KITENDO cha mahakama ya kimataifa ya makosa ya Jinai (ICC) kuamua
kumfungulia mashtaka mke wa rais wa zamani wa Ivory Coast, Laurent
Gbagbo, Simone, ni cha kimapinduzi kwa bara la Afrika.
Hivi karibuni ICC ilitoa hati za kutaka kukamatwa na kufikisha kwenye
mahakama hiyo Simone akikabiliwa na makosa ya ubakaji, mauaji na uharifu
dhidi ya ubinadamu yaliyotendeka wakati wa mwisho wa utawala wa mumewe
mapema mwaka juzi kuja mwaka jana.
Gbagbo aliangushwa baada ya majeshi ya Umoja wa Mataifa na Ufaransa kuingilia kwenye mzozo nchini mle mnamo Aprili 2011.
Jumuia ya kimataifa iliamua kuingilia kwenye mgogoro wa Ivory Coast
baada ya Gbagbo kuandaa uchaguzi na baadaye kudharau matokeo ya
yaliyompa ushindi mpinzani wake Allasane Ouattra rais wa sasa.
Kitendo cha Gbagbo kugoma kuachia madaraka kilimfanya mpinzani wake aungane na waasi waliokuwa upande wa Kaskazini.
Kitendo hiki kiliigawa Ivory Coast kati ya Kaskazini kwenye waislamu
wengi na watu wenye asili ya Burkinabe na Kusini kwenye wakristo wengi
na waliojiona kama wenye haki ya kutawala kwa sababu ya asili yao ya
hapo hapo Ivory Coast.
Mvutano baina ya Gbagbo na Ouattra ulidumu kwa miezi mitano. Hata
hivyo, matokeo ya hali hii hayakuwa mazuri. Kwani watu wapatao 3,000
walipoteza maisha huku mamia wakikimbia nchi yao. Pia mvutano huu
uliivuruga Ivory Coast kiuchumi, kisiasa na kijamii. Bado nchi inauguza
madonda baada ya kuondolewa kwa Gbagbo aliyetolewa kwenye handaki akiwa
hoi bin taabani kutokana na kuishiwa matumizi.
Baada ya Gbagbo kutolewa shimoni, alipelekwa sehemu mojawapo ya Ivory
Coast na baadaye akasafirishwa kwenda The Hague ambako alikuwa
ameishafunguliwa mashtaka. Tangu wakati huo Gbagbo amekuwa akishikiliwa
mjini The Hague akingojea kusikilizwa na kuamriwa kwa kesi yake.
Baada ya kupelekwa Gbagbo The Hague wengi walidhani ulikuwa mwisho wa
sakata. Hawakujua kuwa kumbe na washirika wake hasa mkewe na waziri wake
mkuu wa zamani wangefikishwa mahakamani kujibu mashitaka sambamba na
Gbagbo.
Simone anasemekana kuwa nguzo na sababu ya Gbagbo kung’ang’ania
madaraka. Pia kama mke wa rais na msomi mwenye shahada ya juu ya PhD
kwenye historia kama mumewe, Simone anasemekana kuwa na nguvu sana
nchini humo kiasi cha kuogopewa kuliko hata Gbagbo mwenyewe.
Na huu umekuwa mchezo mchafu ulioanza kuota mizizi katika tawala
nyingi fisadi na za hovyo za kiafrika ambapo wake wa marais hujigeuza
marais kwa vile wanalala kitanda kimoja na rais. Miaka michache
iliyopita tulishuhudia mke wa rais wa Kenya, Lucy Kibaki akiwachapa
makofi waandishi wa habari baada ya kuvamia ofisi zao na kuwazuia
kurusha habari zilizokuwa zikionyesha ufisadi wake kwenye sakata la wizi
wa mahindi ya umma.
Nchini Zimbabwe mke wa rais Robert Mugabe, Grace Marufu anatuhumiwa
kuibia benki kuu ya nchi hiyo mamilioni ya dola akiyatapanya kwenye
vipodozi na mavazi ya fasheni ya bei mbaya hadi kuitwa Grace Gucchi.
wakati mke wa rais akifanya upuuzi wote huu, wazimbabwe walio wengi
wanakufa kutokana na ukata na kuvurugika kwa uchumi wa nchi hiyo
vilivyosababishwa na ung’ang’anizi wa rais wa nchi hiyo.
Pia hivi karibuni tulisikia kuwa nchini Uganda rais Yoweri Museveni
anamuandaa mkewe kumrithi. Hakika hali ni mbaya kwenye nchi nyingi za
kiafrika. Wake wa marais hata watoto wao ima huingia moja kwa moja
kwenye siasa au kuanzisha NGO na kuzitumia kuibia umma ukiachia mbali
kupata upendeleo kwenye taasisi za kifedha na hata wengine kushiriki
biashara haramu kama vile madawa ya kulevya.
Hivyo, kilichotokea kwa mke wa Gbagbo kinapaswa kuwa somo tosha kwa
wake wa marais wanaotumia madaraka ya waume zao vibaya. Inashangaza
kuona kuwa kizazi cha sasa cha watawala kimekuwa na upofu kiasi cha
kutoogopa kinachoweza kutokea hapo baadaye.
Siyo siri wala uchochezi: Afrika kwa sasa ina akina Imelda Marcos
wengi. Imelda alisifika sana nchini Ufilipino kwa kutumia madaraka ya
mumewe kuiba na kufuja pesa ya umma huku umma ukiangamia hadi siku
serikali ya mumewe ilipoondolewa kwa maandamano ya umma mwaka 1986.
Inashangaza ni kwanini hawajifunzi hata kutokana na matukio ya karibu
kama vile kukamatwa kwa rais wa Misri Hosni Mubarak sambamba na watoto
wake pekee wawili wa kiume. Bado hawajifunzi kutokana na yaliyomkuta
Gaddafi na watoto wake ambapo baadhi waliuawa na aliyetarajiwa kumrithi
anashikiliwa korokoroni huku akikabiliwa na mashtaka mbele ya ICC.
Kitendo cha ICC kumfungulia mke wa rais wa zamani wa Ivory Coast
chaweza kuwa mwanzo wa mwisho wa wake za wakubwa wanaotumia madaraka ya
waume zao vibaya. Ni vizuri nchi za Kiafrika kuanza kubadili katiba zake
na kuweka vipengele vya kuwawajibisha wezi wa madaraka kama hawa
sambamba na waume zao na hata familia zao.
Chanzo: Tanzania Daima Novemba 28, 2012.