AADA ya kuwepo malalamiko mengi sana kutoka kwa wanakijiwe kuwa
mwenyekiti nawafuga wanyonyaji marafiki na washikaji zangu kwa
kuwazawadia ukuu wa kijiwe wa mkoa na wilaya, tumeamua kukata mzizi wa
fitina.
Tumefutilia mbali vyeo na ulaji wa wakuu wa kijiwe wa wilaya na
mikoa ambao kweli walikuwa wanyonyaji niliowalipa fadhila kwa
kuhakikisha kila uchaguzi wa kijiwe napeta.
Nilijua hili ingawa sikutaka kujionyesha kutokana na kuwa fursa nzuri ya kuwahifadhi washikaji na washirika zangu.
Hivyo, taarifa rasmi tunayotoa ni kwamba kuanzia sasa hapatakuwa na vyeo vya mkuu wa wilaya na mkoa wa kijiwe.
Kila kijiwe kwenye ngazi ya wilaya na mkoa kitaendesha mambo yake
kijuavyo na kitakavyo mradi kisifanye ufisadi hadi CAGI aje kuwaumbua
kama ilivyotokea kwa jamaa fulani hadi wakatimuana huku wengine wakilia
kama vichanga kwa kuukosa ulaji.
Meku Sirilo Chaaami upo hapo? Maana huu ulikuwa wizi uliokuwa
umehalalishwa. Hivyo walevi wote mikoani na wilayani watakuwa
wakijifanyia mambo yao bila kulisha wanyonyaji fulani waliokuwa na
connection na mwenyekiti yaani mimi Dk. Mzee mzima Mpayukaji Msemahovyo
wa Nkwazi wa Mhango wa Waambie Walioko juu ili wa chini wasikie.
Hivyo, tuelewane na kukubaliana. Kwa maana nyingine ni kwamba
walevi wametangaza ukombozi na kukata mikatale ya kunyonywa na kikundi
cha watu. Nashukuru sana kunusurika. Maana walevi walikuwa wamepania
kuning’oa kwenye ulaji kama nisingewatoa sadaka washikaji zangu husika.
Nilichukia nusu ya kunyotoa mtu roho lakini ningefanyaje iwapo
wenye mali walikuwa wameamua baada ya kushtukia uteuzi wangu? Hata
hivyo haikuwa kazi rahisi. Maana zali lilipoanza niliamua kujirusha kwa
kufanya ziara nchini Brazil kwenda kuona walevi wa kule wanavyokunywa
kahawa. Nilishawapa taarifa ya matanuzi yangu na shosti wangu huko
kwenye nchi ya soka na samba.
Walevi waligundua kuwa wengi wa wateule wangu walikuwa ama marafiki
zangu wa mke wangu au watoto wangu ambao kusema ukweli walikuwa
wakinitumia kuwasukia ulaji washikaji na washirika wao.
Pia waligundua kuwa kumbe sisi ndiyo tulikuwa chanzo cha umaskini
na mateso yao! Kituko ni kwamba wengi hawakuwa na sifa za kuwa wakuu wa
vijiwe ingawa niliwapa ulaji kwa vigezo ambavyo nilivijua mwenyewe bi
mkubwa na vitegemezi vyangu.
Pia nilikuwa nikitumia fursa hii kuwapa ulaji walamba viatu wangu
hasa makanjanja walevi waliokuwa wakijipendekeza na kufanya kazi zangu
chafu ukiachilia mbali nyumba zangu ndogo.
Pia watoto wa wakubwa zangu kama vile Mgosi Machungi, Mipawa, mzee
Maneno na Kidevu nao niliwapa ulaji ili waendelee kuneemeka wao na
familia na koo zao kwa mgongo wa walevi.
Juzi nilimtangazia bi mkubwa kuwa mashoga zake na ndugu zake
niliokuwa nimewajaza kwenye ulaji wa wilaya na mikoa wanapaswa walie tu
kwa vile wenye mali wameshtuka sina jinsi ya kuwabeba. Hivyo chini ya
mfumo mpya wa Uhujumaa na Kujimegea hawa wamepigwa panga.
Wakitaka kusavaivu basi wakauze bwimbwi au kusafirisha kahawa nje ya kijiwe.
Kweli cha mlevi huliwa na mgema wahenga walisema. Ila walevi
wakishtuka humkopa mgema hata kunywa wakakataa kulipa ukiachia mbali
kumshtaki kwa ndata iwapo mgema mwenyewe ni mgema gongo.
Mwanzoni wakati mimi na washikaji zangu tukifanya huu usanii
hatukujua kuwa walevi wangeshtuka. Hakuna mtu alilia kama rafiki yangu
Muongo Rweye aliyepoteza ulaji kwenye kijiwe cha wilaya na Ugosini.
Jamaa pamoja na kujidhalilisha kwa ajili yangu kwa miaka, jamaa
wameamua kummwaga manonihino baada ya mimi kumkumbuka mtwana wangu
mtiifu zaidi hata ya mbwa.
Hakuna kitu kilinikera kama matamshi ya Msomimkatatamaa aliyedai
kuwa washikaji zangu waliokuwa wakinisaidia kuongoza vijiwe wilayani na
mikoani ni sawa na kupe. Eti alisema eti walevi ni ng’ombe na wateule
wangu walikuwa kupe wanaonyonya damu ya hawa ng’ombe tena waliokondeana!
Wakati wakubwa wenzangu wa kaya wameamua kupanua genge la walaji
wao, mie nimevunja langu baada ya wanakijiwe kunijia juu. Nadhani hili
litakuwa somo kwa walevi kuwashughulikia wakubwa zao na kuwazuia
kuendelea kuwatumia kama punda au the beast of burden kama ilivyo sasa.
Nisionekane nafanya uchochezi, acha niwaachie wahusika wajipime na
kuamua wenyewe. Maana waliogeuzwa hayawani na mataahira ni wao na si
mimi. Deontologically even teleontologically, they need to do
something. They should forget political tradeoffs. Lol! Nimejisahau na
kumwaga ung’eng’e! Nisameheni ni hasira tu zinazonichochea kumwaga
ung’eng’e huu.
Naona mzee Kidevu alishaanza kuinua kibendera kwa kuona nazidi
kupuyanga na utasha asijue ni mihasira ya kukosa pa kuwaficha na
kuwahifadhi washirika zetu. Hata hivyo, sikuzidiwa kete zote. Maana
bado niliweza kuwateua watoto wa marafiki zangu kushika nafasi nyingine
nyeti kijiweni.
Hamjamuona mtoto wa swahiba yangu Mgosi Machungi wa Makambale
akitesa kama hana akili nzuri? Hamumuoni daktari Hoseini anavyotesa
kama hana akili nzuri? Sisi wasanii ni wajanja siku zote inapokuwa
kwenye kuonyesha mazingaombwe yetu wakati tunapopambana na ombwe la
ulaji.
Muhula huu nina kazi kweli kweli. Nina kibarua cha kuandika Katiba
mpya ya kijiwe. Kazi inayonikabili ni kuhakikisha inaandikwa Katiba
ambayo itatulinda mimi, shosti zangu na vitegemezi vyetu kutokana na
mazabe tunayoendelea kuyafanya.
Bila kufanya hivyo kuna siku walevi wanaweza kunigadafi kama siyo
kunimbaraaka kama jamaa zangu wa kule Maghreb. Ingawa nimelazimika
kuwateua kina Msomimkatatamaa kuandika Katiba, sina raha na watu hawa.
Maana wanaweza kunibadilishia kibao nikajikuta nanyea debe bila sababu.
Hata hivyo, time will tell.
Kwa vile bado nimeshikilia usukani, lazima nipambane kuhakikisha
nikistaafu sipewi namba lupango. Naona dege lenye mafua la rafiki yangu
Njaa Kaya linakaribia kutua likitokea Aids ya Baba. Acha niwahi kumlaki
ili animegee mbinu ya ku-survive.
No comments:
Post a Comment