Ingawa mbunge wa Ubungo John Mnyika (CHADEMA) aliposema rais Jakaya Kikwete ni dhaifu alitolewa nje ya bunge hivi karibuni, ukweli unabaki pale pale kuwa Kikwete ni dhaifu tena sana. Leo sitazungusha mjadala huu ili kuepuka kumchosha msomaji.
Nitaanza kumuunga mkono Mnyika kuwa Kikwete ni dhaifu tena sana kwa sababu za kisayansi zifuatazo:
Mosi anapenda kukwepa majukumu yake na kwa kupenda kusafiri hovyo hovyo na kutumia pesa yetu hovyo. Rejea alivyokimbilia Davos Uswisi wakati wa mgomo wa madaktari uliogharimu maisha ya watanzania wengi wasio na hatia zaidi ya kumchagua yeye.
Pili ni mwoga kuchukua maamuzi kwa mfano, kama si bunge kumtimua waziri wake mkuu wa zamani ambaye pia ni mshirika wake, Edward Lowassa asingeweza kufanya hivyo. Rejea alivyokuja na mkwara wa kujivua gamba. Alipotolewa ukali na Lowassa na watuhumiwa wengine kama Andrew Chenge aliishia wapi kama siyo kuchomoa hoja kinamna huku akiendelea kuaibika na kuonekana wazi alivyodhaifu.
Tatu, hakushindwa tu kuwawajibisha akina Lowassa, ameendelea kumlipa Lowassa pesa ya ustaafu ambayo hastahili. Pia Kikwete ameshindwa hata kumkemea Lowassa kuacha kukigawa chama kwa matamshi yake yenye kupingana na maazimio ya chama chake. Ameunda chama ndani ya chama kupitia mtandao wake. Rejea, kama mwenyekiti wa chama chake, kumtumia Nape Nnauye kuwananga akina Lowassa na baadaye kuchomoa na kumwacha Nnauye na maadui wa kuundiwa na Kikwete
Rejea kuwahi kudaiwa kuridhia ongezeko la posho ya wabunge, Kwa udhaifu wake umma ulipokuja juu akawatupia mzigo waziri mkuu Mizengo Pinda na spika Makinda
Nne Kikwete si msafi kimaadili maana alitajwa wazi wazi kuwa urais wake ulitokana na wizi wa EPA uliotikisa uchumi wetu ambao Kikwete hajawahi kutolea maelezo wala kujitetea. Ukitaka kumpa taabu Kikwete mtajie wizi wa EPA. Nimeshaandika mara nyingi juu ya hili na kilichofanyika ni kwa watu wa Kikwete mara kutishia gazeti kwa kutafuta kasoro ndogo ndogo bila mafanikio. Na hili limemfanya Kikwete ashindwe kupambana na ufisadi kwa sababu naye ni sehemu ya tatizo ukiachia mbali kuwa mshirika mkuu. hii ndiyo sababu iliyomfanya ashindwe kuwachukulia hatua mawaziri walioboronga akina Ibrahim Msabaha (Bangusilo), Nazir Karamagi na wengine waliotimuliwa kutokana na shinikizo la bunge ambalo siku hizi limegeuka nyumba yake ndogo baada ya kuwa na spika asiye na udhu wala uchungu na nchi kama ilivyokuwa kwa mzee wa viwango.
Tano, Kikwete hupenda kufanya mambo yasiyo ya muhimu kuwa muhimu na ya muhimu kwa ya hovyo. Rejea alikvyowenda Brazil mwezi Aprili mwaka huu kwenye mkutano wa maendeleo ya kiuchumi akaishia kupoteza muda mwingi na aliyekuwa kocha wa mpira wa miguu, Maxio Maximo.
Sita Kikwete tangu aingie madarakani ameanzisha na kulea mitandao ambayo licha ya kukigawa chama imekidhoofisha hata kumdhoofisha Kikwete mwenyewe. udhaifu huu umetumiwa na watu mbali mbali kuanzia mkewe hata mwanae kujihusisha na siasa hata kwa kuonyesha mgongano wa maslahi wa wazi kati ya ikulu na umma.
Sita, Kikwete anasifika kwa kuwa rais aliyeshuhudia kudhoofika kwa uchumi tokana na mipango, usimamizi na matumizi ya hovyo. ni rais aliyesimamia serikali inayofanya mambo kiholela kiasi cha kuonekana kama mhimili wa ubadhirifu. Ameshindwa kusimamia uchumi kiasi cha kushindwa hata kuangalia raslimali kama madini na wanyama. Kutokana na hili Kikwete ameshindwa hata kutangaza mali zake ajabu serikali yake eti inawataka watumishi wa umma kutangaza mali zao wakati mkuu wake anaendelea kujifanya hili halimhusu!
Saba, kushindwa kusimamia na kuimarisha muungano. Rejea kuendelea kuwa kimya wakati taifa likikabiliwa na changamoto ya Uamsho. Je Kikwete anawaunga mkono uamsho nyuma ya pazia kama ilivyokuwa mihadhara wakati wa utawala wa Ali Hassan Mwinyi aliyefuga kila aina ya kashfa kwa jina la mihadhara?
Nane, ukimya. Rejea Kikwete alivyokaa kimya wakati wa mgomo wa madaktari kiasi cha kumuachia mzigo waziri mkuu huku yeye akikwepa lawama na kusubiri kusifiwa kama tatizo lingetatuliwa. Hata madaktari wanapotishia kugoma tena bado Kikwete ni kama hayupo wala hili halimhusu. Baba gani anaacha mambo yaharibike ndipo atoe sauti yake? Pia ukimya wa Kikwete unaweza kuuona kwenye mgongano baina ya taarifa zinazotolewa na watendaji wake. Kila mtu anasema lake na hakuna anayewajibika. Rejea maneno ya waziri wa mambo ya Nchi za Nje Bernard Membe alipoamua kuwamwagia sifa CHADEMA kuwa wajiandae kuingia madarakani huku waziri wake Stephen Wassira akisema vingenevyo.
Tisa, Kikwete ni dhaifu sana katika kutoa maamuzi. Makala ya wiki jana niliongelea uteuzi wa hovyo. Hata baadhi ya mambo anayofanya kama kubembea alipokwenda nchini Jamaica ni vitu ambayo vingeweza kuepukwa kama rais angekuwa jasiri.
Ukiachia Hilo hata baadhi ya maamuzi kama kuunda mikoa na wilaya mpya wakati uchumi wetu uko taabani ni ushahidi kuwa rais wetu ni dhaifu sana.
Kumi, Kikwete ni mgumu wa kujifunza. Rejea kurudia makosa yale yale karibu kila mwaka. Kwa mfano ripoti ya kila mwaka ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa pesa za Serikali (CAG) imekuwa ikionyesha wizi wa kutisha kwenye mawizara na serikali za mitaa. Kikwete hajawahi kuchukizwa na hili na kutoa tamko hata karipio.
Ukiamua kuandika udhaifu wa Kikwete wote, unaweza kujaza kitabu. Kwa leo tunaishia hapa kwa kuungana na mbunge Mnyika kuthibitisha udhaifu wa rais Kikwete.
Chanzo: Tanzania Daima Juni 27, 2012.
No comments:
Post a Comment