BAADA ya vyombo vya habari kuanika wazi ukwasi wa waziri wa wanyama na mali za siri Heze Maige, Mpayukaji napanga kwenda kuomba kazi ya ulinzi kwenye hekalu lake angalau nionje raha ya viyoyozi nilivyoona vimelitona hilo hekalu.
Hakuna kitu kimewahi kunistua kama utajiri wa jamaa huyu kijana tena ambaye bado hata maziwa hayajakauka mdomoni. Mie pamoja na miaka yangu sabini na ushei sifikirii kununua hekalu kama lile waliyosema jamaa alinunua tena kwa pesa ngumu.
Hata tukichanga na ukoo wangu wote na wa mgosi Machungi hatuwezi kununua hata choo ya hekalu lile ambalo mie naona lingeitwa Taj Mahar ya Danganyika. Je, haya ndiyo maisha bora waliyotuahidi wakaishia kujipa wao wenyewe wakati sisi tukizidi kuteketezwa na ulofa?
Ama kweli wamejua kututenda. Yaani watu wazima wanatudanganya kuwa tuwape kura za kula nao watupe maisha bora kwa wote kumbe maisha yenyewe ni kwa wao wote bila sisi! Hakika nimelewa.
Katika ujinga wangu wa kizee nilijaribu kufanya mahesabu ya haraka haraka kuona kama kibarua kinaweza kununua hekalu kama lile. Ili kuweza kununua hekalu la Bwana Maige ni kwamba unapaswa kufanya kazi kwa miaka 35 ukiwa unalipwa shilingi 2,666,666.67 kwa mwezi bila kutumia hata senti. Je, nani anaweza kufanya hivyo?
Kwa umri wa ndugu yangu Nkwingwa ni kwamba amefanya kazi si chini ya miaka 10. Hii maana yake ni kwamba alikuwa akilipwa mshahara wa si chini ya milioni kumi na ushei ili kuweza kununua hekalu lake kihalali.
Je, hapa nani anamdanganya nani na kwanini? Je, ndugu zangu wa TAKUKURU hapa wana kisingizio gani cha kushindwa kumchukulia hatua huyu jamaa yetu ambaye ni fisadi moja kwa moja? Je, kama ghetto ni mabilioni kama hayo, akaunti yake ina vijisenti kiasi gani? Je, hizo mali nyingine nazo?
Kwa vile TAKUKURU wanaonekana kuwa kwenye pochi yake, mie namtaarifu kuwa nitakula naye sahani moja iwe kwa uadui au urafiki. Hivyo napendekeza awe rafiki yangu ili anipe siri ya mafanikio yake kabla sijampiga juju. Tena ajue mie juju langu si huu upuuzi wa Nigeria au Sumbawanga. Mie namtwanga zongo na akinishinda hapa namlisha mamba popote atakapokuwa.
Pia lazima anitajie washirika zake nao niwatoe upepo as soon as convenient kabla wengine hawajawawahi hasa jamaa zangu wa TAKUKURU.
Pia namtaarifu ngosha aniombe msamaha kwa usumbufu niliopata toka kwa bi mkubwa wangu. Hakuna kitu kiliniuma kama bi mkubwa wangu kutishia kwenda kuolewa na Maige kwa vile anatoka kwenye kabila ambako lazima uwe na nyumba ndiyo uwe mwanaume.
Kwa vile Bwana Maige ni ndugu yangu na swahiba wangu mtarajiwa, hivi na uteke wake ana mifweza kama hiyo hao kina Mustaafu Mkulu, Pesatatu Mrambaramba, Dan son of Jonah, Anna Tamaa Makapi, Abdi Kigodoka na mafisadi wengine wakubwa wakubwa wana njuluku kiasi gani?
Kwa vile ninataka kuukata kama Bwana Maige, lazima nianze kupeleleza mahekalu yote ya Masaki, Oyesterbay, Mikocheni, Kunduchi, Salasala, Bwagamoyo na kwingineko kujua ni ya akina waziri au aliyekuwa waziri gani ili niwatoe chochote kitu kabla wengine hawajawawahi.
Mijamaa ina mahekalu makali kuliko hata watoto wa Gaddafi! Hii ni kufuru jamani tena ni kuwatia midole kwenye mimacho makapuku wanaokufa kwa kukosa asprin. Hivi kweli kuna dhambi kama hii chini ya jua?
Wiki hii lazima nipige safari kwenda zangu Kahama kuona miradi mingine ya huyu jamaa ili nikija kumbana kijulikane. Siamini kama jamaa anategemea siasa tu kama si fisadi basi jamaa anauza nonino huyu. Duh Maige au nawe utasema hiki ni kijibanda na ulivyotumia ni vijisenti?
Ila jamani eleweni kuna siku tutakuja kuchenjiana. Maana ukila na kipofu usimshike mkono. Juzi mmeuza wanyama wetu tumenyamaza. Mara mnagawiana vitalu vya kuwindia wanyama wetu na kuuziana huko huko bila serikali kujua tumenyamaza. Now this is more than too much.
Mngeuza wanyama bila kutuuza nasi tungewavumilia. Hakuna kitu kiliniuma kama juzi mlivyobomoa vibanda vya wanyonge pale Shule ya Uhuru kwa kisingizio cha kujenga kituo cha mgari yaendayo kasi. Najua mradi utaanza na kufa baada ya muda mfupi halafu mtauziana hilo eneo. Anayebisha atakumbuka unabii siku hili litakapotekelezwa.
Ingawa huu ujambazi wa kuuza wanyama wetu na kununua mahekalu haukuanza jana, kipindi hiki lazima tukomae. Kipindi hiki hatutanyamaza kama tulivyowanyamazia akina nanii walipouza Loliondo na kumuua mwandishi wa habari Stan Katabaro alipofichua uchafu wao.
Lazima tufe na mtu. Mie nasema wazi kuwa kama Ngosha hatanikatia lazima ‘afe’ mtu, haki ya nani sikutegemea kuwa ujamaa ungezaa mafisi, mchwa na mafisadi kama hawa ninaoshuhudia!
Hivi mchonga angefufuka leo si angezimia na kukata roho hata kabla ya kuonana na familia yake? Kwa sasa nitaacha kusoma magazeti kwa muda ili nisije nikageuka gaidi bure na kuwaalkaida hawa wezi wenye maulaji.
Je, ndugu yangu mkuu wa kijiwe, hapa atatufunga kamba gani asiwawajibishe hawa washirika zake? Ila ajabu ya maajabu usishangae kusikia wengine wakiteuliwa ubalozi kesho tu baada ya kutimuliwa uwaziri.
Nani mara hii kamsahau Radisraus Kombeu aliyeshirikiana na Maige na sasa yuko majuu kama balozi wakati ni fisi wa kawaida? Wezi lazima walindane bwana. Hapa lazima mtu awe re-cycled piga ua.
Naona mshirika wangu Maige anaingizana. Wacha nikamkabe koo na akikataa nakata mtama potelea mbali, kudadeki!
Chanzo: Tanzania Daima Mei 2, 2012.
No comments:
Post a Comment