The Chant of Savant

Wednesday 23 April 2014

Kijiwe kumchukulia hatua Lukuviii

BAADA ya Waziri Bill Lukuviii kutangaza mapinduzi dhidi ya mamlaka ya wachovu, kijiwe kimekaa kama kamati kumpa vipande vyake pamoja na kumtaka bosi wake amwajibishe kabla wana kijiwe hawajamtokea na vikombe vya kahawa na kumwacha na ngeu.
Wa kwanza leo kuingia ni Kapende. Leo kauramba kweli kweli. Alivyochomekea suruali yake utadhani matapeli wa Kikongo ambao kila ukutanaye naye ni mwanamuziki. Utasikia anasema: “Moi, je suis musicien et nakobina ndombolo.”
Mara Mgosi Machungi anaingia akiwa anavuta tasbihi yake. Anasema: “Mmemsikia  huyu mpuuuuziiii anayetaka kututishia nyau akitetea upuuzi wao?”
Kapende anachomekea: “Unaongelea huyu kihiyo aliyeghushi vyeti vya taaluma Bill Lukuviii? Sijui kwanini Njaa Kaya naye anamng’ang’ania pamoja na kupokea tuhuma zake? Nasikia jamaa kaenda kuropokea kanisani asijue anachanganya dini na siasa.”
“Nani amtimue nani iwapo wote wamoja?” Anachomekea Mijjinga aliyekuwa akibofya kisimu chake.
“Huwezi kwenda madhabahuni ukafanya uhuni ukaachwa. Kana ni nsikitini watu wanramba bakora huyu. Mwasema tusichanganye siasa na dini wakati nyie mwazichanganya na kuzidhalilisha dini?” anachomekea Mpemba.
Mipawa anakwanyua mic. “Huyu wala hana dini na kama anayo basi ni kujikomba na kughushi. Anadhani mazabe yake hayafahamiki? Ashukuru Mungu Njaa Kaya anamlinda kwa sababu ajuazo. Jitu limekimbia umande halafu linatangaza ukihiyo wake bila hata aibu. Ficheni ujinga wenu na kuonyesha busara jamanini.”
Sofi Lion aka Kanungaembe kaguswa pabaya. Anadandia mic.“Mie sioni makosa ya Bill hasa ikizingatiwa kuwa kuna watu wanahubiri shari. Hivi hamkumbuki yaliyotokea Rwanda jamani?”
Kanji kama ada hawezi kutomtetea mshirika wake. Anadungua mic. “Ile tokea Rwanda hapana tokea hapa. Sisi iko country ya amani bana. Ile yote nataka leta vita hapana jua baya ya vita.”
Kapende anatia tena timu. “Kanji kamwambie kada mwenzako Lukuviii kuwa hatudanganyiki wala kutishika. Vita ataileta yeye anayetaka kupindua sirikali yake mwenyewe.”
Msomi aliyekuwa kimya wakati wote anaamua kuingilia kati. “Waheshimiwa, sioni uhusiano na mauaji ya kimbari ya Rwanda ambayo Bi. Sofi anataka kututisha nayo. Nadhani mauaji ya Rwanda yalisababishwa na utawala kama huu wa akina Lukuviii, unashikilia usanii na visingizio badala ya kuangalia ukweli. This guy must be told to his face that he is a goon. How dare he compare Rwanda and us?”
Mbwamwitu anaamua kuingiza utani wake. “Nasikia Rwanda walighushi sana kama Lukuviii kiasi cha kujisahau kuwa yana mwisho. Kwanza, wanaotaka kutumia yaliyotokea Rwanda hapa wanapaswa kuambiwa wakaombe na wakaiombe Rwanda msamaha kabla haijawashukia.” Kijiwe hakina mbavu.
Mgosi aliyekuwa akiongea kwenye simu na bi mkubwa wake, tena kwa kupaza sauti kutokana na kutomuachia uchache wa mboga anaamua kutia guu. “Huyu Ukuvi hana adabu na anapaswa ashike adabu kabua ya kumshikisha adabu. Ana bahati. Angesema huu upupu na utumbo wake wakati wa Mchonga si angefikia lupango.”
“Pamoja na kuchonga kwenye kilongalonga ulikuwa unayanyaka maongezi yetu siyo?” Anatania Mchunguliaji.
Mpemba wala hangoji Mgosi ajibu. Anakwanyua mic. “Yakhe mie anshangaza huyu kilaza wallahi. Hivi kama serikali mbili hazikuleta vita pamoja na ufisadi huu wote, tatu zitaletaje vita?”
Mipawa naye anakula mic. “Ami nadhani useme wazi kuwa tuwe na sirikali moja ili kuepuka huu wizi na usanii tunaofanyiwa mchana kweupe. Mie naona wote wanatuchanganya, wawe wa sirikali mbili au tatu. Kwanini wanaogopa sirikali moja ambayo itaondoa ngoa na fitina na ngebe?”
Mpemba anamkata Mipawa jicho la chuki na kukwanyua mic. “Si Visiwani twapinga sirikali moja. Twataka tatu ili tusimezwe.”
Mipawa anafyatua swali la haraka haraka. “Nyie mkitumeza sawa. Kwanini nasi tusiwameze japo kidogo?”
“Yakhe sasa naawe wageuka Lukuviii wallahi. Sie twawameza vipi?” Mpemba anajaribu kujitetea.
Mipawa anazidi kumsonga Mpemba kwa kusema: “Hujui siyo? Kwani huo wali mnaomeza na kuja kutanua huku wakati sie tukienda kwenu mnatusingizia kila jinai huoni? Tukiacha uvivu wa kufikiri na ujanja ujanja, nyie mmetumeza sana. Kwenye kila pembe kuanzia sirikalini hadi mitaani mpo, lakini sisi hatupo kwenu.”
Msomi kuona jinsi ambavyo mambo yanaanza kwenda ndiyo siyo, anaamua kuokoa jahazi. Anakohoa kidogo na kusema: “Naona sasa tunaelekea kubaya. Hakuna haja ya kuanza kubaguana tokana na tunakotoka. Kukata mzizi wa fitina nami nakubaliana na sirikali moja. Maana itaondoa migongano, matumizi mabaya, kutuhumiana, kutumiana na kunyonyana na kuburuzana. Husikii watu wa Kigoma au Lushoto wakilalamikia watu wa Dar au Moshi wala Arusha.”
Anakunywa kahawa yake na kuendelea: “Turejee kwa huyu Lukuviii anayetaka kupotosha umma. Kama kuna vita inakuja basi watakaoisababisha ni wale wanaotaka kutuhadaa, kututisha na kutuburuza kama akina Lukuviii na genge lake la walaji waliofilisika kulhali. Wachovu hawawezi kutoa mapendekezo yao halafu ukaanza kuwatisha. Kwani hii katiba ni ya watawala au watawaliwa?”
“Nadhani anachosema Msomi ni cha kuungwa mkono. Hawa wanaodhani kuwa wataendelea kututishia nyau na kutuburuza ili watuibie wapaswa wajue mambo yamebadilika.”
“Nyie hamjui. Jamaa wanaogopa kuondolewa kwenye ulaji na siri zao kufichuka wakaishia lupango kutokana na wizi waliotufanyia.” Anachomekea Kapende.
“Haki ya Mungu titakuja kutoa mtu roho. Imetiibia miaka yote. Inazani sisi ni wapumbavu kama huyu Ukuvi siyo?” Mgosi anaamua kuzoza kwa hasira.
Mbwa Mwitu anaamua kuchomekea. “Kesho utasikia na kilaza na kihiyo kama huyu eti kapewa tuzo ya utendaji bora wakati ni balaa kwa kaya yetu. Natamani niende huko Dodoma na kuliramba bakora. Sijui ni kwanini wale mabingwa matusi toka Zenj hawakulirushia matusi ya nguoni lilipoanza kuropa?”
“Kaka usinikumbushe wana mipasho na mabingwa wa kufyatua matusi kama yule mama aliyemwambia mwenzie kuwa kashaufyatua sana hadi kazaa watoto watatu.” Anasema Mzee Maneno.
“Kesha ufyatua nini?” Anauliza Mbwa Mwitu.
Mzee Maneno anajibu: “Kamuulize mwenyewe maana mambo mengine yataka uwe fyatu kweli kuyatamka hadharani.”
Kijiwe kikiwa kinanoga si likapita shumbwengu la Lukuviii. Wacha tulifukuze huku tukilitukana matusi ya kizenj. Bahati yake dereva wake aliwahi, vinginevyo tungemtia adabu.
Chanzo: Tanzania Daima Aprili 23, 2014.

2 comments:

Jaribu said...

Toka Lukuvi awe mmoja wa mawaziri wa kwanza kwenda kupata kikombe cha babu, nimekuwa nimemdharau; na hapo nilikuwa hata sijui CV yake.

Lakini Kikwete ndio anaowapenda hao vihiyo wenzake. Hataki kuwa "upstaged" na watu wenye akili timamu.

Ndugu Nkwazi N Mhango said...

Jaribu kumbuka hawa jamaa wengi wao ni waathirika wanaohesabu siku tokana na kutokuwa na la kufanya bali ngono kuazia wanazopata kirushwa na wanazonunua. Hukusoma habari kuwa kwa sasa vyangudoa wametia kambi Dodoma ili kugawana mshiko na wezi wa mabunge yote mawili. Ulitegemea kwa kihiyo kama Lkuvi afanye nini wakati hamnazo?