The Chant of Savant

Friday 4 April 2014

Hawa ni majaji au ma-junk?

Taarifa kuwa jaji Jon Utumwa (Si jina lake Halisi) kutoa huku mu usiku si za kusikitisha tu bali kustaaajabisha.  Sikuweza kuamini kuwa jaji angetoa hukumu saa 2:30. Laiti kama habari hii ingetoka kwenye magazeti ya udaku huenda ingeingia akilini haraka. Hata hivyo si uzushi. Hili lilitokea kama lilivyoripotiwa na vyombo vya habari. Kesi husika ilihusisha kampuni tata ya kuzalisha umeme ya IPTL ambayo imehusishwa na utapeli na ufisadi usio kifani.  Chombo kimoja cha habari kiliandika, “Hukumu hiyo iliyotolewa na Jaji….. katika Mahakama Kuu ya Dar es Salaam, Januari 17, mwaka 2014 saa 8: 30 usiku, imezusha maswali kutokana na umuhimu wa Tanesco kwa wananchi wengi.” Pamoja na kusoma kwangu sheria sijui sheria yoyote inayompa mamlaka hakimu au jaji kutolea hukumu nyumbani kwake tena usiku. Maana kisheria hukumu inapaswa kutolewa mahakamani na mahakama inaelezewa kuwa ni washitaki na washitakiwa, waendesha mashitaka (kwa mhakama za juu) na lazima iwe imekamilika.
Kuonyesha kuwa hukumu hii ina mshikheri kiasi cha aliyeitoa kutia shaka, Alipoulizwa kwanini alifanya hivyo badala ya kutoa majibu yanayoingia akilini alikaririwa akisema, “Mbona wenzako wameshaandika kuhusu hiyo kesi, wewe ndiyo unataka kuandika leo? Mimi nimeshatoa hukumu siwezi kuizungumzia tena, wasiliana na Msajili wa Mahakama.”
Msajili wa Mahakama Kuu Kanda ya Dar es Salaam, Amiri Musumi naye alionyesha mshangao akisema, “Kwa kweli ndiyo nasikia kwa mara ya kwanza kuwa hukumu ilitolewa saa 8:30 usiku.”
Imefikia mahali kuna majaji na mahakimu hawasifiki kwa ujuzi wa sheria wala utendaji haki bali kuwaachia wauza unga. Inaonekana kuna mtandao kama aliosema rais Jakaya Kikwete wa majangili ambapo kesi fulani chafu hupangiwa jajifulani mchafu au junk.
Hata hivyo hii si mara ya kwanza kwa baadhi ya majaji kufanya madudu tena wazi wazi. Mfano, wamekuwapo majaji wanaolalamikiwa kuwaachia ima mafisadi au wauza unga. Mfano gazeti la moja liliwahi kuandika, “Mheshimiwa Jaji huku akifahamu kuwa kesi hiyo imefika mbele yake kwa ajili ya kusikiliza maombi ya dhamana tu, na kuwa ilikuwa haijafikishwa Mahakama Kuu kwa taratibu wa sheria, aliamua kumfutia kesi mshitakiwa na kuamuru kuwa yuko huru."
Kadhalika Mbunge Ester Bulaya alikaririwa akiliambia bunge kuwa kuna mtandao wa maovu unaowahusisha watendaji wa mahakama polisi na taasisi nyingine nyeti za umma. Bulaya alikaririwa akisema.  “Kwa kutumia mtandao huo, baadhi ya Majaji wamekuwa wanatafsiri sheria kwa jinsi wanavyotaka na kuwapa dhamana watuhumiwa wa kesi za dawa za kulevya ambazo hazina dhamana. Mfano mzuri ni kesi Na.6/2011, Jamhuri dhidi ya Fred William Chonde na wenzake ambao walikutwa na kilo 179 za Heroine yenye thamani ya shilingi Bilioni 6.5.”
Bulaya aliendelea kusema, “ Washitakiwa hawa wanashitakiwa kwa kosa la kusafirisha dawa za kulevya ambalo kwa mujibu wa kifungu cha 148(5)(a)(ii) cha sheria ya Mwenendo wa Makosa ya Jinai pamoja na kifungu cha 27(1)(a) cha Sheria ya Kuzuia usafirishaji wa dawa za kulevya halina dhamana.” Je baada ya mbunge kulalamika ni hatua gani zilichukuliwa? Hakuna. Maana kama zingechukuliwa huyu aliyetoa hukumu usiku asingefanya hivyo bila shaka.
Mbali na mbunge Bulaya gazeti la Jamhuri mwaka 2012liliandika hivi, “Jaji Pendo Msuiiya, wakitambua kuwa sheria sheria inazuia. Bila kuchukua jalada wala kuwasiliana na Mahakama ya Kisutu, huku Jaji Msuiiya akijua fika kuwa kilo 175 ambazo thamani yake ni zaidi ya Sh bilioni tano, na watuhumiwa hawapaswi kupewa dhamana; yeye kwa mamlaka aliyonayo kama Jaji aliamua kuwapa dhamana watuhumiwa hawa. Baada ya kupata dhamana, Wapakistani walirejeshewa pasipoti zao na wakakimbia nchi. Hawajakamatwa hadi leo.” Si Bulaya tu aliyelalamikia kadhia ya kuwa na majaji wasio waadilifu. Mbunge wa Singida Kaskazini Tundu Lissu amewahi kuwalipua wengi. Aliwataja Fatuma Masengi na Mbaruku Salumu Mbaruku aliyesema elimu zao ni ya utata, Latifa Mansoor aliyesema alifukuzwa kwa udanganyifu na ubadhirifu akiwa mfanyakazi katika Manispaa ya Ilala.  Lissu aliwataja pia Kassim Nyangarika na Zainab G Muruke kuwa hawakuwa na maadili. Pia Lissu alimtaja Mwendwa Malecela liyesema kuwa tangu ateuliwe mwaka 2006 hajawahi kusikiliza kesi hata moja. Badala yake Lissu alidai kuwa jaji huyo huenda matibabu India tu.
 Ajabu hakuna hatua iliyochukuliwa zaidi ya watuhumiwa kuendelea kuwa kazini wakifanya madudu kama kawaida. Je mamlaka zinazowateua zina maslahi gani katika jinai hii ya kutisha ambayo kimsingi inadhalilisha mahakama na kushusha hadhi yake ukiachia mbali kukosa imani ya wananchi katika mfumo wetu wa sheria.
Gazeti liliendekea, “Julai 30, 2012 baada ya Jaji Dk. Fauuuz kutoa hukumu hiyo ya ajabu, mawakili wa Serikali ambao ni upande wa mashitaka wakawasilisha nolle chini ya Section 91 ya CPA.”
Gazeti liliendelea, “Tulishangaa, kwamba kwanza Mahakama hii haina mamlaka ya kusikiliza kesi hii, lakini pia baada ya kupita siku 60; bila mamlaka kisheria, Hakimu Luagooo (si jina lake halisi) akaifuta. Hakimu huyu ni kero.” Kwa mujibu wa gazeti la Jamhuri la Agusti 2013, hakimu Luangoo alihamishiwa Lindi akagoma kwenda. Hii inaonyesha mtandao wa maovu ulivyo na nguvu kiasi cha watu kujipangia ni wapi wafanyie kazi kwa maslahi yao.
Kama hali inayoendelea haitarekebishwa, kuna uwezekano Mahakama zetu licha ya kuendeshwa na vihiyo, zitaendeshwa na wahalifu wanaotumia sheria kuwaokoa wenzao. Je nini chanzo cha kazia hii? Ni ule uteuzi wa haraka au vodafasta ambapo majaji wenye mabaka kama vile kuwahi kuhonga kwenye kesi za wateja wao walipokuwa mawakili na wengine wenye elimu ya kutia shaka kuteuliwa? Je kwanini mamlaka zinatuletea majaji wabovu kama hawa hata kama si wote? Maana majaji kama tulioainisha hapo juu wamezidi ya kuzidisha wameishiwa na kuisha kiasi cha kuchusha na kupaswa kuwa magerezani badala ya mahakamani. Hapa hujaongelea maaskari wanaoshirikiana na wahalifu au viongozi wanaokula na wawekezaji wanaohujumu uchumi wetu kwa kutolipa kodi na kuingia mikataba ya kiwizi.
Chanzo: Dira Machi, 2014.

5 comments:

Anonymous said...

Kule kwenye kikao chetu cha kijiwe, Rais wa kijiwe cha walevi ametuambia cheo cha ujaji ni kazi ili kupata fedha ya ulabu na siyo ujuzi unaohitaji maarifa ya kitaaluma kutenda haki kwa mujibu wa sheria

Ndugu Nkwazi N Mhango said...

Anon,
Naomba hiyo anwani ya kijiwe chenu nije nigombee ujaji nitoe haki. Kusema ukweli kwa majanki na majanga tulio nao hata mimi naweza kuwa jaji mzuri.

Jaribu said...

Shida ni kwamba hiyo inaanzia juu Ikulu mpaka chini kwa tarishi. Nani atamwajibisha mwenzie? Kila mtu ana madudu yake. Ikiwa huyu Dr Clueless daima ana orodha ya majangili lakini hawafanyi chochote, huwezi kutegemea hao majaji wataogopa kuchukuliwa hatua.

Ndugu Nkwazi N Mhango said...

Jaribu usemayo ni kweli. Wetu ni uoza wa kimfumo ambapo kundi la majizi limejilimbikizia madaraka na mali kiasi cha kupasiana kila ulaji. Ni bahati mbaya kuwa linakula kwa mikono na miguu bila kunawa huku likionyesha tabia kama aliyowahi kuonya jamaa mmoja kuwa ni kama mainzi yalayo kutapika na kunya mle mle yanamolia.

Anonymous said...

Nyerere alisema ikulu si mahala pa kukimbilia
Ikulu pagumu
Ukiona mtu anakimbiliia ikulu ana lake