Epistle to Afrophobic South Africa

Epistle to Afrophobic South Africa

Wednesday, 30 November 2011

Lowassa kajivua gamba, kamvika mwenye gamba

HAKUNA ubishi kuwa Rais Jakaya Kikwete alipokuja na dhana ya kujivua gamba, alilenga kutua mizigo ambayo imemwia mizito tangu alipoingia madarakani.
Kwa mawazo yake, alidhani mizigo hiyo ni swahiba wake, Edward Lowassa, Rostam Aziz na Andrew Chenge. Lakini kwa kadiri Rais Kikwete alivyoutega mtego wake, umemnasa hata kabla wale aliowalenga hawajanaswa.

Wakati Kikwete akiandaa mtego alisahau kitu kimoja. Alisahau kuwa alioutega kwenye njia moja hiyo hiyo ambayo alitaka kupitia kurejea salama nyumbani.

Je, angeleaje nyumbani kupitia njia hiyo hiyo asiutegeu mtego au asinaswe nao? Sasa si siri.

Lowassa amemvisha gamba Rais Kikwete kiasi cha kushindwa kuelewa gamba ni nani na nani si gamba. Ingawa Lowassa amejitetea kuhusiana na Richmond, bado hawezi kukwepa kunaswa na mtego wa marehemu baba wa taifa.

Kwa wanaofuatilia hali ya mambo na jeuri ya akina Richmond hadi walipojibadili jina na kuitwa Dowans, wamepata siri ya jeuri yao. Kwa maneno ya Lowassa, hakuna shaka yoyote Richmond-Dowans ni Kikwete.

Hebu tunukuu baadhi ya maneno yake. “Mwenyekiti utakumbuka kwamba mimi nilishaamua kuvunja mkataba wa Richmond mapema, lakini baada ya kukupigia simu ukiwa katika safari nje ya nchi ulisema tusubiri, kwani ulikuwa umepata ushauri wa makatibu wakuu wa wizara, sasa leo hii ninahukumiwa nakuitwa fisadi kwanini?”

Je, Rais Kikwete aliingilia mchakato mzima bila faida binafsi? Je, anayevunja kanuni na kuvuruga utawala wa sheria anafaa kuendelea kuongoza nchi ambayo kimsingi anaikwamishwa kwa sababu zake binafsi?

Hapa hakuna shaka kuwa kitendo cha Rais Kikwete kumzuia Lowassa kuvunja mkataba kililenga kulinda masilahi fulani ya rais ambayo hata hivyo hayatajwi kwenye utetezi huu jadidi wa Lowassa.

Je, tujiulize swali moja, kwanini utetezi huu haukutolewa mapema? Jibu analitoa Lowassa kuonyesha kuwa la Rais Kikwete na Lowassa ni moja.

Anasema, “Nilijiuzulu kuwajibika kwa ajili ya kuilinda serikali yangu na kwa heshima ya chama changu, sasa kwanini leo nahukumiwa kwa jambo hili, tena natukanwa na wana CCM wenzangu na si wapinzani nchi nzima kwamba mimi eti fisadi?”

Kwa jinsi Lowassa alivyoyapanga maneno yake, kwanza anataka aonewe huruma kama mbuzi wa shughuli tuseme alitolewa kafara.

Pili, anataka kumkumbusha Kikwete kuwa asingejitoa kuubeba msalaba wake naye Rais Kikwete kwa pamoja wote wangekuwa msalabani.

Pia ni taarifa kwa Rais Kikwete wakati wake naye kubeba msalaba wa Lowassa ni huu. Na kweli, Lowassa amefanikiwa kuzima harakati na shinikizo la kuvuliwa nyadhifa zake na kuadhirika.

Laiti Rostam Aziz asingefanya papara, naye angegoma. Maana mgomo na ushawishi na siri vya Lowassa havikumwokoa peke yake bali hata mwenzake Chenge.

Kimsingi, hoja ya Lowassa ina mashiko kuwa magamba ndani ya CCM si mawili wala matatu bali wote. Hali inakuwa mbaya zaidi gamba kuu linapokuwa rais na mwenyekiti wa CCM ambaye kwa kiasi fulani anaweza kuonekana mnafiki kuanzisha harakati hii bila kujua kuwa naye ni sehemu ya gamba tena nene kuliko yote.

Kimsingi, Lowassa amefanikiwa kuvua gamba lake na kumvisha mwenye gamba. Tumesema. Lakini hatukusikilizwa.

Kitu kingine ambacho Lowassa amefanya ni kuthibitisha ukweli wa madai ya Dk. Willibrod Slaa, Katibu Mkuu wa CHADEMA aliyetoa orodha ya mafisadi kule Mwembe Yanga ikiongozwa na Rais Kikwete mwenyewe.

Rais Kikwete alijitahidi kutojibu tuhuma za Dk. Slaa akidhani zitajifia na kuwang’ang’ania wenzake, asijue ikifika siku ya kifo kila mtu atapambana kuokoa nafsi yake kama alivyofanya Lowassa.

Hivyo tuhitimishe kwa kusema kuwa mchawi aliyekuwa akitafutwa na CCM kumbe ni mwenyekiti wao! Je, Rais Kikwete ameelewa amedhalilika kiasi gani kwa kuwahadaa watu wake kuwa anaweza kupambana na ufisadi wakati yeye pia ni kati ya watuhumiwa wa ufisadi huo huo?

Tumalizie kwa maneno mengine ya Lowassa. Anasema, “Mwenyekiti nikukumbushe mwaka 1997 kule Zanzibar, kina mzee Daudi Mwakawago walikuja na mafaili yakiwa na tuhuma dhidi ya mtizamo hasi wa jamii dhidi yako, kwa hiyo wakati ule kama si busara za kina mzee Mkapa (Benjamin) leo usingekuwa hapo ulipo.”

Kauli hii ina ujumbe mahususi kuwa Rais Kikwete asijisahau. Pili, ni kumkumbusha kuwa, licha ya kuchafuka kiasi cha kutotamanika, bado ana rungu la urais ambalo anaweza kutumia kumwokoa Lowassa ili aweze kuendelea na mbio zake za kuusaka urais mwaka 2015.

Ukweli huu umo kwenye maneno haya ya Lowassa, “Mwenyekiti nikukumbushe jambo jingine, kule Zanzibar mwaka 1997 walipoleta tuhuma za mtizamo wa umma dhidi yako, ulisema kwamba kuwa rais ni mipango ya Mungu.”

Wengi wanangojea kuona kitu gani kingine atafanya Kikwete kuepuka aibu hii. Pia hapa ndipo siri ya kuenguliwa kwa spika wa zamani na Waziri wa Jumuiya ya Ushirikiano wa Afrika Mashariki Samuel Sitta inapojulikana.

Maana, kimsingi, Bunge ilipaswa likae na kuangalia kashfa ya Richmond upya pamoja na ukweli kuwa rais na Lowassa (waziri) mkuu licha ya kulidanganya Bunge na taifa, walificha ukweli kwa faida zao binafsi.

Hakika, huu ni mtihani mwingine kwa Spika wa sasa Anne Makinda na tuhuma kuwa alipachikwa pale kufua nguo chafu za serikali. Ajabu ya maajabu, bado magamba haya yanawafuatafuata kina Sitta kutaka kuwaadhibu pale ambapo wanapaswa kuadhibiwa wao.

Je, wabunge wetu nao watakubali kugeuzwa nepi za vigogo Ikulu? Pia kuna haja ya kuangalia upya hata haya malipo ya Dowans bin Richmond. Maana kutokana na shutuma hizi mpya ni kwamba anayelipwa ni mwenzetu na watu wake na ndiyo maana hataki kutetea wananchi dhidi ya ujambazi huu wa mchana.

Hakika Kikwete naye tuseme ni gamba. Anapaswa kujiwajibisha au kuwajibishwa mara moja kutokana na tuhuma hizo.

Hapa ndipo upinzani unapopaswa kuachana na majadiliano na kuingia mitaani ili haki itendeke - kieleweke. Kazi kwetu.

Chanzo: Tanzania Daima Nov. 30, 2011.

Mwenye Richmond kafunuliwaBAADA ya kuomboleza kifo cha rafiki, kipenzi na ndugu yangu Ya Mlamali bin Mohammad bin Abdussalaamu bin Humahidi bin Abu Minyaaaar bin Humahid bin Nairal al Fusso Kashafi, sasa umefika wakati wa kusoma hitma yake.

Hivyo wiki hii wanywa kahawa watakunywa kahawa na kula kashata bure ili kumkumbuka mwenzetu.

Hata hivyo katika kumkumbuka ndugu yetu huyu, nitatumia fursa hii kujirekebisha na kurekebisha baadhi ya mambo kuhusiana na ninavyotawala kijiwe. Hivyo, huu utakuwa ni wakati mkubwa wa kutafakari mustakabali wa kijiwe.

Katika kufanya tafakuri jadidi nitafanya baadhi mambo ambayo nataka kila mwanakijiwe ajue.

Mosi, nitakomesha kuendesha kijiwe kama mali ya familia au shamba la bibi. Mke wangu na kitegemezi changu na walamba viatu wote kijiweni nimeishawaambia kuwa nitawavua magamba.

Mie sitaogopa kama wale wanyama wenye magamba wanaoogopa kuvuana magamba. Niseme wazi. Hata gamba liwe nene kiasi gani nitalivua bila woga wala kuzungusha.

Hakuna cha gamba kugomea kiunoni wala urafiki wa chumbani wala barabarani kama wale. Maana nimejifunza kuwa kutawala kwa kutumia ukoo, kujuana, udini, uanachama na kulipana fadhila hauna tija na kama tija ipo si nyingine bali mauti tena ya aibu kama yaliyomkuta rafiki yangu Kashafi ya kuuawa kama kibaka mwizi wa kuku wakati alikuwa mtu mkubwa tu.

Nimeamua vitegemezi vyangu vijitafutie kama nilivyojitafutia badala ya kuniganda mgongoni kama kupe. Mbona vitegemezi vya mzee Mchonga vimejitafutia na vinaheshimika? Hakuna haja ya ukupe bila sababu tena kwa mgongo wa wanywa kahawa.

Hata bi mkubwa nimempa wazi kuwa ukupe mwisho. Niko tayari hata kumtaliki kama hatataka kubadilika na kuachana na ukupe. Mbona bi mkubwa Mary Mchonga anaishi tena kwa heshima? Kwani yeye ni nani aishi kama kupe wakati kupe mwenyewe anategemea damu ya ng’ombe. Bila ng’ombe kupe hana damu. Ng’ombe akiamua kukanyaga na kumsagasaga kupe hana wa kumzuia.

Kitu kingine ambacho nataka kieleweki ni kwamba nitawapuuzia waramba viatu wangu ambao wengi ni vibaka tu wanaonitumia. Maana likibumburuka na siku yangu ikitimia hawatabeba msalaba wangu nami zaidi ya kunigeuka kama akina Jibirili walivyomgeuka Kashafi na sasa kuula wakati wao hao hao ndiyo waliokuwa wakimtukuza na kumwambia uongo asijue walikuwa wakimchuuza.

Hapa kina Ewassa wangu na Endelea Chenga nasema mlie na mliwe tu. Lazima niwavua magamba bila kuoneana aibu. Nitatumia staili ya kumuua nyani bila kuwaangalia usoni ili nisiwasamehe. Nasema muelewe. Mie si mwoga wala msanii. Nitafanya kweli potelea mbali liwalo na liwe-lazima magamba yavuliwe hata kama ni kwa kuchana ngozi ya mtu.

Na katika hili sitaitisha vikao vya woga na upotezaji pesa za umma wa wanywa kahawa. Nitaamka kama chizi nakwenda kijiweni na kutangaza kuwa fulani na fulani na fulani na fulani nimewatimua uanachama wa kijiwe. Finish. Nisikie mtu akifanya fyoko atajua kama kahawa ni mma au maji.

Kitu kingine ambacho nimejifunza toka kwa Kashafi ni kuishi kwa kujilisha pepo na kupuuzia ukweli nisijue hautanipuuzia wala kunisamehe. Avumaye baharini papa nimegundua.

Nikiendelea kujilisha pepo wakati wanywa kahawa wakizidi kuishi kwa upepo kama magurudumu ya gari na baiskeli wataninyotoa roho siku moja tena kama kibaka. Aku! Singoji yanikute kama Kashafi mie.

Kitu kingine ninachoapa kuachana nacho ni usanii na ubabe. Hauna tija zaidi ya kuwafundisha wanywa kahawa ubabe halafu wanigeuzie kibao kama alivyofanyiwa Kashafi.

Kitu kingine ambacho nimejifunza toka kwa Kashafi na ninakitafakari kwenye hitma yake ni ukweli kuwa kila chenye mwanzo shurti kiwe na mwisho. Isitoshe, nimegundua kuwa unaweza kuwafanya watawaliwa mafala nao wakazuga kwa kujifanya mafala kumbe wanapanga kukunyotoa roho tena kinoma kama walivyomfanyia swahiba na ndugu yangu Kashafi.

Singoji yanifike. Heri nionekane mwoga nipone kuliko kujifanya jabali na mbabe nikaishia kunyotolewa roho nikimwaga michozi kama kichanga kama alivyofanya Kashafi.

Juzi nilimsikia mwanae akiongea habari za ki-al-Qaida akisema eti alijeruhiwa na makafiri na si wapendwa wake wa Libya! Kweli za mwizi zikifika-utasikia kila kitu.

Anadhani Walibya ni mafala wa zama zile za dingi wake. Too late dear, those guys are going to send you to the gallows just soon son. Zamu yenu ya kutesa kwishnei bwana mdogo Sefu al Islaaaam.

Kitu kingine nilichojifunza ni kwamba ngurumbili hawatabiriki wala kuaminika. Ni makosa kuwatabiri na kuwaamini kiasi cha kuwafanyia utakavyo ukidhani ni wanyama kumbe wanadeku kila kitu na kukuchora na kukusanifu hasa siku wakikupata.

Kuwa muwazi na mdemokrasia Kung’atuka kama mzee Mchonga ili nising’ang’anie na kuishia kunyotolewa roho kama kibaka.

Tumalizie na kutoa somo kuwa katika hitma hii tumejifunza kuwa kumbe Richmonduli wapo wawili.

Mzee mzima hatimaye amefichuliwa kuwa ndiye kila kitu na kama ni kuvuana magamba basi avuliwe yeye kwanza.

Maana ushahidi wote umemwingiza na kumbana vilivyo. Kwa vile jamaa ni bingwa wa sanaa na wadanganyika ni wapenzi wa sanaa huenda atanusurika. Ila hali ilivyo, enough is enough.

Haiingii akilini kama watanusurika badala ya kukashafiwa tena kwa aibu zaidi ya Kashafi.

Acha niishie nijiandae kwenda Tahrir Square kudai Njaa Kaya na Ewassa na hata Makidamakida wao wawajibishwe kwa kutiwa kitanzini na kuzomewa kuliko hata Kashafi.

Nasikia ving’ora vyake. Acha nianze kuzomea. Hilo, hilo, gamba kuuu, kubwa.

Chanzo:Tanzania Daima Nov. 30, 2011.

Tuesday, 29 November 2011

Siku kanisa lilipomuasi bwana na kudondokea mfukoni


Edward Lowassa mtuhumiwa mkuu wa ufisadi chamani mwake, amebadili mbinu ya kuusaka urais. Ameamua kuwatumia viongozi waroho na vipofu wa kidini walioishiwa roho mtakatifu na kujaa roho mtakakitu.
Kama kondoo, wanaswagwa kwenda wasikojua isipokuwa matumbo yao. Bahati mbaya sana, mbwamwitu hawa wanataka na kuwaburuza kondoo huko kwa mafisi? Je anachofanya Lowassa si udini wa wazi wazi? Mbona hatumuoni akichangia misikiti? Je makanisa yamefilisika kiakili na kiuchumi kiasi cha kujengwa kwa kutegemea pesa chafu? Tunaipeleka wapi jamii iwapo wanaodhaniwa kuwa viongozi wa kiroho wamegeuka kuwa viongozi wa uroho? Kesho Kikwete akianza kumwaga pesa misikitini maaskofu waanze kumshambulia wakati wako kitanda kimoja na udini na ufisadi vinavyonuka hakuna mfano?

Monday, 28 November 2011

Mlevi akata rufaa kwa papaBarua kwa mheshimiwa sana papa Benedicto wa 16,
Kwanza nakusalimia kwa jina la Yesu. Naamini hujambo pamoja na watu wako hapo Vatikano. Wenzako huku Uwanja wa Fisi na Bongo kwa ujumla hatuna hali hata hivyo gongo tunapata ingawa polisi wanatusumbua kwa kututoa upepo. Mambo yamezidi kutubana kama mikanda huku wanaotwambia tufunge mikanda wakifungua hata zipu. Wanaitana magamba, mafisi, mafisiahadi na majina mengine ya ajabu ajabu.

Kabla ya kukueleza kilichonisibu na kunisukuma kukuandikia waraka huu, ngoja kwanza nikueleze kuwa mie ni msomi lakini asiye na kazi wala hali bali kujinywea gongo lau nipunguze mateso na mawazo.

Mheshimiwa papa nisamehe. Ngoja kwanza nielezee uzoefu wangu na hali ilivyo kwangu kama kielelezo cha walio wengi katika kiza na mateso yasiyomithalika.

Baada ya kuzisahau na kuzishit shahada zangu nilizopata baada ya kuzisotea siyo kupewa wala kughushi toka chuo kikuu cha Harvard, makufuru yaliyofanywa na kanisa kuu la Kirumi la Mwanza yalinifanya nizikumbuke. Kumbe kila shari ina heri na kila heri yaweza kuwa na shari. Wajua nini? Si nilikuta panya wameishaanza kuzinyea. Kumbe ningechelewa wangeweza hata kutafuna shahada zangu na kuzitumia kutengenezea viota vya kuzaliwa panya wengine. Huu nao ni ufisadi wa mapanya so to speak.

Nasisitiza kuwa sikughushi shahada zangu. Nilizihenyekea kula Harvard na aliyenilipia karo na pesa ya kutanua bia wakati ule na kuotesha kirimba tumbo tena majuu si mwingine ni mzee Mchonga mwenyewe na awamu yake ya kwanza ya kila kitu kwa watanzania. Wakati huo Bongo ilikuwa bongo kweli na siyo Danga ya Nyika kama ilivyo sasa.

Je mheshimiwa sorry ndugu papa unajua kuwa huku Danganyana ya Danganyika kanisa lako limeingia kwenye kashfa ya ajabu? Kashfa yenyewe ni kuanza kuwasafisha mafisadi pale wanapotoa pesa. Kinachoendelea hakina tofauti na kile alichokuwa akikifanya muuza mibaraka wa zama za kiza wa kanisa lako kule Ujerumani aitwaye Johann Tetzel ambaye alisema kuwa kadri sarafu idondokavyo kwenye kishubaka cha kukusanyia pesa mwenye roho ya mwenye dhambi hutoka motoni na kuingia peponi. Nadhani unamkumbuka tapeli huyu ambaye makufuru yake yalichochea watu kama Martin Luther, Menno Simmons, Conrad Grebel, Wycliffe John, Melchior Hoffman, John Hut, Balthazar Hubmeier na wengine kuasi kanisa lako na kuunda madhehebu yaliyogeuka tishio baadaye. Anyways, huko kwenye mambo ya radicals and reformation leo siendi nisije nikakuudhi kama hawa walitenda makufuru huku Mwanza.

Ndugu katika Kristo mheshimiwa Papa,
Kwa niaba ya wanywa kahawa wa Danganyika nakuandika mtukutu sorry mtukufu kuwa hekalu la kanisa lako la Kirumi katika jimbo kuu la Mwanza liligeuzwa kuwa pango la wezi pale lilipomkaribisha Eddie Ewassa ambaye huku huitwa gamba kuu namba mbili eti kulichangishia pesa ya kujenga kanisa jingine. Wajua kanisa lako limeuzwa kwa bei gani? Huwezi kuamini lakini ndiyo ukweli-madafu milioni 200. Najua hujui madafu ambayo si kama Lira. Dola moja ni madafu 1900 kwa bei za kilanguzi ambazo zimeanza kuhalalishwa kutokana na wakubwa kuchota pesa za kigeni zilipo na kuzipitisha mlango wa nyuma kuchuma faida.

Ndugu Papa,
Machukizo haya makuu yaliasisiwa na kufanywa na askofu Rulanchi akisaidiana na wadogo zake katika jimbo lake. Baada ya kufanya makufuru hayo, huwezi kuamini eti alifunga safari kwenda kwenye nchi ya voodoo ulipokuwa kukutana nawe wakati huko nyuma aliacha amechafua hekalu! Najua alipofika huko hakukueleza ukweli. Maana hakujua jinsi umma wa walevi ambavyo ungechukulia haya makufuru ya hekalu la bwana kuchangiwa na wezi huku kanisa lako likiwekwa mifukoni mwa watu wezi waroho na wachafu ambao Rulanchi aliwamwagia sifa ambazo hata hajawahi kukumwagia wewe. Hakuna aliyetegemea kuwa vipande thelathini kama vile alivyopewa Yuda kumsaliti Bwana Yesu vingeweza kutumika tena kipindi hiki cha maendeleo makubwa na utajiri wa kutisha wa kanisa lako tukufu. Inashangaza na kukatisha tamaa hadi wanywa kahawa wameamua kukuandikia waraka. Hii ni baada ya kugundua kuwa mamlaka husika huku zimo kitanda kimoja na mafisi wawalao watu ambao sasa wamejipenyeza kwenye hekalu la Bwana.

Huku Uwanja wa Fisi kwenye kijiwe chetu cha kula gongo nasikia maneno machafu yakipita kila mtaa. Wapo wanaosema eti roho mtakatifu siku hizi amepinduliwa na roho mtakakitu. Wengine wanasema kuwa hekalu la Bwana kwa sasa ni halali kuwa pango la wezi ili mradi watoe mshiko. Wapo wanaosema etiuna mpango wa kuanzisha utaratibu wa ubinafsishaji wa Kanisa ili kuongeza mtaji wa kwendea mbinguni. Hali inatisha. Kama wewe au mdogo wake Porikapu Peng’o hamtamchukulia hatua huyu Rulanchi, msichanganye kujikuta mkivuna magugu badala ya mpunga kwenye shamba la Bwana.

Kwa ufupi habari nilizo nazo ni kwamba kuna waamini wa kanisa lako wengi wanaopanga kujiengua na kujiunga na madhehebu mengine na wengine kujinyonga kama hutamwajibisha Rulanchi na genge lake la mafisadi wa kiroho wanaotumia uroho kama roho mtakatifu wakati ni roho mtakachafu.

Nimalizie kwa kukushauri kuwu umwajibisha yeyote mwenye kuvaa ngozi ya kondoo ili kuwahadaa kondoo wa Bwana. Wengi wanashangaa ni dini gani inayoweza kulala kitanda kimoja na mafisadi? Ningeshauri Vatikano isikubali kurejeshwa kwenye enzi za akina Paul Mackincus yule habithi wa kimarekani aliyechafua benki ya Mungu (Banco Ambrosiano) kwa kushikiana na mafia, “Uomini di fiducia”kama akina Licio Gelli, Michele Sindona, Umberto Ortolani, Roberto Calvi na majambazi wengine waliomuua papa John Paul I (Albino Luciano). Kaka papa, nakuomba usiruhusu akina Edwardo Roberto Calvi Ewassa na Andrea Michele Sindano Chenga wa Danganyika waliteke kanisa.

Kwa vile tulivyoheshimiana na Albino Luciani, nguvu zimeniishia na siwezi kuendelea.

Wabanikiwe walioliuza kanisa kwa mafisadi huku waliolinunua wakilaaniwa milele na milele aaamini.

Chanzo: Dira Novemba, 2011.

Thursday, 24 November 2011

Siku Lowassa alipomvisha gamba mwenyewe (Kikwete)
Hakuna ubishi kuwa rais Jakaya Kikwete alipokuja na dhana ya kujivua gamba, alilenga kutua mizigo ambayo imemwia mizito tangu alipoingia madarakani. Mojawapo ya mizigo hiyo ni Edward Lowassa na Andrew Chenge ambaye alimrithi toka kwa mtangulizi wake. Lakini kwa kadri Kikwete alivyoutege mtego wake, umemnasa hata kabla wanyama aliwalenga hawajatia guu mtegoni.

Wakati Kikwete akiandaa mtego alisahau kitu kimoja. Alisahau kuwa aliutega kwenye njia moja hiyo hiyo ambayo alitaka kupitia kurejea salama nyumbani . je angereaje nyumbani kupitia njia hiyo hiyo asiutegeu mtego au asinaswe nao? Sasa siyo siri. Lowassa amemvisha gamba Kikwete kiasi cha kushindwa kuelewa gamba ni nani na nani si gamba. Ingawa Lowassa amejitetea kuhusiana na Richmond, bado hawezi kukwepa kunaswa na mtego wa marehemu baba wa taifa.

Kwa wanaofuatilia hali ya mambo na jeuri ya akina Richmond hadi walipojibadili jina na kuitwa Dowans, wamepata siri ya jeuri yao. Kwa maneno ya Lowassa, hakuna shaka yoyote Richmond-Dowans ni Kikwete. Hebu tunukuu baadhi ya maneno yake. “Mwenyekiti utakumbuka kwamba mimi nilishaamua kuvunja mkataba wa Richmond mapema, lakini baada ya kukupigia simu ukiwa katika safari nje ya nchi ulisema tusubiri kwani ulikuwa umepata ushauri wa makatibu wakuu wa wizara, sasa leo hii ninahukumiwa nakuitwa fisadi kwanini?” Je Kikwete aliingilia mchakato mzima bila faida binafsi? Je rais anayevunja kanuni na kuvuruga utawala wa sheria anafaa kuendelea kuongoza nchi ambayo kimsingi anaikwamishwa kwa tamaa zake?Hapa hakuna shaka kuwa kitendo cha Kikwete kumzuia Lowassa kuvunja mkataba kililenga kulinda maslahi fulani ya rais ambayo hata hivyo hayatajwi kwenye utetezi huu jadidi wa Lowassa. Je tujiulize swali moja, kwanini utetezi huu haukutolewa mapema? Jibu analitoa Lowassa kuonyesha kuwa la Kikwete na Lowassa ni moja. Anasema, “Nilijiuzulu kuwajibika kwa ajili ya kuilinda Serikali yangu na kwa heshima ya chama changu, sasa kwanini leo nahukumiwa kwa jambo hili, tena natukanwa na wana CCM wenzangu na siyo wapinzani nchi nzima kwamba mimi eti fisadi?,”

Kwa jinsi Lowassa alivyoyapanga maneno yake, kwanza anataka aonewe huruma kama mbuzi wa shughuli tuseme kafara. Pili anataka kumkumbusha Kikwete kuwa asingejitoa kuubeba msalaba wake Kikwete wote wangekuwa msambweni. Pia ni taarifa kwa Kikwete kuwa wakati wake naye kubeba msalaba wa Lowassa ni huu. Na kweli, Lowassa amefanikiwa kuzima harakati na shinikizo la kuvuliwa nyadhifa zake na kuadhirika. Laiti Rostam Aziz asingefanya papara, naye angegoma. Maana mgomo na ushawishi na siri vya Lowassa havikumwokoa peke yake bali hata mwenzake Chenge.

Kimsingi, hoja ya Lowassa ina mashiko kuwa magamba ndani ya CCM si mawili wala matatu bali wote. Hali inakuwa mbaya zaidi gamba kuu linapokuwa rais na mwenyekiti wa CCM ambaye kwa kiasi fulani anaweza kuonekana mnafiki kuanzisha harakati hii bila kujua kuwa naye ni sehemu ya gamba tena nenen kuliko yote.

Kimsingi, Lowassa amefanikiwa kuvua gamba lake na kumvisha mwenye gamba. Tumesema. Lakini hatukusikilizwa.

Kitu kingine ambacho Lowassa amefanya ni kuthibitisha ukweli wa madai ya Dk Wilibrod Slaa katibu mkuu wa CHADEMA aliyetoa orodha ya mafisadi kule Mwembe Yanga ikiongozwa na Kikwete mwenyewe. Kikwete alijitahidi kutojibu tuhuma za Slaa akidhani zitajifia na kuwang’ang’ania wenzake asijue ikifika siku ya kifo kila mtu hpambana kuokoa nafsi yake kama alivyofanya Lowassa.

Hivyo tuhitimishe kwa kusema kuwa mchawi aliyekuwa akitafutwa na CCM kumbe ni mwenyekiti wao! Je ni kudhalilika kiasi gani kwa Mwenyekiti wa chama tawala na rais wa nchi kuwahadaa watu wake kuwa anaweza kupambana na ufisadi wakati yeye ndiye fisadi nambari wani?

Tumalizie kwa maneno mengine ya Lowassa. Anasema, “Mwenyekiti nikukumbushe mwaka 1997 kule Zanzibar, kina Mzee Daudi Mwakawago walikuja na mafaili yakiwa na tuhuma dhidi ya mtizamo hasi wa jamii dhidi yako, kwa hiyo wakati ule kama si busara za kina Mzee Mkapa (Benjamin) leo usingekuwa hapo ulipo”.

Kauli hii ina ujumbe mahususi kuwa Kikwete asijisahau. Pili ni kumkumbusha kuwa, licha ya kuchafuka kiasi cha kutotamanika, bado ana rungu la urais ambalo anaweza kutumia kumwokoa Lowassa ili aweze kuendelea na mbio zake za kuusaka urais hapo 2015. Ukweli huu umo kwenye maneno haya ya Lowassa, “ Mwenyekiti nikukumbushe jambo jingine, kule Zanzibar mwaka 1997 walipoleta tuhuma za mtizamo wa umma dhidi yako, ulisema kwamba kuwa Rais ni mipango ya Mungu,”

Wengi wanangojea kuona ni usanii gani mwingine atafanya Kikwete kuepuka aibu hii. Pia hapa ndipo siri ya kuenguliwa kwa spika wa zamani Samuel Sitta inapojulikana. Maana, kimsingi, Bunge ilipaswa likae na kuangalia kashfa ya Richmond upya pamoja na ukweli kuwa rais na Lowassa (waziri) mkuu licha ya kulidanganya bunge na taifa, walificha ukweli kwa faida zao binafsi. Hakika, huu ni mtihani mwingine kwa spika wa sasa Anna Makinda na tuhuma kuwa alipachikwa pale kufua nguo chafu za serikali. Ajabu ya maajabu, bado magamba haya yanawafuatafuata akina Sitta kutaka kuwaadhibu pale ambapo wanapaswa kuadhibiwa wao. Je wabunge wetu nao watakubali kugeuzwa nepi za rais na watu wake? Pia kuna haja ya kuangalia upya hata haya malipo ya Dowans bin Richmond. Maana kutokana na shutuma hizi mpya ni kwamba anayelipwa ni Kikwete na watu wake na ndiyo maana hataki kutetea wananchi dhidi ya ujambazi huu wa mchana.

Hakika Kikwete naye ni bomu au tuseme gamba. Anapaswa kujiwajibisha au kuwajibishwa mara moja kutokana na mateso taifa linayopata kutokana na tamaa zake. Hapa ndipo upinzani unapopaswa kuachana na majadiliano na kuingia mitaani ili haki itendeke-kieleweke. Kazi kwetu.

Wednesday, 23 November 2011

Hoja ya Kikwete kuhusu katiba ni dhaifu

Hivi karibuni rais Jakaya Kikwete alivunja kimya chake cha muda mrefu ingawa kufanya hivyo, hata hivyo hakukuwa na tija yoyote. Wengi walidhani penye kimya kingi kungekuwa na mshindo kiasi cha Kikwete kuja na angalau jambo moja jipya kuhusiana na hali inayolikabili taifa hasa kuzorota kwa uchimi na kuporomoka kwa sarafu yetu. Akiongea na wazee wa Dar es salaam kwenye ukumbi wa PTA, Sabasaba juu ya hali ya uchumi nchini na mchakato wa Katiba, Rais Kikwete alisema atatia saini sheria ya mchakato wa kuunda katiba mpya ambayo inatokana na muswada uliopitishwa na hivi karibuni baada ya kususiwa na wabunge wa upinzani. Hakutaka kugusia uchumi akijua fika atazidi kujipalia mkaa.

Kikwete alikaririwa akisema: “Siku zote katika mchakato wa Katiba, tume huundwa na Rais, sasa iweje sasa?... Rais amepungukiwa sifa kikatiba?” Haieleweki Kikwete alimaanisha nini aliposema siku zote tume huundwa na rais. Kwani lazima rais afanye kila kitu? Kama watawaliwa wanataka katiba mpya kwanini rais aingilie kati utadhani naye ni mtawaliwa. Inaonekana Kikwete bado anafanya mambo kwa kufuata mazoea na mawazo mgando ya kale; badala ya sheria na alama za nyakati. Kama Kikwete angekuwa mweledi wa sheria na mwenye kusoma alama za nyakati vilivyo, asingejidhalilisha kwa kujitetea na kuonekana kung’ang’ania kuwa lazima rais aunde “tume yake” ya kuandika katiba badala ya kuacha umma ufanye kazi hiyo ambayo ni yake kisheria. Inasikitisha; kwani Kikwete ameshindwa kujiuliza swali rahisi- kama awamu tatu zilizopita ambapo marais waliunda katiba- walifanya nini cha mno iwapo hatuna katiba inayoendana na maslahi ya watanzania- hadi kuhitaji katiba mpya. Laiti Kikwete angeelewa suala rahisi kuwa tumo kwenye mchakato wa kuandika katiba mpya inayoendana na mazingira ya sasa baada ya watangulizi wake kufanya mizengwe kwa kuunda tume ambazo hazikufanya lolote la maana zaidi ya kutafuna pesa ya umma na kupokea maelekezo toka kwa walioziunda ili kulinda maslahi yao ya wakati ule na baadaye. Rejea, kwa mfano, rais mstaafu Benjamin Mkapa kuvunja katiba na kuhujumu nchi lakini akaendelea kulindwa na katiba viraka tunayotaka kuipiga teke. Kama tume husika zilizoundwa na marais waliomtangulia Kikwete zingefanya la maana basi tungekuwa tunapoteza muda, pesa na nafasi kuandika katiba mpya.

Alichopaswa kuelewa Kikwete ni kwamba kutia katiba viraka na kuandika katiba upya ni vitu viwili tofauti. Awamu ya kwanza ilitia katiba viraka ili kuendana na mahitaji ya chama kimoja wakati ule baada ya kuunganisha vyama viwili kuwa kimoja. Awamu ya pili iliweka viraka mara tatu mojawapo ikiwa kuvunja na kuua Azimio la Arusha jambo ambalo limetuletea madhara makubwa kijamii kisiasa na kiuchumi. Maana huu wizi tunaoshuhudia ukihalalishwa, ulizaliwa wakati ule. Hata hawa mafisadi wanaotukoga kila uchao wakiiba kila mahali na kulindwa ni zao la viraka vya awamu ya pili. Hili si jambo la kujivunia kwa rais mwenye nia njema na taifa. Je Kikwete anajivunia hili kutokana naye kuwa mnufaika wa ‘mabadiliko” haya ya katiba yaliyowezesha ujambazi kama EPA kufanyika na wahusika kuendelea kuwa kwenye ofisi za umma?

Tukija kwenye awamu ya tatu, kadhalika hamna la maana lililofanyika baada ya serikali kuja na white paper. Serikali ilifanya hivyo kuogopa mawazo ya wananchi yaliyokinzana nayo.

Kwa wanaojua kanuni za uundaji na uandikwaji wa katiba mpya ni kwamba kinachounda katiba si bunge wala kamati teule ya rais bali mkutano wa katiba au constitutional convention ambao hujumuisha asasi mbali mbali na wadau mbali mbali nchi nzima. TumeonaAfrika Kusini na Kenya zilivyoandika katiba zao kutokana na kongamano la kikatiba la umma na si bunge wala tume ya kufinyangwa jikoni mwa rais. Rais anayeng’ang’ania kuandika katiba licha ya kuwa imla ni mwoga wa kushughulikiwa hapo baadaye. Kama kweli Kikwete ametimiza wajibu wake vilivyo anaogopa nini?

Kisheria, katiba ni mkataba kati ya watawaliwa na watawala na ni mali ya umma. Hata kama mamlaka ya rais ni kuunda tume ya katiba kama anavyotaka Kikwete lakini si kuingilia tume husika kama ambavyo imekuwa ikitendeka hapa nchini.

Hivi Kikwete na magwiji wa katiba na sheria kama Profesa Issa Shivji na Joseph Warioba tumsikilize nani? Je kati ya Kikwete na wananchi nani anapaswa kusikilizwa?

Mwaka 1991 na 1992, alisema iliundwa tume nyingine iliyoongozwa na Jaji Francis Nyalali ya kukusanya maoni ya Katiba ya kutoka mfumo wa chama kimoja kwenda vyama vingi. Ajabu maoni ya tume hayakutekelezwa yote au tume haikufanya kazi vilivyo. Maana tusingeendelea kuwa na katiba ya chama kimoja kwenye mfumo wa vyama vingi. Kikwete alikaririwa akisema “Tume hii ilipendekeza sheria 40 zifutwe, zilifutwa na nyingine zinaendelea kufutwa ikiwemo sheria ya kumweka mtu kizuizini,” Huu ni ushahidi wa usanii wa marais. Maana kama suala ilikuwa ni kufuta sheria 40 za kikandamizaji, basi zingefutwa pale pale siyo kwa mdomdo kama ilivyo sasa hata baada ya kupita miaka zaidi ya kumi. Huu ni ushahidi mwingine kuwa tume zinazoundwa na rais badala ya kongamano la katiba ni upotevu wa muda na fedha na usanii wa kawaida ingawa unafanywa na watu wenye madaraka makubwa.

Ingawa Kikwete ametumia muda mwingi kuwashambulia na kuwatisha CHADEMA, tunawashauri wasikubali kutishwa kwa maslahi ya kikundi kidogo cha watu. Kikwete amegeuka imla kwa kupora haki na stahiki ya wananchi na kujiamria la kufanya kuhusiana na mstakabali wao. Rais yupo na atapita lakini umma hautapita. Utakuwapo siku zote. Kikwete hana jipya kwani anatetea tabia ya kuweka katiba viraka ili kulinda maovu ya watawala. Hivyo, umma unapaswa kumpuuzia na kuhakikisha unapambana kupata katiba mpya itokanayo na umma na si rais na wakwasi wenzake wachache. CHADEMA na upinzani kwa ujumla hakikisha mnasimamia hili. Vinginevyo tutaendelea kuchezewa mahepe na CCM kama ambavyo imefanya kwa miaka zaidi ya 50.
Chanzo: Tanzania Daima Nov. 22, 2011.

Siku ahadi hewa zilipotaka kunitokea puani

Mwenzenu nawahabarisha lakini uhai wangu umo hatarini sana. You know what? Si wanakijiwe wamenitolea uvivu na kuniita msukule! Wanadai mimi sina maana wala sababu ya kuendelea kuwa mkuu wao. Kilichonisibu ni vigumu kuelezea hasa baada ya kugundua kuwa walevi wameanza kuzinduka kwenye ulevi na usingizi niliokuwa nikitumia kuwaibia. Sikujua kuwa kumbe walevi nao wana kumbukumbu! Maana, walivyoanza kunizodoa kwa kunipa historia ya jinsi nilivyochaguliwa kwa kishindo cha Tsunami na seiche- (sauti kuu ya Tsunami kwa wale wasiojua seiche). Walinirejesha mwaka 2005 wakati wa uchaguzi ulioniingiza kwenye ulaji wa kijiwe. Walinikumbusha jinsi nilivyoaahidi manywaji na matafunaji ya kahawa na kashata na kunenepeana kama kiti moto au shosti wa kimakonde yule mke wa jamaa yangu anayenenepa kiasi cha kutaka kujaa kwenye ramani ya kaya.

Bado nayakumbuka maneno ya msomi. Alisema, “Nilikuwapo kwenyekampeni ya Mkiti Mpayukaji. Huu ulikuwa ni wakati wa walevi kutwishwa mkenge uliokuwa umetengenezwa na vyombo vya habari vya uchochoron na udaku hasa vya umbea. Vilichonga msukule wetu na kuupa kila aina ya sifa kiasi cha walevi kuuingia mkenge na kuuchagua msukule.” Nilimkata jicho nusu limtoboe ili aache kuniita majina ya ajabu kana kwamba mie ni marehemu.

Yeye hakujali. Aliendelea: “You know what; this msukule did all his flim flams and ended up becoming CEO of walevi.” Mzee Maneno alimkumbusha kwa kuvunja kanuni ya maazimio ya kijiwe. Alisema: “Kimbombo hicho kaka! Hukumbuki tulivyoazimia wiki jana kususia lugha hii hadi jamaa watuombe msamaha?”

Msomi alijitetea haraka na kusema, “Sorry jamani.Lololo! Nimerudia yale yale kama jamaa wa mjengoni wanaobangaiza kimombo na shahada zao za kughushi!”
Alikohoa kidogo na kutupa kipisi chake cha sigara kali na kuendelea: “Samahani jamani. Nilimkumbuka Prince Charles kiasi cha kujikuta naongea kimombo nisijue tumeamua kukisusa hadi watuombe msamaha kwa kutaka kutulazimisha kupitisha sharia za kushikishana ukuta. Si wakawaambie wamanga ambao ni mabingwa wa kamchezo haka au wataliano?”
Kabla ya kumaliza Mbwamwitu alichomekea: “Msikonde wazee. Mei nina mpango wa kwenda kukutana na mama Chazi ili aniombe msamaha kwa niaba yenu au siyo?” Kijiwe hakina mbavu hasa kwa jinsi anavyomtaja mama utadhani ni rahisi kumkaribia kwini! Utani mwingine bwana!

Kuona hivyo Mgosi Machungi alikula mic na kuzoza: “Tinapaswa kurejea kwenye mada ya leo ambayo ni kujadili msukue uliotiingiza mkenge na sasa kuendelea kutitesa bila kutipa kahawa na kashata ulizotuahidi.” Nilimkata jicho Mgosi Machungi hasa nikizingatia kuwa ndiye alikuwa mpamba wangu ambaye alikwenda kuwahonga akina shangingi la Kinshomile Silvia Rweyema, sorry, Rwependekeza kuniandika vizuri.

Baada ya kuona hata wale niliokuwa nikila nao kwa muda mrefu, nilitamani kwenda kwa rafiki yangu Tosh na kuomba aniazime vijana wake wa gesi la kuanzisha fujo liitwalo Fanya Fyoko Ubondwe (FFU) ili liwatie adabu wanywa kahawa kama linavyowafanyia matching guys wanaopinga lisirikali kuwafukuza ili wapishe wale wa kichainizi na kigabacholi. Nilitamani niende mara moja ili wanachopata matching guys wanaoambiwa watafute kwao pa kwenda na kuwaacha wageni wa wateule wanaokula nao kiwapate wanywa kahawa ambao wanaanza kuzibuka kama matching guys na kunikosea adabu kama wanavyokosewa adabu na wale waliowahadaa wakawapa kura za kula.

Nilipokuwa nawaza ni njia gani ya kujinasua na kuhakikisha viherehere wanatia adabu si Mpemba akazidisha maudhi. Alisema: “Si Pemba zama zile kabla ya kufunga ndoa na wabaya wetu tulikuwa na maruhani yakhe. Lakini baada ya maalimu kupata ulaji walahi maruhani yote yametoweka na twaishie raha mstarehe.”

Akiwa anajiandaa kuendelea Mchunguliaji aliingilia kati na kukwanyua mic: “Ami unataka kumdanganya nani? Sema madevu wenu alipowekwa kimada na mafisiahadi kwa kumpa makombo akatulia nanyi mkaingizwa mkenge kama wa Msukule wetu.”

Kabla ya kuendelea nilimuonya. “Mchunguliaji nakuheshimu sana. Chunga ulimi wako ohooooo!” nilimpiga mkwara nisijue kuwa kumbe Mpemba alikuwa na bomu lake!

Maana alikwanyua mic tena na kunena: “Wajua? Heri sie tulipata lau hicho kipande cha ukubwa kuliko huu msukule unokula peke yake nasi tusiambulie hata hicho kipande.”

Nami sikujivunga. Nilizidi kutetea meli yangu isizame. “Msinilaumu bali mjilaumu kwa kuingizwa mkenge. Jilaumuni kwa kupenda hongo. Kwani mie mlinichagua bure? Mara hii mmesahau takrima zangu za kahawa na kashata? Ama kweli hamna adabu wala shukrani.”

Ngonja nitie msisitizo ili mnielewe. Hivi hamkujua kuwa nyie ni watani zangu siyo? Msijeninyotoa roho kama FFU wanavyowanyotoa roho machingas bure.”

Kabla ya kuendelea Msomi aliingilia: Mkiti hatutaki siasa za ki-Njaa Kaya hapa. Ukubali umeshindwa.”

Nami kujiokoa nadandi pwenti ya Msomi na kusema, “ Ni kweli kaya yenu nanyi mnaliwa. Mijitu inaingia kwenye kaya na kujisonda kwenye mabohari na wale watu wa Taasisi ya Kushamirisha Rushwa wanaambiwa. Wakishapata dili wanakwenda kuwatoa upepo na kaya inazidi kujaa mivamizi hadi mjengoni!”

Najifanya hamnazo na kuongea bila kituo: “Mjengoni nako wameishiwa tangu aingie yule mama. Badala ya kujadili maslahi ya walevi wanaonyesha ulevi na ujuha wao! Waulize wadharaulika. Tangu wajifungie mjengoni zaidi ya kulipana marupurupu na posho za makalio wamefanya nini cha maana? FFU inaendelea kunyotoa roho wanywa kahawa wanaoitwa wamachinga wa mawazo na hakuna jamaa wa mjengoni anayelaumu ukiachia wale jamaa wa upingaji ambao wametimiza wajibu wao ingawa wanazidiwa na inzi wa kijani waliojazana huko kutokana na uchafu uliozagaa kila mahali. Yale mainzi yamechana kama malkia wao ambaye amechana kiasi cha kutaka kupasuka!”

Loh! Kumbe kweli nimemix! Basi washikaji mezeeni ilmradi message sent. Ngoja niwahi zangu Idodomya kuona mafisadi wanavyotimuana. See ya guys.

Chanzo:Tanzania Daima Nov. 23, 2011

Saturday, 19 November 2011

Breaking News Saif-al Islam Gaddafi akamatwa


Kila chenye mwanzo kina mwisho. Hatimaye Ridhiwan sorry Saif al Islam Gaddafi mtoto wa imla wa zamani wa Libya aliyeuawa mwezi mmoja uliopitwa amekamatwa na kuashiria mwisho wa utawala wa kimla wa Gaddafi na ukoo wake. Je maimla wanaotumia familia zao kama nguzo ya utawala hasa katika Afrika Mashariki, wamejifunza nini? Kijana mwenye miaka 39 aliyetikisa dunia si kwa sababu ya juhudi zake bali, baba yake kuwa rais hadi yeye kuwazia kuwa rais siku moja, kama baba yake, ameisha kwa aibu ya mwaka, mwezi mmoja baada ya kuuawa kwa baba yake. Tieni akili wahusika.

Thursday, 17 November 2011

CCM kuzikwa au kufufuliwa Dodoma?

Habari zilizofikia vyombo vya habari ni kwamba kwenye vikao vijavyo vya Halmashauri Kuu ya Taifa ya Chama Cha Mapinduzi (CCM), (NEC) na Kamati kuu ya CCM (CC) ambavyo vitaongozwa na Mwenyekiti wake, Rais Jakaya Kikwete vitawavua uanachama makada wake sita kutokana na makosa mbali mbali makubwa yakiwamo kujivua gamba na kuvuruga chama.

cha Hakika hii ni kesi ya mfalme Suleiman. Kikwete na NEC wanapaswa kuwa makini wasije wakakiua chama kilichokwishagawanyika vibaya. Kimsingi, kinachopaswa kufanywa siyo kuongeza namba ya watu wa kufukuza. Maazimio ya kikao kilichokuja na falsafa ya Kikwete ya kujivua gamba yalilenga kuwavua uongozi wanachama watatu yaani Rostam Aziz aliyejivua na Edward Lowassa na Andrew Chenge. Hawa wanne wanaozushiwa tuhuma mpya za kukigawa chama wakati chama kimegawanywa na ufisadi wanatoka wapi? Yetu macho kushuhudia CCM ikiuawa na wale walio wake.
Si vibaya kwa CCM kuongeza idadi ya mafisadi kwa vile inao wengi hata hawa wanaosimamia vikao. Lakini kuwafukuza wale wanaopinga ufisadi itakuwa ni kujipalia mkaa. Upinzani uombe Mungu sana hili litokee unufaike na kuichukua nchi mwaka 2015 ili yale niliyotabiri kwenye vitabu vyangu vya SAA YA UKOMBOZI na NYUMA YA PAZIA yatimie.
Upinzani pia ujitahidi sana kama hili litatokea kuwakataa magamba wanaojulikana. Maana kama watafukuzwa chamani upinzani ukawapokea utakuwa umeruka mkojo na kukanyaga manonihino.

Wednesday, 16 November 2011

Ubadhirifu umechukua nafasi ya uadilifu

TULIPOPATA uhuru mwaka 1961 Watanzania wengi walijenga matumaini kuwa tutasonga mbele na kuondokana na matatizo tuliyokuwa tukikabiliwa nayo.

Mara nyingi, watu waliamini kuwa matatizo kama vile ujinga, umaskini, dhuluma na Maradhi vilikuwa vikisababishwa na utawala wa kikoloni. Hivyo ujio wa utawala wa watu weusi wenyewe ulileta matumaini ingawa hayakudumu kwa muda mrefu.

Serikali ya awamu ya kwanza ilijitahidi kupambana kero tajwa hapo juu chini ya dhana ya maadui wakuu wanne wa taifa.

Mwalimu Julius Nyerere, kwa uadilifu na juhudi vya hali ya juu alipambana na vitu hivi kwa dhati. Mwaka 1976 alitangaza Azimio la Arusha ili kuweza kupata mtaji wa kupambana na maadui wetu wakuu wanne.

Alianzisha Chuo Kikuu cha Dar es salaam na kutaifisha shule zilizokuwa zikiendeshwa na madhehebu ya dini ili kuhakikisha kila Mtanzania anapata elimu tena bure. Alijenga hospitali na kuhakikisha kuwa huduma za afya zinapatikana bure na kuwafikia Watanzania.

Kwa kiasi kikubwa alifanikiwa ikizingatiwa kuwa idadi ya wasomi iliongezeka kiasi cha nchi kuanza kujitosheleza kwa wasomi.

Wakati mwalimu Nyerere akihangaika kupambana na maadui wakuu wanne alikabiliwa na vikwazo kutoka kwa wakoloni wa zamani na mataifa ya kibepari. Lakini hakukata tamaa.

Alifanya alichoweza hadi alipong'atuka mwaka 1985 baada ya kugundua kuwa mambo yalikuwa hayaendi kama alivyotegemea. Kimsingi, mwalimu alituachia mtaji hasa raslimali ambazo alizilinda kwa ajili ya vizazi vijavyo.

Kwa kumbukumbu ni kwamba chini ya Mwalimu, dhahabu tunayochimba na kuuza kwa tani haikuwa imeguswa.

Baada ya mwalimu kuondoka na kuja serikali za shaghalabaghala za ruksa na upuuzi mwingine, ombwe na utapiamlo wa mawazo na sera viliibuka.

Kulianza kuzuka matajiri wa kulala maskini na kuamka wakwasi. Ajabu hakuna aliyeuliza wala kustuka isipokuwa mwalimu aliyehimiza watu kufuata maadili badala ya madili kama ilivyokuja kuzoeleka.

Taratibu taifa letu liliwekwa rehani kwenye mikono ya wezi wa kimataifa walioshirikiana na wale wa nyumbani. Ghafla Watanzania wakajikuta wapweke na wakiwa wasio na wa kuwatetea hasa pale Mwalimu alipoaga dunia.

Taratibu siasa zilianza kutegemea mfuko na uongo wa mtu badala ya sifa na uadilifu. Ubadhilifu ulichukua nafasi ya uadilifu na jinai zikaanza kuhalalishwa chini ya dhana mbali mbali kama vile kukuza uchumi, ubinafsishaji na kasi na ari mpya na mambo mengine kama hayo.

Badala ya wahusika kujenga taifa, walianza kulibomoa kwa kasi ya ajabu kiasi cha taifa letu kuzidi kuwa tegemezi huku uchumi ukiwekwa kwenye mikono ya genge la watu wachache.

Rejea kauli ya aliyekuwa waziri wa viwanda Idd Simba kuwa uchumi wa Tanzania ulikuwa kwenye mikono ya Wahindi wasiozidi kumi. Bahati mbaya tena, Simba alipotoa kauli hii hakuna aliyeshtuka.

Tulianza kuwaona matajiri wakijazana Ikulu hadi mwalimu akaonya kuwa Ikulu ni mahali patakatifu pa patakatifu na si pango la wezi. Nani angemsikiliza wakati alishawapa madaraka?

Mara watawala wakaanza kuuza kila kitu kuanzia rasilimali hadi utu wa watanzania. Ibada za mali na vitu zilianza kushamiri huku uchumia tumbo na utapeli vikahalalishwa kama njia halali za kuupata utajiri.

Mara tukaanza kuona ujio wa marais wadogo watokanao na ukoo wa rais aliyeko madarakani. Mambo yalizidi kuharibika kiasi cha nchi kuwa kama shamba la bibi hadi wafadhili kutuwekea masharti ya kipumbavu kama vile kuridhia ushoga ili tupewe makombo.

Je, hali ikoje? Taifa letu ni kama liko likizoni kiasi cha kila tapeli ajae kuchuma na kuondoka. Rejea wizi kama ule wa Chavda, EPA, Richmond, Dowans, Meremeta, Tangold na mwingine mwingi. Nani anajali iwapo anapata chake cha juu? Je namna hii tutafika au tutalikoroga kama wasemavyo Waswahili kiasi cha kujimbika bila jembe na pakawa hapatoshi? Je, ni kwanini haya hayajatokea?

Sababu kubwa ni utapiamlo wa wananchi kuishi kwa matumaini yasiyokuwepo. Tutoe mifano, ni wapi na lini uliwahi kuona nchi ikikaa kizani kwa zaidi ya mwaka na vurugu za kudai haki hii muhimu zisitokee? Bila shaka ni Tanzania.

Ni wapi sarafu ya nchi iliporomoka kama inaharisha huku gharama za maisha zikipanda na waongo fulani wakaendelea kuhubiri amani waipatayo na kuwawezesha kuhujumu? Bila shaka ni Tanzania pekee.

Ni wapi ambapo watu waliosoma bure walipata madaraka na kuchezea rasilimali za umma huku wakiwauzia watoto wa wananchi waliopigania uhuru na kujenga taifa wanalobomoa kwa kasi ya vichaa na vurugu za kutaka hujuma hii isiendelee zisitokee? Ni Tanzania.

Tanzania Tanzania kila upuuzi na wananchi wanaona na kunyamaza huku wakiishi maisha ya udokozi na jinai nyingine ili bora liende.

Taifa la bora liende ni taifa lenye ombwe na utapiamlo wa kila kitu cha maana.

Wapo wanaosema kuwa taifa letu limechakachuliwa. Karibu kila kitu kimechakachuliwa. Ukweli umechakachuliwa na uongo kuchukua nafasi yake.

Huduma zimechakachuliwa kiasi cha walaji wetu kulishwa uchafu na sumu badala ya huduma. Mfano mdogo ni ulanguzi wa simu ambapo taarifa za hivi karibuni zimeonyesha kuwa ni Tanzania pekee katika Afrika Mashariki kiasi cha kuwalazimisha watanzania waishio nje kupitishia simu zao nchi za jirani hasa Kenya.

Bahati mbaya kuonyesha ombwe na utapiamlo wa sera na mawazo, hili liliporipotiwa si serikali wala mamlaka husika zilitoa maelezo yenye mashiko zaidi ya kunyamaza ama kutupiana mpira.

Kama hamuwezi kutolea maelezo kero za wananchi mnafanya nini madarakani? Kibaya zaidi ni kwamba Watanzania badala ya kukabili matatizo yao ya kutengenezwa na kundi la wezi wachache, wameamua kutumia njia za panya kuendelea kuishi kwa kubangaiza na kusukuma siku.

Mtaishi lini iwapo kila uchao hali inazidi kuwa mbaya? Je, kuna mjomba atakayekuja kuwapigania zaidi ya nyinyi wenyewe?

Ajabu kila siku tunaambiwa kuwa nchi yetu ni shamba la bibi lakini hatuchukii na kuchukua hatua. Badala yake tunanyamaza au kuchekelea. Je, nani alituroga hadi kuwa wa hovyo kiasi hiki na kutendewa mambo ya hovyo na tusichukie. Msemo wangu maarufu ni tuguswe wapi tushituke?

Chanzo: Tanzania Daima Novemba 15, 2011.

Heri nife njaa, ushoga hapana

JUZI nilitaka kuua mtu hivi hivi. Kwanza niwataarifu. Siku hizi nimebadili jina. Naitwa Nkwazi Mhango. Why? Nitawaambia next time.

Si ilitoka habari kuwa Watasha wanataka kutupa misaada kwenye kijiwe lakini kwanza tushikiane ukuta wenyewe kwa wenyewe kijiweni. Kweli akutukanaye, hakuchagulii tusi!

Kwanza mghoshi Machungi aliapa kuua mtu. Maana zilipotoka habari nilimsikia mwenyewe akiongea kisambaa akisema, “Ho tate nane, Mghoshi ndie andose ntambidiza.” (Tafsiri, mie lazima nimmalize atakayenifuata).

Kila mtu alisema lake. Maana kama ni ukoloni huu wa midume kuonana wenyewe kwa wenyewe kisa misaada yao, hapana, tuwaache waendelee wao.

Tukiwa tunatafakari si Mbwamwitu naye katoa mpya eti waziri mkubwa wa Utasha aliyetoa pendekezo la ushoga kumbe naye ni shoga ndiyo maana jina lake anaitwa Davida Kinyonga. Anavaa suti kumbe ni kinyonga ambaye nyuma ya pazia ni shoga la kawaida.

Baada ya habari hii kuibuka, ilizua taharuki na mitafaruko kibao. Msomi Mkatatamaa anasema eti habari hiyo ilifika kijijini kwake ikiwa imechakachuliwa kiasi cha wanakijiwe kuitafsiri eti wameambiwa kuwa wazungu wamemwambia mkuu kuwa wasiporuhusu ndoa za mashoga, hawatapewa misaada.

Mpemba mshenzi kweli. Si alikwenda mbali na kusema, “Wajua, nasikia kuna rahisi wa nchi fulani alikwenda kuomba msaada, akaambiwa ati ashike ukuta.”

Kachokoza nyuki! Kujikomba mwana kijiwe mpya mshabiki wa Chata la Mafisadi alidhani anarushiwa yeye hilo dongo. Alisema, “Uongo mkubwa. Washenzi wakubwa nyie.” Hata kama mkuu wetu wa kijiwe ni ombaomba, nisiwasikie mkisema eti alitaka kuolewa. Laanatullillahi.

“Hivi hawa watasha wana akili kweli?” alihoji mzee Ndevu na kuendelea, “Kwanini wanapenda sana mambo ya kishoga shoga?”

Mzee Maneno alidaki, “Sasa kijiwe kimeazimia kuwasusia. Kuanzia leo hatutaongea kitasha ambacho wajinga wengi hukichukulia kama lugha ya usomi.

Hii ni hatua moja ya kuwasusia hadi watuombe msamaha. Kama wataendelea, basi tutawatuma vijana wetu waende huko huko wamzomee na kumtaka Kinyonga aende akaishi Mombosa, akafanye ushenzi wake aone.” Kijiwe hakina mbavu.

Anaendelea, “ Kama wanadhani huo ni mchezo mwema si watoe wao kwanza waone cha moto kama wanaona mchezo huu mwema, lakini hapa kwenye kaya yetu hapana, tena wakome.

Yaani sipati picha kaya nzima watu wachakachuane kimasomaso kweli? Hii siyo kutengeneza Sodoma na Gomora nyingine?” alimalizia.

Mzee mzima nami nakula mic, “Hata juzi mwanae alipokuja Bongo kuwahadaa wabongo akiwa na kimada wake nilimtokea na kama si polisi kunizuia huenda ningepata kesi kwa kumnasa mtu mbanta.

Anayedhani namfunga kamba ajue siyo. Maana wakati Chaz alipokuwa akitaka kuvuka kwenda zake Kigamboni kushangaa kwanini shilingi inazama na meli inaelea nilikuwa kwenye pantoni ya kwenda Kigamboni.

Baada ya kumuona haraka haraka niliwahamasisha wananchi wamshit. Hata alipopunga mkono wake hakuna aliyejibu. Uliza kama unadhani nadanganya. Nidanganye ili iweje. Nilikuwa nimechukia siku hiyo na kama si jamaa zangu kwenye feri kunikamata ningekufa maji au ningemtia mbanta na kuishia kufungwa.

Najua ningefungwa. Maana pamoja na kuwatukana watu wetu bado baadhi ya wenzetu wenye masilahi naye walimkaribisha kwa bashasha kana kwamba kweli wao si watoto riziki kama alivyowadhania!

Laiti ningekuwa mkuu wa kaya mbona ningemsusa na hata nisingeruhusu dege lake kutua wala kumpa viza ya kuingia nchini. Dhiki nyingine mnaziendekeza hadi kujidhalilisha.

Huu nao ni ushoga wa kisiasa na kimsimamo na mkakati. Chaz alikuwa na jipya gani zaidi yakuja kutalii kwa bei nafuu na kupima maji kuhusiana na kushauriwa tuwape ulaji mashoga kisheria?” Naongea bila kituo ili asitokee mtu akanipoka mic.

Wakati kijiwe kikiwa kimehanikiza kulaani hizi kampeni za kueneza ushoga si Mchunguliaji aliingia na kutufunga macho?

Yeye alisema kuwa amependa sana tusi hili kwa vile wanene wetu wamezidi kuombaomba kiasi cha kutakiwa kulipa eti kwa njia hiyo!

Mchunguliaji alikuwa na furaha utadhani naye alikuwa shoga! Kumbe alikuwa akishangilia jamaa kuumbuliwa kutokana na u-Matonya wao.

Alisikika akisema, “Kaya ina midini kama haina akili nzuri. Mnagawa midini kwa wachukuaji halafu mnakwenda kujidhalilisha kwa kuomba.

Acha wawaombe nanihino mkome.” Pamoja na lugha yake kuwa ya maudhi, kila mtu alishikilia mbavu zake kwa kicheko kiasi cha kuyeyusha hasira iliyokuwa imetawala kijiweni.

Mchunguliaji alikuwa seriyasi kweli. Aliendelea. “ Watasha si wapumbavu kama nyinyi. Wamekuwa wakiwatukana na kugundua kuwa hamstuki. Sasa wameamua kutukana mitusi mizito ili mtie akilini.”

Alikatua kashata yake na kuendelea, “Baada ya kuwatukana tusi la kupamba na miwaya kwa kutangaza ngono mkidhani mnaizuia nanyi kama mataahira mkalishabikia na kuhujumu mila zenu, sasa wameona wawashike pabaya ili mstuke. Maana ukitaka kumpata Mswahili muite shoga.”

Alikunywa kahawa kidogo na kuendelea. “ Hata kama yuko shimoni au darini atatoka na kuja juu hata kama ni shoga kweli.”

Mchunguliaji aliendelea, “Nyie mlishaliwa na kuchakachuliwa sana sema hamjitambui.” Mghoshi aliamka na kutaka kumnasa kibao Mchunguliaji ambaye naye alijitetea. “Mgosi huna haja ya kupandisha ingawa najua wewe bado hujashikishwa ukuta.”

Mgosi alijibu, “Hapo umenena mghoshi. Yaani unatiambia eti wametufanyia ushoga!”

Mchunguliaji hana mbavu anaendelea, “Tuseme ukweli. Tushaliwa sana na kuchakachuliwa sasa wanataka tuchakachuane wenyewe kwa wenyewe tena kiza na hiki we acha tu.”

Mzee mzima nilikuwa nacheka na kuhuzunika kwa pamoja. Niliamua kukwanyua mic na kuwatuliza wanakijiwe.

“Msemayo ni kweli hata kama yanauma. Kaya imechakachuliwa kila kitu. Umeme, kura, madawa, mafuta, bei za vitu, ulaji, hata na nyinyi wenyewe.”

Kikao kilivunjika baada ya jamaa kutaka kuninyotoa kwa kusema eti waliliwa zamani na kuchakachuliwa.
Naona dege la Kameruni linatua. Acha niwahi kumzomea japo kiduchu. Kwa heri!


Chanzo: Tanzania Daima Novemba 15, 2011.

Friday, 11 November 2011

African gay Penguins! Africa must enact pro-gay laws!


African penguins Pedro (R) and Buddy interact with each other at the Toronto Zoo in Toronto November 8, 2011. The Toronto Zoo announced they will separate the penguins after zookeepers noticed behaviour denoting a gay relationship between the two, and pair them with females to help preserve the endangered species. Pedro and Buddy will be reunited after mating with other female penguins.

Are these Penguins real African Penguins or they have became African after the zookeepers noticed that they have some gay behaviours just the same way the British Government wants African government to behave? I am wondering if at all this is the way of exporting homosexuality to Africa or just mere cultural attacks.
After telling African government to enact laws favouring gays, thereafter, the pressure will be exerted to telling African governments to enact law prohibiting dogs to sleep outside houses.
God, where on earth are we heading for? Colonialism? Imperialism? Nihilism? Mental slavery? Sexism? Megalomania? Bulimia? Someone help me out there.

Thursday, 10 November 2011

David Cameron and the West's Perception of Africa


British PM, David Cameron’s warning that his country will not give aid to African countries that don’t favour homosexuality has generated heat amongst Africa countries. According to Zambia, Ghana and Tanzania, this stand is an abuse of high order. In Tanzania, people in rural areas have mistaken the pro-gay edict to mean that Britain wants Africans to embark on homosexuality so as to be given money by donors!

Africans have themselves to blame for this high handed dealing by Britain. African countries have turned donors into a cure-all remedy for their problems, real and unreal. Tired of Africa’s dependence and begging, they have opted for such stupid conditions to cause us thinking on how to emancipate ourselves by utilizing our resources and brains for our good future.

A beggar is a beggar even if he is in a suit or is President. While I do not defend homosexuality, we need to trace the genesis of such unacceptable conditions. When the donors forced us to change our economies for their benefit by embarking on Paris-New-York-London-made deceptive policies that ended up failing, they discovered that we can take any order from them. They thus decided to take us for a ride.

In Tanzania for example, under Structural Adjustment Programs, the government sold all public investment at a throw-away price, worsening the economy. Former president Benjamin Mkapa’s promise that Structural Adjustment Programs would create a modern economy was never realized in Tanzania.

Why should a country like Tanzania that mines gold in tons go cup in hand begging from the same guys it threw gold away to? This is worse than homosexuality so to speak. This is the reason why donors are telling us to do stupid things. They know we are somewhat stupid. They want us to learn. But do we learn?

Begging and dependence has become the means of survival of most African countries. Currently, Tanzania’s budget is 40% dependent on donor aid. Even when we think of unifying East Africa, we still sheepishly go to the donors to fund the venture, the very donors who are afraid that the unity will weaken their influence. We have enough resources to realize the East African Community dream but our lopsided policies, short term thinking and corruption are our undoing.

If we do not put our act together, we have not seen anything yet from our so called ‘development partners.’ The British government must respect Africa and avoid using human rights as a pretext to impose its values on Africa. Why be vocal on pro-gay laws but be silent about other human rights such as worthy education, nutrition, democracy and economic wellbeing that the majority of Africans lack?

Africa ought to know that Western countries are looking for a pretext to stop supporting African countries due to the fact that they have their own burdens at home- the Eurozone crisis. Refer to economic turmoils going on in Greece and Iceland and soon or later Italy.

Africa must urgently identify and address vices that curtail its development. Donors are not smarter than we think. What has brought power to them is nothing but accountability. If Africa embarks on true accountability for whatever governments do, it won’t take time for her to forge ahead and do away with begging.

By giving us stupid conditions, donors are telling us to use our brains instead of stomachs. So who is to blame for such stupid conditions attached on donor money? Our governments that sit on huge resources which they abuse and use as personal property are to blame.

Source: The African Executive Magazine November 9, 2011.

Anayeivuruga CCM kati ya hawa ni nani?

HIVI karibuni gazeti hili liliripoti kisa cha wenyeviti wa mikoa wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), kugawanyika kuhusiana na dhana nzima iliyokwama ya kujivua gamba.

Dhana hii ambayo, kimsingi, ilianzishwa na rais Jakaya Kikwete ama kwa makusudi au bahati mbaya, inaanza kumvua nguo baada ya kuonyesha wazi asivyo na ubavu wa kuwavua gamba watuhumiwa wawili yaani Andrew Chenge, waziri na mwanasheria mkuu wa zamani wa serikali na Mbunge wa Bariadi Mashariki na Edward Lowassa, waziri mkuu wa zamani na mbunge wa Monduli.

Matamshi ya baadhi ya wenyeviti wa mikoa wa CCM yanatia kinyaa ukiachia mbali kuacha swali kama kweli bado CCM ina sera na udhu hata mshikamano. Maana huwezi kuamini kuwa mwenyekiti wa mkoa angeamka na kusema hadharani kuwa waziri fulani afukuzwe uanachama eti kwa vile alimtukana rais.

Tusi lenyewe eti ni kulumbana na spika. Kwanini kwa mfano waziri wa Jumuia ya Afrika Mashariki Samuel (EAC), Sitta atuhumiwe kumtukana rais badala ya spika aliyekuwa akijadili jinsi upatikanaji wake ulivyokuwa mizengwe mitupu?

Kwa mujibu wa gazeti hili la Novemba 2, mwenyekiti wa CCM wa mkoa wa Shinyanga Hamis Mgeja alitaka Sitta atimuliwe kwa vile kwa mujibu wa Mgeja, Sitta alimtukana Rais Kikwete na wajumbe wa CC, kupitia kipindi cha dakika 45, kinachorushwa na kituo kimoja cha TV, akilalamika kwamba waliweka kigezo cha jinsi kwa shinikizo la mafisadi kumuengua kwenye kinyang’anyiro cha uspika ambacho kilijenga mazingira kwa Mama Anna Makinda kupita kirahisi.

Je, si kweli kuwa kigezo hiki walikiweka wao bila kutoa sababu na maelezo ya kufanya hivyo zaidi ya kumzuia Sitta?

Je, kama Sitta ni muongo au alimtukana Kikwete, kwanini Kikwete hakumwajibisha. Hapa anayemtukana Kikwete ni Sitta au Mgeja anayezusha mambo na kutoa ushauri wa uongo na usio na maana? Je Mgeja katumwa na nani kama si mafisadi hao hao ambao wanajulikana walivyo na mitandao nchi nzima. Kwanini kwa mfano Mgeja aone kosa la “kumtukana” rais alilotengeneza kuwa kubwa kuliko anaowatetea ambao, kama ni kumtukana Kikwete wamemtukana matusi ya nguoni kwa kukataa kujivua gamba wakiendelea kushikilia msimamo kuwa hawakukutana na Kikwete barabarani?

Je, ni uongo kuwa Makinda hakuchaguliwa kwa mizengwe ili kumzuia Sitta? Mbona akina Mgeja na wenzake wanakuwa kama hawajui kusoma na kuandika ambapo katiba imeweka wazi kuwa ubaguzi hauruhusiwi nchini?

Nini maana ya binadamu wote ni sawa na Afrika ni moja ambayo ni mojawapo ya ahadi za mwana-CCM. Au ni kwa vile CCM imeegemea wenye nazo kiasi cha kuabudia madili badala ya maadili.

Baada ya kumalizana Sitta ambaye ameishaanza kuwa majeruhi kutokana na kile kinachoeelezewa kuwa ni kula huku na kule, kina Mgeja waliamua kumgeukia Nape Nnauye kuwa anakivuruga chama.

Nape anakivuruga vipi chama? Anataka mafisadi wavuliwe magamba. Wapo wanaoona kama Nape anatimiza maagizo ya bosi wake yaani rais Kikwete ambaye ni mwenyekiti wa CCM. Pia wapo wanaoona kama Kikwete anaogopa kuwakabili watuhumiwa wa ufisadi wanaopaswa kujivua gamba kwa kuogopa wasimvue kofia.

Hili limethibitishwa na maneno ya hivi karibuni ya mtuhumiwa mmojawapo wa ufisadi ambaye alisisitiza kuwa yeye na Kikwete hawakukutana barabarani.

Kwa wanaojua siasa za nchi hii zilivyo chafu walijua kuwa huu ujumbe ulilenga kuwafikia wananchi ili wakate tamaa huku ukimkumbusha Kikwete kuwa ajue rafiki yake anamjua kuliko tunavyomjua. Hivyo apunguze mwendo kwenye kasi yake mpya na ari mpya na nguvu mpya ya kumwagiza Nape awashambulie.

Kuhusiana na Nape ni bahati mbaya kuwa Kikwete hajawahi kukanusha madai kuwa anamtumia kuwashambulia marafiki zake ambao hana ubavu wa kuwaambia “uso kwa uso kuwa tokeni mmechafuka na kuchafua chama.” Wapo wanaoona kama Kikwete hana jinsi na anachofanya ni sawa kwa vile naye alitajwa kwenye orodha hiyo hiyo iliyowazaa hao magamba ya chama chake.

Je, kuna ukweli nyuma ya dhana hii kuwa Kikwete anawagwaya akina Lowassa na hivyo kumtumia Nape? Yote yawezekana. Jiulize Nape anapata wapi jeuri ya kuwakabilia hawa watuhumiwa wakati wengine wamenywea? Yuko wapi Wilson Mukama aliyeingia ofisini na viapo kuwa atakisafisha chama asijue kitamchafua na atanywea kama alivyofanya.

Swali kuu ni je nani wanakivuruga chama kati ya akina Mgeja, Nape, Sitta, Lowassa na Kikwete? Je, kwa wanachama wa CCM kujiweka rehani na kando wasiingilie kunusuru chama chao nao hawakivurugi? Maana inaonekana wanatumika kama kondoo kuswagwa wasipojua wala kutaka bali mswagaji.
Chanzo: Tanzania Daima Novemba 9, 2011.

Mpayukaji aanzisha CCMNAJUA fika kichwa cha habari kitakong’ota wengi hasa wapenzi wa chama twawala. Pia kichwa cha habari kitaaacha hoi kwa mstuko huku viroho vikitweta kudhani nina mpango mchafu wa kukigaddafi kiama tawala.

Sina mpango huu wakati huu na si kwa njia hiyo ingawa kinafaa kufanyiwa hivyo. Kwa taarifa ya walevi ni kwamba nimeanzisha Chama Cha Mahangaiko au Mparaganyiko yaani CCM.

Hii ni baada ya kuona migongano kwenye Chama Chetu cha Magambagamba kuwa na misukosuko na kutaka kunyotoana roho, kuchafuana hata kutumiana.

Juzi hamkuwasikia akina Mjega wakitaka kina Sammy Sixx watimuliwe kwenye kiama wakati wasijue ni wadau wakubwa waliouza kaya kwenye kashfa ya Richmonduli ili wapewe uwaziri wa ulaji baada ya kunyimwa umicrophone.

Turejee kwenye CCM ya Mpayukaji inayochukua nafasi ya TLP yaani Timua Linda Personality yako. Baada ya kusifika kwa kuwafukuza wenzangu Kiarawaarawa, nimeamua kuanzisha zana nyingine ya kuusaka ulaji. Najua wengi wanaguna kusikia kuwa kuna CCM nyingine. Onyo: hii CCM yangu si ya mafisadi wala wasanii wala haina uhusiana na Chama Cha Mapinduzi (CCM). NLangu ni chata la ukombozi wa walevi na wadaganyika toka kizani na kwenye mporomoko wa njuluku na upuuzi mwingine.

Nimekuja na mikakati ya karne ya 21 ambapo badala ya kwenda kwenye majukwaa ya siasa nitatumia misikiti na makanisa kaya nzima kujitangaza na kujenga msingi wa kushinda uchaguzi utakapofika. Kwa vile nimeishachota pesa nyingi ya kahawa na kashata, nitahakikisha wale watu wa “Mungu” waliojazwa roho mtakakitu badala ya roho mtakatifu nawapa misaada kwenye miradi yao ya ulaji ili wanipigie debe na kunisafisha tokana na uchafu niliopakwa na kashfa ya wizi wa pesa ya kahawa na kashata.

Hivyo msishangae kuona siku hizi naingia kwenye nyumba za ibada kama sina akili nzuri. Nani mwenye jeuri ya kuikataa pesa iwapo ana njaa tena aliyoificha nyuma ya joho na jina zuri la mtumishi wa God?

Watu wa God nanyi nawaambia kuwa mchungaji lazima anywe maziwa ya hao awachungao hata kula nyama ya kondoo. Hivyo, msijivunge kuwatumia kondoo wenu kutengeneza ulaji binafsi. Wale ambao wanaendelea kujivunga nawashauri wajiunge nami ili niwatajirishe kwa vijisenti vya kahawa. Pia nasisitiza kuwa kondoo mnaowachunga ni mali yenu binafsi mkimwakilisha “Mungu”.

Msiwaogope wale wanaowaita wapakwa mafuta wa shetani na mbwa mwitu wawararuao kondoo. Kama wanasiasa wanawararua wapiga kura wao kwanini iwe kosa kwenu kuwararua kondoo? Hamuoni akina Katortoise, Gamanyua, Mwakasengesenge, Rwakatarehe na wengine wanavyowararua kondoo na kuwa mabilionea?

Kwa vile mie ni mjanja na si fala wa kutumia masaburi, nimeamua kuanza kampeni mapema. Hivyo kila siku za ibada msishangae kuniona nimezungukwa na mbwamwitu sorry wachungaji wa kondoo wa Bwana. Akina Masikasika na Mokiii wa mwanipata vile.

Najua kuchanganya siasa na dini inakatazwa katika kaya hii. Lakini kwa sisi ambao hatukukutana barabarani na mkuu na kufanya naye urafiki, hili si tatizo. Lazima kulindana. Si mnajua tena. Waarabu wa Pemba. Hivyo msichonge midomo kuanza kuzoza eti jamaa anatumia sehemu za ibada kufanya siasa tena chafu inayoendeshwa na pesa za ufisadi wa kahawa na kashata. Mtajisumbua bure. Mie na jamaa ni damu damu na tumesomea usanii kaya nzima hakuna wa kutufikia.

Juzi nilisikia maadui zangu wakiongozwa na Msomi mkatatamaa aka Sam Six Mwakiwembe kuwa ninatumia fedha za kifisadi kwenye majumba ya Mungu. Ujinga mtupu. Nani si fisadi katika kaya hii? Hata hao wanaoibiwa pesa yao yaani walala kiza si kwamba wanauchukia ufisadi.

Wanatamani ni lini wapate nafasi waufanye. Je, namna hii ufisadi utakwisha? Acha sasa tuupeleke kwenye nyumba za ibada ili ugeuke dini na mungu awe njuluku baada ya yule aliye juu. Mimi sikatai ni fisadi. Je wao si mafisadi?

Kama si mafisadi wanangoja nini kwenye kijiwe iwapo kijiwe kizima kinanuka ufisadi na ufisidunia? Kumbaff nyote mafi ya mbuzi.

Kwa kupeleka njuluku kwenye
mahekalu ya Bwana nasaidia madafu yetu yanayoporomoka kama mgonjwa wa kuharisha kuimarika. Kwa taarifa yenu, kumwaga vijisenti kwangu kunalenga kuimarisha lishiringi lenu linaroporomoka kama ndege iliyozimika injini huku wapuuzi fulani wakizidi kuwaaminisha kuwa haya ni matokeo ya kuvurugika uchumi dunia nzima.

Si kweli, kinachoporomosha madafu yenu ni mipango mibovu, sanaa, ufisadi na matumizi na matanuzi ya wakubwa. Huwezi ukawa na mkuu mzururaji, (Vasco da Gama) njuluku yenu na uchumi vikawa na nguvu. Huwezi kuwa na mafisadi na vidokozi kila kona huku watu wakikwepa kodi wakisaidiwa na waajiriwa wa lisirikali kaya ikasongoa mbele.

Huwezi ukawa na kaya inayowazawadia wezi malipo na marupurupu baada ya kuibia nchi isishuke thamani.

Aloo! Ngoja niwahi chachi nikasuke mipango na wale maaskofu na nikotoka pale nikafanye mikakati na wenyeviti wa mikoa wa CCM yangu. Mpo hapo waliwa?

Naona gari la msajili wa vyama. Acha nimuwahi anisajilie chama chap chap mradi hakitishii maslahi yake binafsi.
Chanzo: Tanzania Daima Novemba 9, 2011.

Wednesday, 9 November 2011

Je huu si unyanyasaji wa wanyama?Mswahili akimning'iniza kuku anakamatwa na kushitakiwa kwa kosa la jinai. Hivi karibuni waziri mhusika alitangaza kuwa atakayewatesa wanyama atafungwa au kutozwa faini kwa maelfu si haba.Ajabu ya maajabu waziri mhusika na serikali yake hakuonyesha kujali kueleza atakachotendwa anayewatesa wanadamu hasa kwa ufisadi na uzembe! Anyway, kuna kipindi wanyama wanakuwa na thamani kuliko binadamu kama mashoga walivyo na haki na thamani kuliko mamilioni ya watu maskini. Turejee kwa wanyama. Picha hiyo hapo juu ni mnyama aina ya kifaru akisafirishwa kwa helkopta umbali wa kilometa 1,500 kama kutoka Dar es salaam hadi DRC tukisie. Zoezi hili lilifanyika huko nchini Afrika kusini. Je kwa kumning'iniza hata kama amekuwa sedated bado si kumnyanyasa? Sina la kusema.

Sunday, 6 November 2011

EID MUBARAK NJEMA

Kapuku akiwa kwenye vazi la "kidini"
Prince Al-Waleed bin Talal Al-Saud na mkewe Ameerah Al Tawaleel
Jakaya Kikwete na mkewe na Al Waleed na Ameerah Al-Tawaleel
Pamoja na kuwatakia Idd Mubarak njema waumini wa kiislam, tunawaletea picha za viongozi wao hasa kutoka Uarabuni na vivazi vyao. Wakati wenzetu wanwavisha mahema wake na dada zao, waarabu wanapiga pamba kinoma. Mmeipata hiyo wajameni? Kwa wenye madaraka ninja kwa wake zao haramun! Tufakari na kujifunza. Unaweza ukaachwa ukaadhini umengojewa.

Friday, 4 November 2011

Mpayukaji kwenda kuchunguza afya India

BAADA ya kuona wazito wote wanaougua wanapelekwa India, Mpayukaji naye ingawa ni mzito wa wanywa kahawa, ameamuru achangiwe madafu kiasi fulani aende kuchunguza afya yake. Sababu nyingine iliyomsukuma Mpayukaji kwenda India ni ile ya maadui zake kwenye kijiwe hasa wale wanaotaka afe wachukue ukuu kudhamiria kumnyotoa roho ima kwa sumu, nondo, kabari au mshale.

Habari za kiintelijensia ambazo Mpayukaji anazo ni kwamba pale kijiweni kuna wabaya wake wanaoongozwa na Mbwamwitu almaarufu akishirikiana na mwenzake.

Shushu wake mkuu mzee Machungi wa Mgosi ametoka Tanga hivi karibuni kutafuta zindiko la uchawi. Kwa vile wabaya wake wanataka kumlisha sumu na juzi amejisikia kuwashwa washwa na ukurutu sehemu za nonihino, ameamua kwenda zake India naye aonje huu ubora unaowapeleka wagogo na vigogo kwenda kutibiwa kule.

Sababu ya tatu ni kwamba kwa vile Mpayukaji anapanga kugombea ukuu wa Kaya, anaenda kule kuona hizo hospitali za kihindi zinazomaliza njuluku za Wadanganyika zimejengwa kwa ubora gani ili akiukwaa azijenge hapa na kuokoa pesa ya walala kizani wa Bongolalaland.

Sababu nyingine inayomfanya Mpayukaji kwenda huko Ugabacholini ni kwenda kuangalia miradi inayoweza kuwa imefichwa kule na wezi wenye maulaji wanaoweza ima kwenda kwenye mahospitali yao au kusuka dili ya kuingiza midawa ya hovyo kama ambayo mamlaka ya midawa inavyolalamikia kutamalaki kwa midawa fweki ambayo mingi inatoka kule na kule kwa Wala kila kitu wa kwa mzee Mao Zedongo.

Kwenda kwa Mpayukaji Ugabacholini ni suto kwa watawala wasiojali masilahi ya kaya zao wakiishia kuzurura na kuficha mifweza nje kama kashafi aliyenyotolewa roho kama kibaka hivi karibuni. Nami nina mpango wa kuwahamasisha walevi na wanywa kahawa tuwanyotoe roho wezi wetu saizi ya Kashafi.

Hata hivyo, mpango wangu wa kwenda kujichunguza afya yangi imayokabiliwa na kuwashwawashwa na ukurutu Ugabacholini haukupita kirahisi. Wanywa kahawa walichachamaa wakidai nakwenda kule kula maraha badala ya kutibiwa kwenye hospitali za hapa.

Mwenzao naumwa kweli. Wao, umaskini wao, walidhani nakwenda kujichana mikuku kule. Kuku gani wawe Ugabacholini iwapo magabacholi wenyewe wanakimbilia Bongolaland wanapokuja mikono mitupu na kuondoka mabilionea kama Chavda? Kule kuna kuku au dhiki tupu na viwanja vya jinai ya kutengeneza ufisadi. Hayo tuyaache kwa leo.

Wapo walioona kama nazusha masahibu ya kutaka kunyotolewa roho ili nipate ujiko na ulinzi wa chee. Waliuliza ni kwanini sikulipoti kwa mandata hasa mkubwa wao yaani PIG. Msisme natukana. Kwa wasiojua kirefu cha PIG ni Police Inspector General na si nguruwe kwa kimombo. Nami niliwajibu kuwa Daktari mwenzangu Mwakiwembe aliporipoti kwa PIG nini kimefanyika zaidi ya kuonekana mzushi hadi yalipomkuta? Nani anajali?

Hata kutoa maelezo hawataki zaidi ya kuahidi kufanya hivyo na kuja na misifa badala ya maelezo. Mwenzenu anaumia nyie mnaleta mashauzi ya kike? Kumbafuni nyote mnaochezea uhai wa wenzenu mkijifanya kuwajali wanapokufa kwa kuwaita mashujaa ambao mapengo yao hayawezi kuzibika wakati mmewazika nyinyi na uovu wenu. Kwani haya hayafanyiki?

Msidhani masihara.

Mwenzenu nawindwa kuuawa ili watu wapate ukuu. Kuna watu wamekwenda hadi urusini na kununua sumu aina polonium ambayo inaua kwa haraka na mateso usiambiwe. Yote haya yanafanyika na hakuna anayejali! Hawa usalama wa Kaya kazi yao nini au kutisha tisha watu na kuchakachua kura za kula? Senzi sana Usalama wa Kaya hamna hata maana. Nyie ni nepi za mafisadi na wauaji mtake mistake. Kumbafuni sana.

Watu wamegeuka wanyama. Yaani pamoja na aibu na mateso yaliyompata Gadhaffu sorry Kashafi bado watu wanatamani madaraka hata kwa kutoa roho za wenzao! Inatisha sana wajameni. Kwa mfano mie na Kijiwe changu tuna nini hadi watu kutaka kuninyotoa roho? Au ni huu ujiko wa shilingi mbili wangu na bi mkubwa kujidai na madaraka ya kijiwe utadhani hayatatutoka siku ikifika?

Nasisitiza. Mie siyo kama Kashafi au M7 na Kaga…malizia. Watu kwa umaskini wa matumbo na vichwa bwana. Kuna nini kwenye kijiwe changu cha ombaomba kila uchao? Kahawa na kashata vya dezo? Mungu naomba uniepushe na makafiri hawa wapenda madaraka hata kama hawana uwezo wa kuyatumia vizuri kama Kashafi. Mtakuja kufanyiwa nchezo mbaya kama Kashafi.

Turejee kwenye mipango ya kutaka kwenda Ugabacholini. Kwanza nikishafika kule, nitahakikisha narejea na siri inayowapeleka kila mtu kule. Je, yawezekana Ugabacholini kunatumika kama kisingizio cha kutoendeleza huduma bora hapa kayani? Kweli yawezekana. Tangu uchumi wa kaya ulipowekwa mikononi mwa kunguru unategemea nini? Mambo yanazidi kuongezeka. Baada ya kuweka uchumi wa kaya na kuridhika na ten percent sasa tunaweka hata afya zetu mikononi mwa magabacholi yarabi. Hili halitakuwa chini ya utawala wangu kama nitafanikiwa kuchaguliwa kuwa mkuu wa kaya piga ua.

Huwa siachi kujiuliza. Kama Kashafi aliweza kutoa elimu bure, wake bure, umeme na makando kando mengine na bado akanyotolewa roho na kufanyiwa vitendo vibaya, ikifika hapa itakuwaje? Hivi hawa wanaofanya madudu wana akili kweli au ni mataahira wasio na hata kumbukumbu? Mwenzenu Kashafi kanyolewa kwanini msitie maji badala ya kuendelea kukenua na kujipa matumaini kama paka kukalia mkia akadhani kakalia bonge la kochi.

Shauri yenu. Mwenzenu naelekea Ugabacholini hivi karibuni ili kufichua siri zenu na kuja hapa na kuwaumbua. Maana sielewi kwanini hata mwenye ugonjwa wa ukurutu anaenda kutibiwa India? Kaeni chonjo Mpayukaji aja.

Acha niwahi eapoti kununua tiketi kwa ajili ya safari yangu ya Ugabacholini.

Chanzo: Tanzania Daima Novemba 2, 2011.

Wednesday, 2 November 2011

Makinda amedhalilishwa au kuambiwa ukweli?
Vyombo mbali mbali vya habari hivi kariubni viliripoti kile vilichokiita kudhalilishwa kwa spika wa Bunge Anne Makinda kunakodaiwa kufanywa na mtangulizi wake Samuel Sitta waziri wa ushikiano wa Afrika Mashariki.

Kwa safu hii si mara ya kwanza wala ya mwisho kuandika kuhusiana na mnyukano huu baina ya maspika wawili aliyepo na aliyepita.

Maneno yaliyochukuliwa na vyombo vya habari kuwa yalilenga kumdhalilisha au yalimdhalilisha Makinda yalisemwa na Sitta aliyenukuliwa akisema, "Mwanzoni hakukuwa na suala la viti maalumu katika suala hili (la kuwania uteuzi wa kugombea uspika)...walidhani wataweza kutumia fedha kwa wabunge ndiyo maana tukagombea wengi, lakini wakaona haiwezekani kabisa, nikiingia nitashinda kwa kura, siku moja kabla ya uteuzi ndiyo wakaweka sharti hilo la mgombea awe mwanamke, hilo likanishinda..."

Tuangalie maneno ya Sitta. Je pesa haikutumika? Je ubaguzi, tena wa kijinsia, haukutumika tofauti na katiba isemayo ubaguzi ni mwiko? Je Makinda hakuchaguliwa kwa shinikizo la watu fulani waliotumia jinsia kama sababu tu? Kwanini Makinda siku zote alipokuwa akitakiwa kukanusha kuwa ni chaguo la mafisadi alikuwa akikaa kimya?

Ingawa safu hii haina tabia ya kumtetea mtu kutokana na kwamba hailipwi kwa kazi ya utetezi kama wasemaji wa wakubwa, kwa hili Sitta hajakosea. Amepiga kwenye kidonda na huenda bubu atasema kujibu mapigo na ukweli kujulikana. Maana, kwa wanaokumbuka mzengwe uliotembea kuhakikisha Sitta hakalii kiti cha spika bado wanakumbuka jinsi Makinda alivyochomolewa huko alikochomolewa na kusimikwa hapo alipo. Hili halina kudhalilishana wala kusingiziana. Je hawa wanaoona Makinda kadhalilishwa au hakupatikana kwa mizengwe wanawaona watanzania kama dagaa ambao hawana hata kumbukumbu?

Hata ukiwalinganisha Makinda na Sitta kielimu na uzoefu, Makinda hana uwezo wala sifa ya kumzidi Sitta kama tukiondoa makengeza. Kazi ya spika mara nyingi ni kazi ya kisheria yaani kutunga sheria. Ukiangalia mabunge yote ya nchi za Afrika Mashariki, ni Tanzania tu ambayo ina spika asiye na taaluma ya sheria. Hata ukiangalia kiwango cha elimu cha wawili hawa, utagundua kuwa Makinda hana elimu kumzidi Sitta hasa kwa kuzingatia uzito wa kazi ya spika. Je kwanini Makinda alifaa kuliko Sitta? Jibu ni rahisi kuwa kwa vile hana elimu wala uzoefu wa kutosha, ni rahisi kutumiwa na watu wachache kupitishia mambo yao bungeni. Makinda si hatari kwa mafisadi kama alivyokuwa Sitta.

Tangu Makinda aingie madarakani, ameishanusuru wakubwa zake. Mfano mzuri ni pale alipoamua kumfukuza mbunge wa Arusha Godbless Lema kwa kudai waziri mkuu Mizengo Pinda alilidanganya bunge na taifa aliposema watanzania waliouawa na jeshi la polisi kwenye maadamano ya CHADEMA ya Arusha ni watatu wakati ni wawili. Spika alipandwa na hasira kana kwamba aliyekuwa kaambiwa kadanganya si binadamu bali Mungu. Mfano huu mdogo waweza kukuonyesha tunachomaanisha tunaposema kuwa Makinda ni rahisi kutumiwa kutokana na upeo mdogo wa masuala ya kisheria na bunge.

Ukiachia kiwango cha elimu na uzoefu, hata ukiangalia nani anajulikana kwa watanzania kati ya Makinda na Sitta utaona tofauti. Kwa mfano, mwandishi wa makala hii anajua kuwa Sitta ni mume wa Magreth Simwanza Sitta. Ukimuuliza mwandishi mume wa Makinda, hawezi kukupa jibu. Japo suala la familia ni suala binafsi lina umuhimu katika uongozi wa umma. Familia zetu ni kielelezo cha sifa na uwezo wetu kwa taifa. Hivyo, kuna haja ya kujua maisha ya Makinda ya kifamilia na ikiwezekana kwa spika ajaye sawa na rais lazima familia yake ijulikane. Tunasema hivi kutokana na hivi karibuni nchi ya jirani ya Kenya jaji mkuu wa sasa Dk Willy Mutunga aliponea chupuchupu baada ya habari kutoka kuwa alikuwa kwenye taratibu za kuachana na mke wake. Ingawa alifanikiwa kuvuka kikwazo hiki, bado ithibati ya kifamilia ilionekana kuwa kitu muhimu katika uongozi. Hapa najua kuna wanaoweza kuja na utetezi kuwa watu kama Askofu Makarios wa Cicilia hakuwa na mke wala imla wa zamani wa Malawi Hastings Kamuzu Banda. Ukweli ni kwamba walikuwa na udhaifu mkubwa sana hasa Banda aliyefikia mahali pa kutaka kufilisi taifa kwa kutumia kimada wake Cecilia Kadzamira.

Turejee kwenye mada ya leo ya udhalilishaji. Makinda, kama hakupatikana kutokana na mizengwe baada ya mtangulizi wake kuonekana habebi mafisadi hasa kashfa ya Richmond, ni sifa gani ya muda aliyo nayo angalau moja acha nyingi? Tumalizie kwa kumshauri Makinda akubali ukweli kuwa uspika wake ulipatikana kwa njia haramu ya ubaguzi wa kijinsia ili kumkomoa Sitta kwa kuwashughulikia wezi wa Richmond ambao bado wana ndoto za kuwa rais wa Tanzania. Bila Makinda ama kutoa maelezo yanayoingia akili au hata kujiuzulu kutokana na kuendelea kuonekana tunda la mafisadi, ataendelea kukumbushwa ukweli huu. Historia ndivyo ilivyo.
Chanzo: Dira Novemba 3, 2011.