Saturday, 12 April 2014

`Madaktari` wengine wana PhD za mitusi

Wanawake wataka kuzichapa bungeni
Dk Ave-Maria Semakafu  kushoto na Leticia Nyerere kulia (pichani) walinusurika kupigana huko Dodoma hivi karibuni
Mlevi aliamini kuwa yeye ndiye bingwa wa mitusi kutokana na kusumbuliwa na kanywaji na mibangi anavyofakamia ukapa na usanii unapomkwaza.
Kumbe wapi? Juzi nikiwa kwenye misele yangu baada ya kutoa mada kwa Bunge la Kitabu, sorry Katiba Mpya aka ‘Constipation Assembly’ si nikaingia mitaa ya Dodoma. Onyo, sikwenda mitaani kutafuta vyangu kama jamaa wanaopokea njuluku za dezo.
‘I went there to learn how Danganyikans, Boozers and other earthlings perceive this shop talk.’ Sorry, nimeongea kinyasa na kusahau kuwa si lugha ya Dziko ili! Hayo tuyaache.
Si nikiwa napanga kudandia mshangingi wangu wa Kijep wakatokea wamaza wabee wanaoonekana kuwa wa heshima ingawa hawana hiyo heshima kutokana na walichonionyesha.
‘You know what?’ Si walikuja mbele yangu na kuanza kuvuana nguo! Japo hawakufanya hivyo ‘practically,’ midomo yao iliyopaswa kuwa mitamu iliwavua nguo. Maana hiyo mitusi waliyokuwa wakimwaga tena kwa mashindano haijawaacha na nguo ‘so to speak.’
Kuna mitusi mingine sikutegemea ingetoka kwenye kinywa cha mtu anayeitwa mama aka lady.
Sikuwahi kusikia mwana mama akimtukana mwenzie matusi yanayohusiana na jinsia ya maza wake, hayo tuyaache maana uga huu si wa udaku,
Hakuna kitu kiliniacha hoi kama kugundua kuwa hawa wamama wanaonekana wasomi japo mmoja wao alithibitisha kuwa ima alighushi PhD yake au alipoteza muda darasani.
Maana mitusi aliyokuwa akirap siwezi kuamini kama kweli ana PhD hata kama ni ya hishima.
Baada ya wamama hawa kunusurika kuvaana wakiwa wameachana uchi baada ya kuchaniana nguo wakigombea katiba, nilifanya uchunguzi.
Niligundua kuwa madaktari wengine wana PhD za mitusi.
Mfano ni Dokita Ave-Mary Semakufuru aliyewatusi wabunge wote wa upingaji kuwa ni maroboti yasiyo na akili bila kujua naye ni roboti aina ya CCM.
Japo bibi wa kimura aitwaye Let Nyenyere alipandisha sana, alijizuia kumwaga mitusi.
Sana sana alichonisaidia ni ile hali ya kuhoji kama mimi jinsi huyu Semakufuru anayeonekana kuwa kiwanda cha matusi alivyopata au kupewa PhD wakati maneno yake yanamuonyesha kama hamnazo? ‘I wonder. I wondered. I shall keep on wondering so to speak.’ Huyu angehudhuria darasa langu angefeli hasa ikizingatiwa kuwa wakati napiga chaki kwenye university ya chuo kikuu sikuwa tayari kuhongwa iwe njuluku, nkojo hata ngono. Hayo tuyaache.
Hakuna kitu kimeendelea kunisumbua kama kugundua uhovyo wa baadhi ya wajumbe wa Bunge la kuula ambao uwezo wao wa kufikiri haufikii hata urefu wa pua zao.
Hata hivyo, nashukuru Subhana kuwa Sam Sixx amekubali karipio langu la kutaka abadilishe uteuzi wake wa kisanii. Maana angepuuzia ningemtokea na walevi na michupa yetu na kumtoa mkuku kama si ngeu.
Kwa vile Sam Sixx ni kijana wangu, napanga kwenda kumpa shinikizo atoe tamko la kulaani kumdhalilisha jaji Wariboa ambaye anaonekana kuandamwa na wahuni kama Salva Rweyependekeza na wengine wasijue kufanya hivyo ni kumtukana hata huyo mungumtu wao aliyewaumba na kuwapa ulaji wakati ni makanjanja na vihiyo.
Hata hivyo, sishangai. Nakumbuka malalamiko ya mlevi mmoja aliyehoji kuwa ikuu inapokaliwa na wahuni mtegemee nini? Aliendelea kulalama akisem: Omba Mungu wapatikane wakazi wenye uchungu na kaya waisafishe na kuibadili toka kuwa pango na majizi na machizi kama akina Salva Rweyemaaamu aka Rwependekeza aka Rwechanganya aka Rwecontradictmu.
Turejee kwa hawa warembo walioamua kujigeuza sinema tena ya bure. Je! walikuwa wakigombea katiba au kitu kingine kwa kisingizio cha katiba? Nilitaka kuwasogelea lau niwaliwaze kwa kuwasihi niwapeleke sehemu na kuwapa ofa kidogo lau watulie kama si kusuuzika.
Lakini nilipokumbuka mitusi ya huyu anayeitwa dokta Ave-Mary Semakufuru nilichelea anaweza kunitia aibu mbele ya washikaji zangu wakaamua kumalizia mibangi na migongo yao kwa kumuangukia kinomi au vipi?
Kusema ukweli kitendo cha hawa kinamama wanaopaswa kuwa kioo cha jamii kujivua nguo tena mbele yangu kwenye parking lot kiliniacha na uchungu kiasi cha kuendelea kutaka kuwajua kwa undani zaidi na zaidi. Maana niliinyaka kuwa yule binti mura naye anasomea PhD. Nilitaka nimshauri asomee PhD ‘in Neuroscience or Parapsychology’ ili aweze kubaini aina ya ugonjwa mwenzake anaoumwa.
Huyu daktari Makufuru amenikumbusha vituko vya waganga wa kienyeji kujiita daktari hata profesa.
Hilo tisa. Kumi tabia za huyu daktari hatari na bingwa wa mitusi zimenikumbusha madaktari fweki na wa kughushi kama akina Bill Lukuvii, Emmy Nchimvi, Merry Nyago, Dolorous Kamala, Diddie Massaburi aka Makalio, Makorongo Muhanga na wengine wengi ambao Daktari Njaa Kaya aka Dr 0… we koma, ameamua kufa nao kwa sababu ajuazo.
Kuna mlevi aliyedai kuwa ‘birds of a feather flock together’ akimaanisha kuwa waarabu wa Pemba hujuana kwa vilemba huenda alighushi ingawa hatujui.
Anayedhani namuonea mrume huyu arejee jinsi hivi karibuni ilivyofumka kashfa ya kughushi ambapo baadhi ya watu walioomba kuajiriwa vilipatikana vyeti zaidi ya elfu moja feki.
Kama hili si balaa kwa kaya ni nini ambapo kaya inaajiri watu feki na wa hovyo tena wezi kiasi cha kusifika kwa mambo ya kipuuzi, ufisadi, ujangili, udokozi, uzembe, umbea, unywanywa, ulimpyoto, upogo na madude mengine?
Hakuna kitu kimeendelea kuniandama hadi bi mkubwa anauliza kunani kama kujua kuwa daktari Semakufuru ni mhishimiwa mbunge.
Kama hii ndiyo ‘crop’ ya wahishimiwa waishiwa tulio nao tumekwisha. Kitendo cha huyu mdada aliyetukana wenzake kuwa ni maroboti wakati yeye akiwa kiongozi wao, kimenifanya nifikirie hata kuacha kutumia PhD zangu.
Sijui huyu mama kama ana mume na kama anaye basi namsikitikia sana tena sana.
Heri angekuwa kanunga kama Annae Makidamakida au Sofi Lion.
Leo sitasema mengi zaidi ya kuwashauri wahusika na wote wenye tabia chafu kama hii wajirekebishe.
Pia wakubwa wetu waache kushabikia jinai kama vile kughushi na ufisadi na ujangili.
Salamu za leo ni kwa Keinerugaba Msemakweli bingwa wa kupambana na kughushi.
CHANZO: NIPASHE Aprili 12, 2014. 

No comments: