Joni
Mnyika ametufungu macho ingawa tulikuwa tukijua. Tuliogopa kuonekana
wachochezi. Sasa wanaitana machizi wenyewe sisi tuwaite nani?
kutokana
na mzee mzima kutoongea kwenye kikao kwa muda mrefu, leo nimelianzisha
kwa kutaka kujua mawazo ya wana kijiwe kuhusiana na akili za waheshimiwa
wao mjengoni.
Swali langu lilianza hivi: Jamani, hivi hawa waheshimiwa wa chama kilichopo kwenye ulaji ni wazima kiakili?
“Dk
Mgosi Machungi anakuwa wa kwanza kula mic, “Kama titawaangaia
kisaikoojia, hawa jamaa ni machizi kama aivyosema Joni Mnyika. Maana
timeshuhudia wakipitisha vitu vya kipuuzi kuonyesha wasi wasima kiakii.
Isitoshe kama wao wanaitana machizi unataka sisi tiwaiteje zaidi ya
machizi fyatu?”
“Du Dk Mgosi unachambua kama vile wewe ni daktari wa saikolojia!” Alichomekea Dk Mbwa Mwitu.
Dk
Mgosi kasifiwa anaamua kurejea, anasema, “Kwani saikoojia umeona ni
somo kubwa kuiko yote? Kwa taifa yako timesoma haya mambo tena kue kue
ushoto kama hujui ujue.”
Kijiwe hakina mbavu kwa jinsi anavyosifia Lushoto utadhani Oxford.
Tukiwa
tunacheka, Dk Mipawa amepata upenyo kutongoa, “Huyu kijana Joni kwanza
namfahamu sana. Alikuwa mwananfunzi wangu na isitoshe baba yake huwa
tunakunywa wote bia sometimes niwapo na pesa. Alichosema kijana ni kweli
hasa ikizingatiwa kuwa waheshimiwa wetu wengi hasa wa chama twawala
wanawakilisha matumbo na si majimbo yao.”
Kabla
ya kuendelea Dk Kidevu anaingilia, “Hakuna mheshimiwa mdharauliwa na
mpuuzi kama wangu. si mlisikia alivyokumbwa na kashfa ya kusafiri na
zana za kivita utadhani alikuwa Somalia? Kama siyo mkwerere kumuokoa,
angekuwa analia kama bosi wange Bill Ngereza.”
Dk Maneno anachomekea haraka, “Unasema hicho kitoto kilichodandia kwenye umaarufu wa baba yake?”
“Ndiyo.
Siku hizi umekuwa ndiyo mtindo wa maisha. Riz kwenye mgongo wa Njaa,
Sal kadhalika naye, kwanini hichi kizinzi kisitumie umaarufu wa dingi
wake?”
Dk
Mpemba anachomekea, “Mie naona huyu kijana hata kama wa hovyo
mwamuonea. Mbona wako wengi njengoni walioingia kwa umaarufu wa baba
zao? Wategemea nini toka kwa watu waloingia njengoni kwa kutegemea umaarufu wa baba au mama zao, kuhonga, kughushi na kuchakachua?”
Profesa
Dk Msomi Mkatatamaa anaamua kula mic naye, “Ule mjengo ni wa machizi
hasa ukiondoa waheshimiwa wa upingaji na wachache wasio watumwa wa
ufisi. Hivi unategemea nini toka kwa watu kama LivingJiwe Lushindo,
Annae Abudala, Sofia Lion hata huyo bosi wao ambaye juzi alinichekesha
kudai eti waache matusi na kurejesha heshima ya mjengo wakati yeye ndiye
chanzo kikuu cha aibu na uchizi wao?”
Kabla
ya kuendelea, Dk Mchunguliaji anachomekea, “Hamkumsikia Joni Ngereza
akitapika mbele ya wenzake kwa hasira ya kunyang’anywa ulaji? Mie naona
tungeondoa mjengo ili watu wachache waache kututumia. Maana zaidi ya
kuwawakilisha wake zao, watoto zao na matumbo yao hawatuwakilishi zaidi
ya kwenda kule kutuchuuza.”
“Kama
kuna chizi si mwingine bali kile kijimama shangingi na changu
kinachosimamia hawa machizi. wajua nimaanishacho. Annae achezaye
Makindamakida.” Aliingilia kati Dk Mipawa.
“Mie
naona hata mkuu angetimuliwa maana naye ni chanzo cha upuuzi wote huu.
hivi wadanganyika hawaoni anavyowalostisha kwa matanuzi na kuruhus
mamisab wake na kitegemezi ukiachia mbali waramba viatu kuiba njuluku
zetu?” Alichomekea Dk Kidevu.
Dk
Mpemba hakujivunga; alikamata mic, “Mie naona heri tuwe hatuna
lisirikali tokana na kutuumiza sana. maana watufanyia vitu vya ajabu
ajabu.”
Kabla ya kuendelea Dk Machungi alidandia mic, “Ami mbona hatikueewi. wanamifanyie vitu vya ajabu ajabu vipi au popo bawa?”
Dk
Mpemba, “Mambo ya popobawa waulize kina Lushindo na mkuu mwenyewe na
Simbacheni waniojua kuchovya huku na kule. Mie simaanisha mambo ya
Popobawa yakhe. Naamisha huu wizi wa fedha zetu. Ingawa twasema wao
machizi nasi machizi maana twaibiwa nchana.”
Kabla ya kuendelea Dk Mipawa anadakia, “Nkwingwa, kwanza lushindo kikwetu matusi makubwa tu. Je ni kweli Simbacheni amefumaniwa na mke wa askari au siasa za mitandao?”
Dk
Profesa Mkatatamaa baada ya kuona mambo ya popobawa na mafumanizi ya
Kimchembachemba yanaanza kutawala anaamua kuvaa daruga kurejesha mada
kwenye mstari. Anasema, “Mie mambo ya kufumaniana hayanihangaishi kama
uchizi wa hawa jamaa ambao wanapitisha libajeti linaloumiza wale
wanaowawakilisha.”
Kabla
ya kuendelea, Dk Machungi anaingilia, “Mgosi, usiseme eti wanawakiiisha
watu. hawatiwakiishi bali matumbo yao. hivi ni mdhaauiwa gani
anawakiisha yeyote zaidi ya mabwana zao, chama chao na matumbo yao.”
“Unamaanisha hata makamanda wa magwanda wa upingaji nao nyanya?” Aliuliza Dk Mbwa Mwitu.
“Hapa
hatuongelei jamaa wa upingaji kama vile Mzito Kabwela, Mtuhuru Mboe,
mchungaji Msigua, Hole Lissu, Joni Mnyikani na wengine machachari. Hawa
si machizi ni machizani.” Alichomekea Dk Mchunguliaji.
Nami
profesa mzima kuona chansi nikaamua kuitumia na kusema: Mie naona wote
machizi sema uchizi wao unatofautiana. Wale wa Chama Cha Mafisi fisadi
(CCM) ni machizi wa kughushi, kujuana, kulindana, EPA, Richmond, usanii,
ujambazi na madhambi yote wakati wa upinzani ni machizi wa Ukombozi.”
“Du!
Kweli wewe profesa kuliko hata yule profesa wa Kafu wa pumba.
Nimekukubali kichaa wangu. Yaani kwa mtindo huu unaweza kusema na mkuu
ni chizi wa usanii na dogodogoz au siyo?” Alidakia Dk Mchunguliaji.
Dk
Profesa Msomi anakatua mic na kuendelea, “Kwa taarifa yenu kaya hii
kila mmoja ni chizi ndiyo maana kila mtu ana nafasi ya kufanya uchizi.”
Kabla
ya kuendelea Dk Machungi anaingilia, “Ami una maanisha hata sisi ni
machizi tinaofanya mambo ya kichizi au una mpango wa kutitukana siyo?”
Dk
Profesa Msomi anakatua mic tena huku akimalizia kubwia kahawa, “Sasa
kumbe. Bila kuwa machizi tungeruhusu vipi machizi walipane mishiko
kuanzia ya matako sorry makalio hadi umbea bila kuingilia kati?”
Dk Mgosi, “Kwani sisi tinakwenda kwenye mjengo?”
Dk
Profesa Mfilosofe Msomi, “Tunakwenda mjengoni kwa kukubali kuwakilishwa
na machizi kama alivyosema dogo Joni Mnyika. Hakika huyu dogo jina Lake
Limanfaa. Maana ni nabii aliye nyikani. Bila kuwa machizi tungekuwa
tumeishaingia tahrir kuondoa uoza huu. You know what I mean.”
Tukiwa tunaendelea kutongoa si daladala moja likaturushia maji machafu kiasi cha kwenda kumtia adabu dereva wake!
No comments:
Post a Comment