Uteuzi wa Ladislaus Komba ambaye
anatuhumiwa wazi wazi kujihusisha na uhujumu na ufisadi katika wizara ya
Maliasili na utalii hasa kusafirishwa kwa wanyama 130 kupitia uwanja wa
ndege wa kimataifa wa Kilimanjaro ni aibu kwa taifa na aliyemteua.
Kashfa hii ilivuma sana huku
ikiwahusisha watendaji wakuu wa wizara ya Maliasili na Utalii hasa waziri
Ezekiel Maige na katibu wake mkuu Komba. Kamati ya Bunge ya Ardhi, Maliasili na
Mazingira ilizidi kupigilia msumari kwenye tuhuma hizo kwa kushauri wahusika
wawajibishwe. Taarifa iliyotolewa na mwenyekiti wa kamati James
Lembeli ilisema kuwa usafirishaji wanyama nje bila kufuata
taratibu uliifanya kamati kupendekeza Bunge liiagize serikali
kuwachukulia hatua kali za kinidhamu, aliyekuwa Katibu Mkuu wa Wizara ya
Maliasili na Utalii, Ladislaus Komba, na wale wote waliohusika na utoaji wa
vibali vya kusafirisha wanyama.
Inashangaza kuona kuwa pamoja na
shutuma zote hizo, rais Jakaya Kikwete alipuuzia hata kamati ya bunge na kumteua
mtuhumiwa kuwa balozi wa Tanzania nchini Uganda. Mtuhumiwa kama huyu anaweza
kuiwakilisha nchi kwa maslahi kweli? Je kwanini rais aliamua kumteua haraka bila
hata kungoja tume ya Bunge imalize kazi yake? Je kuna namna rais au hata watu
wake walihusika na utoroshaji wa wanyama pamoja na ufisadi mwingine unaodaiwa
kutendwa na wahusika? Hakuna kitu kinakatisha tamaa kama maneno
yaliyosemwa na mchungaji Peter Msigwa hivi karibuni bungeni aliyekaririwa
akisema, “Kule KIA (Kilimanjaro International Airport) vijana wanalalamika kuwa
kuna baadhi ya watu wanaokuja kugongewa passport zao huku wenyewe wakiwa kwenye
ndege.” Je hawa ni akina nani kama siyo wauza unga hata magaidi?
Je rais ana nini na waharifu kama hawa? Si afadhali achague moja kati ya
wananchi na hao wafanya biashara za utajiri wa haraka. Kwa nchi yenye uongozi
wenye kujua unachofanya maneno ya Mbunge yangefanyiwa kazi siku hiyo hiyo. Maana
ni ushahidi wa kuwapo tishio kwa usalama wa taifa. Je kama hao wanaogengeshewa
mihuri wakiwa kwenye ndege kinyume cha sheria wanaachwa tumueleweje rais? Nini
kazi ya genge la usalama wa taifa? Kama ni hivyo hakuna haja ya kuwa na watu
kwenye viwanja vya ndege wala mipakani ili ijulikane kuwa hii ni No Man’s Land.
Au hao nao wamebinafsishiwa uhuru wa Tanzania? Hivi rais anategemea wajukuu zake
wataishije kwa uchafu huu anaoendelea kuuvumilia asitumie mamlaka
aliyopewa?
Kuhusu yanayoendelea kwenye utoroshaji
wa wanyama Lembeli alikaririwa akisema, “Kamati ya Bunge inapendekeza kwamba
Bunge liitake serikali kumwajibisha Waziri wa Maliasili na Utalii, Ezekiel
Maige, kwa kutengeneza mazingira ya rushwa ikiwa ni pamoja na kuyanyang’anya
makampuni 16 vitalu vilivyogawiwa,”
Ajabu wakati kamati ya Bunge
ikipendekeza waziri husika awajibishwe, rais ameendelea kukaa kimya. Ili iweje
na kwanini kama hana maslahi na uoza huu?
Hapa tunaongelea watu wawili. Bado
kuna wengine wengi ambao bunge limetaka wawajibishwe lakini rais ameendelea
kulidharau bunge. Je kwanini wabunge wasiachane na siasa chafu za kulindana na
kumshughulikia rais kama nao hawaridhiki au kushiriki uchafu huu? Kama kamati ya
bunge inatoa mapendekezo yasitekelezwe maana yake ni kwamba bunge halina maana
hata sababu ya kuwepo huku wabunge wanaowakilisha wananchi wakizidi kuonekana
kama vikaragosi mbele ya mawaziri na makatibu wa wizara kama ilivyotokea kwa
Komba.
Watu wenye mapenzi na taifa letu
wanashangaa jinsi ambavyo Kikwete ameendelea kuwa mlinzi na muhimili wa watu
wanaojulikana wazi kutokuwa na udhu wa kukaa kwenye ofisi za umma.
Hivi kwa mfano waziri wa nishati na
madini na naibu wake wanangoja nini wakati wameishavuruga kwa viwango vyote?
Rais ana faida gani na watu hawa?
Hivi mawaziri wanaojulikana kwa mfano
kughushi vyeti vya taaluma wanangoja nini kwenye ofisi za umma wakati ni
waharifu wa kawaida kwa vile hawakutaka kukanusha madai yaliyotolewa dhidi yao?
Ingawa Kikwete amekuwa akijigamba kuwa serikali yake si ya ubia, ukitazama
vizuri madudu anayoendelea kuyakingia kifua, unagundua kuwa kuna watu wana hisa
kubwa kwenye serikali ya Kikwete.
Ukisoma ripoti ya Mdhibiti na Mkaguzi
mkuu wa fedha za serikali (CAG) unapata kichefuchefu na kujiuliza nini kazi ya
serikali hasa rais. Kwa mfano kwenye ripoti ya hivi karibuni iliitaja tena
familia ya rais mstaafu Benjamin Mkapa kuwa mkewe aliuza majumba ya Msimbazi
kinyume cha sheria. Ukiuliza kwanini Mkapa hachukuliwi hatua
kutokana na ufisadi wa wazi aliotenda unaambiwa ana kinga. Unazidi kushangaa ni
kwanini kinga ya Mkapa inakuwa yake, mkewe, wanae, wakweze hata marafiki zake?
Kwa hali ilivyo, nchi yetu inaanza
kuonekana kama nchi ya vibaka ambapo mtu akiiba anazawadiwa kama ilivyotokea kwa
Komba aliyeteuliwa balozi au Edward Lowassa aliyevurunda akazawadiwa marupurupu
ya ustaafu wakati hakustaafu. Je namna hii rais wetu hajawa chanzo cha mauti
yetu? Ajabu ni rais huyu huyu anayewanyamazia washirika wake anayelalamika kuwa
serikali haina pesa. Anataka pesa ipi iwapo watendaji wake mawizarani, serikali
za mitaa na kila taasisi wanaguguna kila kitu huku naye akichekelea na
kuwalinda? Hakuna maneno mabovu aliyowahi kutoa Kikwete kama aliyotoa
alipoulizwa swali juu ya kumshughulikia Mkapa akiwa nchini Sweden na kusema eti
wamuache mzee Mkapa ajipumzikie. Wengi walishindwa kuelewa Ni kwanini rais wao
ni mgumu kushughulikia ufisadi kiasi hiki kama hana faida na huo ufisadi. Kwa
tabia yake ya kuwalinda wanaotuhumiwa kwa uharifu Kikwete na wenzake
wametukamata mateka kiasi cha kutufanya tuendelee kuwa maskini wakati watu
wachache wakitajirika kwa kutuubia. Kunogesha ngoma, Kikwete kaendelea kuwateua
hata mawaziri uozo wanaojulikana kwa kashfa mbali kuanzia kughushi vyeti vya
taaluma na upuuzi mwingine. Je nani atamkabili Kikwete na kumwambia
imetosha?
Chanzo: Tanzania Daima Mei 9, 2012.
No comments:
Post a Comment