Tuesday, 19 June 2012

Kumbe Bajeti yenyewe ya walevi!


DK. Mbwa Mwitu anaingia akiwa amekunja uso huku akionekana wazi ana jambo tena kubwa tu. Hata hawapi watu nafasi wamjulie hali hasa kutokana na kupatwa msiba wa kumpoteza rafiki yake, Pofesa Joji Saitoshi kule kwenye nchi ya Nyayo.
Analianzisha: “Waheshimiwa hiki kiini macho kiitwacho bajeti mmekionaje au ni mimi peke yangu ninayeona kama ulevi ulevi mtupu?”
Dk. Machungi hangoji: “Mgosi unaongeea huu uhuni tunaofanyiwa kia mwaka tisiamke? Mie niishangaa kusikia eti wazii huyu mpya ni mtaamu wakati wote baba na mama yao moja. Kwei kambae wote wana mashaubu Wagosi.”
Dk. Mpemba anachangamkia mic: “Yakhe Mgosi wasema kweli tupu. Huu kweli uhuni na kiini macho. Hawa wapaswa waamshwe kwa wanakaya kuwachukulia hatua mujarabu wallahi.”
Kabla ya Ami kuendelea, D. Mipawa anakwanyua mic: “Mami usemayo kweli. Ila hawa Uamsho nao hawana maana. Hapa siyo cha kutaka Uamsho wala Uangusho bali wanakaya kuacha unafiki wa kulalamika lalamika wakati wana uwezo wa kufanya kweli. Hivi kulikuwa na utawala mbovu na katili kama wa Mwamali Kashafi au Hossenni Kibaraka? Mbona wote wamepigwa kibuti?”
Dk. Mpemba anajirejeshea mic: “Ami usemalo kweli. Mie nimesoma Libya kwa Kashafi. Maisha ya jamaa hawa huwezi linganisha na upuuzi unaoendelea hapa. Nkitoka Libya mara nyingi kwenda Masri. Wenzetu wako mbali sana, lakini bado wafanya kweli. Mie naona tatizo ni ile hali watu kupendaliwa.”
“Mgosi unamanisha nini? Unasema eti tinapendaiwa? Namna gani? Wewe hujui kuwa bajeti ya walevi ikipangwa na walevi inakuwa ulevi mtupu na haiwezi kuwa na maana kwa vile akili zao zimelewa?” Dk Machungi anauliza kwa hasira. Mara nyingi huwa hapendi hili neno kuliwa hata kama ni kweli kuwa Wadanganyika wanaliwa.
“Asemacho Dk. Mpemba ni kweli kuwa kweli tunaliwa na si kuliwa tu, hata pesa yetu inaliwa, nchi yetu inaliwa, mali zetu zinaliwa kila kitu kinaliwa,” Dk. Mbwa Mwitu anaongezea kwa hasira na kuonesha wazi kukata tamaa.
Anaendelea: “Kama hatuliwi ni nini iwapo tunaambiwa wanakusanya kodi kwa asilimia 160 na kuomba kwa asilimia 80, ukichanganya yote haya unagundua kuwa kumbe zoezi zima ni ujambazi wa kawaida. Je kwa kuendelea kufanyiwa hivi na kukubali hatujaliwa Mgosi?”
Dk. Mgosi anajibu mapigo: “Mgosi tiheshimiane kama kuiwa waiwa wewe. Subutu watishia kula mai akini kuiwa mie matusi, kwani niliwe mie ubwabwa?”
Dk. Profesa Mfilosophe au Msomi anatinga dimbani akiwa na mahasira yake kama wenzake. Baada ya kuwa kimya muda mrefu anaamua kuingia mzima mzima, hasa baada ya kuona lugha ya kuliwa inaanza kuharibu mada. Anakatua mic baada ya kunywa kahawa yake: “Japo wanakijiwe ni walevi wa kahawa na wengine bia, bajeti hii inaudhi hakuna mfano. Kwanini bwana Mginwa ameamua kuja na kiini macho wakati tunaambiwa ni mtaalamu wa mambo haya?”
bila kungoja kujibiwa anaendelea: “Kila anayekuja kila mwaka anapandisha bei ya vilevi na vivutwa. Hii maana yake ni kweli kama wasemaji waliotangulia walivyosema ni bajeti ya walevi. Hii inawafaa sana wao kwa vile wanapata malipo ya bure kuanzia ya makalio, kuuchapa usingizi hata kuongopa ukiachia mbali rushwa ya akina Badwill. Je, taifa hili limehiari kuwa la walevi na matapeli?”
“Pasua baba maana wamezidi. kila mwaka wanaahidi pepo wanatupa jehanamu. Au ni ulevi wa madaraka uliosababisha walewe hadi kuwa na bajeti ya walevi?” Anachomekea Dk. Maneno.
Dk. Madevu naye anaona upenyo anaamua kuutumia: “Mie mwenzenu sina hamu na usanii huu. Bi. Mkubwa amekuja juu kuwa mwaka huu kama hatujengi lau chumba atanipa talaka kwa vile anaona kama nchi hii haina warume tena. Wao wanasamehe matrilioni wanakwenda kuombaomba mabiloni, akili au matope! Kweli hawa wana akili au tunazidiana akili?”
Dk. Profesa Msomi anaendelea: “Akili wataipata wapi wakati wanasumbuliwa na laana ya uhujumu na ujambazi? Mara hii mmesahau HEPA? Bila hujuma pesa wanayokusanya kwenye kodi inatosha kuendesha kaya bila hata kuwa na deni. Hebu jiulizeni jamani. Juzi watu wa majoho wamefichua kuwa kaya inapoteza dolari milioni mbili na ushei wakati huo huo ikitukamua kiasi kama hicho eti kulipa deni la kaya. Akili au matope?
“Matope.” Tukajibu wote kwa pamoja kwa hasira utadhani tumeambizana!
Anaendelea: “Nina wasiwasi na wapingaji hasa baada ya kuona Chakudema wakimkumbatia yule fisadi wa kigabacholi. Maana, wangekuwa wanaaminika walipaswa kutumia mwanya huu kulinyonga hata kulitimua lisirikali. Kwa bajeti hii ulikuwa ni wakati muafaka kuondoa hili balaa badala ya kusubiri miaka thelathini ijayo. Je, tatizo ni nini au wote wale wale?”
Akiwa anatoka jasho kwa hasira na usongo anaendelea: “Ili kuwadanganya wafa na jembe wanawambia kuwa sera yao kwa sasa ni kilimo kwanza! Kilimo kwanza au kusamehe na kuiba kodi kwanza?”
Kabla ya kuendelea, Dk. Mbwa Mwitu anachomekea, “Hapa si kilimo kwanza wala nini bali wizi kwanza. Wanafanya maisha yetu yakose hata maana. Mwenye ubavu wa mbwa naye kapandisha kodi kwenye bajeti yake ya kilevi na kishenzi kama wao. Hapa kila mwizi atapandisha kodi au bei kwa kisingizio cha bajeti.”
Dk. Mipawa anachomekea: “Bila shaka tutaanza kunywa gongo na kuvuta bangi kutokana na bia na sigara kupandishwa bei. Ingawa Mgosi Machungi hapendi neno kuliwa, ukweli ni kwamba tutaliwa tu tutake tusitake.”
Dk. Machungi ameguswa pabaya. Anajitetea: “Usiseme titaliwa sema utaiwa mwenyewe kama uko tayai kuiwa.”
Dk. Mipawa hamjibu. Anaendelea na kusema: “Vile tutaanza kusafiri kwa ungo baada ya nauli kupanda ukiachia mbali kulala baa baada ya kodi ya nyumba kupanda. Bado tunajiuliza kwanini kodi zipande na hata bei za vinywaji wakati watu wanazidi kuongeza idadi ya mashangingi ya kupanda. Sisi tunapandishiwa gharama za maisha wao wanazidi kuzishusha kwa upande wao.”
Wakati tukijadili bajeti tulikuwa tukimsubiri Mgimwa na wasaidizi tuwatie kitimoto. Lakini hawakuwa wametokea. Ghafla tunaona mashangingi yao. Tunaokota ma--- we koma!
Baada ya kuona zegere linaanza nikaamua kujitoa kinamna.
Chanzo: Tanzania Daima Juni 20, 2012. 

No comments: