The Curse for Salvation

The Curse for Salvation

Thursday, 9 April 2026

Fyatu afyatua vitegemezi vyake tegemezi na wapenda dezo mgongoni mwake

 


 Baada ya kushuhudia kilichotokea kaya jirani kwa fyatu mwenzangu hayati Ken Aliyeunda kaya, nimestuka na kuogopa japo najiamini sana. Kwa wasionyaka inshu ni kwamba, kule Dhambia, kitegemezi cha munene wa zamani kilijikuta pakanga. Katika kufanya uchunguzi na unoko, lisrikal la kule kwa ‘roho’ mbaya yake si liliinyaka kuwa kitegemezi cha munene wa zamani aliyenyotoka roho kule kwa Fyatu Madiba kilikuwa na ukwasi wa kutisha. Kila mwanakaya alishangaa namna kitegemezi ambacho hakijawahi kupiga mzigo wowote  hata kufagia chumba chake zaidi ya kubukanya mali za mafyatu kilivyokuwa na ukwasi wa kunuka. Je, viko vingapi kama hivi kwenye bara hili lililopotea kwa uzwazwa wakati lina uchumi lakini linaukalia?
            Inshu iko hivi. Mtoi wa mdosi wa kule wa zamani alikuwa anamilki mahekalu, madude ya bei mbaya usipime ambavyo hakuna maelezo ya miujiza iliyotumika kwa fyatu kula kulala alivyoipata. Je, aliupataje huu ukwasi ambao unawahangaisha na kuwashinda Mafyatu wachakalikaji? Simpo. Dingi wake alikuwa dingi wa kaya. Hivyo, kwa kutumia mamlaka na ubini aka surname wa dingi, jamaa alipiga njuluku ndefu pakubwa. Wakati wanakaya wakisota hadi kunyotolewa roho na ukapuku, mtoi alikuwa akijienjoi tu na kuwacheka na kuwashangaa. Je, wapo wangapi kama huyu chawa, au tuseme funza, barani kwetu? Kweli, usiposhangaa ya Abudili aka mtoi wa madili, utashangaa ya Dalie mwana wa rungu. Jamaa alikuwa na ndinga kama mia hivi na mihekalu kama hamsini. Hapa, hatujagusia njuluku alizosweka ughaibuni na zile anazotapanya akijichotea ujiko kumbe jizi tu. Anyways, hayo ndo maajabu ya bara letu linaloitwa kapuku wakati ni tajiri wa kunuka.
            Juzi, tulifanya kikao cha ghafla na Bi Mkubwa na kudurusu kadhia hii nyemelezi ya mafyatu nyemelezi watumiao unene wa madingi au ndugu zao. Tulikuja na mkakati wa kuokoa mali za Mafyatu na kulinda hesima yetu. Baada ya hapo, tuliwaita vitegemezi wetu wote na kuwapasha inshu na uamuzi wetu kuntu.
         Kwanza, hawakuamini. Walidhani tulikuwa tunawatania wakati huwa hatuna utani nao. Ilibidi waumie tu na kukubali haya mabadiliko adimu duniani japo kwa shingo upande.        
            Pili, walijaribu kupinga. Niliwapa wazi kuwa unene wangu si wao. Nao, wakatafute wao kama ni rahisi kama walivyokuwa wakifyatua njuluku za mafyatu kwa kunitumia. Mie ni faya na nomi kinomi. Siyo kama akina Mobutu na M7.
        Tatu, walistuka na kuchukia. Baada ya kuwapasha inshu, tuliazimia kuwa, kuanzia sasa, maulaji yangu kama prezo wa Mafyatu utakuwa wangu na Bi Mkubwa tu. Hivyo, wajiju,    
         Nne, tumepiga marufuku kutumia ubini wetu kuwapiga Mafyatu. Tumewapa wazi kuwa tunachelea mafyatu wanaweza kufyatuka wakatufyatua kwa kuwafyatua kizwazwa. Wewe uliona wapi mtoto mchanga kunyonyesha? Uliona wapi?
            Zamani, nilidhani wachunwao na vyaungudoa ni warume wakwere. Kumbe na wanene wanachunwa tena na vitegemezi vyao, jamaa, mashosti, na marafiki zao! Fyatu zima linaacha kuchapa kazi. Linanyonya na kuwafyatua mafyatu kwa vile ni rafiki, toi, au shosti la munene. Acheni uvivu. Tafuteni ngori mheshimike.
            Kwa vile mie naona mbali, nimeamua rasmi kukomesha upigaji wa kutumia mamlaka yangu. Hata Bi Mkubwa tumekubaliana afute ile asasi yake ya ulaji Ulaji iitwayo  BiMkubwa Opportunity and Maulaji ya Unene (BOMU). Hata ile bajeti iliyokuwa ikipangiwa ofisi yake nimeipiga panga. Lazima kieleweke. Kuanzia sasa, nakinukisha kwa wale wote wapenda dezo kwa kutumia migongo ya madingi wao wanene. Nimewaamuru vitegemezi vyetu kutafuta kazi halali. Kwa vile vimeishatimiza umri wa mafyatu wazima, havitaruhusiwa hata kupewa ndinga za mafyatu. Kwani, alivichagua nani na vinamtumikia nani zaidi ya matumbo na tamaa zao? Lazima tubadilike kabla hatujabadilishwa. Isitoshe, ulaji wa dezo na unene vina mwisho.
    Vitegemezi nilivyovipa uteuzi sasa naubatilisha vikahangaike nyenyewe nymbaff kabisa.
            Katika kutenda haki, kuanzia sasa, nimetoa amri ya watoi wote wa wanene na wanene wenyewe kusoma alama za nyakati. Itawabidi wajiandae kusomea kwenye shule za Kayumba kama mafyatu wengine.  Kwa wanene, hakuna kupeleka watoi ughaibuni au kwenye intaneshno skuli wakati shule na vyuo tunavyo hapa tena vya kumwaga. Hii, itasaidia kuwazuia wanene kupiga njuluku za mafyatu. Pia, natoa amri wanene wote kwenye Fyatuland kuacha kwenda ughaibuni kujichunguza afya zao wakati hapa tunayo mahospitali lukuki.
            Kuongoza kwa mfano, nimeamuru vitegemezi vyetu viwili vilivyogoma kwenda chuo, vitafute vyuo na kuchukua nkopo  kama mafyatu wengine. Hakuna cha kutegemea jina langu tena kuishi dezo kana kwamba havina mikono na vichwa. Nimechukua hatua hizi adimu duniani kwa kuogopa kuendelea kuwafyatua mafyatu hadi wafyatuke wanifyatue. Mwenye macho asikie uzuri. Mwenye masikio ajionee.
        Lazima ningoze kifyatu tena kwa mfano. Kuanzia sasa, hakuna ndugu yangu awe wa kweli au wa kuokoteza atapewa upendeleo. Hata kule kijijini kwetu ambako tulikuwa tumeanza miradi ya upendeleo, nimepiga kalamu. Nimesemaje? Kwani, niko wapi?
Chanzo: Mwananchi Jtano jana.

Sunday, 5 April 2026

Msiuane kwa mali mtakamatwa au kuziacha


Kuna visa vinavyozidi kuongezeka ambapo wanandoa hutoana roho kisa mali. Japo tutakachojadili hapa si kipya, kuna mafunzo mapya tunaweza kutoa tokana na ima uzoefu wetu au wenu. Hivi karibuni,visa vya wanadoa kutoana uhai juu ya mali vimezidi kushamiri. Si kwamba havikuwepo. Hasha. Vilikuwapo. Ila siku hizi vimezidi. Hii ni kutokana na utanda wazi na welewa wa binadamu juu ya dhana nzima ya mali au utajiri.
            Kwa wale wa kizazi chetu, yaani wa kuanzia miaka 50 kwenda juu, wimbi la mauaji baina ya wanandoa wakigombea mali ni jambo ambalo halikuzoeleka japo lilikuwapo si kwa kiwango cha sasa. Hata hivyo, kwa wengi waliokua wakati wa mfumo wa ujamaa, tulifundishwa kutopenda vitu bali utu. Hata hivyo, hii haizuii zile jamii zinazojulikana kwa uovu huu ambazo ziliendelea na tamaa, unyama na uvivu wa kutafuta vya kutaka kuvuna wasipopanda. Kwanini kuaana kwa ajili ya mali kana kwamba mtaondoka nazo mtakapokufa?
            Ni ukatili na unyama kiasi gani kuuana kwa ajili ya vitu vinavyoweza kutafutwa vikapatikana? Tokana na matukio mengi tuliyodurusu kwa muda kitambo, tuligundua kuwa hao wanaowaua wenzao ili wachukue mali peke yao, mara nyingi, hubainika na kuishia gerezani kama siyo damu za waliowaua kuwataabisha.
            Kuna kisa kimoja cha kusikitisha kilichotokea nchini Marekani mwaka jana kwenye jimbo la Texas ambako mwanamke mmoja katili alimuua mumewe kwa kumpiga risasi tatu ili achukue mali zake za mamilioni. Pamoja na kujitahidi kuficha ushahidi ukiwamo mwili wa marehemu aliyetoweka, alikamatwa. Sasa anangojea haki ichukue mkondo wake akiwa korokoroni.
            Mama huyu unayeweza kumuita shetani, aliuficha mwili wa marehemu chini ya sehemu ya kuhifadhia takataka na kudai kuwa mume wake alikuwa nchi jirani akijirusha na kimwana wakati alishamnyongelea mbali. Baada ya majirani kutomuona mume, walipiga simu polisi ambao walikuja na kumhoji akatoa taarifa za kujichanganya na kuwafanya watafute hati ya upekuzi na kugundua mwili wa marehemu ukiwa umeishaoza baada ya kufichwa kwa miezi minne.
            Katika kufuatilia visa hivi vya kikatili na kinyama, tuligundua kuwa wengi wa wanaofanya unyama huu ni wavivu wa kutafuta, wakatili, wajinga, waroho na wapenda vya dezo. Kwanini kumuua mwenzio tena kwa mali alizotafuta mwenyewe kama kweli wahusika siyo kama chawa wapendao kunyonya wenzao? Hata chawa huwa hawawaui wale wanaowanyonya.
            Pamoja na madhaifu tajwa hapo juu, kesi nyingi za aina hii zinaonyesha kuwa kuna uwezekano wa ugonjwa wa akili unaowasumbua wauaji hawa ambao hawana tofauti na wauaji wengine. Wapo wanaosema kuwa mauaji na ukatili huu ima husababishwa na chuki, hasira, visasi, woga, na mengine mengi kama hayo yatokanayo ya kuachika au kuchelea kuachika.
            Katika baadhi ya jamii, yapo makabila yenye mchezo huu yatokanayo na mashindano na tamaa ya utajiri. Watu hawa huolewa kwa makusudi wakijua wanachopanga kufanya baadaye. Mara nyingi, huwalenga wenye nazo na siyo hohehahe. Katika jamii hizi mke au mume kumuua mwenzake kwa ajili ya tamaa ya utajiri wa haraka ni jambo la kawaida.
            Kitu kingine kilichojitokeza kwenye jinai na kadhia hii ni wahusika kuishia kutofaidi hizo mali japokuwa wapo wachache wanaofanikiwa. Hata hivyo, bado wanaonusurika huishi kwa matatizo yawe ya kiafya au kiakili tokana na hisia za hatia waliyotenda.  Japo hatujafanya utafiti wa kisayansi, kuna imani kuwa yeyote amwagaye damu ya mwenzake, damu hiyo itamuandama. Kuna ukweli katika hili. Wauaji wanaweza kuficha mateso wanayopata au kupitia, ukweli ni kwamba wanatesema kwa hatia hasa nyoyoni mwao.
            Mwisho, badala ya jamii kuangalia na wengine kushabikia hata kushangilia hawa wale wenye uvivu wa kutafuta lakini wakawa na tamaa ya mali, inabidi ianze kuchukua hatua kama vile kupinga ujahili na unyama huu. Ukitaka kujua ukweli wa haya tunayoandika, kama kuna yeyote aliyewahi kufanya hivi unayemjua au kumsoma, jikumbushe mwisho wake. Wengine wanaishi kwa kutegemea madawa ya usingizi na ulevi kutokana na mateso ya dhambi na ukatili walivyowafanyia wenzao. Haiwezekani uue ambacho huwezi kukiumba uwe salama. Na kama utakuwa salama ni kwa muda.
Chanzo: Mwananchi Jpili leo.

Mila, ndoa, na sherehe vya ajabu

Leo, tutaongelea baadhi ya mila za ufungaji ndoa katika baadhi ya jamii za sasa na za zamani duniani. Huko Usikochi, marafiki huwapaka rangi nyeusi iliyochanganywa na masizi, manyoya, maziwa yaliyochacha, na unga, hasa bwana harusi na wakati mwingine bibi harusi. Hii huwaandaa kwa ugumu maishani na hii hufanyika hadharani.
        Huko Uchina, katika jamii ya Watujia, bi harusi hupaswa kulia kwa saa moja kwa mwezi mzima akiwa kwa wazazi wake. Baadae, bibi na dada zake humsaidia katika kulia kama namna ya shukrani. Nako Kongo, kwa kipindi kizima cha harusi, watarajiwa hawapaswi kucheka bali kununa! Nako nchini India, wanawake waliozaliwa kwenye hali fulani za kinyota waitwao Manglik dosha huolewa na mti, hasa mgomba, ambao baadae hukatwa ili kuondoa laana.
        Nako Korea ya Kusini, bwana harusi hufungwa kifundo cha mguu na kuchapwa na samaki makanyagioni kuthibitisha ushupavu wake kitabia. Nchini Ujerumani, kwenye mkesha wa ndoa, vifaa vyote vya udongo huvunjwa na watarajiwa husafisha kila kitu kumaanisha umoja katika kutatua matatizo. Katika tukio hili, ni mwiko kuvunja glasi kwa vile huleta mkosi.
Kwa wamasai, baba humtemea mate  bintiye mtarajiwa kwenye kichwa na kifua kama ishara ya baraka. Baada ya hapo, bi harusi huondoka bila kutazama nyuma ili asivuruge bahati yake. Nako Indonesia kwenye jimbo la Java, bi harusi huoshwa na nduguze wazee kwa maji yaliyotiwa maua kama ishara ya kutakaswa. Huko Uswidi, waalikwa hawafichi furaha yao. Bwana harusi akitoka kidogo, wageni wa kiume hupanga mstari kumbusu bi harusi sambamba na bi harusi akitoka wasichana na akina mama huenda kumbusu bwana harusi.
        Huko Romania, marafiki wa bi harusi hutekwa na marafiki zake hadi wajadiliane namna ya kumrejesha. Hii hulenga kupima utashi na utayari wa bwana harusi kumrejesha. Nako nchini Ugiriki, rafiki wa bwana harusi hunyoa ndevu siku ya harusi kuonyesha uaminifu baina ya marafiki hawa. Baadae, ndugu wa familia humlisha asali na matunda ya mti wa mlozi. Hii, huashiria ndoa itakayofana.
Turejee tena Kaskazini mwa India. Kuna kitu kiitwacho Joota Chupai, ambapo ndugu wa bi harusi huiba kiatu cha bwana harusi pindi aingiapo nyumbani kuashiria ushindani na inaweza kuisha kwa kutoa dau kubwa. 
            Kule nchini Mongolia, kabla ya ndoa, lazima achinjwe kuku mchanga na kutolewa ini ili kupata ini lenye afya. Lisipopatikana, utaratibu huu utaendelea hadi lipatikane linalofaa. 
Huko Chekoslovakia, ndugu na marafiki huweka kichanga kwenye kitanda cha watarajiwa kabla ya ndoa kuashiria ndoa itakuwa na watoto. Pia, mchele na nafaka husambazwa kitandani kuonyesha wingi wa neema. Kule Japan nako, kuna sherehe ya San-San-Kudo Sake au nilohunshu kinywaji kitokanacho na mchele uliochacha ambapo watarajiwa hawabadilishani pete. Badala yake, hunywa mara tisa, tatu tatu kila mara toka vikombe vitatu vya sake kuashiria kuwaunganisha watarajiwa na familia zao. Na hii huchukuliwa kama ishara iliyobarikiwa kuliko kula viapo.
        Huko Afrika Magharibi, baadhi ya jamii ambazo bi harusi huwekwa kwenye vibanda maalumu na kulishwa na kunenepa ili kupata unene unaoridhisha. Kuna imani kuwa bi harusi wanene wanapendeza na wana uwezo wa kuzaa watoto wenye afya! Funga kazi ni kule Spartan huko Ugiriki. Bwana harusi hupigwa kwa fimbo na mawe ili kuonyesha uvimilivu na ustahimilivu katika maisha. 
Kwenye mila za Waceltic kule Ulaya uhitaji kitanda cha maharusi kubarikiwa na makasisi wakati waliohudhuria sherehe wakiangalia. Sherehe uhusisha unyunyiziaji maji ya baraka kitandani. Unyunyiziaji maji huu ulidhaniwa kuwa ilikuwa ni alama ya ulinzi na uzazi kwa wanandoa. Warumi nao walikuwa na yao. Mabwana harusi waliwabeba bi harusi na kuwusha vizingiti maalumu kuepuka pepo wabaya kuwaingia kupitia miguuni. Warumi waliamini kuwa pepo wabaya ambao huishi ardhini na wanaweza kuingia kwa wanawake waingiapo kwenye nyumba mpya. Hivyo, kuwabeba kuliepusha wao kukutana na nguvu hiii ya ajabu.
Mwisho, wapo wayahudi. Hawa wangelinganisha watarajiwa na ndoa hufungwa kwa kutema mate ardhini kabla ya kupeana mikono. Wayahudi waliamini kwa mate yana nguvu ya kinga za kuweza kufukuza pepo wabaya.
Chanzo: Mwananchi Jpili 29 Machi, 2026.


Wednesday, 1 April 2026

Fyatu kutumia wese kufyatua mafyatu

Si kwamba najidai. Hasha. Kwa tunaomilki mikweche na mbavu za mbwa, imekula kwetu. Mwenzenu nimeweka kweche langu juu ya mawe. Naona yule anabeua midomo. Unadhani mchezo usawa huu wa kufyatuliwa na kufyatuana? Kama hujafyatuliwa, usinicheke wala kujihadaa. Utafyatuliwa tu. Tangu Tarampu na Niitenyau wakinukishe kule kulikoungua jembe ukabakia mpini, si mafyatu wachovu tutaipata. Tokana na vita hii ya kujitakia si wese limepaishwa. Leo, kila mwiz, sorry, fyatu anapanga kupandisha bei ya kila kitu. Ukiuliza kwai, waambwa vita. Unapata somo hapa? Hivi wese tutakalolanguliwa si liliingizwa miezi mingi iliyopita? Sasa itakuwaje kupandishia bei wakati wese tunalonunua ni kiporo kilicholetwa miezi mingi iliyopita?
            Juzi, niliwaita wapangaji wangu kuwaandaa kitakapoumana.Niliwaamsha usiku na kuwapa inshu! Walidhani kulikuwa na la maana la kuwapasha kumbe maumivu matupu! Si niliwafyatua kuwa kuanzia sasa kodi ya pango itapanda mara mbili! Walipouliza kwai, niliwajibu kuwa watazame runinga na siyo kushobokea shoo za kizwazwa. Niliwaliwashangaa wanaishi dunia gani wasijue wese limepanda. Si fyatu mmoja alidakia “kwani ubavu wa dogi, sorry, nyumba nayo inatumia wese kama gari?” Wee! Acha nifyatuke! Si alijifanya msomi tena wa sayansi ya wese. AlijibuNilimuuliza alichosomea na wapi kiasi cha kutojua bei ya wese ikipanda, kila kitu kinapaa.
            Nilibanja sana na kuwapa kavukavu kuwa atakayeona kupanda kwa kodi hakuwezi, atafute pa kwenda. Walipodadisi, niliwapa shule kuwa wese ndiyo roho ya biashara zote na wafanyabiashara wanaongeza cha juu watakavyo na hii ni fursa sawa kwa wote. Sijui nayo ilifia wapi? Kweli, kufa kufaana! Niliwapasha kuwa nilikuta bidhaa zote sokoni zimepaa. Hivyo, nimeamua kupaisha bei ya bidhaa yangu yaani pango. Tokana na mtanange huu, nimegundua kuwa hakuna fyatu salama vinginevyo awe sehemu ya lisirikali ambalo tukianza kupigwa na kufyatuliwa litaangalia na kutafuta namna ya kutufyatua zaidi. Usishangae hata ndata wakapandisha dau la kitu kidogo.
            Kuanzia sasa, nina mikakati ya kupambana na makali ya kufyatuliwa.
        Mosi, nitapunguza leshini home. Hakuna kula hovyo. Milo mitatu kwa siku mwisho. Huu ni uharibifu wa chakula na miili.
        Pili, ukiondoa vitegemezi vyetu vichanga, waliobaki kayani lazima waanze ‘mfungo wa wese.’
            Tatu, sitapokea wageni, vinginevyo wawe wemefunga. Sina bajeti ya wageni tena. Sifanyi hivi kwa roho mbaya, uchoyo, au ulafi. Wese limepanda jamani. Pia, wale waliozoea kuja kupiga soga wakati wa msosi, huu mwisho wao.
        Nne, nitaokoka. Sitakata kalaji kama nilivyozoea. Pia, nashauri ifuatavyo:
        a)     Wachunaji wanaotusumbua kwa fungu la kumi na sadaka wafunge hadi vita iishe.
        b)     Wanene wapunguze matumizi, safari, na vikao visivyo vya lazima. Najua watajifyatua ufahamu. Wakumbuke. Kama hawatapunguza kwa vile mali ya umma haiumi, Gen Ziro bado wapo. Watauma kama walivyofanya mwaka jana.
        c)     lisirikali lisijitoe ufahamu. Liingilie kati vinginevyo kinaweza kunuka. Si mnajua tena. Wakati tulio nacho kidogo tukilia, vipi hawa wasio na ajira wala kipato? Msitake kuongeza idadi ya majambazi na vibaka.
         Tano, kwa wenye viliba tumbo, huu ni wakati mzuri wa kupunguza uzito. Badala ya mafyatu wazima kukimbizana na barabara, punguza kubukanya na kupiga kanywaji mfurahie neema ya kupaa kwa wese.
        Sita, wauza vyakula na wenye vyombo vya usafiri, muogopeni Mungu. Siyo muanzishe vita yenu wenyewe kwa kupatupandishia bei mkisingizia wese.
        Saba, kwa vile nimeamua kuokoka na kuacha kupiga kanywaji, hata nyumba ndogo naachia. Nani atunze nyumba ndogo usawa huu wa kupaa wese? Na wale waliozoea kubomu, nao nawashauri wangoje vita iishe japo wese lishuke.
        Nane, kupunguza bili za umeme unaoliwa na miwaya, kuanzia sasa, kuangalia runinga ni saa moja tu. Baada ya hapo, wasiopenda lazima waanze kujifunza kulala mapema ili kupunguza matumizi ya umeme.
        Tisa, wale wote wanaonidai nawashauri wanifutie madeni au wangoje vita iishe pale bei na hadi pale bei ya wese itakaposhuka kama kweli itashuka. Maana, kwangu, hakuna kinachozalisha. Wajua kuwa hata bata na kuku wetu siku hizi hawatagi kutokana na kupanda kwa bei ya wese?
        Kumi, wale wa vikoba na kausha dau walie. Wasije kutusumbua na bi Mkubwa hadi vita iishe vingenevyo wanataka vita ya sisi kwa sisi.
        Kumi na moja, vitegemezi vyetu vilivyokuwa kwenye shule za upigaji na ufyatuaji za bei nawarejesha kwenye shule za Kayumba hadi wese lishuke. Kwa waliokuwa wanahudhuria tuisheni ndo mwisho hadi vita iishe. Maana, juzi kuna ticha kanipandishia bei ya tuisheni kwa sababu wese limepanda hadi kufikiri na kuandaa notice kunammalizia wese.
        Kumi na mbili, lisirikali lianze kumwaga njuluku. Yale ya maza anamwaga njuluku ambayo hajawahi kunimwagia, nayataka sasa kama ni ya kweli na si rongorongo za kisiasa za visasi. Wauza wese na lisirikali Mungu hata Sheitwani wanawaona.
Hivi leo nimekunywa chupa ngapi?
Chanzo: Mwananchi Jtano leo.