Gazeti la kila siku la Kiswahili la Mwananchi Jumatatu 9 Aprili mwaka huu lilinistua sana kutokana na kichwa cha habari lilichobeba siku hiyo. Kichwa chenyewe kilisomeka, “Mwanzo, mwisho wa Steven Kanumba, JK aahirisha safari ya ughaibuni kumlilia, kuzikwa kesho.”
Kutokana na kuishi mbali na kutokuwa shabiki wa filamu hasa za kisasa zilizojaa matusi na mambo ya mapenzi tu, ni bahati mbaya kuwa sikumjua Kanumba. Hii ikichangiwa na kutozipenda sanaa za Tanzania hasa muziki ambapo wasanii huimba mapenzi kuanzia asubuhi hadi asubuhi, ni bahati mbaya sana kuwa siwajui wasanii wetu wengi hata kama wanajulikana. Ukiongeza na ukweli kuwa Kanumba alianza kujulikana baada ya mimi kuondoka Tanzania ndiyo basi.
Katika kichwa cha habari tajwa hakuna kitu kilinishangaza kama kusoma kuwa rais Jakaya Kikwete aliahirisha safari ya ughaibuni si kwa kuogopa kuwaongezea mzigo watanzania kutokana na tabia yake ya kupenda kusafiri bali kumlilia Kanumba, nilishangaa na kuanza kujiuliza huyu Kanumba ni nani ambaye umuhimu wake ni mkubwa hivi kiasi cha kuvunja rekodi ya Kikwete katika utendaji wake? Nilijiuliza swali hili kutokana alichofanya wakati wa mgomo wa madaktari ambapo hakuahirisha safari yake kwenda kwenye mkutano ambao hakukuwa muhimu sana kule Davos.
“Nimeguswa na msiba huu, nilikuwa nisafiri lakini nimeamua kuja hapa kuwapa pole ndugu na wasanii wote,” alikaririwa akisema Kikwete. Kumbe Tanzania watu wanazidiana! Kikwete hakuguswa na vifo vya watanzania wakati wa mgomo lakini aliguswa na kifo cha Kanumba. Wasanii wanasifika kwa rais Kikwete kuliko madaktari na wengine? Acha aitwe msanii huenda ni msanii mwenzao. Ama kweli waarabu wa Pemba hujuana kwa vilemba! Huku ndiko kufanya mambo ya hovyo muhimu na ya muhimu hovyo kama tutatangalia ukweli. Niliwahi kulalamikia tabia ya watanzania kuwekeza katika glosari na nyumba za kulala wageni huku wakenya wakiwekeza kwenye viwanda na waganda kwenye kujenga mashule. Hii maana yake ni kwamba tukiungana afrika mashariki, ukitaka maraha utayapata Tanzania. Ukitaka biashara utakwenda Kenya na ukitaka elimu bila shaka Uganda.
Je ni kwanini wasanii ni bora kuliko madaktari? Jibu liko wazi kuwa wanaburudisha na hii ni nchi ya burudani. Ukitaka kujua nimaanishacho, nenda kituo cha polisi kuomba ruhusu ya kucheza ngoma wiki nzima hata kwa kufunga mtaa utapewa. Lakini ukienda kuomba kibali cha kuandamana kupinga uongozi wa kifisadi wa mtaa utawekwa ndani bila shaka. Hii ndiyo Tanzania ya sanaa na maraha. Hata ukiangalia miziki yetu, huongelea burudani hasa mapenzi. Kama wapo wanaoongelea maisha ni wachache sana ukilinganisha na majirani zetu. Hebu sikiliza miziki inayochezwa kwenye vituo vyetu vya radio hata runinga, ni mapenzi, mikasi, matusi na upuuzi mwingine. Zama za miziki inayohimiza kilimo, kuamka mapema kwenda kazini na kusoma kwa bidii ishapitwa na wakati. Hata watawala waliohimiza wananchi kufanya kazi kwa nguvu na kujiendeleza walishapitwa na wakati. Tuna watawala wanaokwenda sambamba na wasanii hasa wanaowatumia kwenye kila kampeni zao za ulaji.
Ingawa kitendo cha rais Jakaya Kikwete kukaririwa akisema kuwa aliahirisha ziara ili kumuomboleza na kumzika Stephen Kanumba kinaweza kuonekana ni cha utu, ukweli ni kwamba kinaacha maswali mengi. Wengi tunajiuliza: Kanumba ni bora kuliko watanzania waliopoteza maisha wakati wa mgomo wa madaktari uliosababishwa na uzembe wa Kikwete?
Je Kikwete amefanya hivyo kwa dhati au kutafuta tukio la kufunika aibu iliyokipata chama chake kushindwa kule Arumeru Mashariki? Je Kikwete ana uchungu na msanii mwenzake kuliko watanzania wenzake? Kikwete alinukuriwa na magazeti akisema, "Nimeguswa na msiba huu, nilikuwa nisafiri lakini nimeamua kuja kuwapa pole ndugu na wasanii wote," Wenye kumbukumbu wanajiuliza: Mbona hakufanya hivyo wakati wa mgomo? Mbona hakuguswa na misiba ya watanzania wakati wa mgomo alipoamua kuwaacha wakilia akaekea zake Davos Uswisi kwenye mkutano ambao hakuwa na umuhimu?
Laiti Kikwete angeahirisha safari yake kwa kuguswa na vifo vya watanzania wakati wa mgomo, angejizolea sifa na heshima kubwa. Maswali yanaendelea. Je ni kutafuta sifa rahisi rahisi au kutaka kujionyesha kama mpenda watu? Je lipi bora, umahiri wa kuhudhuria mazishi na misiba au kutatua kero za wananchi? Washauri wa Kikwete wanapaswa kurejea darasani kujifunza upya. Wafanye hivyo haraka ili kurejesha heshima ya taasisi ya urais bila kujali kuwa anayewashauri kufanya hivyo ni Nkwazi Mhango au nani. Msiangalie majina yetu bali tunayowaambia ili kuepusha aibu inayoendelea kuikumba taasisi ya urais kiasi cha kuanza kuonekana kama taasisi ya urahisi na si urais.
Ingawa ni haki ya rais kumuombolezea ampendaye, anafanya kufanya hivyo kwa kuangalia mantiki ya kufanya hivyo akionyesha hadhi ya cheo chake. Vinginevyo hata kwenye msiba tajwa angeweza kumtuma waziri husika lakini siyo kujifungasha yeye, mkewe, waziri mkuu, makamu wa rais na wengine wengi bila sababu. Kama hakuna namna au tuseme kukwepa aibu ya kichapo cha Arumeru Mashariki, mbona hatukuona umuhimu kama huo kwenye  mazishi ya aliyekuwa shujaa wa vita ya Kagera na mkuu wa majeshi marehemu General Mwita Kiaro?
Chanzo: Tanzania Daima Aprili 18, 2012.