The Chant of Savant

Wednesday 30 April 2014

Kijiwe kuliambia bunge si kuliombea

          Baada ya kijiwe kusikia baadhi ya wababaishaji, wataka sifa na wachovu eti kuombea bunge la Katiba lililoharibikiwa, kimeamua kukaa na kuwakemea wote waombaji na waombewa.
Mgosi Machungi anaingia na salamu zenyewe, “Wagoshi mmesikia huu ubabaishaji wa wasaka tonge wanaosema eti wamikwenda Dodoma kuombea Bunge la Katiba la ulaji wa dezo? Tate nane. Huyu sasa roho mtakakitu si mtakatifu tena!”
 “Mgosi  usinichekeshe. Eti kulifanya nini Bunge la Mipasho na mitusi?” Anachomekea  Mipawa.
“Kuiombea iache mitusi na mipasho,” Anajibu Mgosi huku akibusu kombe lake la kawaha.
Kapende aliyekuwa anatoka kuongea na bi mkubwa wake ambaye inaonekana wana ugogoro, anakwanyua mic, “Msiwashangae hawa. Kaya imezoea kuombaomba kila kitu.   Huu ndiyo uvivu wa kufikiri.Wanadhani na Subhanna ni kigeugeu kama wafadhili wao wanaowatumia kila wakati? Usishangae  maombi yakageuka sera ya vijidhahabi vya kuchongwa vinavyotafuta ulaji na umaarufu.”
“Nadhani wanaokwenda kuliombea Bunge badala ya kuliambia ukweli mchungu wanapaswa kuambiwa kuwa wao ni sehemu ya tatizo. Kama kuomba ni big deal, hawa waombeaji wa wenzao wanapaswa kuombewa, kama alivyosema mchungaji Msigua, ni wazinzi na si uchumi wa kaya wala wanasiasa. This is outrageously downright nonsensical move to gain some mileage if not money. Hii ni sawa na kuombea uchumi wakati unalala kitanda kimoja na mafisadi na mafisi.” Anangurumu Msomi Mkatatamaa.
Mijjinga aliyekuwa akionyesha wazi alivyo na usongo wa kumwaga pwenti anazoa mic, “Nadhani wanakwenda kuwatoa upepo wasaka ngawira wanaozidi kuchuma njuluku zetu kwa kupiga kelele na mipasho.  Wameona ulaji wakatafuta mbinu ya kuhomola. Bongo hii jameni! Mbona dini nyingi ni biashara. Huoni wachungaji mabilionea kama Rwakatarehe Ka-tortoise na matapeli wengine? Huvuna wasipopanda na kupanda wasipovuna. Hamkumsikia mwenzao Mtetemekea wezi mjengoni?”
Sofia Lion Kanungaembe anatia timu, “Kuomba muhimu vinginevyo muwe wapagani tu. Kuna kosa gani kuliombea Bunge?”
Kanji kama kawa anatia timu kumpa tafu mshirika wake. Anasema, “Sofi ambia yeye. Kama Bunge natukanana Mungu pasa ambia aache tukana tusi kubwa kubwa. Veve ona mtu fyatua tusi kubakuba nyamaza?”
“Tuache utani. Muhimu ni kuwapasha hawa waishiwa kuwa wamezidisha ujinga badala ya kuwaombea. Hivi kuwambia watu waache mipasho na mitusi nako kwahitaji dua jamani?” Mipawa anahoji.
Mpemba aliyeingia akiwa amechelewa anakwanyua mic, “Yakhe mie kama wataka ombewa basi tuombe ushuke moto uwachome wale wote waniotutishia vita ya kimbari, waongo, watukanaji matusi ya maungoni na wanaokula njuluku zetu kwa kufanya kazi ya kutukana ati. Mijitu mizima yageuza midomo makalio ya kutolea ushuzi ashakum tena hadharani bila aibu.”
“Ami umeua. Hakuna nilipoachwa hoi kama kusikia yule bi Hawa wana Ghasia akimwambia jaji Joseph Waryuba kufunga mdomo wake asiangalie domo lake mwenyewe.” Mbwa Mwitu anaamua kula mic. Anakunywa kahawa yake na kuendelea, “Mie nadhani wangepelekwa pale madaktari wa magonjwa ya akili na Takokuru kukamata walioingia mle kifisadi na wale wanaovuta mibangi kama alivyowahi kusema Jobless Nduguy kiongozi wao.”
Msomi aliyekuwa akisoma jarida la Mail on Wednesday anaamua kurejea kumwaga mipwenti. Anakohoa kidogo na kunywa kahawa yake na kusema, “Mbwa Mwitu nakupongeza sana kwa kuwa serious na kutoa pwenti makini. Hakuna ubishi kuwa mambo yanayoendelea pale, licha ya kuzamisha njuluku zetu, yana uendawazimu fulani hata kama yanatendwa na wale wanaoitwa waheshimiwa wanaofanya mambo yasiyostahiki heshima.  Ni bangi hii kushindwa kujua kuwa wachovu wanataka katiba na si matusi wala mipasho. Ni upungufu wa akili kusema eti maoni ya wananchi yadharauliwe kwa kisingizio cha kusema eti Waryuba aliandika mambo yake. Upuuzi mtupu. Kwani alijiteua au ni ujinga unaosumbua watu tena wazima wenye mavyeo makubwa tu?”
Anakohoa na kuendelea, “Wanaokwenda kuombea Bunge hawana lolote zaidi ya njaa na kutafuta connections. Walikuwa wapi wakati mambo yakiharibika?  Kaya haiwezi kuendeshwa kwa maombi. Bunge linapaswa kuambiwa kuwa wachovu wamechoka na usanii na usaka tonge ukiachia mbali mipasho, mitusi na kuvuana nguo. Hakuna wanachonikera hawa wanaojifanya watu wa God kama kutufanya hatunazo. Wanadhani tumesahau kuwa wao ndio waliingiza ukoloni hata utumwa barani mwetu? We need to tell them to go to hell.”
Mijjinga hangoji Msomi amalizie. Anakula mic, “Msomi usemayo ni kweli tupu. Mijitu mipumbavu inakwenda kwenye mahekalu yao na kuhubiri siasa za maangamizi wanaiangalia na kungoja iondoke badala ya kuishushia bakora. Halafu wanakuja na usanii eti wa kuliombea Bunge. Mara ngapi wameomba na hakuna lililotokea. Jibu si maombi bali kuchenchiana. We waache wafanye upuuzi tutawaumbua watakapomaliza hayo maigizo yao ya kusakia ulaji.”
Sofia haridhiki na mawazo haya. Anakwanyua mic, “Mie nasema kuomba lazima mtake mistake halo halo! Tena muache kutukana watu kuwa ni wapumbavu eti kwa kusemea mahekaluni. Kwani kazi ya mahekalu ni nini kama si kuwasiliana na umma?”
“Dada yangu Sofia umeingiliwa na nini? Yaani hata kama ni unazi sikutegemea kama ungeunga mkono huu upuuzi wa kuchanganya dini na siasa dada’angu.” Anasema Mchunguliaji.
“Hata mie namshangaa dada yetu sijui nini kimempata maana huko nyuma hakuwa hivyo.” Anachomekea  Mbwa Mwitu.
“Kanji mbona unatoa macho bila kumuunga mkono mshirika wako Sofi?” Anachokoza Kapende.
“Pende acha mimi. Hapana unga kono kila kitu ya Sofi hata kama napenda yeye.” Kanji anajitetea.
Kabla ya kuendelea, Mbwa Mwitu anachomekea, “Eti unapenda yeye sana? Kama veve penda yeye peleka jamatini.”
“Swahili hairuhusiwi ingia jamatin vinginevyo iwe fagiaji au ongozi au vipi Kanji?” Anachomekea  Mzee Kidevu.
“Kama mimi penda Sofi wewe husu nini? Halo halo! Mbwa hapana changanya siasa na dini hapa. Iko penda hata veve.” Kanji anaamua kuja juu.
Mgosi Machungi anaamua kukatua mic, “Mgosi Kanji emu muombee msamaha mwenzio. Eti unampenda ii umfanyi nini?”
Kabla ya kuendelea Mchunguliaji anadakia, “Amkameruni.”
Kitendo cha Mchunguliaji kusema eti Kanji amkameruni Mbwa Mwitu kimezusha mtafaruko hadi watu kutaka kushikana mikono. Kuona hivyo, kila mmoja anajikata kivyake kuepuka ndata kuja kutubambikizia kesi.
Chanzo:  Tanzania Daima Aprili 30, 2014.

2 comments:

Anonymous said...

Asante tumekupata hapo tena hawa hao makasisi ndiyo chanzo kuwapumbaza wananchi kuingiza mkenge kuendeleza hii symbiotic relationship!

Ndugu Nkwazi N Mhango said...

Anon,
Tunashukuru kwa kuliona hili. Nadhani hao makasisi nao wameipata na huenda watalifanyia kazi hata kama hawatajibu hapa. Tuendelee kuwaandama angalau historia siku moja itusafishe kuwa hatukukaa kando na kuwa watazmaji.