NDUGU rais,
Kwanza samahani kwa kukuita ndugu badala ya mheshimiwa. Binafsi nachukia cheo cha mheshimiwa kutokana na ukweli kuwa siku hizi kinatumiwa na watu wasiostahili heshima hata chembe.
Heshima gani inaweza kupatikana kwa kulazimishwa na sheria? Pia sitakuita Dokta kama ambavyo mavuvuzela wengi wanapenda kukuvisha kilemba cha ukoka. Hii ni kutokana na kuchukia shahada hii ambayo siku hizi imeishiwa heshima kiasi cha kila mtu kujiita dokta. Nadhani unawakumbuka mawaziri wako ambao wengi wao wana hizo PhD lakini feki.
Kilichonisukuma kuandika barua hii ya kwanza kwako ni habari kuwa una mpango wa kuvunja na kusuka upya baraza la mawaziri. Kama Mtanzania yeyote ninaamini kuwa ni haki yangu kukushauri hasa ikizingatiwa kuwa huwa nakuheshimu kuliko binadamu yeyote hata wazazi wangu.
Mie ni shabiki na kipenzi chako ambaye sifanyi hivyo kama wale waliotajwa na Jimmy Millya kuwa wanaishi kwa matumaini na kujipendekeza ili wapate ukuu wa wilaya au mkoa kama si kuishia ukatibu kwenye ofisi za wilaya na mikoa.
Najua kuwa unajua kuwa wapo wengi chamani mwako wakijikomba na kuzusha hili na lile ili wapate ulaji hasa ukuu wa wilaya au mkoa. Wala mimi sikupendi na kukuheshimu ili niteuliwe balozi wala waziri. Hivyo, nitakayosema ni ya msingi na kweli kuliko ya waramba viatu na watafuta madaraka.
Taarifa za hivi karibuni ni kwamba chama chako kimeridhia shinikizo la wabunge kuwa uvunje baraza la mawaziri ambalo limejaa mchwa wanaotafuna pesa za umma.
Siwaiti mawaziri wako mchwa. Waliowaita hivyo ni wabunge wala si mimi wala wapinzani. Hivyo, lengo la kwanza la waraka huu ni kukutaka uhakikishe mchwa hawarejeshwi kwenye baraza lako la mawaziri.
Pili napenda kukushauri kuwa mawaziri wanaopaswa kuwajibishwa siyo tu wale wanaoguswa na kashfa iliyotokana na ripoti ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG). Napendekeza hata wale wote waliotuhumiwa kwa kashfa mbali mbali kama vile kughushi vyeti vya kitaaluma, uzinzi, kumilki silaha za kivita na kuzitumia vibaya, kumiliki mali nyingi kuliko stahiki yako uhakikishe hawarudi. Pia nashauri usibadilishe chupa na kutuletea mvinyo chakavu ule ule. Naamini unajua nimaanishacho.
Pia ndugu rais, nashauri upunguze ukubwa wa baraza la mawaziri hasa wakati huu ambapo uchumi wetu uko ICU.
Ndugu rais, Najua wewe ni kipenzi na chaguo la watu. Kweli unapenda watu hata kufikia mahali kuambiwa una huruma sana. Huruma nayo ikizidi sana uharibu mtoto. Hivyo, ndugu rais, hakikisha wabovu wote wanaachia ngazi bila kujali huruma wala nini. Wahenga walisema: Ukitaka kumuua nyani usimwangalie usoni. Kadhalika, nawe usiangalie nyani wala mchwa usoni.
Ndugu rais, Kwa vile wewe ni kipenzi cha watu, naamini u kipenzi cha wengi na si wachache kama ambavyo inaonekana sasa hasa watu wanapogeuza nchi kuwa shamba la bibi huku watu wake wakigeuzwa mataahira wasioona wala kusikia. Hebu nikupe mfano.
Hivi karibuni waziri wako kijana, Ezekiel Maige amedaiwa kununua hekalu kwa dola 700,000. Naamini hata wewe huna wala huna haja ya kuishi kwenye hekalu kama lile wakati watu wanaendelea kuteketea kwa umaskini wa kusababishiwa na waroho wachache kama huyo waziri tajwa.
Watu wa namna hii hawapaswi kuachia ngazi tu bali kufikishwa mahakamani na kutaifishwa mali zao. Ndugu rais, hapa lazima niseme. Chanzo cha ujambazi huu wa wakubwa na familia zao ni kuua maadili ya uongozi na kuingiza madili ya uongozi.
Sikulaumu ila nakushauri uliangalie hili sana ili nchi yetu isijikute pabaya kutokana na baadhi ya watu wanaojiona wateule kuwatumia walio wengi kujineemesha.
Ndugu rais, watu wako ima kwa kukuogopa, kubembeleza kitumbua au kujikomba hawakwambii ukweli. Wanaogopa utachukia hata wengine kuwawajibisha. Mie naongea toka nje ya mtandao wako. Ukweli ni kwamba kwa sasa hupendwi kama ulivyochaguliwa. Hii ni kutokana na walio karibu nawe kukudanganya na kukutumia kujineemesha.
Kwa mfano, walio wengi nawasikia mitaani wakilalamika kuwa NGO ya WAMA nayo ni chaka la ufisadi. Maana wanajiuliza inakuwaje aanzishe NGO baada ya wewe kuwa rais kama ilivyokuwa kwa mtangulizi wako ambaye mkewe anaendelea kuandamwa na kashfa za ufisadi kila uchao.
Nisingetaka haya yakukute utakapokuwa umeondoka madarakani. Nayasema haya kwa mapenzi makubwa. Niko tayari hata kuuawa kwa kukueleza ukweli ili hapo baadaye ukweli wangu ukuweke huru.
Ndugu rais, kitu kingine ambacho nakisikia mara kwa mara kwenye daladala, baa hata harusini ni kwamba wewe unapenda sana kusafiri nje kiasi cha watu kuamini kuwa unatumia pesa nyingi. Hivyo, kusababisha matatizo yao.
Hili likichangiwa na ukubwa wa serikali yako, limefanya watu wakuite majina ya ajabu ajabu. Pia nilisikia juzi watu wakisema kuwa ukienda ughaibuni huwa hutaji wale unaoandamana nao. Hii ni kinyume ingawa si kosa lako bali wasaidizi wako.
Kama nilivyokwishaeleza hapo juu ndugu rais, wewe ni kipenzi cha watu ingawa kwa sasa uko mbali na watu na ndiyo maana hujui wanayokusema. Nimesikia si mara moja wala mbili kwa masikio yangu kuwa kwa sasa umekuwa mbali na watu ingawa unasifika kwa kuwapenda sana kiasi cha kutumia hata muda wako adimu kuhudhuria mazishi ya wapendwa wao.
Wananchi wanasema hii haitoshi na si muhimu kama kuhudhuria matatizo yanayosababisha hata saa nyingine vifo vya wapendwa wao. Nakumbuka wakati wa mgomo wa madaktari ulipokwenda Davos. Wengi walisema mengi kuwa ulikimbia matatizo.
Hata juzi kwenye sakata la kutaka mawaziri wako wajiuzulu ulipokuwa Brazil, wengi walisema kuwa ulikuwa umekimbia majukumu kwa vile ule mkutano ulikuwa wa mawaziri.
Mimi siamini hivyo ingawa nakubaliana na wakosoaji kuwa unapaswa kuwa karibu na watu ili ujue matatizo yao na kuyatatua.
Naona nafasi haitoshi. Hivyo, kwa taadhima na mapenzi ya hali ya juu na unyenyekevu wa aina yake naishia hapa hadi hapo nipatapo fursa nitakuandikia tena kama kuna baya nitakalosikia. Nakutakia kazi na utekelezaji mwema wa hayo.
Chanzo: Tanzania Daima Mei 2, 2012.
No comments:
Post a Comment