The Chant of Savant

Wednesday 25 April 2012

Mmeigeuza Tanzania nchi ya majambazi?

Mkurugenzi wa Uendeshaji Biashara wa NHC, Shambwe na  Meneja Uhusiano wa NHC Sanguya wakizindua utapeli wa nyumba kuuza nyumba za Ubungo mwaka 2011..
Hakuna kitu kimetutisha na kutushangaza kama tangazo la Shirika la Nyumba la Taifa (NHC) la kuuza nyumba maeneo ya Ilala. Ukiangalia tangazo mwanzoni ni zuri tu. Lakini ukifikia kwenye kipengee cha bei ya nyumba zinazoitwa za watu wa kawaida, unapata kichefuchefu.  Bila aibu wanasema eti nyumba moja ni shilingi 168,239,748.62 tena bila VAT! Kwa mujibu wa Mkurugenzi wa Uendeshaji Biashara, David Shambwe, hiyo ndiyo eti bei wanayoona inamfaa mwananchi wa kawaida!  Ukifanya hesabu ya haraka ni kwamba ili mfanyakazi au mkulima kununua nyumba moja anapaswa kufanya kazi kwa miaka 35 akiwa anapokea mshahara wa shilingi 400,578.83 kwa mwezi. Na kama anapata kiwango hicho cha mshahara ahakikishe hatumii hata senti tano ndipo aweze kuwa na kiwango kinachotakiwa. Utakaposhangaa nusu ya kufa ni pale utakapogundua kuwa wengi wa watakaonunua nyumba hizi tena bila kukopa benki kuwa vijana ambao hawajafikia hata miaka 50. Je ni watanzania wangapi wa kawaida wanapata mshahara kiasi hicho? Shame on you! Hivi kweli watu wa kawaida ambao karibu kwa maisha yao wengi wao walikuwa wajamaa haya mamilioni ya shilingi wayatoe wapi kama siyo kufanya ujambazi na ufisadi? Je hii ni biashara au ni aina nyingine ya wakubwa kutumia cha biashara kuhalalisha pesa yao chafu? Haiwezekani mtu wa kawaida mkulima na mfanyakazi akapata hiyo pesa bila kuwapo jinai nyuma yake. Je namna hii siyo kuigeuza Tanzania nchi ya majambazi na wauza unga? Ajabu hata serikali nayo inachekelea wakati hii ni taarifa kuwa asiyeliibia taifa au kujihusisha na biashara haramu alie tu hatapata kuwa na nyumba kwenye maeneo yaliyopimwa na yanaoyoeleweka.

No comments: