Katika makala ya wiki iliyopita tuligusia japo kwa ufupi udhaifu wa waziri mkuu aliyeachia madaraka kutokana na kashfa ya Richmond. Edward Lowassa. Kashfa hii ililiingizia taifa hasara ya zaidi ya dola za Kimarekani 170,000,000 ukiachia mbali kutumbia kizani kwa miaka sasa. Kiasi hiki kwa taifa maskini kama letu si pesa ndogo.
Pia ni kiasi kikubwa sana cha hasara kusababishwa na mtu mmoja kwa maslahi yake binafsi. Je ni mangapi yaliyofichika ya mtu huyu ambayo yalilisababishia taifa hasara? Je Lowassa hapa naye hapaswi kufanya maamuzi magumu na kuyatoboa, kukiri na kuomba msamaha kabla ya kuanza kutuaminisha kuwa ana uchungu na taifa hili alilochangia kusambaratisha? Kwa wanaokumbuka wajumbe wa Kamati Teule ya Bunge iliyoongozwa na mbunge wa Kyela Dk Harrison Mwakyembe walivyosema kuwa kuna mengine waliyaacha, atajua tunachomaanisha. Je hii ndiyo sababu ya Lowassa kuachia ngazi kirahisi na kutotaka kujitetea kwa kujua wakitaja yote ataumbuka zaidi?
Kutokana na ufinyu wa nafasi, tumelazimika kurejea mada ya jana ili lau iwe changamoto kwa mhusika kutenda haki anayotaka wengine watende. Hapa lazima tutahadharishe. Hatumaanishi kuwa serikali aliyoishauri Lowassa kufanya maamuzi magumu ikiwemo kumshguhulikia yeye isifanye maamuzi magumu.
Katika makala ya leo, tutatumia fursa hii kukazia maoni tuliyotoa kwa kumtaka rasmi Lowassa naye aongoze kwa mfano kwa kufanya maamuzi magumu anayohimiza wenzake wafanye. Katika kufanya hivyo, ahakikishe anaeleza ukweli kuhusiana na yale yanayomhusu binafsi na kama kiongozi hasa uadilifu wake, malengo yake na yote katika yote ataje mali zake.
Tusingependa kurejea aliyosema Lowassa au tuliyoandika wiki jana. Lakini kama tutaangalia ukweli wa aliyosema Lowassa na nafasi yake katika kutekeleza ushauri aliotoa kwa wengine, tunagundua vitu vya ajabu. Kwa mfano, kuna maswali yanaweza kuibuka. Kwanini Lowassa awashauri wengine kufanya kile alichoshindwa kwa zaidi ya miaka kumi? Je alimaanisha nini aliposema ni heri kufanya maamuzi magumu hata kama ni ya makosa ukalaumiwa kuliko kutofanya maamuzi? Je maamuzi magumu ya hovyo kama Richmond ni bora kuliko kutoyafanya kabisa kweli au tunadanganywa? Maana kama Lowassa, kwa mfano, asingefanya maamuzi "magumu" kama ya Richmond, kwa kutofanya maamuzi haya angeweza kuokoa mabilioni ainishwa hapo juu. Tunajaribu kutoa hizo takwimu kuonyesha kuwa si kila maamuzi magumu ni muhimu. Je uamuzi wa kuingiza taifa hasara katika kashfa ya Richmond ni sehemu ya maamuzi magumu? Je kuendelea kuacha nchi iwe kwenye kiza ni maamuzi magumu? Je kutowafikisha akina Lowassa mahakamani si maamuzi magumu kama Richmond?
Kuna swali gumu ambalo linapaswa kuulizwa tena na tena. Kwanini Lowassa ameauona ugonjwa wa kutofanya maamuzi magumu hata kama yanastahili lawama baada ya kuachia ngazi? Na kwanini Lowassa amekaa kimya zaidi ya miaka 15 sasa tangu kurushiwa shutuma za awali za Mwalimu Nyerere? Tujikumbushe kidogo. Lowassa aliumbuka mwaka 1995 pale baba wa taifa alipoamua kumtolea uvivu akasema alikuwa amejilimbikizia mali nyingi isiyo na maelezo. Wakati ule Nyerere akinadi kile kilichokuja kujulikana kama kinyago cha mpapure ulikuwa ni wakati mwafaka wa kujibu hoja na si kunywea. Ni wakati ule umma ulipokuwa umewapokea Kikwete na Lowassa kama marais watarajiwa kabla ya mwalimu kuwakata makali. Tangu wakati ule Lowassa hajawahi kujitetea ukiachia mbali kuongelea kashfa hii inayoonekana kuwa ukweli mtupu kutokana na ithibati ya mwalimu na Lowassa kula jiwe. Hivyo basi, naye atende haki kwa kufanya maamuzi magumu kuelezea anachojua juu ya shutuma zake. Je ya Lowassa ni yale ya nyani kutoona nonihino lake au usanii mtupu? Bomu jingine la Lowassa ni kuendelea kuuhadaa na kuuaminisha umma kuwa alistaafu wakati alitimuliwa kutokana na kashfa ya Richmond. Kwanini naye asifanye maamuzi magumu akaondokana na huku kudanganya na kujidanganya kuwa ni waziri mkuu mstaafu wakati siyo?
Mbali na sifa ya ustaafu asiyokuwa nayo Lowassa, amekuwa akilipwa marupurupu ya ustaafu. Je Lowassa haoni huu ni wizi wa kawaida kupokea malipo asiyostahiki wakati akijua? Je Lowassa alipoishutumu serikali kutofanya maamuzi magumu hakuona kuwa huu nao ni uamuzi mugumu tena wenye lawama kumlipa mtu mamilioni ya shilingi kinyume cha stahiki na sheria? Je kwanini serikali haifanyi maamuzi mepesi yasiyotaka lawama yaani kusimamisha malipo ya Lowassa? Je kama Lowassa amesema aliyosema kwa kutaka aonyeshe alivyo na uchungu na taifa hili, ni kwanini haoni uchungu pale anapoliibia mamilioni asiyostahiki wakati alishasababisha hasara ya mabilioni na nchi kuingia kizani? Hapa hatujagusa hasara aliyosababisha Lowassa kwa kutumia pesa na muda wa umma kwenda Thailand eti kuleta wataalamu wa kutengeneza mvua ambayo nayo haikutengenezwa.
Hili la Lowassa kuendelea kulipwa marupurupu ya ustaafu lapaswa kuangaliwa sana kisheria na kimantiki. Kwanikuendelea kuvuna marupurupu ya ustaafu wakati muda aliokaa madarakani hauruhusu kisheria ukiachia mbali kutoelezea upande wa ukweli aujuao kuhusiana na kadhia hii ni ufisadi tosha. Je Lowassa alisema aliyosema kwa kusukumwa na kisasi cha kuwa nje ya ulaji au kuusaka urais kama inavyodaiwa na asikanushe? Kama kweli Lowassa anautaka urais kama inavyodaiwa na asikanushe sijui kama naye anaamini kuwa anweza kuwa rais wa taifa hili hapo baadaye! Je atufanyie lipi jema wakati uliyokwisha kututenda yanatosha?
Watanzania wanajua kuwa Lowassa ndiye aliyeanzisha mitandao ya kupakana uchafu kwenye uchaguzi. Je Lowassa yuko tayari kufanya maamuzi magumu na kutoa maelezo yake kuhusiana na hili huku akieleza tunavyoweza kutibu majeraha na madhara yaliyotokana na mitandao hii? Lowassa amezungukwa na maswahiba wenye kutia kila aina ya shaka. Wapo walioghushi hata shahada. Je kwanini hafanyi maamuzi magumu kuwashauri nao wafanye maamuzi magumu waachie ngazi?
Tumalizie mjadala wa leo kwa kumshauri Lowassa afanye maamuzi magumu kwa kuanza kutoa utetezi wa kashfa zake. Afanye hivyo kwa kutoa utetezi unaoingia akilini na uliosheheni ukweli na si siasa na kuukwepa ukweli. Haki Lowassa nawe fanya maamuzi magumu.Kwa kufanya hivyo utakuwa umetenda haki kwako binafsi na kwa watanzania kwa ujumla. Kazi kwako bwana Lowassa.
Chanzo: Dira ya Mtanzania Julai 12,2011.
1 comment:
mmetumwa na Mengi na membe nyie dira maskini wakubwa
udsm
Post a Comment