Je hatuongopi hata kuongopewa au kujiongopea tunapopaswa kusema na kuambwa ukweli? Wakweli wanachukiwa ilhali waongo wakipendwa. Wasafi wanachukiwa ilhali wachafu wakipendwa. Ni mapenzi gani haya ya hasara? Tunasifu tupaswapo kulaumu. Hatuishii hapo. Tunafurahi tunapopaswa kuchukia. Tunacheka, na kukenua, tupaswapo kununa na kulia. Tunakaa kimya tunapopaswa kupayuka. Kwanini tusifyatuliwe? Tunafyata badala ya kufyatuka! Halafu tukifyatuliwa, tunalalamika. Usipofyatuka ukafyatua, utafyatuliwa kuufyata kama si kufyata mkia. Kwa Kisambaa, huitwa the law of nature au kanuni asilia. Kazi mbi si mchezo mwema. Mjue.
Jiulize. Hatukubali tunapopaswa kutaa? Hatuungi mkono tupaswapo kupinga? Unapata unachotoa na kutoa unachopata. Ukipanda mbigiri, hutovuna mbirimbi. Hatupwakii tunapopaswa kususa na kutapika? Kwani, hayapo? Tunapopaswa kupoka haki, tunaiomba! Nani kakudanganya kuamini kuwa haki inaombwa na siyo kupokwa? Haki haiwezi kuwa hisani wala hisani kuwa haki. Uongo tumegeuza ukweli. Ujinga tumegeuza ujuzi. Tunaishi kwa fadhila badala ya haki. Tunaficha na kufichwa tunapopaswa kuweka wazi! Unafiki unatawala pahitajikapo kusema wazi.
Tunaogopa tunapopaswa kupambana. Tunakuwa wapole tupaswapo kuwa wakali. Tunadanganywa hadi tunajidanganya na kudanganyika mbali na kudanganyana! Je tunamdaganya nani wakati wahanga ni sisi na vizazi vyetu? Waweza kufua nguo au kuoga kwa maji machafu ukawa safi? Hamjaambwa kuwa ukiwachekea gendaeka, utavuna mabua? Utamlaumu nani? Wangapi wanalala njaa lakini wanajiaminisha wameshiba? Wezi wanaitwa waheshimiwa ilhali watenda haki wakiitwa wanoko! Hamjayaona haya?
Inatisha. Inaogopesha. Maskini anaitwa mwenye mali wakati yu hoi na hohehahe! Inawezekanaje fisi na mbwa wakalinda nyama au majambazi na wezi kulinda benki? Je hiki si chanzo cha ukapuku wetu? Wenye nguvu wanakula kwanza na kusaza ilhali wanyonge wakinyong’onyea hata kunyongwa na shida! Wapo wasemao eti ni haki na sawa! Kivipi? Haki vipi wakati ni dhuluma? Kwanini nisiogope na kusikitika? Je hili ni jibu au kufyatua? Heri nafyatua ili mfyatuke mfyatue, na ikibidi, tufyatuane kieleweke. Huwezi kuitwa mwenye mali wakati mali yenyewe huioni zaidi ya takwimu. Huwezi kuambwa kaya ni yako wakati ni yao. Kama ni yako, yao ni ipi, na kama ni yao, yako ni ipi? Haya ndiyo matokeo yangu kuwa fyatu mfyatuzi asiyeogopa kufyatua ili asifyatuliwe.
Nani ataishi milele huyu mjanja tumuone? Je tumewaona wangapi wenye vifua kama ninga waliofyatuka wakaacha kila kitu wakatokomea kwenye kaburi la sahau? Mfalme aweza kuwa mfalme bila watawaliwa? Je wawili hawa nani anamhitaji au kumtegemea nani? Mbona faru na nyati huishi bila malkia wala mfalme? Nani mfalme wa ndege, viumbe huru waendao watakapo na kula watakacho japo hawazalishi? Farasi na ampandaye nani umhitaji na kumtegemea nani? Je farasi akibwaga mzigo ataumia au kupata nafuu? Mwoga na mpumbavu huogopa kifo na kuishia kufa. Si heri kupambana na adui ukafa kuliko kumuacha akudhalilishe? Heri kufa umesimama kuliko kuishi umepiga magoti.
Leo, sifyatuki sana. Wala sifyati bali kuwaadhi. Hivi ni mchana au usiku?