Wednesday, 25 April 2012

Nakwenda zangu Brazil kubembea


Image Detail

BAADA ya kuona walevi wakinisakama kuwa kijiwe kimedorora na wakitaka eti nipunguze safari zangu kutembelea vijiwe vingine, niliamua kuwa kichwa ngumu na kwenda zangu kwenye nchi ya Samba ili kupunguza mawazo. Si unajua nilivyochoka kule Arushameru kabla ya aibu kujiri.
Wale wenye mzuka wa ujambazi msianze kujiandaa kuninyotoa roho nikirejea midhani nimejaza midola uvunguni mwa kitanda kama jamaa yangu mwendazake Bingwa wa Muthangarika alivyokutwa amejaza midola baada ya kurejesha namba.
Ukweli ni kwamba pesa niliyotumia na bi mkubwa na washikaji zangu wengine kina Mbwa Mwitu, Muhunidini Misupu, Mgosi Machungi na wengine ambao ni top secret kwenda kuwaona kina Romario, Maximo, Ronaldo, Robinho, Bebeto na wengine, zilitoka kwa wafadhili.
Pia msihangaike kulaani kuwa natumia vibaya. Mali ya umma haiumi. Hivi nani anakataa kulipwa tena kwa pesa za kigeni kwa kwenda kutalii na kujilisha pepo? Hivi kweli ungekuwa wewe ungeutema huu ulaji wa dezo?
Basi mwenzenu mseme sana hata mniite majina ya mtalii, Vasco da Gama, Sindbad, Mzamiaji na mengine mabovu mie siachi kula kuku na shosti wangu.
Kwanza, kwenye kijiwe hatuna mambo ya kipuuzi ya kina Mamadou Sanugu Haya. Najua fika kuwa wenye wivu wananiita kila majina kuanzia hayo niliyotaja hapo juu hata mengine ya ajabu kama mpenda ulaji hasa kujipeleka misibani ili kupata sifa au ubwabwa na mambo mengine.
Kwa vile mimi ni mpenzi mkubwa wa mpira wa miguu na samba, nilikwenda kuona uwanja maarufu wa mpira uitwao Maracana, almaarufu Estádio do Maracanã. Kitu kingine ambacho wanaonipinga na kunipiga madongo hawajui kuwa nilikwenda kutafuta wawekezaji kwenye soka baada ya kugundua kuwa kahawa na rongo rongo nyingine havilipi.
Kwa taarifa yenu nimeongea na Maximo kunitafutia kocha aliyekuwa anaifundisha timu ya Brazil iliyobeba Kombe la Dunia mwaka jana. Hivyo, wapenzi wa soka tegemea maisha bora kwa wote kupitia soka. Maana nshachoka kuona watu wanapoteza muda kuangalia mimechi ya kwa Kameruni wakati nasi tunaweza kuwekeza kwenye mpira wa miguu badala ya vijiwe vya kahawa.
Ngoja niwamegee vinono vya safari yangu. Kwanza, tulifikia kwenye Hoteli ya Golden Tulip Park Plaza.
Alameda Lorena, 360, Jardins, huku wengine waliokuwa kwenye ujumbe wangu kwenda kulala kwenye hoteli mbalimbali kama vile InterCity Premium Ibirapuera kwenye mtaa wa Limao karibu na ule wa Lapa.
Chakula cha Kibrazil nilikuwa nikipata kwenye mitaa ya Tutuape, Pineiro, Pindamonhangapa, Santana na mingine mingi ambayo majina yake nimesahau.
Baada kwenda kwa wenyeji wetu waliokuwa wameahidi kutupa tuisheni ya jinsi ya kulima na kunywa kahawa, nilipewa bonge la ‘hat’ nikatinga kama Cowboy wa jirani ya Brazil pale Texas kwa kina Joji Kichaka wakati wa kuwinda nyoka na kupanda farasi. Ukiona picha yangu nikiwa nimeweka hilo pama lililoandikwa Endakula Embar…. utaipenda maana nilipendeza kichizi.
Baada ya uchovu wa kupigwa tuisheni na kuuramba kama cowboy, tulishuka zetu kwenda kupata mahanjumati ya Kibrazil yaliyokuwa yakiletwa na vimwana wa bei mbaya na warembo sina mfano.
Kama si kuadamana na bi mkubwa si haba ningefaidi kama saba hivi au kufanya UjakobZuma hivi hivi. Basi washirika, tulipikiwa vyakula vitamu vilivyoungwa na nyanya za Kibrazil.
Wenzetu kumbe wana uchungu na kaya yao wakati sisi tuna uchu na yetu! Hili kweli lilinisuta sana kusema ule ukweli ingawa nilikuwa nikichekacheka kama kawa. Kila msosi walioleta ulikuwa na mtu wa kuupigia debe. Kuna kipindi udenda nusu uniue kutokana na jamaa kupiga sana lecture huku akiacha roho ikiniuma kutokana na kunichelewesha kula msosi wa Kibrazil.
Tulijichana makulaji ya Kibrazil kama vile Ambrosia, Feijoada (supu ya nyama), Polenta, Banana Frita (ndizi za kukaangwa), Quejadinhas mahanjumati yaliyoungwa na nazi na mengine mengi nimesahau majina yake. Ila tumbo liliniuma kutokana na kubukanya kama sina akili nzuri.
Kwanza ulizuka ugomvi chumbani na bi mkubwa baada ya kumuuliza kama anaweza kuunga lau nusu ya mahanjumati yale. Lazima nikiwa rais niwatume wapishi wangu kuanzia wa ikulu hadi nyumba ndogo wachukue mafunzo ya upishi kule Brazil.
Kuna watu waliota mchana hadi wakapinda kwa mizengwe yao eti bila ya mimi kuwepo walitaka kuwafukuza washirika wangu kina Mbwamwitu na Machungu kulaleki! Kijiwe ni mali yangu na washirika zangu siyo mali ya wanywa kahawa. Sisi tunakula kijiwe nyinyi mnataka tule jiwe? Hafukuzwi mtu ukiona hapakufai tafuta pa kwenda. Wateule huwa hawaguswi na wachafu. na mtaona nawambia.
Turejee kwenye safari yangu ya Brazil ambayo bahati mbaya au nzuri ilifikia wakati mmoja na ile ya mkuu wa kijiwe ambaye nasikia licha ya kukimbia matatizo ya chama chake akingojea kwenda kumzika Mutarika, alikuwa amempeleka shosti wake English course nchini Brazil pamoja na kupitia New York kuweka vijisenti kwenye akaunti zao.
Nasikia ameamua kumpeleka English course ili kuondoa aibu wanayopata anapokuwa ughaibuni hasa akiombwa kusalimia au kutoa hotuba kwa wale anaowabomu kunufaisha mradi wake binafsi wa kujitajirisha wa MAWAWA.
Pia nasikia alikwenda kumuona bi mkubwa Aisha Rizi Miguriro ili kumwambia asiwe na shaka atachelewesha kuvunja genge lake ili ampe nafasi nyeti. Hayo tuyaache ni yake na mabalaa yake.
Mwenzenu lazima niende kumzika mshirika wangu Bingu the Conqueror or Ngwazi kama wasemavyo wenyewe. Kutokana na kijiwe kupata wafadhili wengi, hata nikienda kwenye msiba nalipwa.
Sasa kwanini niache kwenda wakati kwenda kule inalipa? Kufa kufaana bwana! Isitoshe Mutarika alikuwa swahiba wangu wa karibu kama ambavyo Muludzi alikuwa kwa Che Nkapa ambaye alimtumia Joni Kukomba kuibia Malawi. Hayo tuyaache. Kwa visa zaidi vya Sindbad bin Vasco da Gama tuonane mara nyingine.
Chanzo: Tanzania Daima April 24, 2012.

No comments: