Wednesday, 9 April 2014

Huu si Muungano bali mgongano

HAKUNA ubishi kuwa Muungano wa Tanganyika na Zanzibar uliodumu kwa zaidi ya miaka 50 umekuwa ukikumbwa na misukosuko kila wakati.
Hivyo, hali hii hutukumbusha kuwa yanahitajika marekebisho katika baadhi ya mambo kuhusiana na muungano.
Kwa sasa muungano huu ni mgongano zaidi ya muungano.
Kuna malalamiko kila aina toka pande zote kuanzia hofu ya kumezwa kwa upande mmoja na kupoteza utambuliko kwa upande wa pili.
Hivi karibuni utata wa muungano umejitokeza wakati wa kukusanya mawazo juu ya kuandikwa kwa katiba mpya.
Utata umeendelea hadi kwenye Bunge la Katiba (CA) ambapo Chama Cha Mapinduzi (CCM) kinataka serikali mbili ilhali upinzani na Watanzania walio wengi wakitaka serikali tatu.
Suala hili limezusha sintofahamu, kushutumiana hata kutoaminiana kiasi cha Bunge la Katiba kupoteza muda mwingi katika kutafuta jinsi ya kuelekea suala hili.
Ili kuondoa sintofahamu hii na kukata ngebe, hata mzizi wa fitina, tunapendekeza kueleweka na kufanyika baadhi ya mambo.
Tuanze na sababu ya kuungana. Historia inatwambia kuwa muungano wa Tanzania ni matokeo ya hofu ya wakati wa vita baridi baina ya wakomunisti na mabepari.
Hivyo, ifahamike kuwa muungano wetu ambao siku zote umekuwa mgongano si wa hiari bali wa kulazimika. Ni bahati mbaya kuwa watawala hawakupenda kuufanyia marekebisho ili kuendana na wakati na matakwa yake.
Inafahamika kuwa Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Nyerere, rais wa kwanza wa Tanganyika, hakutaka Zanzibar iende kwa mabepari ilhali Sheikh Abeid Aman Karume, rais wa kwanza wa Jamhuri ya Watu wa Zanzibar aliridhia muugano wa haraka kwa hofu ya kupinduliwa baada ya kumpindua sultani.
Hivyo, dhana nzima ya muungano ni ulazima au ‘necessity for survival not a choice’, tofauti na unavyochukuliwa.
Hivyo basi, kama pande mbili zitazingatia sababu za kuungana tena kwa haraka, zitaamua vizuri.
Kwa mfano, kama Tanzania Bara ikiamua kutumia ukweli wa kihistoria na kutaka kuuvunja, atakayeathirika zaidi anajulikana, hasa ikizingatiwa kuwa kitisho cha kwenda kwa mabepari hakipo tena.
Kwa upande wa Visiwani bado hali ni tete. Leo wakiondoka kwenye muungano, kutazuka mgawanyiko baina ya Afro na Hizbu.
Hivyo basi, Zanzibar wanauhitaji muungano saa nyingine kuliko Bara kwa vile unawapa kinga dhidi ya vurugu.
Angalia kinachoendelea Comoro ukitaka kujua ‘future’ ya Zanzibar nje ya muungano.
Najua nitakayoandika yanakera japo ni ukweli. Lazima kufanyia muungano marekebisho. Ni bahati mbaya kuwa watawala wa sasa wanatuhimiza tuheshimu mawazo ya waasisi ya mwaka 64. Hii haliwezekani.
Wapo wanaotumia visingizio kuwa waanzilishi walisema ili au lile. Hatuwezi kuendeshwa na mawazo ya mwaka 64 katika karne ya 21, vinginevyo tuwe tumedumaa na kuganda kiakili.
Matatizo yaliyosababisha muungano yametoweka kwa upande wa Bara ambapo hofu ya kumezwa haipo tena.
Hata hivyo, kuna madai ambayo hayajathibitishwa vizuri kuwa hadi Karume anauawa, alikuwa haongei na Nyerere tena. Hata hivyo, kuna ukweli kwenye madai haya. Maana Nyerere aliwahi kusema kuwa ingekuwa ni uwezo wake basi angesukumizia visiwa vya Pemba na Unguja mbali na Tanganyika.
Huyu hakuwa na raha katika ndoa yake isiyo tenda haki. Haiingii akilini, kwa mfano, kipande kidogo cha ardhi kama Visiwani eti kiwe na haki sawa na Bara.
Hata katika huo muungano wa muda mrefu na wa kudumu wa Marekani, nchi kubwa zinazouunda kama vile Texas na California zina kura nyingi za maamuzi kuliko nchi ndogo kama Hawaii. Mfano California wana kura 55 za turufu katika uchaguzi ikilinganishwa na Hawaii kura 4.
CCM wanashabikia mvutano baina ya serikali mbili na tatu ili utupotezee muda na kuacha kujadili mambo ya msingi kama vile uwajibikaji, maadili ya uongozi, kupambana na ufisadi uliotamalaki, kinga za viongozi hata wanapotuibia, maendeleo, uchumi, madaraka ya rais, ukubwa wa serikali na mengine mengi.
Japo wanaonyesha kutoa povu mdomoni kuhami hoja yao ya serikalli mbili, moyoni wanachekelea kuwa tumeingia mtego wao na kuepuka kugusa mambo yaliyowawezesha kutawala kwa muda mrefu ukiachia kujadili namna ya kupambana na kushughulikia madhambi yao ya miaka hamsini.
Wanaomba Mungu sintofahamu hii iendelee ili wanusurike. Mfano, tumeishapoteza zaidi ya mwezi mmoja kujadili kanuni ndogo kama vile ni aina gani ya kura itumike.
CCM wanajua kuwa itafika mahali Bunge la Katiba litajikuta limeishiwa muda. Hivyo, kuomba au kubanwa liharakishe au hata kupangiwa muda wa kupatikana katiba. Hapa ndipo mambo ya muhimu yatajadiliwa na kupitishwa kwa haraka kiasi cha kuinusuru CCM mtegoni.
Bado ni ukweli kuwa CCM haitaki suala la serikali tatu ambalo kimsingi linainyima mamlaka juu ya visiwani. Ukitaka kuiua CCM basi sema tunataka serikali moja ili kutenda haki kwa pande zinazokinzana jambo ambalo litaifanya siku hiyo Visiwani ijitoe kwenye muungano bila hata mashauriano japo baada ya hasira kuisha ima watarejea au kuanza kuonja adha ya kuwa nje ya muungano.
Wangepatikana viongozi wa kuwaambia upande wa pili kuwa sasa ni serikali moja liwalo na liwe, hasira na vitisho vingeibuka, lakini mwisho wa yote zingeshuka hasa kwa kuangalia uhalisia wa kinachowasubiri mbele ya safari.
Hebu tutoe mfano mwingine. Leo Burundi, Kenya, Rwanda na Uganda zinaihitaji Tanzania na Sudan ya Kusini kwenye jumuia yao kuliko hizi nchi mbili zinavyowahitaji wao kutokana na ukubwa wake kwa kila kitu.
Huu ni ukweli usiopingika hata tungeupuuza vipi. Tembo hawezi kuungana na sungura wakagawana kila kitu kwa usawa bila kujali ukubwa wa wahusika. Hii ni kanuni.
Hivyo, hakuna haja ya kutoana roho kwa serikali mbili au tatu ambazo kimsingi zinatuzuia kuungana na kujadili mambo ya msingi. Kama wote tuna nia safi na muungano, basi tuunde muungano wa serikali moja, asiyetaka aliache litote tugawane mbao. Kama wasemavyo Visiwani.
Ukitaka kujua faida au hasara ya muungano, uvunje. Hatupaswi kuwa na Tanganyika wala Zanzibar, hasa ikizingatiwa kuwa tuliungana na kuunda taifa moja la Tanzania.
Chanzo: Tanzania Daima Aprili 9, 2014,

5 comments:

Jaribu said...

Ingekuwa poa kama jamaa wangekuwa wanaelewa huu ukweli na wana uwezo wa kufanya "maamuzi magumu". Shida ni kwamba bongo mbili jumlisha mbili ni tano.

NN Mhango said...

Jaribu usikonde wataelewa. Samahani nilichelewa kukutundikia email yangu ambayo ni mpayukaji@yahoo.com
Sasa tunaweza ku-touch base independently and privately. Hili la Muungano jaji Warioba amelichambua vizuri alipoonya wasimtumie Nyerere kama hirizi na kuwa Nyerere wanayemtumia alikuwa akielekea kwenye muungano wa serikali moja. Nangoja kusikia spin doctors na honchos watajibu nini kama wataweza.

Anonymous said...

naona kila siku mpo nyie tuu jaribu na muhogo

Anonymous said...

Anon, Wewe unapenda idadi iwe watu wangapi?

NN Mhango said...

Anon mbona nawe upo leo au wewe si mtu?