Hii ni mara ya pili kuandika barua ya
wazi kwa rais. Sifanyi hivyo ili kutafuta ujiko au kuwa karibu naye ili nipewe
ukuu wa wilaya au hata wa mkoa huko tuendako. Sina shida na ukuu wowote zaidi ya
kuwa na shida moja-kumkubusha ndugu rais awanusuru watu wetu na taifa letu toka
kwenye kadhia na jinai vinavyozidi kubarikiwa na kuhalalishwa wakati ni janga
kwa taifa.
Nakumbuka mwaka 2006 rais Jakaya
Kikwete aliwaambia umma wa watanzania kuwa ana orodha ya wauza unga, majambazi,
wala rushwa, hata wezi wa bandarini kutaja wachache. Hii ikiunganishwa na ahadi
yake aliyotoa ya maisha bora kwa watanzania wote, kwa rais makini na mkweli,
unapata jibu kuwa kweli kuna maisha bora yaliyoahidiwa. Lakini kwa upande
mwingine ukijumlisha ahadi za rais na kutotimiza hata moja, unapata jibu japo
chungu kuwa maisha bora kwa watanzania ilikuwa ni changa la macho kama wasemavyo
watoto wa mjini.
Leo kwa mara nyingine naandika barua
hii kwa rais ingawa ni ya wazi. Naandika kumkumbusha jambo moja
kati ya mengi anayopaswa kukumbushwa. Naandika kumkumbushia kuwashughulikia
wauza unga ambao kwa sasa umekuwa balaa la kitaifa. Ingawa wachache, tena
viongozi wakubwa kama alivyodai mchungaji mmoja hivi karibuni, wanapata utajiri
wa haraka na wa kutisha, taifa linaangamia. Sijui ni rais gani anataka kuongoza
taifa linaloangamia au kuacha historia kuwa alifanikisha biashara ya mihadarati?
je rais ananufaika vipi na biashara ya mihadarati kiasi cha kuendelea kuifumbia
macho wakati ana orodha ya wauzaji?
Kwa maneno mengine, ukimya wa rais
unafanya watu waanze kujenga dhana potofu kuwa kuna jinsi rais au watu wake
wanafaidika na biashara hii hatari. Ni juzi juzi tuliambiwa kuwa
ulikamatwa unga kule Mtwara ukiwa unasafirishwa na mtoto wa Amatus Liyumba
aliyewahi kufanya kazi benki kuu na kuishia kusababisha upotevu wa mabilioni.
Kesi hiyo imefikia wapi? Haisikiki tena. Juzi juzi alikamatwa mdogo wa
mfanyabiashara tata Rostam Aziz aitwaye Abdulrasul. Ajabu kesi yake ilikimbizwa
kama gari la wagonjwa na kuachiwa haraka huku akiacha walalahoi wakiteketea na
mambo yakaishia hapo kana kwamba kilichofanyika ni kitu cha kawaida! Je
tutapigana na vita ya mihadarati kwa kukangalia umwenzetu na urafiki au kuna
faida nyuma ya pazia wakuu wanapata kama alivyodai mchungaji? Je namna hii
mnamdanganya na kumfanya mpumbavu nani?
Kutokana na kesi ya hii ya mdogo wake
Rostam imefikia mahali watanzania wamejenga dhana kuwa huyu jamaa ana hisa
kwenye serikali ya Kikwete kutokana na mkono wake kuwa karibu kila mahali. Nenda
Kagoda, utaambiwa Rostam. Nenda Richmond, yupo Rostam. Na sasa mihadarati,
Rostam anatajwa. Na ushahidi zaidi ni kwamba kila uchafu unaofanywa na Rostam
hashughulikiwi mtu kutokan ana ukaribu wake na ushirika na rais.
ingawa wasiojua sheria na jinsi
ufisadi na jinai hii vinavyolindwa wanawalauma majaji kwa kutoa hukumu
iliyoonekana kumpendelea ndugu yake Rostam, ukweli ni kwamba mfumo wetu ndiyo
unawezesha haya na rais analijua hili. si siri kuwa, kisheria, ukitaka kumsaidia
mharifu unamfungulia mashitaka chini ya vifungu visivyo kisheria na jaji
anatupilia mbali shitaka au kutoa haki kwa mhusika hata kama hakustahili.
Kinachofanya wakubwa walaumiwe kwa uchafu huu, ni ile hali ya kutumia udhaifu
huu kupitisha na kusaidia watu wao. Hakuna ubishi kuwa hukumu iliyomwachia mdogo
wake Rostam ni pigo kwa mapambano dhidi ya mihadarati. Kinachogomba ni ukweli
kuwa kumbe rais anawajua wauza unga lakini hawashughulikii. Hata wachovyo na
mafisi fulani wakitumia vifungu vya sheria vibaya kuwaachia hakuna anayejali.
Mbona, kwa mfano, katibu mkuu kiongozi wa zamani Philemon Luhanjo alipomrejesha
ofisini kinyume cha sheria katibu mkuu wa zamani wa wizara David Jairo rais
aliingilia kati? je kama hakuna namna mbona Kikwete haingilii kati kwenye suala
zima la kuachiwa huru kwa mdogo wake Rostam? ni kwa sababu ni mdogo wake Rostam
mshirika wa Kikwete na mwezeshaji mkuu katika kutunisha mtaji
binafsi?
Itakuwa ni utoto wa ajabu kwa
watanzania kuendelea kuamini kuwa Kikwete anaweza kupambana na wauza unga iwapo
watu wake wa karibu wanaachiwa hivi hivi nan aye anajifanya
kutojua.
Umefika wakati wa kumbana Kikwete
ashughulikie wauza unga aliodai ana orodha yao. Maana miaka inazidi kuyoyoma
nasi tunapewa matumaini ya kitoto ya kesho kesho. Wahenga walisema kesho huwa
haipo na ukitaka deni njoo kesho kwa maana ya kuwa hutapewa mkopo. Kwanini
tumeligeuza taifa letu kuwa la waharifu na jinai? Ajabu ya maajabu tunaendelea
kuwaheshimu waharifu eti kwa vile wana pesa au wako karibu na wakubwa. Rais
Kikwete tafadhali shughulikia wauza unga kabla ya kuondoka ofisini. Kama utaamua
kunyamaza kama kawaida yako, uje siku moja utakuja kuulizwa na namna
utakavyoulizwa haitakuwa ya kufurahisha kwako binafsi na taifa. na isitoshe,
wafanyabiashara wenye pesa itokanayo na uchafu huu watakuabudia leo kwa vile uko
madarakani. Ukishaachia madaraka watakukimbia na hata kutoa ushahidi dhid yako.
Mungu epusha mbali hili lisikutokee ingawa laweza kutokea kama hatua madhubuti
kupambanana jinai hii hazitachukuliwa mapema.
Chanzo: Tanzania Daima Mei 30, 2012.
No comments:
Post a Comment