Tuesday, 19 June 2012

Bajeti isaidie kuing’oa CCM


HAKUNA ubishi bajeti ya mwaka huu, kama itatumiwa na wananchi vizuri, inaweza kuwakomboa Watanzania si kwa uzuri wake bali ubaya wake. Ni bajeti ya hovyo inayopaswa kuamsha hasira na uasi kiasi cha kutongoja mwaka 2015.
Itakuwa ni ajabu ya maajabu kama bajeti hii ya hovyo haitasababisha na kuamsha chuki ya wananchi dhidi ya utawala usiowajali na badala yake unajali wawekezaji na wezi wengine wenye uhusiano na watawala wezi wachache.
Uhovyo wa bajeti hii yenye kuzua maswali mengi kuliko majibu unaweza kuupata kwenye maneno ya Waziri wa Fedha, Dk. William Mgimwa, aliyekaririwa akisema kuwa kiasi cha sh trilioni 2.314 za fedha za maendeleo, zitapatikana kutoka kwa nchi wahisani watakaokubali kuisaidia nchi, huku uwezo wa serikali kuchangia shughuli hizo ukiwa ni sh trilioni 2.213. Matumizi yanayoitwa mengineyo, yametengewa sh trilioni 4.065, mishahara sh trilioni 3.781 na kulipa deni la taifa sh trilioni 2.745. Nini maana yake na kwa ajili ya nani au ni fungu la siri la watawala kutanua kwenye ziara na mambo mengine ya kijinga?
Nini mantiki ya serikali kupoteza kiasi cha pesa hiyo kila mwaka kutokana na uzembe na ufisi wa watendaji wake? Hivi karibuni viongozi wa kidini waliiumbua serikali kwa kutafsiri vizuri ripoti ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG). Akiwasilisha tamko la viongozi wa kidini Askofu Paul Ruzoka, Mwenyekiti wa Kamati ya haki za kiuchumi na hifadhi uumbaji, alikaririwa akisema, “Ripoti hii imetufumbua macho na kubaini kuwa kila mwaka takriban dola bilioni moja za Marekani sawa na sh trilioni 2 kiasi ambacho ni moja ya sita ya bajeti ya serikali ya mwaka 2009/2010.”Serikali haikukanusha. Hii maana yake ni ukweli. Je namna hii tukishinikiza serikali iwajibishwe tunachochea au kujitendea haki hata na serikali yenyewe? Hii pesa inayotolewa kama misamaha si ya mamlaka ya mapato wala serikali bali jasho la Watanzania wanaoendelea kuteseka na kuteketea kutokana na magonjwa yanayotibiwa ukiachia mbali kuumia kwa ughali na ugumu wa maisha wakati watawala na washirika wao wanaowasamehe kodi wakila na kusaza. Hata mbwa wao wanakula na kuishi vizuri kuliko Watanzania ambao ndiyo walipa kodi zinazowaneemesha wezi wachache wenye madaraka na ushawishi.
Kwa tafsiri nyepesi ni kwamba pesa zinazopotea zinaweza kutosha kulipia deni la nje au kuendesha Wizara za Elimu na Ujenzi. Hapa tukisema serikali yetu ni ya kijambazi ni matusi? Je, tukisema kuwa serikali imeshindwa kazi hivyo isipewe muda zaidi wa kufanya madudu ni uchochezi? Kama kila mwaka tunapoteza bilioni mbili ina maana kwa miaka kumi ambayo serikali ya rais Jakaya Kikwete itakuwa ni zaidi ya dola 10,000,000,000 ambazo kama zingekusanywa zingeweza kutoondolea utumwa wa kulipa deni la taifa ambalo kila mwaka linazidi kuongezeka kutokana riba na kukopa zaidi.
Kwa deni la sh 2,200,000,000,000 maana yake ni kwamba kwa miaka 20 iliyopita tungeweza kulipa deni hili na kujikomboa. Hii ni hesabu rahisi isiyohitaji uwe na shahada ya uchumi. Bila kuwabana watawala wetu tutazidi kuingizwa kwenye utumwa wa kujitokea utokanao na ujinga, ubinafsi, uroho na upogo wao.
Kituko kingine unaweza kukiona kwenye maneno ya Waziri wa Mgimwa ambaye aliyetenga jumla ya shilingi sh bilioni 192.2 zimetengwa kwa ajili ya shughuliza kilimo na hifadhi ya chakula.
Huu ni utani wa ajabu na matusi ya nguoni kwa wananchi. Tutathibitisha hili. Hebu jiulize mantiki ya kutenga sh bilioni 128.4 kwa ajili ya maendeleo ya viwanda huku maendeleo ya rasilimali watu na huduma za jamii zikitengewa sh bilioni 84.1.
Wakati waziri akisema hayo, ripoti ya CAG inaonyesha kuwa kwa mwaka mmoja serikali inapoteza zaidi ya Sh 680.6 bilioni kupitia njia ya msamaha wa kodi kwa taasisi zake na baadhi ya watu binafsi. ripoti ya CAG inasema, “Endapo kiasi hiki cha Sh. 680,667,900,000 ambacho ni sawa na asilimia 14.7 ya makusanyo yote kingekusanywa, ni dhahiri kuwa kiasi cha Sh.391,235,100,382 kilichokusanywa pungufu kwa Tanzania Bara kisingekuwepo na badala yake, kungekuwepo ziada ya sh 289,432,799,618.” Je, hii maana yake kama siyo kuonyesha uhovyo hata utaahira wa watawala wetu ashakum si matusi? Inashangaza kuona huu upuuzi unafanywa na watu wanaoitwa wasomi tena katika karne ya 21. Je, hawa ni wasomi au wana vyeti visivyoendana na ujuzi wao? Je hawa wana tofauti na Mangungo wa Msovero ambaye hata hivyo anawazidi kwa vile alisaini mikataba ya kuuza nchi bila kujua kusoma na kuandika?
Mangungo wa kisasa ni wabaya na hatari kuliko wale wa zamani. Hivyo kwa bajeti ya kipuuzi kama hii ingekuwa vizuri kama wananchi wangechukua hatua badala ya kuwa kama punda ambao wanabebeshwa mzigo wa uchafu huu.
Hatuwezi kuishi kwa bajeti inayotegemea upandishaji wa vinywaji badala ya mipango madhubuti ya kulitoa taifa kwenye uombaomba na kukopakopa bila ulazima zaidi ya uvivu wa kufikiri na vipaumbele uchwara.
Kinachosikitisha na kuudhi sana ni kuona wale waliosababisha upuuzi huu kama vile waziri wa zamani wa fedha, Mustafa Mkulo na wakuu wa TRA bado wako bungeni na maofisini wakiendela kuchonga dili kama ilivyotokea kwenye uwanja aliwauzia Mohamed Enterprise ambaye mkuu wake ni mbunge wa Singida. Hivi rais ametengewa shilingi ngapi kwa ajili ya ziara zake zisizokwisha? Au nayo ni top secret?
Chanzo:Tanzania Daima Juni 20, 2012.  

No comments: