Wednesday, 9 April 2014

Kijiwe chamshukia Mkamia magazeti

LEO tena Mgosi Machungi amekuja kijiweni bila gazeti. Anaonyesha waziwazi alivyokerwa na huu ushenzi wa kutishia kufungia vyombo vya umbea kutokana na kukataa kulala kitanda kimoja na mafisadi walioko kwenye ulaji, tena wa bure.
Hasira yake imeongezeka kiasi cha kutaka kuvamia mjengo kuwatimua wasasi wa ngawira wanaokwamisha katiba mpya. Walidhani vyombo vya umbea havitaandika umbea na unywanywa wao.
Leo kijiwe kina hasira sana, hasa baada ya kugundua kuwa kila uchao wanakula njuluku zetu for just doing nothing. We are tired of your hanky panky monkey business.
Kijiwe kimedhamiria kutoa taarifa kwa wote wanaodhani watashinda kuichakachua katiba kukaa mkao wa kuliwa.
Mgosi baada ya kuamkia anasema: “Wagoshi, mnaonaje huyu mdudu wa kutishia kufungia magazeti eti kwa vile hayakubali kuwekwa mfukoni mwa wababaishaji na mafisadi?
Mlimisikia Jumaa Mkamia Magazeti juzi akibwabwaja? Tate nane titaua mtu hapa. Hamiwezi kutinyima habai kuficha madhambi yenu.”
Mpemba anajibu haraka haraka: “We washangaa hili la kutishia kufungia vyombo vya habari? Twaona watu wavurunda kwenye kusaka katiba badala yake wajivua nguo kwa kutunisha nsuli kwa magazeti. Si waache kutenda uovu basi? Yapo mengi yanaendelea ya kutufumba mdomo japo wao wataka tufumba macho.”
Mipawa anakatua mic: “Nkwinga nashangaaga. Watu wameishiwa. Wakiambiwa ukweli wanafungia magazeti. Mtafunga magazeti, lakini hamtafungaga macho wala akili zetu. Leo wanaweza kutishia kufunga vyombo vya umbea ila hawatazuia umbea wao kutufikia. Ipo siku nasi tutawafungia. We waache wacheze makidamakida kama Makida wa Mjengoni aliyesimikwa na mafisadi.”
Msomi Mkatatamaa anaweka gazeti lake la The Mail on Monday pembeni na kudema: “Nilikuwa nasoma taarifa hizi za kutisha na kutia aibu. Naona hata vyombo vya haki za binadamu na uhuru vimeishaipata na kutoa sauti. Hata hivyo, viziwi wetu wanasikia bila kufanyiwa kweli? Eti naambiwa huyu Mkamia Magazeti naye ni mwandishi wa habari. What an epic loss! He won’t achieve that which he wants to achieve before hitting the road Inshallah.”
“Msomi wachanganya Kikameruni na kiarabu au inshallah nalo neno la Kikameruni?” Anasema Mpemba.
“Watasikiaje wakati wamelewa ulaji chakari? Mkamia Magazeti basi nenda kafunge The Mail on Sunday lililomvua nguo bosi wako kwa kumhusisha na ujangili.” Anajibu Kapende huku akibwia kahawa yake.
Mijjinga anaingilia kati: “Huyu mjivuni Mkamia Magazeti hana ubavu wa kufungia The Mail on Monday hata ikiripoti uchafu wao. Wajifungie wakose njuluku? Nashangaa hata hizi kaya zinazojidai kuendelea. Zinatufundisha demokrasia. Tukiifanyia kazi yanatuacha solemba. Sijaona zikiingilia kati na kuondoa njuluku zao kwa genge letu ili tuone kama litaweza kujiendesha.”
Bi Sofi hakubali: “Acheni kulalamikalalamika hovyo. Hatuwezi kuacha wambea wajiandikie kila uzushi huku wakitoboa siri za usalama wa kaya.”
Msomi anarejea kwa hasira: “Sofi ndugu yangu umelogwa na nani? Usalama gani unaoongelewa hapa, wa majangili na mafisadi kuogopa kufukuzwa kwenye ulaji na wenye kaya siyo? Hivi kweli kuna siri kwenye mambo ya umma, hasa ya kaya? Kwani kaya ni ya hao wanaotuibia na kutaka kuficha jinai yao au ya wanakwaya? We can’t allow them to objectify us in any way. Indeed we can’t.”
Kiingereza chake kigumu kinawaacha hoi baadhi ya wanakijiwe, isipokuwa mimi msomi wa wasomi mwenye magunia ya PhD za ukweli na si za heshima na kughushi kama za kina Nchimvi Makorongo, Luku-vii, Masaaburii na Nyagu.”
“Wallahi mie haya ya kutishia kufungia magazeti hayanishughulishi kama kuchakachuliwa kwa katiba wallahi. Yaani walituhadaa tutoe mawazo wakati wanayo yao au walitaka tuimbe ngoma moja ya kuliwa wakati twaliwa na wao? Mbona hawajawahi fungia yale yanayoeneza kampeni chovu na za kipuuzi kama lile la Udhulu na Mzaalendoo au haya nayo si magazeti?” Analalamika Mpemba.
Mgosi hangoji Mpemba aendelee. Anadakia: “Kama kuiwa waiwa wewe si mimi. Subutu! Mtu anile nimuache bila kumpiga zongo suai (akimaanisha surely)?”
Kijiwe hakina mbavu jinsi Mgosi anavyojihami akiogopa kuliwa wakati kweli analiwa ukiachia mbali Kiinglishi chake cha Kisambachi.
Mpemba anajitetea: “Yakhe wanionea. Mie sina utani nawe. Nisemacho ni kwamba kama tutaendelea kuburuzwa hivi kuna siku tutaliwa wallahi.”
Mipawa anaamua kumliwaza Mgosi Machungi. Anasema: “Mgosi usiogopege kuliwa. Hata hao wanaotula wanaliwa na wale wanaowatumia kutula sisi. Hapa ni kula na kuliwa. Nawe mgosi unao unaowalaga. Hivyo, kuliwa kidogo si vibaya ingawa si kama tunavyoliwa.”
Msomi anaamua kurejea ili kuweka mambo sawa. Anasema: “Nadhani wenzangu mnakosea maana ya neno kuliwa. Kimsingi, wanaotumia kodi zetu kutuchezea wanatula hata kama si kama vile mnavyodhani. Kitendo cha kutuletea katiba iliyochakachuliwa kama hakitazuiwa basi ni kujiruhusu kuliwa kulhali na kila mahali. Kuepuka hilo mie napendekeza tuwabane tuwe na sirikali moja badala ya huu utitiri wa walaji.”
“We achia hapo. Eti kuliwa kila mahali! It can’t be me sir.” Anachomekea Kapende huku akichanganya Kiswangilishi kama waheshimiwa wachakachuaji wa katiba.
Mpemba hakupendezwa na pendekezo la serikali moja. Anasema: “Somi hapa unkosea wallahi. Wataka tuwe na sirikali moja halafu sisi Visiwani tumezwe? Sie twataka sirikali zote, yaani mbili na tatu ilimradi msiguse maslahi ya Visiwani.”
Mijjinga aliyekuwa akisoma gazeti la The Mail on Sunday anaamua kupoka mic. Anazoza, “Yakhe hapa sasa wantafuta wallahi. Sie twasema sirikali moja ili kukata ngebe. Kumbe mwenzetu changu kichungu chenu kitamu siyoo? Sasa twasema tena kwa sauti ya juu kuwa twataka sirikali moja na Ugunja na Pembi muwe mikoa kama wengine.”
Kanji aliyekuwa kimya anaamua kula mic: “Dugu yangu hapana gombana. Kaka sisi wote dugu moja, basi ive na sirikali moja. Tapendeza eenh?”
“Kanji usinchokoze. Kama waona sirikali moja mali basi nenda kaunganishe India na Pakistan uone.”
Kijiwe kikiwa kinaanza kunoga si Nesaa mkewe Mgosi akatokea kikataka kuumana na Sofi. Kila mtu alichukua hamsini zake huku tukimuacha Sofi ametoa mimacho kama panya aliyenaswa mtegoni.
Chanzo: Tanzania Daima April 9, 2014.

4 comments:

Anonymous said...

Kwani Nani huyu
Hakuna wa kumshulikia bongo
Hata jina lake halipo kwenye wanted msitupozee muda
Ashughulikiwe mapema kabla hatujalewa
Shoga Mchanga asiyekujwa kuchamba
Ana nini

NN Mhango said...

Anon
Nadhani ujumbe wako umewafikia wahusika. Je shoga mchanga ina maanisha nini?

Anonymous said...

Shoga mchanga Hana hili wala lile
Sadaka ya hitima ijumaa
Bwabwa tena boko boko

NN Mhango said...

Kiswahili chako kigumu sana sijaelewa unachomaanisha.