The Chant of Savant

Wednesday 25 April 2012

Barua kwa Waziri wa Mawasiliano, Sayansi na Teknolojia


Image DetailTanzania ...
Ndugu waziri,
Naamini u mzima wa siha. Mie mwananchi mwenzako si mzima hasa mfukoni kutokana na madudu uliyoridhia nifanyiwe pamoja na wananchi wengine.
Sitaki kuonekana mlalamishi asiye na sababu. Ninalalamika na nina sababu tena si moja bali nyingi na za msingi ndugu waziri. Kabla ya kukwambia tatizo langu, kwanza nakuuliza: Hivi huwa unapiga simu na kulipa toka mfukoni mwako au unalipiwa nasi walipa kodi unaowaumiza ima kwa makusudi ua vinginevyo? Je, una habari kuwa mawasiliano bora ni mojawapo ya vichocheo vya maisha bora na kukua kwa uchumi ambavyo bosi wako aliwaahidi Watanzania wakati wa kampeni?
Najua huwa unapiga simu tena sana. Pia najua nyinyi wakubwa huwa hamlipii huduma mnayotumia kama sisi walanguliwa na wanyonywaji wa kila tapeli na mwizi. Laiti ungekuwa unalipa bills za simu zako ungejua nisemacho. Hata hivyo, unakijua japo hutaki kukishughulikia. Maana mimi si wa kwanza wala wa mwisho kulalamikia jinai tunayotendewa na makampuni ya simu.
Unapiga simu tena kutoka nje ukilipa kwa dola, unaambiwa huna salio la kutosha. Wakikuonea aibu ya kukwambia upuuzi wao waliorekodi kwenye kompyuta wanakukata pesa tena bila hata kutoa sauti! Hapa hujajumlisha muda unaotumika kwenye kutafuta kuunganishiwa bila mafanikio huku ukiambiwa kila upuuzi na uongo. Je, huu si ujambazi wa mchana hata kama umehalalilishwa? Tufikie mahali tuwe na uchungu na taifa letu badala ya kuendekeza uchu wa kuliuza na kulipiga mnada kila mtu kivyake na kwa nafasi yake. Kuna kesho jamani.
Ndugu waziri, samahani sitakuita mheshimiwa maana heshima hutokana na matendo ya heshima siyo shuruti za kisheria wala kujipa. Mie ni Mtanzania niishie Kanada. Nina ndugu na marafiki karibu katika nchi zote za Afrika Mashariki. Ukiondoa Tanzania na Uganda, nchi zilizobaki sina lawama nazo. Napiga simu kule naongea na kuridhika. Ningekuwa na uwezo ningefunga makampuni yote ya simu Tanzania ili kuepusha huu ujambazi unaoendelea. Ukipiga simu Tanzania kutokea hapa Canada unakatwa senti 27 za dola huku ukipiga Kenya unakatwa senti tano tu za dola ya Kikanada. Ajabu ukiongea na mtu aliyeko Kenya licha ya kuongea muda mrefu, mawasiliano ni mazuri yenye kusikika na si kama Tanzania ambapo ni mikoromo mitupu mara nyingi.
Naona wizara yako inaitwa ya Mawasiliano Sayansi na Teknolojia. Ukweli ni kwamba wizara yako inapaswa kuitwa wizara ya maibiano, ukale na tekelinalotujia. Maana kama utachunguza hata hiyo mitambo inayotumiwa na mashirika yako ya simu si ya kisayansi wala teknolojia zaidi ya kuwa mikangafu waliyorithi ambayo iliachwa na Nyerere.
Kama ni sayansi basi inatumika sayansi ya kutuibia na teknolojia si teknolojia kitu bali teke la ujambazi. Au tuiite hiyo teknolojia tapelijia. Maana wenzio tunatapeliwa.
Kwa walio ndani ya nchi hali unaijua. Inakuwa kama vile mmeamua hata watu wasiwasiliane. Ili iweje? Hayo ndiyo maisha bora mliyowaahidi nao wakaingia mkenge wakawachagua ili muwauze kwa wawekezaji?
Naomba ndugu waziri usinijibu kama yule waziri wa fedha aliyeulizwa swali tena na mheshimiwa mbunge kuhusu faida za uwekezaji akamwambia eti aende ofisini kwake.
Itafikia kipindi mtatwambia twende kugonga kwenye mageti yenu halafu walinzi wenu watupige risasi uwe mwisho wa adha.
Nani anajua? Kama ingekuwa huku, huyo waziri angeachishwa kazi hapo hapo kwa vile hajui anachofanya. Ila kwa vile ni huko ataendelea kupeta na kutesa.
Ndugu waziri, hivi hujui kuwa hii ni karne ya 21 ambayo kila siku tunawasikia majukwaani mkisema ni ya sayansi na teknoljia? Mbona majirani zetu wana huduma nzuri na nafuu wakati hawana raslimali kama zetu?
Je, tatizo ni nini? Tatizo ni ile ya kuwa nyinyi mnaoidhinisha uwekezaji licha ya kupewa chenu, mnapewa huduma safi huku wananchi wakilanguliwa na kulishwa huduma mbovu? Au ni yale yale ya TBS ambayo maana yake imegeuka kuwa Tanzania Bureau of Substandards?
Nisingependa niandike mengi leo zaidi ya kukutaarifu kuwa janja ya wawekezaji hasa kwenye nishati na mawasiliano ilikwisha kujulikana kwa Watanzania.
Kilichobaki ni kukutaarifu kuwa wenzako tunajua kinachoendelea. Tunaumia lakini baya zaidi tunaumiza uchumi wetu na mustakabali wa vizazi vijavyo kwa sababu tu ya upofu na upogo na uroho wa watu wachache wasioona mbele. Kama walioko chini yako hawakwambii ukweli kuhusu ubovu na uhovyo wa huduma za simu basi mie najitoa mhanga kukwambia ili kukuondolea aibu hupo baadaye.
Maana kila kazi na wadhifa vina legacy. Kwa vile Watanzania wameanza kuamka, natumia fursa hii kuwaomba waijie juu wizara yako ikibidi kama hali itaendelea kuwa hivi wewe uwajibishwe ima na yule aliyekuteua au nguvu ya umma. Maana nchi yetu imegeuka shamba la bibi katika kila idara.
Ndugu waziri, kwa ufupi hizo ndizo salamu na lawama zangu leo. Nategemea kusikia toka kwako mapema iwezekanavyo ima kwa kujibu kupitia vyombo vya habari au kurekebisha makosa niliyotaja. Kwa heshima na taadhima.
Chanzo:Tanzania Daima Aprili 25, 2012.

No comments: