Rais mstaafu wa Baraza la Mapinduzi la Zanzibar Amani Abeid Karume pichani.
Rais mstaafu wa Zanzibar, Amani
Abeid Karume, amekumbwa na kashfa akidaiwa kutoa amri ya kukodishwa kwa majengo
ya Mambo Msiige bila kufuata utaratibu na sheria.
Tume iliyoundwa na Baraza la
Wawakilishi Zanzibar kuchunguza pamoja na mambo mengine, ukodishaji wa ardhi na
majengo ya Serikali, imebaini Mambo Msiige ilikodishwa kwa miaka 99 thamani ya
dola za Marekani milioni 1.5 kinyume cha sheria
Kwa mujibu wa Ripoti ya Uchunguzi
wa kamati hiyo iliyoongozwa na Mwakilishi wa Chakechake, Omar Ali Shehe,
majengo hayo yalikodishwa kwa Kampuni ya ASB Holdings Limited kupitia taratibu
ambazo hazikuzingatia maslahi ya Taifa.
Ripoti ya kamati hiyo inaonyesha
kuwa ukodishwaji huo ulifanyika baada ya Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais (Ikulu)
Dk Mwinyihaji Makame Mwadini, kupewa agizo na Rais Karume (mstaafu) kwa
maandishi.
“Dk Mwinyihaji aliiambia kamati
kuwa yeye ndiye aliyepokea agizo kwa wino mwekundu kutoka kwa Rais na
Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk Amani Abeid Karume kuwa Serikali imepata
mwekezaji kampuni ya ASB Holdings Ltd, “sehemu ya ripoti hiyo ilikariri maelezo
ya Waziri Mwadini alipohojiwa na kamati hiyo.
Kwa mujibu ripoti hiyo, Dk
Mwadini aliiambia kamati kuwa Rais aliagiza kampuni hiyo ikodishwe kwa mkataba
wa malipo ya Dola milioni 1.5 na kulipa kiasi cha Dola 10,000 kwa mwaka.
Kwa agizo hilo, Dk Mwadini
alimwandikia barua Katibu Mkuu Wizara ya Fedha na uchumi Zanzibar akimwarifu
kupokea fedha kutoka kwa mwekezaji huyo ili aweze kujenga hoteli ya nyota tano
na kwamba baada ya kupokea malipo hayo afungue akaunti maalum ya kutunza fedha
hizo.
Hata hivyo, kwa mujibu wa ripoti
hiyo, Dk Mwadini alipotakiwa kutoa mbele ya kamati ushahidi wa agizo la rais
alikataa na kusema kutoa dokezo la rais ambalo limeandikwa kwa wino mwekundu
siyo sawa.
“Mpaka wakati huu tunawasilisha
ripoti hii agizo la maandishi kutoka kwa rais halikutolewa na Dk Mwadini mbele
ya kamati ya uchunguzi.” Kwa mujibu wa ripoti hiyo yenye kurasa 224.
Hata hivyo, ripoti hiyo imesema
kwamba pamoja Kamati hiyo kumtaka Katibu wa Baraza kumwandikia Barua ya Desemba
8, mwaka 2011 ya kumtaka kuwasilisha ushahidi wa agizo la Rais mstaafu
ameshindwa na kuendelea kutetea msimamo wake kuwa ni “Siri ya serikali.”
Kamati hiyo ya uchunguzi imebaini
kuwa nyaraka za mpango wa ukodishwaji majengo na ufukwe wa Shangani zimepotea
Wizara ya Ardhi, makazi, Maji, na nishati katika mazingira ya kutatanisha.
“ Katika mafaili ya Ofisi hakuna
hata barua ya maombi ya ukodishwaji yaliyofanywa na mwekezaji mwenyewe, kwa
ufupi hata faili lenye kumbukumbu za “Lease’ ya majengo ya Mambo Msiige na
Starehe Club halipo.” Imeeleza Ripoti hiyo.
Chanzo: Nipashe Jumapili.
No comments:
Post a Comment