KUKAMATWA kwa mtoto wa rais wa zamani wa Zambia, Rupia Banda, Andrew, kumeleta matumaini kwa wapingaji ufisadi nchini Zambia na nje ya nchi.
Ingawa habari za kukamatwa kwa Andrew hazikupewa uzito mkubwa nchi kutokana na kuelekeza masikio na macho kwenye vurugu na visa vya uchomaji wa makanisa Zanzibar, kuna somo la aina yake kwa wengine wenye tabia za kutumia madaraka vibaya.
Andrew alikamatwa kwa tuhuma za kukutwa na kumiliki jumla ya kwacha 360,000,000 au dola 67,000 kwenye akaunti yake bila kuwa na maelezo ya jinsi alivyopata pesa hii.
Kwa viwango vya Tanzania kiasi hiki ni ‘vijisenti’ ambavyo haviwezi kumweka ndani mtu kama mtoto wa rais. Wapo viongozi waliokwapua mabilioni serikalini, lakini wameweza kuondoka bila kushughulikiwa.
Tukirejea kwa Andrew, wengi wanaokumbuka alivyokuwa akitumia madaraka ya baba yake kama silaha ya kujipatia pesa, wanaamini hii pesa imepatikana kifisadi. Msemaji wa Idara ya Makosa ya Jinai ya Zambia, Namukolo Kasumpa alikariri akisema kuwa Andrew alikamatwa kutokana na makosa ya jinai kama vile ufisadi na kupatikana na pesa inayoaminika kupatikana kutokana na ufisadi.
Ingawa wengi wanamwangalia Andrew kwa vile yumo mikononi mwa polisi, kuna akina Andrew wengi karibu katika nchi zote za kiafrika ambao hutumia madaraka ya baba zao kujipatia utajiri haramu na wa haraka. Nani mara hii kasahau watoto wa rais wa zamani wa Kenya Daniel arap Moi walivyotumiwa na mhindi Kamlesh Pattni kufikia kutaka kuifilisi Kenya?
Hivi karibuni kulikuwa na tuhuma dhidi ya mtoto wa rais wa Afrika ya Kusini, Duduzane maarufu kama ‘Dudu’ kutumiwa na wafanyabiashara wa Kihindi kuibia taifa hilo.
Nani mara hii amesahau tuhuma za Dk. Willibrod Slaa dhidi ya mtoto wa Rais Jakaya Kikwete, Ridhiwan, kuwa amejipatia utajiri mkubwa kwa njia za haramu kutokana na baba yake kuwa madarakani.
Pamoja na Ridhiwan kumtishia Dk. Slaa kuwa angemfikisha mahakamani kwa kumchafua, hakufanya hivyo. Kwanini?
Wapo wanaosema eti aliogopa asiumbuliwe zaidi. Wengine wanasema alichosema Dk. Slaa ni ukweli mtupu. Kila mtu anasema lake ingawa ukweli uko wazi kutokana na ushahidi wa kimazingira. Kinachoshangaza wachambuzi wa mambo ni ile hali ya baba yake naye kunyamaza kiasi cha kufanya watu waamini yaliyosemwa na Slaa ni ukweli mtupu.
Katika nchi za kifisadi za Kiafrika, urais umegeuka kuwa machimbo ya utajiri wa haraka. Kila aliye karibu na rais kuanzia mkewe, watoto wake, waramba viatu na hata matapeli wa kawaida wanautumia kuwaibia maskini kama anavyodaiwa kufanya Andrew.
Kinachofurahisha ni ukweli kuwa kiwango alichokutwa nacho Andrew ni kidogo kwa viwango vya wizi wa watoto au jamaa za wakubwa. Kinachofurahisha zaidi ni ile hali ya Rais Michael ‘Cobra’ Satta kuanza kutimiza ahadi za kuisafisha Zambia alizotoa wakati wa kampeni.
Maana Andrew si wa kwanza wala wa mwisho. Satta ameisha washikisha adabu wengi. Kuhakikisha anashinda vita dhidi ya ufisadi, Satta alianza vita yake kwa kumfukuza aliyekuwa mkurugenzi wa Tume ya Kupambana na Ufisadi, Godfrey Kayukwa kwa kumteua Rosewin Wandi.
Hii ni baada ya Kayukwa kutuhumiwa kuwahifadhi mafisadi shutuma ambazo zimekuwa zikimkuba mkurugenzi wa TAKUKURU hapa Tanzania ingawa rais hataki kumwajibisha kutokana na sababu anazojua mwenyewe.
Zambia inasifika kwa kuwa kinara wa mageuzi Kusini mwa Afrika. ni nchini Zambia ambako rais wa zamani, marehemu Frederick Chiluba na mkewe walisimamishwa kizimbani kutokana na kutumia madaraka vibaya na kuliibia taifa. Wengi wangependa kuota moto uliowashwa na Zambia kusambaa kwenye eneo lote la Kusini, Kati na Mashariki mwa Afrika ambapo urais umegeuka kuwa kama ujambazi uliohalalishwa hasa tukizingatia yaliyowahi kutokea kwenye nchi kama Kenya, DRC, Congo, Gabon, Msumbiji, Uganda na kwingineko ambapo jamaa za marais waliiba mabilioni ya shilingi bila kushughulikiwa.
Njia nyingi zimekuwa zikitumika kufanikisha wizi huu. Watoto au wake za wakubwa huunda NGO au makampuni na kuyatumia kupata tenda nono nono au kuwa makuwadi wa wafanyabiashara matapeli wa kimataifa. Nani mara hii kasahau tuhuma za hivi karibuni zilizomhushisha mke wa rais wa zamani kuuza flats za Msimbazi. Nani amechukuliwa hatua? Hapa tutakana kuwa Tanzania siyo nchi ya kifisadi?
Hata Zambia chini ya Chiluba na Banda hali ilikuwa hivyo. Baada ya upinzani kuchukua madaraka mambo yamebadilika. kwa wasiopenda ufisadi wanapaswa kuhakikisha wanachagua upinzani ili kuisafisha nchi na kukomesha dhuluma inayotendwa na wateule. pia ni vizuri walioko madarakani wakakubali na kuelewa kuwa mambo huwa yanabadilika. Kilichotokea Zambia kinaweza kutokea popote.
Kukamatwa kwa mtoto wa zamani wa rais wa Zambia kwapaswa kuwa somo kubwa kwa Watanzania hata watawala wao. Hata hivyo, ukweli umedhihirisha kuwa walioko kwenye vinono ni vipofu au wazito kujifunza kutokana na kuleweshwa na madaraka.
Hata Andrew alipokuwa akiwaimbia wazambia alikuwa haoni wala kusikia akiamini kuwa madaraka ya baba yake licha ya kuwa ni haki kwake kuyatumia, yalikuwa ya milele asijue ni koti kwenye mabega tena koti lenyewe la kuazima! Wahusika tieni akilini na mbadilike kabla hayajawakuta.
Chanzo: Tanzania Daima Juni 6, 2012.
No comments:
Post a Comment