupa wosia wa mwisho. Nasema tena kwa kinywa kipana. Usiombe ulinzi wa polisi walioshindwa kukulinda kabla hayajakukuta. Ukifanya kosa watakumaliza. Walitaka kukumaliza Mungu akaingilia.
Usidhani Mungu siku zote atafanya kazi ya kukulinda wewe hata pale ambapo ungekwepa ushenzi na unyama huu. Je, sasa ufanye nini? Nakushauri usirudi. Maisha ni popote tena penya usalama kuliko nyumbani kwenye uhasama na mambo ya hovyo hovyo. Ukijidanganya kuwa ukirudi utatendewa haki uliyoikosa kabla ya kuumizwa jua umejimaliza.
Kwa wenye mamlaka haki ni wao kutenda wafanyavyo hata kama ni kuvunja na kuhujumu haki tena za walio wengi. Usifanye kosa ndugu yangu. Unadhani nguruwe anaweza kutoa harufu ya uturi au uvundo? Jibu unalo. Wanijua nakujua.
Fikiri juu ya hili ndugu yangu. Shika nasaha na busara zangu. Usikubali kung’atwa na nyoka mara mbili. Usidanganywe na tabasamu na maneno mazuri ya watesi wako. Usiwaamini wala kuwasikiliza wauaji waongo, wasanii na majambazi waliokubuhu. Waogope kama ukoma.
Ndugu yangu Kibanda, kwa leo haya yanatosha. Nasema moja tu. Pema ujapo pema ukipema si pema tena walisema wahenga.
Chanzo: Tanzania Daima April 3, 2013

2 comments:

Anonymous said...

Ndo maana fani ya uandishi ilinishinda kabadilisha fani! haikuwa uoga bali ni kuepuka upumbavu wa serikali iliyojaa rushwa, unyama na craps zote. Wanapenda uwe unawaandika kwa mazurii hata wakiwa wanafanya mabaya. Wapo tayari kukudanganya na viji coca cola na vimaji vyao ili ufiche mabaya yao. Unapoandika mabaya ni kosa kubwa ambalo litachukua maisha ya mwandishi. Ila huyu "RAHISI" asiye na mwelekeo na wala uwelewa amezidi. UDHAIFU wake anataka kuuficha kwa komesha wale ambao wanajua amaovu yake. SHAME ON HIM na kizazi chake chote...

Ndugu Nkwazi N Mhango said...

Anonymous hapo juu usemayo ni kweli. Jamaa anapenda sifa kiasi cha kujizungusha wapumbavu na waimba sifa wasiomsaidia bali kuzidi kumuumiza huko tuendako. Kwa sasa nchi yetu inatawaliwa kihuni na kipumbavu.