Monday, 2 April 2012

Je huu ni mwanzo wa mwisho wa CCM?


Image Detail


Hakuna ubishi kuwa Chama Cha Mapinduzi (CCM) kimeisha, kimeishiwa, kinachusha na kimeishachokwa na watanzania kutokana na uhuni ambao kimekuwa kikiufanya kwa miaka zaidi ya 50.


Baada ya kung'atuka kwa mwanzilishi wake marehemu mwalimu Julius Nyerere, mvuto wa chama ulikwisha hasa baada ya kuanzishwa kwa sera mama ya ufisadi iliyojulikana kama Ruksa chini ya aliyemrithi mwalimu, Ali Hassan Mwinyi ambaye hata hivyo hatajwi sana kwenye ufisadi ingawa ndiye chimbuko lake.


Mwinyi licha ya kuanza kubomoa misingi madhubuti hasa maadili ya uongozi, alimchosha Nyerere kiasi cha Nyerere kudhani kuwa angeweza kupata mtu aliyemuamini na kumfahamu ambaye angerejesha chama kwenye mstari. Kosa kubwa! Mwalimu alimpendekeza na kumpigia debe mwanafunzi wake Benjamin William Mkapa aliyekuwa rais wa awamu ya tatu na ambaye atakumbukwa kwa kusimika mizizi ya ufisadi na ujambazi kwenye serikali ya Tanzania. Mkapa alivuruga akafanya biashara ikulu na kujimilkisha mali ya umma. Ili kujihakikishia usalama baada ya kufanya uhujumu kwa taifa, Mkapa alianzisha na kuunga mkono wizi wa pesa ya umma chini ya kashfa maarufu ya EPA.


Pesa ya EPA ilitumika kuhonga, kuchafuana,kupambana na hata kumalizana kisiasa nyenzo alizotumia rais wa sasa Jakaya Kikwete ambaye naye ameonekana kushabikia ufisadi kuliko hata Mkapa kutokana naye kuwa tunda la ufisadi. Huo ndiyo uhuni wa CCM tangu aachie ngazi Mwalimu Nyerere.


Ila kadri siku zinavyokwenda watanzania wanaanza kung'amua uhuni wa CCM kiasi cha kuanza kuitia adabu. Mfano wa karibu ni uchaguzi mdogo uliopita huko Arumeru Mashariki ambapo CCM ilipoteza pamoja na kujaribu upuuzi na uhuni wote bila mafanikio. Hakuna jambo ambalo limeivua nguo CCM licha ya uhuni wake wa muda mrefu kama kuwatumia wapiga debe wasiopiga miswaki sawasawa. Hawa ni kuanza Mkapa, waziri katika ofisi ya rais, Stephen Wassira na baba yao Livingstone Lusinde waliogeuza sera za chama kuwa uongo na matusi tena ya nguoni.


Hakika CCM inaanza kupata pensheni ya uhuni wake huku ikivuna ilichopanda. Je huu ni mwanzo wa mwisho wa CCM? Alluta Continua.

No comments: