Tuesday, 29 April 2014

Nyalandu anamdanganya nani?

Hakuna kitu kimetuacha hoi kama kauli iliyotolewa na waziri wa Maliasili na Utalii Lazaro Nyalandu mkoani Mara, alipokuwa akizungumza na waandishi wa habari mara baada ya kuhutubia mahafali ya 10 ya Chuo cha Musoma Utalii.  Nyalandu alikaririwa akisema, “Mimi niseme tu kwa sasa mipango niliyoweka kwa kushirikiana na watendaji wangu, polisi, jeshi la JWTZ na wadau wengine ni kuhakikisha wahusika wote wananaswa na kutajwa majina bila ya hofu wala kuoneana haya, hata kama ni kigogo wa serikali nitamtaja jina.”
Kwa kauli ya Nyalandu kuna ukweli kuwa kuna vigogo wa serikali katika kadhia ya ujangili kama lilivyowahi kudai gazeti la Uingereza la The Mail on Sunday. Ni bahati mbaya kuwa watuhumiwa waliamua kufunika kombe ili mwanaharamu apite. Je Nyalandu alimaanisha nini anaposema “hata kama kuna kigogo wa serikali”?
Nyalandu aliongeza,“Niseme tu hawa wanaofanya biashara ya mkaa, kuvuna magogo na kukata miti hovyo na hata wale wafugaji wanaoingiza mifugo yao kwenye hifadhi na wao pia nawaona kama majangili tu, adhabu yao ni sawa na majangili wa meno ya tembo.” Hapa ndipo ubabaishaji wa Nyalandu unaweza kuuona wazi wazi. Je sheria inasemaje kuhusiana na tafsiri ya neno jangili?  Hivi kweli wachoma mkaa waliosikinishwa na sera mbovu wanapaswa kuitwa majangili? Je kuwakamata ndiyo jibu wakati wakiendelea kufukarishwa huku mikataba mingi ya nishati ikiwa ya kiwizi kama ilivyobainika kwenye kashfa za Richmond, IPTL na nyingine nyingi zihusianazo na nishati? Hapa ni kama Nyalandu anataka kukwepa wajibu wake na kuwatwisha mzigo watu maskini wanaotafuta riziki zao baada ya kuwa mashuhuda wa maliasili na utajiri wao ukiwanufaisha wageni. Kesho watakamatwa wachoma mkaa na kutangaza kuwa amewakamata vigogo wa ujangili.
          Tumkumbushe Nyalandu kuwa si wa kwanza kuja na viapo kama hivi. Alianza waziri wa Usafirishaji Dk Harrison Mwakyembe alipodai kuwa atawashughulikia wauza unga. Tangu atoe tishio hili, Mwakyembe hajawahi kukamata hata mmoja. Sana sana siku hizi amenywea kuonyesha kuwa ameshindwa na alijipayukia. Kama Mwakyembe, Heri Nyalandu angejinyamazia. Kama bosi wake yaani rais Jakaya Kikwete amenywea, yeye ni nani? Kama Kikwete ameweza kuwateua hata baadhi ya watuhumiwa wa kusafirisha nyara za taifa kama katibu mkuu wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Abdulrahaman Kinana, Nyalandu ni nani awakamate wateule hawa? Kama serikali yake imeshikwa na kigugumizi kueleza ni kwanini wale wapakistani waliotorosha wanyama hai waliruhusiwa kutoroka, leo Nyalandu ana jipya gani zaidi ya kuwa sanaa na ngonjera za kuwalewesha wananchi. Kamata na kuonyesha hao majangili ndipo utangaze badala ya kuapa. Maneno matupu hayavunji mfupa. Watu wanataka matendo na si viapo na matishio. Maana mwenye kukamata au kutaja huwa hatangazi zaidi ya kutenda na kuuonyesha umma. Anachofanya Nyalandu nadhani ni kuwastua wahusika kuwa kuna kitu kibaya kinaweza kuwakuta hivyo wasimamishe shughuli zao haramu au kubadili mbinu.
          Ni bahati mbaya kuwa watawala wetu wenye maneno na ahadi nyingi wameligeuza taifa letu kuwa shamba la bibi hata la chizi. Hata hao majangili wanaokamiwa na Nyalandu wanajua hili fika. Hawataacha kutenda jinai yao ambayo inawaingizia mabilioni ya fedha.
          Kimsingi, tatizo la ujangili ni suala la kimfumo ambapo Tanzania inaruhusu mtu kutajirika bila kutoa maelezo ya ni namna gani amepata utajiri husika.  Wezi na majangili na wahalifu wengine watashindwa nini kuendelea kutengeneza fedha iwapo hata viongozi wetu wamekataa na kushindwa kutaja mali zao. Je wanaogopa nini kama utajiri wao hautokani na jinai hizi wanazodai watapambana nazo?
Turejee yaliyoandikwa na The Mail on Sunday na serikali ikakaa kimya. Gazeti liliandika, “Utawala wa Rais Kikwete umetawaliwa na mauaji ya tembo yaliyovunja rekodi katika historia ya nchi yake. Kibaya zaidi, wahifadhi wanasisitiza kuwa, ndani ya Serikali kuna viongozi wanaoshiriki biashara hiyo.” Kama madai haya yangekuwa ya kizushi bila shaka serikali ya Kikwete ingekwenda mahakamani ili kujisafisha na kutoa somo juu ya nini ni ukweli au uongo wa madai haya.     
Je ni kwanini serikali iliamua kunyamaza kama hakuna ukweli? Gazeti liliendelea, “Miongoni mwao ni  matajiri wakubwa nchini, wafadhili na wanachama wa CCM na ndugu wa karibu wa Rais Kikwete. Lakini wanao marafiki wakubwa, huku majaji, waendesha mashtaka na polisi hurubuniwa kwa urahisi.”
Je hawa ndiyo vigogo wa serikali anaosema Nyalandu? Je anao ubavu wa kuwataja achia mbali kuwakamata? Kinachofurahisha ni ukweli kuwa Nyalandu hata Kikwete wanawafahamu hawa majangili papa kama walivyowahi kudai kuwa kuna mitandao yenye majangili kati ya 40 na 320. Sasa kama mnawafahamu na hamtaki kuwakamata, mnatupotezea muda wa nini kuapia kuwa mtawashughulikia?
Kuonyesha kuwa kuna ukweli unaofichwa, ni Nyalandu huyu huyu na wizara yake waliomgharimia mwandishi wa The Mail on Sunday Martin Fletcher kuja kuwasafisha. Hata hivyo, Fletcher aliendelea kuwavua nguo hadi wakachanganyikiwa na kunywea. Fletcher alikuja na kulipiwa malazi na kila kitu kwenye hoteli ya kitalii ya Serena. Je kama si kutaka kumziba mdomo mwandishi, ingawa hawakufanikiwa, walikuwa wanamlipia kama nani? Kimsingi, Fletcher alipaswa kuwa mgomvi wao ambaye walipaswa kukutana naye mahakamani na si kwenye hoteli ya kitalii huku wakiteketeza fedha ya umma. Je Nyalandu na wizara yake walikuwa wanamlipia Fletcher kwa kazi gani? Haiingii akilini hata kidogo.
Tumalizie kwa kumshauri Nyalandu akamate ndipo atangaze badala ya kutangaza kabla ya kukamata hao majangili wake anaowajua hata kwa idadi kuepuka kuchukulliwa ni kama sanaa  tu. Vinginevyo kinachoendelea hakina tofauti na tambo za Kikwete aliyesema ana orodha ya majina ya wauza unga lakini asiwakamate. Hana tofauti na Mwakyembe aliyejivua nguo na akaendelea kujitoa kimasomaso kwa kunywea baada ya kuonyesha wazi alivyoshindwa na wauza unga sawa na bosi wake. Je Nyalandu anataka kumdanganya nani wakati kila kitu kiko wazi kuwa hana ubavu wala nia ya kuwakamata majangili papa anaowajua kwa sura na majina?
Chanzo: Dira Aprili 2014.

No comments: