Liberal Peace Conflict, Gender, and Peacebuilding

Liberal Peace Conflict, Gender, and Peacebuilding

Friday 6 September 2024

Tumechatwa Hadi Tumechakatika Haswa


Juzi, mtukufu doktari rahis alipofyatua na kuchakata, viherehere, vibwengo, na visebengo waso adabu wenye wivu waliawashwa midomo wakafyatua yasopaswa. Alipowaweka kando njemba wawili waliozoea kupayuka bila midomo kuwasiliana na bongo, wapo waliompongeza na kulaumu kwa kutumbua majipu, kujivua magamba, na kutua mizigo. Hakika, mafyatu si binadamu kama wajumbe! 
        Alipochakatua na kuchakata kwarejesha wakongwe wabee, vibabu tena chakatwa badala ya gen Z. walianza, mara “anatuletea Gen Zees makapi.” Jamani, mnataka afanye nini mfurahi au kuridhika? Akiteua wakweze, mnasema ufamilia na ufalme. Akinyamaza kama chura, mnasema mwoga!
            Ukizungukwa na jalala, kila kikufaacho ni uchafu tokana na kuwa nyenzo pekee jalalani. Jikumbusheni profedheha mwenye jina kama kabundi kadogo aliyechemolewa jalalani na aliyemfinyanga kisiasa. Ukitumia nyundo, kila tatizo ni msumari. Ukizoea kunyonga, yanini kuchinja?
            Mnafyatuka eti kazi sasa ni kuchakata na kuchakatua hata maiti. Kazi ya urahisi ni nini? Akisafiri, mnazoza. Afanye nini wakati urahisi ni uungu mtu unaompa madaraka yaso mipaka kufanya atakalo akasifiwa hata akikosea? Akirejesha vibabu, yawahusuni? Mwataka ateue wajukuu zake au wapingaji kama Looter kule kwa jirani? Kwani, hamuoni?
        Nawashangaa.  Mshindwe na waregee. Kitu gani siyo recycled? Mmesahau, uchakachuaji, sorry, uchaguzi uliopita uliochakata hawa mnaowaita recycled materials? Ebo! Nani, mara hii, kasahau mchakato wa bao la mkono? Je huku siyo kuchakata tena kisiasa ambako nyie huita uchakachuaji? Ni uchakataji kuanzia chini hadi juu, juu hadi chini na kila kitu kimechakatwa. Sera hazitoki majuu? Shopping na wachukuaji siyo majuu?
        Kwanini tumegeuka kaya ya uchakataji aka recycled kaya? Mosi, ni ukosefu wa nyenzo aka materials zifaazo. Jiulize. Kisiasa, maadili yamegeuka madili na siasa sasa ni sanaa na usanii bila kusahau misifa na usifiaji hadi njemba nzima zinampigia magoti mja utadhani Mungu.                         Tumeishiwa sera nini? Sifa zinageuka sera na sera zinageuka maudhi, uongozi umegeuka uongo, ukale umegeuzwa usasa na usasa ukale. Tunazalisha pamba. Tunavaa mitumba. Tunasomesha na kuzalisha mitumba. 
        Hizi ni zama za kujihudumia badala ya kuhudumu, na kutumikisha badala ya kutumikia. Haki na stahiki vimegeuzwa hisani, ukweli umegeuka uongo, ubangaizaji umegeuka kazi, haramu imehalalishwa na halali imeharamishwa. Akina Yero wamegeuzwa wakimbizi Kayani mwao. Kwani, hamuyaoni jamani? Mnasema ujanja kupata? Mwataka nifyatuke vipi mnielewe muache kulalama mfanye kweli?
        Pia, kijamii, ni kuchakata kwenda mbele. Jitu jeusi ja mkaa linatoja tojo (tattoos) nyeusi likiigiza watasha. Mingine mibwabwa na misagaji. Kama haitoshi, siku hizi, imbaba mizima inavaa hereni, vipuri, miregezo, kuonyesha ‘undaweya’ chafu bila aibu, kusuka na kutoboa masikio mbali na miziki recycled na wanamuziki walochakatwa kiubunifu waharibuo maadili nasi tukishuhudia kana kwamba haituhusu? Mwachakatuliwa na kuchakatwa bila chekeche. Mwacheza chakacha!
            Kiuchumi, zamani ulikuwapo uchumi si uchumiatumbo. Tulikuwa na wachumi si wachumaji, wawekezaji wamegeuka wachukuaji, watawaliwa wamegeuka watu waliwao, wafadhiliwa wamegeuka wafadhili. Wezi wanalinda fedha na mbwa kulinda nyama. Mnalalamika nini wakipiga njuluku na kutajirika mkageuzwa makapuku na walalamikaji wasiochukua hatua? Mnadhani kuna wafadhili watakuja kuwakomboa? Thubutu yenu!                             
Jikomboeni. Uchumi mmeugenisha. Mmegeuzwa manamba kwa kisingizio cha kutengeza vibarua muitavyo ajira. Kwanini kutegemea ajira? Kuweni wabunifu mjiajiri na kuwaajiri hao wageni wanaowaajiri? Imefikia mahali Afrika inakodisha ardhi kwa wageni kuzalisha chakula kwa ajili ya watu wao kukwepa kukinunua kwa bei mbaya wakati inaagiza hata nyanya na mayai visa toka ughaibuni halafu inasema iko huru. Uhuru au udhuru?                                     Wanene  watanuaji wanatanua sirkal na mikanda wakati nyie mkiambwa mfunge mikanda. Mtakula lini au mwangoja muingie peponi ambako hamna uhakika mbali na kuingia bila midomo wala matumbo? Mla kala leo kesho kalani.
        Siku hizi, uchatakataji umevamia hata anga za kiroho na kugeuza uroho kuwa dili na dini. Zamani, tulikuwa na mashehe kwelikweli siyo mashehena waliosheheni uroho hadi wanauza mali za wakfu au kugeuka wapiga ramli na waganganjaa wa kienyeji. Msiseme nazusha. Kumbuka mwendazake alivyoshupalia kurejesha baadhi ya mali za baadhi ya wale ambao siwataji. Wamejaa wachungaji waliogeuka wachunaji kondoo waliopaswa kuwachunga. 
            Wanawatoza njuluku eti kuwapa huduma wakati ni hujuma tupu. Kwani hawapo? Hamkusikia zile kashfa za ngono? Hamuoni kuibuka utitiri wa manabii na mitume uchwara?             
    Zamani, dini ilikuwa huduma si hujuma. Siku hizi, imechakatwa nasi tukiangalia tu na kugeuzwa biashara ya mabilioni. Utapeli na mauzauza vinaiitwa miujiza wakati ni wizi itumiayo mijizi iliyojificha nyuma ya imani sawa na ile imani ya amani katikati ya vurugu, utekaji, ujambazi, upigaji njuluku za umma n.k. Kwani, hayapo? Nasi tumevamiwa.Tuna makanjanja wanaosaka bahasha badala ya habari wajaze mitumbo yao isiyotosheka.
            Nimalize. Muacheni bibie achape kazi, kutanua hasa usawa huu anapokwenda kusaka kura ya kula ili kuendelea kukamua. Mwenye wivu ajinyonge. Msitupigie kelele vinginevyo tutawasweka lupango kama akina Tunda Lishe aka lion na wenzake. Juzi, nilisikia akichangisha njuluku kutengeza gari lake. Kwani halikuwa na bima? Nimesemaje?
Chanzo: Mwananchi Jumatano juzi.


Sunday 1 September 2024

Hakuna Daktari, Mchungaji/Mganga wa Ndoa

Ndoa nyingi zimevunjika kutokana na wanandoa kutojiamini na badala yake wakaamini miujiza au ushirikina. Hakuna muujiza kwenye ndoa zaidi ya wanandoa wenyewe. Hakuna ushirikina unaoweza kuimarisha ndoa. Wahenga walisema; hakuna dawa ya mapenzi. Kama ipo si nyingine ni uaminifu, upendo, utayari, usiri, uwajibikaji, matendo, na maneno mema baina ya wahusika. 
        Tumeweka ushirikina na ushauri pamoja kutokana na uzoefu wetu. Tunajua. Kuna wanandoa walioishiwa hadi kuamini kuwa maombi, tunguli, n.k. vinaweza kuokoa ndoa ambazo wameziua tokana na ujinga na upumbavu wao. Tangu tumeoana, hakuna kitu tulichojiepusha nacho kama kuweka mambo yetu ya ndani siyo nje tu ya nyumba yetu bali nje ya chumba chetu cha kulala ambayo ndiyo makao makuu ya ndoa yetu. 
        Haiingii mtu yeyote humo isipokuwa watoto wetu wachanga tu. Siri za humo hazitoki hata kwa viboko. Hivyo, unapoanza kuingiza mashoga kwenye chumba chako cha kulala na baadaye kwenye kitanda chako ujue unamtafuta na kumtengeneza mchawi au wachawi wa ndoa yako. Tusisitize mambo makuu yafuatayo:

            Mosi, ndoa yako ni siri yako binafsi asiyopaswa kujua mtu yeyote. Ndoa siyo gazeti wala kitabu ambacho unaweza kusoma na wenzako. Ndoa yako ni siri kuliko hata nguo zako za ndani, maana huwa unazinunua au wengine kuzianika zikaonekana. Ndo ani kama moyo wako. Anayeweza kuuona ni daktari wako pekee na Mungu aliyeuumba.

Pili, chumba chenu cha kulala ni sehemu ya siri asiyopaswa kuijua wala kuingia mtu yeyote isipokuwa wawili nyinyi. Hivyo, wale wanaowaruhusu mashoga au wasichana wao wa kazi kuingia kwenye chumba chao cha kulala ni makosa makubwa.

Tatu, matatizo yako ya ndoa yanapaswa kutatuliwa na wawili. Kwanini iwezekane kuyatengeneza mshindwe kuyatatua? Ushauri wa mashoga na marafiki hausadii. Hawajui thamani ya ndoa yako. Na lolote baya likitokea, wao hawatakuwapo. Kitanda usicholala hujui kunguni wake. Hapa lazima usiri uwepo na si usiri tu bali hata hofu na kutomwamini mtu yeyote. Hata inapotokea ukapata ushauri, lazima uupime kwa kuangalia thamani ya ndoa yako na si mawazo ya aliyekupa ushauri. Kupewa ushauri ni jambo moja na kulifanyia kazi ni jambo jingine.

Hakuna anayefungwa na ushauri wa mtu yeyote. Kupanga–––tujue–––ni kuchagua. Unapopanga au kuchagua, fanya hivyo vizuri ukijua wazi. Ndoa yako ni sawa na kaburi. Tunatoa mfano huu siyo kwa sababu ya kukutisha. Tunataka upate ujumbe kama ulivyokusudiwa. Hebu piga picha mtu anapokufa. Kuna mtu anaweza kumsaidia kukaa kwenye kaburi lake? Msaada pekee hapa ni kumchimbia kaburi na kumuingiza wakimuacha mhusika aingie na kuishi kwenye kaburi lake. Unaweza kuugua au kuhisi njaa na kupata msaada lakini si kwenye kaburi. Samahani kwa kutoa mfano wenye majonzi ingawa ndiyo hali halisi.

Kitu kingine wanachopaswa kufahamu wanandoa ni mategemeo au matarajio yao. Wengi wanapofunga ndoa huangalia upande mmoja yaani wa kufaidi. Wanasahau kuwa­­­–––kama ilivyo katika nyanja nyingine za maisha–––kila kitu lazima kiwe na majaribu na mitihani mbalimbali yenye changamoto juu ya kujifunza namna ya kutatua matatizo. Hivyo, unapoingia kwenye ndoa, lazima uangalie pande zote. Ndiyo maana baadhi ya dini na mila hufundisha kuwa ndoa ni kifungo ambamo mhusika asitegemee vinono tu hata machungu. Hata hivyo, ikitokea mitihani, dawa si kuachana wala kukimbiana. Kwani unaweza kumkimbia mjuzi ukajikuta uso kwa uso na mamba. Hii maana yake ni nini? 

    Ni kwamba mwanandoa mzuri unaweza kudhani ni wa mwenzako kwa sababu kitanda usicholalia hujui kunguni wake. Kila binadamu ana matatizo awe hata rais au msomi wa kiwango cha juu. Huu ndiyo ubinadamu tunaopaswa kuukubali na kuufanyia kazi si katika ndoa tu bali katika maisha yetu yote. Maisha ni safari ndefu yenye kona, mabonde, mito, milima, vikwazo na hata lift.

Ni bora kuhitimisha tukisema wazi. Pig aua. Jua. Hakuna Daktari, mchungaji, mganga, fundi wa ndoa wala mwalimu bali wanandoa wenyewe kuwa tayari kuilinda ndoa yao, kujifunza, kufundisha, kujielimisha, na kuelimishana. Tumeyaona. Tumeyapitia.

Chanzo: Mwananchi leo.


Thursday 29 August 2024

TUKUMBUKE ZAMA ZILE NA MAMA MIA YA SAHLOMON



Ni CcM policy au geshi la polishi?


Katiba ya mafyatu inatoa haki na uhuru kwa kila fyatu kukutana na fyatu yeyote unayemtaka kutembea au kuandamana na unayemtaka kwenda unakotaka kusema unalotaka imradi usivunje sheria ya kaya ambayo nayo siyo maagizo au mapenzi ya ndata na wanaowatumia tena vibaya. Unapozuiwa kufanya hayo hapo juu na mengine kama au kukaribiana nayo, anayefanya hivyo havunji sharia tu bali katiba yetu virakaviraka ya mwaka 47. Kisharia, bila kujali cheo au sura ya yeyote, anayezuia uhuru wa kikatiba ni mhalifu sawa na wahalifu wowote.

 Kikatiba, haki na uhuru tajwa hapo juu siyo utashi wala hisani toka kwa yeyote hata awe mnene kiasi gani. Kaya ya mafyatu hutawaliwa kikatiba na siyo kichata wala kichawa. Uhuru ni haki ya kila fyatua. Msigeuze uhuru kuwa udhuru. Mbona mkipiga njuluku au kuzitumia vibaya Hamshikwi na kuswekwa lupango? Mbona mkipiga mnada kaya hamshikani, kufungana, hata kuswekana lupango?
            Mbona mafisi na mafisadi walioingia mikataba inayoanza kututokea puani hawakamatwi au ndata hawawaoni au wanawaogopa kwa vile wengi ni wanene au makuadi na washirika wao? Mbona tunawaona wakipeta na wengine hata kupewa ulaji zaidi ili wavimbiwe wafe, au kuna namna?

Wako wapi waliouza bandari, maji, na hata hewa? Wako wapi walioingiza madudu kama Buzwagy, Mwanakaya, IpTL, Kagoda, Eskorow, waliochoma banki yetu kuu na wengine wengi waliokwisharejesha namba? Kwani mtaishi milele kumbaff nyie?

Leo, tena kwa hasira na kifyatu, nitafyatua sakata la kuwadaka na kuwatia adabu viongozi wa upingaji. Japo mimi si wakili wao wala sitaki kujifanya kuwa, kwani wapo kisheria au kihiari? Je siasa ni haki au hisani? Hamjui kuwa maulaji yana mwisho? Wako wapi waliowabia kura za kula, wengine kuwapoteza mbali na walionusurika mitutu? Si wameyaacha maulaji na kutokomea kwenye kaburi na sahau? Hamuoni maulaji yaliyowahangaisha sasa yanaliwa na wengine tena ambao hawakuwa na nchango wowote zaidi ya unafiki na ufichi?

 Nashauri maulaji yasituchoganishe na kutufanya kunyatuana roho, kudhalilishana, na kutesana bure. Duniani tunapita. Kwanza, maulaji yenyewe ni ya mafyatu ukiachia kuwa ni ya muda. Kuepuka udhalilishaji, ukandamizaji hata uonevu, basi futeni vyata vya kisiasa na kusajili geshi la polishi kama chata cha siasa muone, maana limekosa kazi mbali na kufanya kazi za kisiasa na siasa za visasi na kutumika hovyo. Japo sipendi wala si mwanasiasa, napanga kuingia kwenye siasa ili nikomeshe siasa za visasi. Kwa nilivyo gwiji na nguli mwenye ushawishi, naamini nitabadili upepo wa kaya kisawasawa na kufanya kiumane nchana kweupe. Nashangaa. Tunaambwa vyata vipo kikatiba, vinapiga ruzuku mbali na kelele halafu vinakandamizwa. Basi, tangazeni kaya ya chata kimoja tujuwe na muone watasha watakavyowawashia moto na kuwanyima misaada japo Uchumi mnao lakini mnaukalia kama alivyowahi kusema mzee Nchonga (RIP sana tu).

Kila uchao mafyatu wanatekwa na kuibiwa. Ajabu hakuna ndata wa kuwalinda au kuwashukia wezi. Ajabu ya maajabu, magari ya wagonjwa na madawa hakuna wala njuluku ya kuajiri matibabu ila ipo ya kununua mibomu ya kutoa machozi, risasi, virungu, na zana nyingine za ghasia! Vitegemezi vya makapuku vinakaa chini na kukosa maticha ilhali ndata wanatesa! Hata nao hawajitambui. Hawa wanaowadhalilisha na kuwatesa ni ndugu zao hata kama hawawataki wala kuwaheshimu na kuwajali. Msitupeleke Bangla--- ambako mama alitemeshwa ulaji baada ya kulewa maulaji na kujisahau akayafanya kuwa urathi wa kifalme asijue hajui kuwa hajui.

Nani aliwachagua nyinyi na kuwapa power na utashi ya kukandamiza wenzenu wanaofanya usanii kama nyinyi? Tangu tunyake udhuru, sorry, uhuru, mmefanya nini cha maana zaidi ya kujihudumia kwa migongo yetu? Leo hii bei ya kila kitu imepaa huku wanene wachache wakitanua na kutapanya kama hawana akili nzuri. Mnataka tunyamaze au kupongeza wakati tunaumizwa na kudhalilishwa?  Kwani mafyatu hawajui wala kuona?

Zamani nikirejea toka kuutwika, lau, nilikuwa na jeuri ya kuwaletea vitegemezi pipi. Siku hizi, narejea home kwa kujificha kama mwizi ili vitegemezi visinione na kutaka zawadi. Ni maisha gani usawa huu wa karne ya sayansi na tekelinalokujia? Wanene wachache wasiojali mafyatu wanazidi kuongeza nafasi za ulaji hata zisizo kwenye katiba kama ule wa Dot p’Bitek, waziri mkubwa mdogo. Kwani hatujui wala kuona? Nawashangaa hata wanasharia wetu. Kwanini msiende kwa pilato na kuzuia israfu hii ya wazi au hamuoni? Lo! Nimepayukaje? Nimesema eti cheo cha p’Bitek ni unconstitutional au? Hayo tuyaache. Wajinga ndio waliwao. Mwalimu wangu usinibaini. Nikipata kumi tano zako. Hiv ndata wanaoatwanga wapinganji wanakumbuka viapo vyao? Ikitokea wanaowachapa wakaukwaa unene watakuwa wageni wa nani? laiti wangejua kuwa kazi ngumu ni kupanda na siyo kushuka! Wangejua hili, wangefanya wafanyayo kwa haki na tahadhari. Ngoja nikapate kanywaji nipate usingizi na kuepuka makelele ya yule kiumbe ajifanyaye ananipenda. Nimesemaje?

Chanzo: Mwananchi Jumatano iliyopita.

Unapochagua Mchumba Jua na Zingatia Yafuatayo

Kuoa au kuolewa, au kuoana kama wasemavyo siku hizi, si suala la kukurupuka au siku moja kama kununua tiketi ya bahati nasibu au kukodisha taxi. Katika kuchagua mwenza wako (wa maisha au vinginevyo kama hamtafanikiwa), unapaswa uwe makini tena sana. Usikurupuke kuamua kuingia uhusiano ambao una mwanzo lakini hauna mwisho isipokuwa kifo hasa kwa wale wanaofunga ndoa za kikristo (hata walio kwenye ndoa tofauti wangetamani iwe ni ‘kufa na kuzikana). Hivyo, ni muhimu kumjua mwenzako kwa madhaifu na ubora wake. Lazima uwe na orodha ya vitu ambavyo ungependa mwenze wako awe navyo kama vile umri, atokako, tabia, urefu, uwezo wa kufikiri, mvuto, mengine mengi kulingana na utakavyo bila kusahau kama nawe unavyo au unapimwa hivyo. Kama ilivyo kwenye kujenga nyumba au kununua gari, lazima ujue ukubwa hata muundo wa nyumba. Kama ni gari, ungependa kujua aina, ulaji wake mafuta, nguvu (horsepower), rangi, mwaka wa kutengenezwa na hata ubora na udhaifu wake.

            Kwa vile ndoa ni taasisi unaoingia kwa sababu za upendo na uhuru wa kuchagua, siyo sawa na kuzaa watoto au kuzaliwa. Wazazi hawachagui watoto wala watoto hawachagui wazazi kwa sababu hawana uwezo wa kufanya hivyo. Kwa upande wa ndoa, una chaguo huru ambalo likishafanyika, huodoa uhuru huo. Hivyo, unapaswa kuwa makini, mvumilivu, na mwelevu kufikia kusema I do.

            Tofauti na gari na nyumba, ndoa siyo mali yako binafsi. Ni mali ya jamii hasa kwa jamii za Kiafrika ambapo familia za pande mbili huanza machakato na hatua mpya ya uhusiano wa karibu usio na mwisho vinginevyo ivunjike japo si lengo lake. Hivyo, tofautisha kumchagua rafiki mnayeweza kufarakana na kuamua kuvunja urafiki. Ndoa ni zaidi ya urafiki maana, rafiki hana haki kisheria kumrithi au kumrithisha rafiki yake mali zake pale inapotokea kufariki. Tofauti, mwanandoa anakuwa na haki hata zaidi ya wazazi na ndugu kwenye kukumilki wewe na mali zako. Hivyo, huyu si mtu wa mchezo au wa kukwapukia. Siyo mchezo wa pata potea wala kamari bali jitihada makusudi zinazolenga kujenga uhusiano wa karibu katika maisha yenu yote. Hakuna anayefunga ndoa anayeomba au kutegemea ivunjike japo nyingi zinavunjika.

            Katika mila za Kiafrika, ndoa huwahusisha wazazi, ndugu, na jamaa katika kuanza kuijenga, hata wakati mwingine kuimboa na hufanya familia mbili tofauti kuwa moja. Familia mbili uhusisha familia nyingine nyingi ambazo hazikuhusiana kabla kuingia katika uhusiano usio na mwisho japo una mwanzo. Ndiyo maana tuna washenga, makuwadi, na wengine wengi tunawaowahusisha kwenye kuanza msingi wa ndoa ambao, kimsingi, ni watu wa karibu na wanaoaminika walio karibu nawe kwa uhusiano wa damu ambao, mara nyingi, huteuliwa na wazazi wetu tokana na ukaribu na imani yao kwao. Hii ni kutokana na wahusika kuwa na uzoefu wa muda mrefu mbali na ujuzi ambao huchukua miaka mingi kuupata.

Tunadhani utaratibu huu ndiyo uliowawezesha wazazi na mababu na mabibi zetu kutokuwa na talaka kwani ulikuwa siyo shirikishi tu bali wenye umakini zaidi katika kutafuta wahusika wanaofaa na kufaana tokana na walivyowajua. Kwa Waafrika hata neno talaka ni la kigeni litokanalo na lugha ya kiarabu iliyoleta Uislam. Kabla ya hapo, hatujui dhana hii ilivyotafsiriwa. Japo talaka zinatolewa, huwa si jambo la kufurahisha wala kutamani liwepo ukiachia mbali kwenye zile ndoa ambazo ni rahisi kuoa na kuacha kulingana na misingi na taratibu zilizojiwekea.

Kumalizia, bila kuzama zaidi kwenye mada tokana ufinyu wa nafasi. Wanyama hawana send offs, vyeti vya ndoa wala mikataba yanayojulikana kwa binadamu, wana dalili zinazoashiria thamani ya ndoa ikizingatiwa na maarifa ambayo binadamu ameyachota kwao, lina mashiko au ghorofa bila kuangalia kichuguu? Hii ni elimu mwanadamu aliyoipata toka kwa mwalimu mchwa. Kama tukubalivyo kupata ujuzi huu toka kwa mwalimu huyu, kadhalika tukubali na ukweli juu ya taasisi hii ya ndoa toka kwa viumbe mbali mbali waliotuzunguka.

Chanzo: Mwananchi Jumapili iliyopita.


Wednesday 21 August 2024

Hongereni Mafytu Kumpenda Mama

Mwanafalsafa’ maarufu wa Uganda, alhaj, Doktari, field Marshall, profedheha Idi Amin Kaidada  Oumee aliyepata elimu yake mtaani aliwahi kusema kuwa lazima watawaliwa wawapende watawala bila kujali lolote au wanawatenza vipi. Lazima wawasifie hata wakikosea. Wawachekee hata kama wanapaswa kulia. Wawaabudu ikibidi hata kama wao si Mungu. Kwani, kufanya hivyo, huleta ‘amani na maendeleo’ hata kama kuna kero. Kwa kuzingatia ushauri huu wa kitaalamu wa fyatu aliyewafyutua waganda akataka hata kutufyatua kabla ya JWTZ kumfyatua na kumg’oa, mafyatu juzi walionyesha upendo usio kifani. Si walimnunulia maza chopa kwa ajili ya kuivinjali kaya yake tukufu. Ni jambo la kupigiwa mfano na kumshukuru Mungu aliyewapa moyo wa upendo.
            Dunia hii we acha tu. Si walijitokezea wenye wivu tena wa ki-female wakaanza kusema eti ni hongo na kielelezo kuwa kutakuwa na uchakachuaji. Maana, wanasema tena bila aibu kuwa mafyatu waliomnunua chopa, kwanza, wamepataje njuluku na wanategemea kuzirejesha vipi. Wanasema. Akishafyatua ulaji, nao watamfyatua kwa kutaka alipe fadhila. 
        Wanahoji kwanini wasinunune ambulances za kubebea wagonjwa. Au ni yale ya ndata kuwa na ndiga wakati wagonjwa hawana? Hayo si yangu.
        Wafyatuane au la, hayanihusu. Muhimu wasinifyatue na mafyatu wenzangu. Je kama ni kweli kuwa huku ni kufyatuana kunakolenga kulipana fadhila, mafyatu tutanusurika wakati kaya itakayofyatuliwa ni yetu? Je tutakubali kufyatuliwa na hawa wanaofyatuana ili watufyatue? Je tutawafyatua kwa kutowapa kura ya kula ili wasitufyatue au tutafyatuliwa mkenge? Niliwahi kuwadokezea mafyatu wa upingaji walivyowahi kuhoji tukutuku zilizosambazwa nkoani wakisema kuwa bi Nkubwa anawahonga watendaji. Walihoji alikopata hii njuluku tena mabilioni, ananunua, nani, nini, na anategemea kupata nini. 
        Kwa vile mie siyo mpingaji wala muungaji au msifiaji bali mfyatua, natimiza wajibu wangu wa kufyatua bila kuwaudhi wanene ambao hata nikiwaudhi hawana grounds au locus standi kwa lugha ya kisharia, kunifikisha kwa pilato. Hii jamani nayo ni sanaa. Ukiona umefyatuliwa, huna haja ya kunichukia au kulalamika bali kujirekebisha au kufyatua kijanja. Hayo tuyaache. Mibangi hii! Sasa naanza kufichua siri!
            Turejee kwenye ununuzi wa chopa na umuhimu wa watawala kuwapenda watawaliwa hata kama wanawaponda au kuwafyatua.             Kwanza, ni jambo bora kumchangia mama kipenzi kuliko kuwapa njuluku matapeli wa kidini wanaotoza njuluku eti kutoa maombi aka huduma wakati ni huduma. 
        Juzi nilimsikia jembuz mmoja toka kaya ya jirani anayejiita kiboko ya wanga wakati naye ni tapeli wa kawaida. Hivi inakuwaje kaya yetu inageuzwa shamba la bibi tena mwenye kipofu? Kwanini mnaruhusu matapeli tena wenye mtindio wa mawazo na wavivu wa ubunifu kuja na kuwafyatua mafyatu wenu mliowasikinisha na kuwajaza ujinga na kukata tamaa hadi wakaamini kila upuuzi? Au hao nao wanawasaidia kuwafyatua kwa sababu wanawaaminisha mafyatu wachovu na wavivu wa kufikiri kuwa ukapuku wao ima ni kazi ya muumba au wachawi?
         Sijawahi kujua kwanini mafyatu wetu wamekuwa wa hovyo hivi. Hivi, kweli kwa anayejua umaskini waliotegeneza akina Mobutu, kuna la maana unaweza kupata kwa jamaa hawa mabingwa wa utapeli sawa na wale kutoka kwa akina Buhari ambao ujanja wao ni utapeli tu na siyo ubunifu wa maana? Nasikia siku hizi kila tapeli anatumia gea ya kuwowa mabinti wa kidanganyika wasiojua hili wala lile ili kuishi kwenye kanani ya Afrika chini ya mama kipenzi.             Mtaachwa Solemba. Hawa jamaa wakishapata wanawaacha na vitegemezi vyenu kiasi cha kugeuka wajane bila kufiwa. Kuna haya ya kuanzisha safu ya kuwaelimisha mabinti zetu waache kushobokea wageni wasijue hakuna la maana zaidi ya kuwa visa za kuishia kayani. Huku Ulaya ni jambo la kawaida. Wanachotuzidi watasha ni kwamba waswahili wanaotaka kuishi hapa kwa gea ya kuoa, lazima watimize matakwa ya wadada wa huku na kugeuzwa mashine ya kunonihino. We! Koma. 
        Wapo wengi wananyonywa sawa na mabinti zetu wanaonyonywa na hawa matapeli uchwara. Hali ni hiyohiyo bondeni. Nakumbuka mwanamuziki wa kwaya aitwaye Debbie Fraiser aliyeingizwa mjini na tapeli toka kwa akina Buhari na kumharibia maisha hadi kunyotoka roho.  
        Mna habari kuwa hata Brenda Fassie aliponzwa na matapeli haya? Fumbueni macho ya mabinti zenu waache kutumika kama ilivyokuwa zamani ambapo vijana wengi wa kibongo walibebeshwa miunga na kuishia kufungwa na kugeuzwa mashoga kwa tamaa na ukumbaff wao.
        Kimsingi, kumnunulia mama kifaa ni ushahidi kuwa mafyatu wanampenda kama siyo kufyatuliwa na baadhi wenye ukwasi ili wamtumie. Pia, inaonyesha kuwa si mafyatu wote ni mataahira wa kuibiwa na kila tapeli kama yule jambazi toka kwa akina pedejee wanaokuja na kuwaibia au waganga wa kienyeji wanaowaibia wakidai wanawasaidia kutengeneza utajiri wakati wao ni maskini wa kunuka.
        Tumalizie tukiwapongeza mafyatu na kuwashauri wawe macho kuona huu mchezo utaisha vipi nani atamfyatua nani na nani atazembea akafyatuliwa. Hivi nimesemaje? We koma.
Chanzo: Mwananchi leo.

Thursday 15 August 2024

Nashauri Kununua Majenereta Kuendeshea SgR


Baada ya kuwafyatua kwa SgR kufanya majaribio, nilionya kuwa safari zingeanza pindipo mwana wa Adam­­­––––yule fyatu wa kiyahudi anayeabudiwa na mafyatu wengi duniani hadi wenzake mafyatu wanasema kwanini tusiwaabudie wote wakati hawana lolote zaidi ya mikwara na kuiona bora kuliko wengine wakati ni hovyo–––akirudi si waliamua kunifyatua na kujifyatua na kuanza majaribio. Nikiri. Nilikosea. Juzi mtukufu mpendeka, msikivu, mwenye maone, Doktari rahis Mama alizindua safari za mwanzo. Je hizi safari zinazopigigiwa upatu ni endelevu na fyatu au danganyifu? Wale wanaoelewa nilichofyatua, wako wanafyatua maandalizi ya kuja kwa njemba hii iliyopumbaza wengi kuwa iliwaokoa wakati iliwatonya kuwa kila fyatu atabeba furushi lake mwenyewe siku ile ikifika. Chonde chonde, wale makanjanja wenye uroho wa kiroho msianze kuwafyatua na kuwachuna mafyatu zoba yanayoamini kila kitu hadi wanaitwa kondoo na kuchungwa na wachunaji wanaoishia kuwachuna na kuwasikinisha wakijiona kama mataahira. Yangu mato.
        Gwaijimmy, Katortoise, Gamanyie, Mwakasegie, Lusekelelo, Godavie, Muingirer, Mwamposer, Mutalemewa, na matapeli wachunaji, sorry, wachungaji mnanipata? Yaani hamuoni ni dhambi kuwafyatua mafyatu wasio na hatia bali ukumbaff na kukata tamaa? Je mnajua yaliyoibuliwa kuhusiana na mwenzenu Tii Bii Joshuer, beberu fyatu aliyefyatua watumishi wake njuluku hata uroda? Mnamfyatua nani wakati soon mtafyatuliwa na God mnayemtumia kuwafyatuliwa na kuwatapeli mafyatu majuha? Mshajiuliza, mkizeeka na kukaribia kufyatuliwa mtafyatua nini lau kuepuka kuingizwa motoni hata kama hamuamini kuwa moto upo?
        Kwanza, sijui kama hawa walioamua kunizodoa kwa kufyatua kiini macho wana umeme, uaminifu, utaalamu, uwajibikaji, na uzalendo vya kutosha kunifyatua kwa kufanya kweli kabla sijaja na fyatuafyatua na zomeazomea zaidi hadi kuwafyatua mafyatu wakawafyatua tofauti na mlivyotegemea wala kuotea. Basi, ngoja niwafyatulie kweli. Mnaweza kujimwabafy kuwa bwawa la Mzee Mchonga limeanza kufyatua umeme msijue watendaji wetu uchwara wanaweza kulihujumu au kuzembea kikaumana tena. Jikumbusheni jinsi bundi na ngedere walivyoifyatua SgR juzijuzi.
            Hivi tunakosa umeme tokana na kukosekana umeme au ubunifu na uzalendo wa kutunza miundumbinu yetu mbali na lisrikal kupenda kutumia umeme tena hovyo bila kulipa ukiachia mbali kuwa linapigwa njuluku kila siku na linabaki kutoa mimacho kama panya aliyefyatuliwa na ntego? Huwezi kutegemea mambo yaende kisayansi na vyedi wakati wahusika wanaishi kwa kujikomba, kusifiana, hata utopolo bila kuchapa mzigo. Huwaoni? Kila anayeongea utamsikia “napenda kumshukuru Mwenyezi Mungu yada yada yada… na ukumbaff kibao.’ 
            Anaendelea “pia, napenda kumshukuru mno na sana bila kukoma wala kukomaa mtukufu, mpendwa, mpenzi, mwenye mapenzi yasiyomithalika kwetu hata kuliko mshirika wake wa bedroom, mwenye masikio makubwa na asiye na mdomo, asiyejivuna hata akijivuna, doktari, profesa emeritus, al- hajat, ustaadha, sheikha,  sayidat rahis yada yada yada na pumb’a kibao.” Unategemea mafyatu kama hawa wasiojiamini, wanaodanganya, wanaodanganyana, na kusifiana badala ya kufyatuliana ukweli wanaweza kupambana na tatizo kama hili linalohitaji umahiri, ukweli, na weledi bila kusahau ufyatu?
            Hapa tunachoona ni kupakana mafuta kwa mgongo wa chupa kwa kufyatuana kwa kusifiana kwa sababu tunapenda kusifiwa na kuabudiwa. Mie mafyatu wangu, pamoja na kujua ni daktari wa kweli na siyo hawa madoktari wa heshima, niliwapiga marufuku kuniita daktari. Ndiyo maana hata kwenye uga huu huoni udaktari wangu tena usiofeki kama wa akina au wa kuzawadiana au wa kununua kama wa akina Gwaijimmy na matapeli wenzake. 
            Kesho mtasikia na waganga wa kienyeji wakiitwa doktari hata maprofesa! Hata hivyo, kama maprofesa wenyewe ni akina wa jalalani, tutegemeeni? Tokana na uzoefu wetu, kufyatuliwa, kuanza safari na kufanikiwa ni vitu tofauti. Kwa vile kaya yetu ni ya majaribio, wanaweza kufanya majaribio hata milioni. Je lengo la kuzamisha matrilioni ya madafu kwenye mradi huu ni kufanya majaribio au kufanya kweli? Je hizo njia zilizojengwa na makandarasi wa kutia shaka, zinaaminika na zina thamani sawa na njuluku tunayopigwa baada ya wanene wachache kula dili? Je tatizo hapa kama ambavyo imekuwa, ni nini kama siyo wanene wetu?  Kesho umeme ukigoma, tutapigwa kwa kisingizio cha kununua portable jenereta za kuzalisha umeme wa SGR. Unacheza na kaya hii sanii siyo?
        Najua mafyatu wengi hawakuambua. Niliposema majaribio nilimaanisha majaribio ya kufanya kweli siyo kutuonyesha vichwa viwili vitatu vya treni na kuminya. Narudia, hili halifanyiki na kufanikiwa hadi mwana wa Adam arudi. Atarudi lini? Msiniulize. Kawaulize wao. Pia, hakuna haja ya kuchukiana maana mie si wa kwanza kutoa ahadi hii. Atarudi kweli au la? Nani anajua wakati wote mtakuwa mmeishafyatuliwa na kulala milele bila kujua ukweli mchungu yote ilikuwa fumbo la imani la kuwafyatulia mafyatua wasifyatuane kinyama. 
        Naona yule anatikisa kichwa na kufyatua midomo kwa hasira. Huna haja ya kunichukia. Simpo, anapofyatuka fyatu na kurudi kwa mfyatuaji wake huwa si mnasema uilaze pema roho yake milele baada ya kumuweka kwenye makazi yake ya milele. Unajua maana ya milele? Hivi safari za majaribio zimefikia wapi na zimefanikiwa au kukwama kiasi gani? Je usafiri wa kweli utaanza lini, maana kwenye mitandao sioni kitu tena? Basi, jiandaeni kununua majenereta kuendeshea SgR. Vipi mafuriko Bwala la Mwl Mchonga? Du! Kumbe napanga kuwasaka bundi na ngedere niwatie adabu!
Chanzo: Mwananchi jana.


Thursday 8 August 2024

FYATU MFYATUZI: Ukweli nchungu kuhusu uchaguzi wa mwaka 2025


Nikiwa kwa akina Nshomile, wapo wachionjiua wala lengo langu. Nilipochema ukweli walidhani namwaga ntama kwenye kuku wengi baada ya kuchoshwa na dhuluma wanaona kama ulijifanya nshomile. Kuna mmbea mmoja kanitonya eti nilikuwa nimepewa ka-nshomile nilikolala nako kakanizingua nikafyatuka na kufyatua niliyofyatua nikasahau kuwa ningewaudhi wengi hacha wanene wa chata wanaotaka chacha nifyatuliwe wachijue chi vizuri.                                     Kilichowakosha mafyatu ni kufyatuka na kufyatua ukweli, sorry, upupu ulioacha Chama cha Mafyatu (CcM) hoi japo hai. Wapo wanaozusha eti nilikuwa amefyatua lubichi, kimpumu, gongo, na waragi toka UG. Wapo waliochema eti nilivuta chigara kubwa chiku hiyo ikanifyatua nifyatuka hadi kufyatuliwa. Wangejua kuwa hata juichi huwa chinywi kwa kuogopa inaweza ku-ferment ikanifyatua, wachingefyatua wanayofyatua. Hata kama nilipata kanywaji wao yawahuchu nini? 
Hata kama nimefyatuliwa, najivunia nilivyopayuka, chorry, kufyatuka wachijue mie ni Fyatu Mfyatuzi aka Mpayukaji Mchemahovyo zamani kabla sijabadili dini na kuwa na dini ya Mwananchi hadi nikapewa chafu hii. Nimechemaje? 
            Chiogopi wala kuchononeka. Hii kwa kimakonde huitwa collateral demage. Chijali. Ukifyatuka ukafyatua lazima ufyatuliwe. Kamuulize mhariri wangu. Chamtaim, hutaka kunifyatua. Huwa tunayamaliza kichikaji. Hivo, pliji, don’t take me chiriyachili. Hayo tuyaache njomba.
             Eti wanashangaa Nilivyochema eti kwenye uchakachauaji ujao, kama kawa, kutakuwa na upigaji halafu wahuchika watatubu na kuomba Chir God awachamehe. Kwani chili? Hawajali mafyatu watafanya nini? Wanadai eti ninawaona mafyatu kama hamnazo kama mie wanayedhani eti china akili na ujachiri mkubwa chana wakati nimeonyesha wazi nilivyosheheni kwangu. Nilimchikia mmoja akiniita mkumbaff achijue ukumbaff mwingine unalipa njomba. Kama unafanya ukumbaff unachinda, shida iko wapi? Kwanini nao wachifanye ukumbaff huo huo kuwazuia na wakachinda?
Nawachangaa wanaonichangaa na kunitukana. Mbona yupo waziri aliyechema eti chichi tunakopa kwa vile tu matajiri wakati raichi anachema anadhalilishwa kwa kukopa na hakuchukuliwa hatua? Mbona yupo aliyetengeneza uhaba wa chukari na bado anatecha? Mbona hata aliyetuhumiwa upigaji Mirerani amepandishwa cheo?
Zifuatazo ni chababu kuntu za kujipongeza:
        Fechiti, najua wengi hawanijui. Hii ni chiri uchiwambie hawajui nimerithi ujachiri wa dingi wangu? Mara nyingi wengi wakiniona humwaga chozi. Maana ni kama huwa wanamuona njomba kanali Mucha mwenyewe baba yangu mzazi.
        Chekandi, napenda ukweli na uwazi kama njomba Ben Nkapa. Hii ni achili yetu. Kuchema ukweli njomba. Nadhani huko Njomba Nkapa alipo atakuwa anafurahia kaburini mwake.
        Three, japo mimi chiyo chehe, nimetabiri vizuri kuwa Chichiemu itashinda hata kama ni kwa goli la mkono kama ilivyotokea 2015 nilivyotabiri bila kukochea au kupitia nje ya chanduku la kula kama ambavyo itatokea mwakani. Nani hajui hili japo wengi tena wanene wanaficha? Hawajui kuwa mie chiyo ntu wa utani utani!
        Nne, nimethibitisha kuwa ni gwiji la hichitoria. Rejea zilivyokuwa zikifyatuliwa kula za kura kama nilivyowahi kuchema kuwa ni goli la nkono. Naamini hii itarudiwa uchawa huu ambapo mnachema mitano tena kwa maza. Kwa wachio kujua nawachauri warejee hichitoria. Nakumbuka kicha cha kule Ntama ambako mshindani alipotea kabla ya kurejesha fomu nawe tukapeta? Nani hakumbuki kuwa hata aliponyatuka Mwendaze nilichema eti Mungu kaamua ugomvi? Hawa nazani wamechahau au wanijui au wanajifanya kutonijua. Wanachahau kuwa niliwahi kuchema kuwa huwezi kuchonga kinyago halafu kikakutisha. Chijui kinyago ni nani hapa.
        Tano, kama ushauri wangu utazingatiwa, tunaweza kuokoa njuluku ambazo zimekuwa zikipotezwa kwenye uchakachauaji ambao matokeo yake hujulikana hata kabla ya kufanyika kama ilivyo kwa majirani zetu wa Rwanda na Uganda. Kwanini kupoteza njuluku wakati tunacholipia ni kujitia hachara na kinachotakiwa kinaweza kupatikana bila kutumia njuluku. Bahati mbaya, wanaokulaumu hawalioni, kulijua, wala kulikubali.
        Kabla ya kumaliza, ngoja nimguchie pia rafiki na mshirika wetu Mgoshi wa Bumbui. Naye alifyatua maulaji hadi yakamfyatua akafyatuka kabla ya kufyatuliwa. Chijui mzee wake anajichikiaje chacha. Maana, aliwahi kututambia kuwa vitegemezi vyake vina akili chana na lazima kuteuliwa uwaziri achijue kuna na kutumbua aka kufyatua. 
Chijui huyu naye chiku hiyo alikunywa kanywaji gani hadi kuchema eti hawampendi mtukufu raichi doktari mpendeka. Tate nane tate nane.                         Niliwaonya kuwa kuchifia kupita kiachi chaa nyingi hupitiliza na kuchababisha kukufuru kama huyu aliyemponda maza wakati alikuwa akijionyesha kuwa anampenda. Nadhani mlichahau mlilvyotumbuliwa na Mwendazake akawachamehe na akafyatuka mkaendelea kumchengenya. Hayo tuyaacha. Nangoja kuona wengine kama wale wa walitengeneza uhaba wa chuga, wenye kachifa za mirerani japo naona wengine wamepandishwa, na wale wote wachiomchaidia mtukufu raichi daktari. Hivi leo ni chiku gani?
    Chanzo: Mwananchi jana.

Monday 5 August 2024

Epuka au Usiwe, Kuoa au Kuolewa na RST

Tumeumbwa watu kila aina wabaya hata wazuri. Kwa vile ndoa hufungwa na wanadamu, tunaomba tugusie suala nyeti bila kuonekana kama tunabagua au kuwawekea utu ubaya. Hivyo, siyo uzushi kusema dunia ina watu wazuri na wabaya. Leo tutaongelea tutakachokiita RST bi maana ya Roho mbaya, Sura mbaya na Tabia mbaya. Kwanza, tukubaliane. Kuna watu wenye sifa hizi.
Tutaanza na kisa cha kijana mmoja wa kiume mtanashati na handsome (hatuna Kiswahili chake). Kijana huyu alijaliwa elimu na kazi nzuri vilivyompatia kipato mbali na biashara zake. Pamoja na yote, tokana na makuzi yake ya kizazi cha zamani, hakuwahi kuwa kwenye mahusiano tokana na sababu zifuatazo:
        Mosi, malezi yake yalikataza uhuni au uhuria unaoanza kujitokeza kwa kuigiza wazungu ambapo watu wasiooa au kuolewa huanza mambo ya wanandoa. 
        Pili, alichelea kuzaa kabla ya kuoa jambo ambalo hakutaka liwe kikwazo katika ndoa yake. 
        Tatu, hakutaka watoto wenye mama tofauti aka rangi mbili.
        Nne, alikuwe mwenye aibu na mwenye kujitunza vitu viliviyomtenga na mambo ya starehe. 
        Tano, alitunza fedha ili baadaye awe na familia yenye maisha mazuri. Mfano, alijenga nyumba na kununua gari kwa ajili ya shughuli zake za kikazi na kibiashara kabla ya kuoa. 
    Sita, aliogopa kuwakwaza wazazi wake kwa kujiingiza kwenye mambo ambayo, kimila lazima yapate ridhaa yao. Hivyo, alingoja kupata mwenza atakapoamua kuoa.
        Pamoja na kijana yule kutotaka kuoa kabla ya kukamilisha malengo yake na kuheshimu taratibu, hakukosa akina dada waliompenda ima kwa sababu ya u-handsome wake, elimu yake, au fedha. Mwenyewe aliendelea kujijenga ili awe tayari kuanzisha familia yake. Siku ya kutafuta mchumba, alipata taabu sana. Kwanza, alikuwa mwenye aibu na ambaye hakuwa na uzoefu wa kuwa na mawasiliano na akina dada hasa akichelea wangemuingiza majaribuni.
        Kadri siku zilivyokwenda, dada wengi jirani waliomjua walimuona mdenguaji au mwenye tatizo. Hivyo, waliacha kumsumbua na kukosa imani naye. Hapa ndipo tatizo lilipoanza. Akiwa yuko tayari kutafuta mchumba, alijikuta hajui pa kuanzia. Akiwa katika mchakato, aliajiriwa dada mmoja kazini kwake ambaye, licha ya umri kwenda, alikuwa si mwenye sura nzuri na wala hakuwa mechi ya yule kijana si kwa tabia wala sura. Hivyo, tutamuita jimama.
        Tokana na muda kwenda, jimama lilipogundua kuwa yule kijana mtanashati hakuwa na mke wala rafiki wa kike, lilianza kumzoeazoea kiasi cha kuanzisha urafiki wa kawaida. Jimama lilikuwa lilishafanya kila aina ya ufuska, utoaji mimba, uhuni wa kila aina kuchumbiwa hata kuvunjika uchumba kutokana na tabia mbaya. 
        Yule kijana–––tokana na kutokuwa na uzoefu––––si jimama likamzidi ujanja likamshawishi kuanza mahusiano. Haukupita muda, jimama lilimtegeshea mimba. Kabla ya hata kujua la kufanya, jimama lilihamia nyumbani kwake kwa kisingizio cha mimba yake. Kwa vile hakutaka kuzaa bila kuoa, kijana alijikuta akiingia matatizo makubwa kwa kukubali kulioa lile jimama japo hakulipenda toka rohoni.
           Kwa upande wa jimama, lilishinda mambo matatu kwa mpigo. Lilipata mume tena msupu au mhandsome kama wasemavyo wakenya tena mwenye fedha na historia ya kutokuwa mhuni, na mtoto. Ni kama ilikuwa ndoa ya mwewe na njiwa. Alilitambulisha kwa wazazi wake, walistuka na kuhofia kulikuwa kuna namna lakini wasiingilie kwa kuogopa kumvunja moyo mtoto wao au kuingilia chaguo lake. Yule kijana aliamua kulioa hilo jimama.
                Maisha yalianza. Jimama lilokuwa pole kabla ya ndoa, ghafla, lilianza vituko kwa vile lilikuwa limeishaolewa na kumzalia mtoto. Mungu hamfichi mnafiki. Lijisahau. Lilianza kumchuna yule bwana kwa vile lilijua lilivyolazimisha ndoa. Hivyo, lilihofia huenda jamaa angeamka usingizini na kulipiga teke. Hivyo, zile tabia zake asili yaani RST zilianza. Kama tulivyogusia, jimama lilianza kuonyesha uhalisia wake. Lilianza kuwachukia ndugu za mumewe. Lilianza mahusiano na marafiki zake wa zamani wakiwamo hata ndugu wa karibu maana lilitoka kwenye  makabila ya wapenda fedha na ambao huchukuana ndugu kwa ndugu.
         Baada ya mume kustuka na kuanza kuwa mkali, jimama lilikosa kujiamini likaanza kusaka madawa ya mapenzi wa waganga wa kienyeji lisijue hakuna dawa ya mapenzi bali tabia njema, uaminifu, na mapenzi ya kweli. 
        Kufupisha kisa kizima, jimama liliishia kuachika tokana na RST. Hivyo, mnaopanga kuoa hata kuolewa, mjiepushe na RST iwe mke au mume. Tabia njema ni silaha tuliaswa. Kwa waoaji wasio na uzoefu, washirikisheni wazazi wenu yasiwakumbe yaliyomkuta kijana huyu asiye na hatia. Msikurupukie mahusiano bila kujiridhisha kuwa mnaingia kwa kuzingatia uchaguzi wenu. RST ni sawa kilema. Haitibiki. Iepuke. Ni vizuri wanandoa wakaendana kulhali japo wakati mwingine mapenzi hayachagui. Muhimu, tusilazimishe ndoa. Haitadumu. Tusitafute dawa ya mapenzi. Hakuna. Tusiingizane mkenge katika ndoa. Tuwaingizao watakengeuka na kulipiza kisasi.
Chanzo: Mwananchi jana.

Wednesday 31 July 2024

Sir God Ameniamuru Nilete Dini ya Ukombozi

Baada ya kugundua kuwa mafyatu wake wengi wameharibikiwa na kuchanganyikiwa kiasi cha kufyatuliwa na kudhalilishwa na kila tapeli, Sir God ameniamru nilete dini ya Ukombozi. Hii ni baada ya kuona kuwa matapeli wengi wanawafyatua mafyatu waliogoma kuelimika wakawafyatua wanaowafyatua. 
        Nimeona mafyatu wangu wakiuziwa kila upuuzi kuanzia maji tena machafu, mafuta tena ya kishirikina, notebooks, kalamu, leso tena chafu, wengine wanavuliwa hata nonihino na kushikwashikwa vyote ukiwa ni utapeli kuwaibia wajinga ufanyawao na wajinga wenzao waavivu wa kufikiri na kubuni mambo ya manaa. Ni ujinga pande zote matapeli na wanaotapeliwa. Wengi hata hiyo elimu hawana. Wala hawana ubunifu wa kubuni vitu visivyo vya kikumbaff kama hivi. Wote wanahitaji ukombozi utakaoletwa na dini ya Ukombozi. Mafyatu wanadhalilika hakuna mfano. Wanahitaji Mkombozi ambaye ni mimi na ukombozi ambao ni dini ya Ukombozi. Wale uliotegemea wawazindue, wanawafyatua au kushirikiana au kuwafumbia macho wanaowafyatua.Wahenga kweli walisema wajinga ndiyo waliowao.
            Kwa vile imemfurahisha Sr God nipambane na jinai hii kwa kunishushia dini yake, msishangae mkisikia naongea lugha msizoelewa. Hata hivyo, hamtashangaa. Kama matapeli toka kaya nyingine wanakuja na kuwafyatua, kwanini mnishangae mie ninayewashangaa? Hamjawasikia wanaokuja na kujianzishia madhehebu ya kinyonyaji na kitapeli huku wakiuwauzia ujinga na woga? Naona yule anatikisa kichwa akishangaa sirkal iko wapi? Kwani wawili hawa wana tofauti? Kazi ya sirkal si kuwafumbua macho mafyatu. Kazi yake ni kuleta wachukuaji, sorry, wawekezaji waje wafaidi vinono vya kaya yetu. Tena nimekumbuka. Dini ya Ukombozi itawasaidia hata wanasiasa wanaotaka kushinda uchaguzi. Nawashauri waje niwaombee ilmradi walete mbuzi na ng’ombe na kutembelea Chegama.
        Kuanzia sasa nitaitwa Daktari, Genero, Papa, Mtakatifu,  Mtukufu, Mwenye maono, Mponyaji, Muota ndoto, Mtabiri Dk, Alhaji, Mhashamu, His Excellency, His Eminence, HH etc. Fyatu Mfyatuzi bin Mfyatuaji bin Mfyatukage wa Mfyatulizi mwana wa Mfyatukizi mjukuu wa Fyatuafyatua mwana wa Mfyatuizi kijukuu cha Mpayukaji Msemahovyo Msemakweli.
        Kijiji changu cha Chegama, kuanzia sasa, ni sehemu takatifu kuliko zote duniani. Hapa ndipo Mafyatu tulipotua tulipotoka mawinguni na kuanza kuijaza dunia. Mafyatu wote duniani walitokea kijiji hiki ambacho wao huita Bustani ya Edeni. Tokana na utukufu wake, Mafyatu wote duniani wanaamriwa kuja kutembelea sehemu hii takatifu mara tano katika maisha yao bila kujali ni makapuku au wakwasi.
        Nyumba nilimozaliwa, kuanzia sasa, ni hekalu la Sir God pia sehemu ambapo mafyatu watakaokuja kuonyesha utii wao watazunguka na kubuni lolote la maana watakalo na kulipata hapo hapo.
        Kwa vile Sir God amenipa madaraka ambayo hajawahi kutoa kwa yeyote isipokuwa mie,  kuanzia sasa, picha zangu zitasambazwa dunia nzima na mafyatu watakuwa wakiziweka kwenye sehemu maalumu za ibada. Kila picha itauzwa kwa dolari za Kiamerikani elfu tano. Itabidi kila kijiji kuchangishana na kuhakikisha wanakuwa na picha yangu kama mwakilishi wa Sir God aliyeniamuru kuleta dini ya ukombozi.
        Kuanzia sasa, kila fyatu atapaswa kutoa kafara ya mbuzi au ng’ombe jike kulingana na maelekezo yangu anapotembelea sehemu takatifu ya Chegama. Hawa wanyama watatunzwa hadi siku ya mwisho watakapochinjwa kwenye karamu ya mafyatu wote duniani. Hivyo,  nitaiamrisha sirkal kupanua eneo la kijiji ili kuweza kutunza zawadi hizi za Sir God mwenyewe.
        Kuanzia sasa sitatembea kwa miguu. Sir God ameniamuru niiambie sirkal kunijengea hekalu kila kaya, kuninunulia mashangingi idadi nitakayo, mashua na ndege ili kuniondolea msongo wa mawazo nna kuweza kuizunguka dunia haraka na kwa raha nikitangaza ukombozi wa mafyatu wote duniani. Nitatumia mahekalu yangu matakatifu kwa ajili ya kuwakirimu watakaokuja kuonyesha heshima yao Chegama. Mashangingi na ndege vitanisaidia kutembelea duniani nikionyesha utajiri wa Sir God na upendo wake kwa mafyatu wanaoibiwa na matapeli wanaomtumia.
Kuonyesha kuwa mie si mganganjaa, msakatonge, tapeli au jinga kama wale, kuanzia leo nitakuwa nafanya muujiza mkuu ambao ni kutoa mhadhara kuwa hakuna miujiza duniani bali ukumbaff na ujinga. Kupitia ufyatukaji, nitakuwa nikifungua vichwa vilivyogandishwa na woga wa uvivu wa kuchapa kazi. Nitawaelimisha mafyatu namna ya kufyatua wezi wanaowaibia ili waweze kutajirika badala ya kutegemea kuombewa.
        Nitafanya miujiza ya kuwafyatua mafyatu waache ukumbaff. Mfano, wote wanaotegemea waganga wa kienyeji au wachunaji waitwao wachungaji walewe kuwa ni wakumbaff. Kwani hawapo? Ni wangapi wanawajaza mafweza wanganganjaa na wachunaji eti wapate utajiri bila kufikiri wala kuchapa kazi? Ni akina mama wangapi walioishiwa kimaadili wanakimbizana na kudhalilishwa kwa waganga wa kienyeji eti wakitafuta dawa ya mapenzi wakati hakuna? 
        Siku hizi wameanza kuua zeruzeru kutafuta bahati wakati ni ukumbaff. Wangapi wanaamini kwenye ukumbaff wa kutoana kafara ili watajirike? Wangapi wakiwaona mataahira kwenye jamii fulani tajiri zinazosifika kuoana ndugu kwa ndugu na kuzaa mataahira wakadhani eti hao mataahira ndicho chanzo cha utajiri wasijue chanzo ni kuoana ndugu kwa ndugu? Kwani hayapo haya?  Hili ndilo lengo la kuanzisha dini ya Ukombozi. Semeni hamna.Hivi kumeishakucha?
Chanzo: Mwananchi leo.

Monday 29 July 2024

For and in the memories of Hugh Masekela and Tebogo Modingoane

https://www.youtube.com/watch?v=7StGJtI7SSI

Mwenye mapenzi anaona tena sana


Kuna imani au tuseme usemi kuwa mwenye mapenzi haoni. Je kweli mwenye mapenzi haoni hata kama macho anayo? Je ukweli ni upi haoni au anaona tena sana? Ingawa “mwenye mapenzi haoni” ina tafsiri nyingi kutegemea na hali yaliyomo mapenzi, ukweli ni kinyume. Tutatoa sababu zifuatazo:
        Kwetu mwenye mapenzi lazima aone na aone kwelikweli. Utawezaje kuujua uzuri na mvuto wa mwenzako kama kweli mwenye mapenzi haoni? Ingekuwa hivyo, watu wengi wenye changamoto za aina mbalimbali za ulemavu ambazo ni kazi ya Mungu wasingenyanyapaliwa, kukataliwa, na wengine kutoolewa kabisa au kuachika tokana na changamoto ambazo siyo matokeo ya kazi wala utashi wao. Pia, ukitaka kujua mwenye mapenzi aone, jiulize ni visa vingapi wanandoa waliopeanda haswa walipoachana au kuuana baada ya mmojawapo kumtendea mwenzie mabaya? 
            Kuna kisa cha wanandoa wawili ambapo mke alikuwa si mzuri wa kuvutia ikilinganishwa na mumewe ambaye alimpenda mkewe vilivyo. Hata hivyo, kwa kujua anapendwa, mke alipata msukosuko wa ndoa akatembea na mganga wa kienyeji. Pamoja na mapenzi makubwa yaliyovutia wengi, mume alimuacha mkewe bila hata kumpa nafasi ya kujitetea. Kwa ufupi ni kwamba mwenye mapenzi anaona tena mambo mengine ambayo katika hali ya kawaida huwezi kuyaona wala kudhania yanaweza kuonekana. 
        Kisa kingine ni cha jamaa tunayemfahamu mwenye ulemavu wa macho. Ndugu zake walimtafutia mke toka nchini kwao kuja Kanada bila kumwambia ukweli kwa vile aliwahakikishia kuwa anampenda yule Bwana. Kufanya mambo kuwa magumu zaidi, walimuonyesha picha ya mdogo mtu badala ya muoaji mwenyewe wakiamini akifika Kanada, atazubazwa na uzuri na hali nzuri ya maisha. Pamoja na kuwaonya kuwa walipaswa kumueleza mchumba mtarajiwa kuwa ndugu yao alikuwa na changamoto ya kutoona, hawakufanya hivyo wakiamini mtarajiwa akifika asingeweza kumwacha mtu aliyemfadhiri kuja Kanada. Waliogopa kumwambia wakiogopa kuwa mtarajiwa angeweza kutumia fursa hii kujia Kanada kama ambavyo wengi wako tayari hata kuzama bahari au kudhalilishwa na wasafirishaji binadamu ilmradi wafike majuu. Na kweli, huyu bibie alipata fursa kuingia Kanada kama ilivyotokea. Jamaa akiwa amefurahi kuwa amepata jiko na ndugu zake kadhalika wakifurahi wamemhifadhi ndugu yao, mama alipofika, alilala siku mbili. Kwa sababu mwenye mapenzi anaona, yule mama alishangaa na kuchukia baada ya kugundua kuwa kumbe yule aliyeonyeshwa hakuwa mtarajiwa wake. Alikaa kimya ili lau ajipe muda wa kupokea hali ile iliyomfadhaisha sana.
         Siku ya tatu alisema bila aibu wala kumuogopa Mungu kuwa hawezi kuolewa na kipofu! Je hapa tatizo ni nini? Kuna matatizo mawili. Kwanza, yule mama alikuwa akitarajia mumewe angekuwa mwenye kuwa timamu kwa sababu hakuambiwa kuwa alikuwa na changamoto au tuseme ulemavu wa macho. Pili, yule mama alikuwa na matarajio tofauti na hali aliyoikuta. Alifichwa ukweli ili kuamua kama alikuwa tayari kuishi naye au la pamoja na mapungufu yake.
Kufupisha hadithi ndefu, tunapoandika, hatujui huyu bibie aliishia wapi zaidi ya kujua kuwa alikataa kuishi na mumewe licha ya kumdhanimi kwa matarajio kuwa wangeungana kupiga maisha majuu. Alichoacha ni sononeko kwa yule mume na nduguze.
Turejee kwa mwenye mapenzi haoni. Anaona. Hebu jiulize. Ulipokuwa ukimtafuta au kutafutwa na mwenzako ni vitu gani ulikuwa unaangalia kwa vile ndivyo vilikuwa vigezo vyako vilivyokuvutia? Mwenye mapenzi anaona tena sana. Wakati mwingine anaona visivyoonekana. Vinginevyo wafitini wasingevunja au kuyumbisha uchumba hadi Waswahili wakaja na busara kuwa ficha uchumba na kutangaza ndoa kwa kuhofia mambo yanayoweza kuzushwa na wafitini na yakapewa umuhimu hata kama ni fitina na uzushi. Ndiyo maana tuna sifa na vitu vya kupatikana kwenye yule unayetaka kuoana naye. Ingekuwa hivyo basi kusingekuwapo na kuwahusisha jamaa kumuangalia na kumpima mtarajiwa wako. Unawaonyesha ili iweje kama siyo kutaka kusikia wanamuonaje? 
J            amaa mmoja nchini Saudia aliona picha ya msichana mrembo wa kimisri aliyekuwa anatafuta mchumba mtandaoni. Alimpenda na kuridhika na sura yake kiasi cha kutoa mahari dola za kimarekani laki tano. Kitu ambacho msaudia hakujua kuwa kumbe yule msichana aliyekuwa ameweka picha yake kwenye mtandao alikuwa na dada yake mwenye makengeza ambaye hakuwa amebahatika kuolewa kutokana na mwonekano wake. Jamaa baada ya kulipa mahari ilifika siku ya kwenda Misri kuchukua jiko. Alipofika akiwa na hamu ya kumuona mkewe, alionyeshwa dada mtu. Jamaa alipomuona, aliruka futi mia na kusema yule aliyeonyeshwa hakuwa yule aliyemuona na kumpenda. Kufupisha hadithi ndefu, jamaa alitaka arudishiwe fedha yake haraka. Wake walitia ngumu. Jambo hili lilifikishwa serikalini baada ya Saudia kutishia kuvunja uhusiano na Misri kama raia wake asingerudishiwa fedha yake. Je kama mwenye mapenzi haoni, si huyu Msaudia angebeba alichopewa?
        Mwisho, je mpaka hapa, bado unaamini mwenye mapenzi haoni au anaona sana tu? Kwa ufupi, mwenye mapenzi anaona sana tu. Siyo kila usemi unapaswa kuchukuliwa bila kufikiri hata kuhojiwa kama ilivyo dhana hii potofu kuwa mwenye mapenzi haoni wakati anaona sana.
Chanzo: Mwananchi Alhamis iliyopita.

Ndoa inahitaji maandalizi kisaikolojia

Kama ilivyo kwenye uanachama wa chama au taasisi yoyote, anayefanya hivyo lazima, kwanza ajielimishe aweze kujiunga na chama au taasisi inyomfaa kutokana na uchaguzi, malengo, na matarajio yake. Kufanya hivyo, mhusika anapaswa kumjua anayetaka au kutarajia kumuoa au kuolewa naye. Tofatuti, mwanachama wa vyama vingine au makundi tofauti na ndoa, anaweza kuondoka wakati wowote na kujiunga na vingine. Kwenye ndoa ni tofauti. 
        Wengi huingia wakitarajia maisha yenye furaha na mafainiko hadi kifo kiwatenganisha. Hata hivyo, ambao hushindwa na kuachana jambo ambalo mwanzoni mwa kuingia mahusiano haya huwa si moja ya malengo wala matarajio ya wahusika. Hili linaweza kuepukika kama wahusika watafanya utafiti wa kutosha na kujielimisha kuhusu wenzi japo na majaliwa yana nafasi yake. 
Lazima wahusika wajue ubora na udhaifu wao, welewa hata ujinga wao kama binadamu kwenye safari hii yenye milima na mabonde na misukosuko lukuki. Kuyajua haya hutoa fursa kwa wahusika kujiandaa kisaikolojia na kulhali kuishi pamoja wakifundishana na kuelimishana somo la maisha.             Nani anaajiriwa bila kutakiwa kuonyesha taaluma, akili, uzoefu, na uwezo wa kufanya kazi anayomba? Tusikubali kuingia au kuingizwa kwenye ndoa bila maandalizi na utayari. Wahusika wasikilize roho zao na sauti zao za ndani bila kulazimishwa au kushawishiwa na yeyote kwani ni wao watakayoyaishi maisha wanayoingia.                         Tunasema hivi kutokana na kuzuka mtindo kwa baadhi ya wazazi kuwalamisha watoto wao waolewe au kuoa watu fulani kwa kuangalia vitu kama vile mali na wadhifa wa familia watokazo wasijue vinaweza kuwa chanzo cha maanguko kama wahusika hawakuchagua wenyewe. Hili ni muhimu kwa sababu ndiyo wao watakaofurahia au kuumia mambo yakienda yalivyopangwa au ndiyo siyo. 
        Kama tulivyosema hapo juu, tofauti na chama au taasisi nyingine ambako mhusika anaweza kuhama na kujiunga bila kuumia au kusababisha matatizo kwake binafsi na wengine, ndoa ni tofauti kabisa. Ikishindikana au kutofanikiwa, huleta hisia hafifu kuwa ndoa ni kifungo au ndoana.
         Mfano wa pili, huwezi kununua gari na kuanza kuliendesha kabla ya kujifunza namna ya kufanya hivyo. Hii hutokana na hatari ima ya kuiparamia gari na kusababisha ajali hata kifo au kununua bovu ukaambua hasara. 
            Kwa Waafrika walio wengi, kabla ya kuoa au kolewa au kuoana kama wasemavyo siku hizi, kulikuwa na kipindi maalumu cha kujifunza taasisi hii, nini vinahitajika, havihitajiki, mbinu na miiko ya kuifanikisha na kuifaidi. Pia, kulikuwa na kipindi cha mhusika na wanafamilia yake kumchunguza mtarajiwa ili kujiridhisha kama anakidhi matarajio na viwango vyao. Kwenye jamii nyingi, walichunguza vitu hatarishi vya kifamilia kama magonjwa ya kuambukiza, tabia mbaya kama uchawi, ulafi, kujinyonga, na vingine kama hivyo kulingana na kabila au jamii wanamotoka wahusika. Kwa Waswahili, kulikuwa na jando kwa wanaume na unyago kwa wanawake. 
        Tunaposema Waswahili, hapa tumaanisha Watanzania ambao lugha yao ya taifa na kitambulisho ni Kiswahili au Waafrika kwa ujumla kwa vile tunafanana kisura na kimila ukiachia mbali kuwa Kiswahili ndiyo lugha kubwa pekee ya Kiafrika inayoongelewa zaidi Afrika na ulimwenguni. Hivyo, dhana ya Waswahili inaweza kumaanisha Watanzania hata Waafrika kwa ujumla kulingana na anayeitumia na anavyokubaliana nayo.
        Kitu kingine muhimu ni kujua historia, tabia, sura, umri, na utayari wa anayetaka kufunga ndoa. Kisheria, kuna umri unaoruhusiwa kufanya maamuzi. Hivyo, wahusika wasifichane umri wala tabia zao. Vitu hivi unaweza kuvificha kwa muda. Baadaye vitafichuka hasa ikizingatiwa kuwa unaingia kwenye uhusiano wa kudumu. Kuna kisa cha mwanandoa mmoja aliyemdanganya mwenzie umri wake. Walifunga ndoa na wakaishi kwa furaha tele japo kitambo. Tatizo katika kuficha umri, mhusika hakuwaambia au hakuwa na uwezo wa kuwaambia wote wanaomfahamu. Siku moja wanandoa hawa wakiwa hawana hili wala lile, mwanandoa aliyemficha mwenzie umri alipatikana. Mara nyingi, umri huwa tatizo kwa wanawake kuliko wanaume. 
        Mume wa mhusika akiwa kazini, aliajiriwa mwanamke mmoja akiwa mfanyakazi mwenzao mpya. Katika kutamjitambulisha kwa wafanyakazi wenzake, alisema kuwa anatokea sehemu fulani ambacho kilikuwa ni Kijiji cha mke wa mwanandoa huyu. Baada ya kumaliza utambulisho wa kiofisi, mwanandoa huyu alimwendea yule mfanyakazi mpya. Walisabahiana kwa uchangamfu na akamuuliza moja kwa moja, “unamjua fulani?” Yule mfanyakazi mpya alijibu, “fulani, alimtaja jina. Namfahamu tumesoma wote. Na isitoshe tumetofautiana siku mbili kuzaliwa.” 
              Mwanandoa alimuuliza, “una maana ulizaliwa tarehe” alitaja tarehe. Yule mfanyakazi mpya aliyeonekana dhahiri kuwa mkubwa ikilingaishwa na mkewe alijibu. “Ndiyo, wote tulizaliwa mwaka” aliutaja. Yule jamaa alitabasamu ingawa aligundua kuwa mkewe alikuwa mkubwa miaka sita zaidi ya umri aliokuwa amemwambia. Alianza kujiuliza “je amenificha mangapi na kwanini?”
            Kukatiza kisa kirefu, mwanandoa alimkabili mwenzie na kumuuliza. “Hivi una cheti cha kuzaliwa?” Mwenzake aliuliza, “unataka cheti cha kuzaliwa cha nini?”
Tumalizie. Ndoa inahitaji maandalizi kisaikoloji, kiakili, na kulhali.
Chanzo: Mwananchi jana.

Sunday 21 July 2024

Mwenye mapenzi anaona tena sana

Kuna imani au tuseme usemi kuwa mwenye mapenzi haoni. Je kweli mwenye mapenzi haoni hata kama macho anayo? Je ukweli ni upi haoni au anaona tena sana? Ingawa “mwenye mapenzi haoni” ina tafsiri nyingi kutegemea na hali yaliyomo mapenzi, ukweli ni kinyume. Tutatoa sababu zifuatazo:
        Kwetu mwenye mapenzi lazima aone na aone kwelikweli. Utawezaje kuujua uzuri na mvuto wa mwenzako kama kweli mwenye mapenzi haoni? Ingekuwa hivyo, watu wengi wenye changamoto za aina mbalimbali za ulemavu ambazo ni kazi ya Mungu wasingenyanyapaliwa, kukataliwa, na wengine kutoolewa kabisa au kuachika tokana na changamoto ambazo siyo matokeo ya kazi wala utashi wao. 
            Pia, ukitaka kujua mwenye mapenzi aone, jiulize ni visa vingapi wanandoa waliopeanda haswa walipoachana au kuuana baada ya mmojawapo kumtendea mwenzie mabaya? Kuna kisa cha wanandoa wawili ambapo mke alikuwa si mzuri wa kuvutia ikilinganishwa na mumewe ambaye alimpenda mkewe vilivyo. Hata hivyo, kwa kujua anapendwa, mke alipata msukosuko wa ndoa akatembea na mganga wa kienyeji. Pamoja na mapenzi makubwa yaliyovutia wengi, mume alimuacha mkewe bila hata kumpa nafasi ya kujitetea. Kwa ufupi ni kwamba mwenye mapenzi anaona tena mambo mengine ambayo katika hali ya kawaida huwezi kuyaona wala kudhania yanaweza kuonekana. 
        Kisa kingine ni cha jamaa tunayemfahamu mwenye ulemavu wa macho. Ndugu zake walimtafutia mke toka nchini kwao kuja Kanada bila kumwambia ukweli kwa vile aliwahakikishia kuwa anampenda yule Bwana. Kufanya mambo kuwa magumu zaidi, walimuonyesha picha ya mdogo mtu badala ya muoaji mwenyewe wakiamini akifika Kanada, atazubazwa na uzuri na hali nzuri ya maisha. 
            Pamoja na kuwaonya kuwa walipaswa kumueleza mchumba mtarajiwa kuwa ndugu yao alikuwa na changamoto ya kutoona, hawakufanya hivyo wakiamini mtarajiwa akifika asingeweza kumwacha mtu aliyemfadhiri kuja Kanada. Waliogopa kumwambia wakiogopa kuwa mtarajiwa angeweza kutumia fursa hii kujia Kanada kama ambavyo wengi wako tayari hata kuzama bahari au kudhalilishwa na wasafirishaji binadamu ilmradi wafike majuu. Na kweli, huyu bibie alipata fursa kuingia Kanada kama ilivyotokea. 
            Jamaa akiwa amefurahi kuwa amepata jiko na ndugu zake kadhalika wakifurahi wamemhifadhi ndugu yao, mama alipofika, alilala siku mbili. Kwa sababu mwenye mapenzi anaona, yule mama alishangaa na kuchukia baada ya kugundua kuwa kumbe yule aliyeonyeshwa hakuwa mtarajiwa wake. Alikaa kimya ili lau ajipe muda wa kupokea hali ile iliyomfadhaisha sana.
         Siku ya tatu alisema bila aibu wala kumuogopa Mungu kuwa hawezi kuolewa na kipofu! Je hapa tatizo ni nini? Kuna matatizo mawili. Kwanza, yule mama alikuwa akitarajia mumewe angekuwa mwenye kuwa timamu kwa sababu hakuambiwa kuwa alikuwa na changamoto au tuseme ulemavu wa macho. Pili, yule mama alikuwa na matarajio tofauti na hali aliyoikuta. Alifichwa ukweli ili kuamua kama alikuwa tayari kuishi naye au la pamoja na mapungufu yake.
Kufupisha hadithi ndefu, tunapoandika, hatujui huyu bibie aliishia wapi zaidi ya kujua kuwa alikataa kuishi na mumewe licha ya kumdhanimi kwa matarajio kuwa wangeungana kupiga maisha majuu. Alichoacha ni sononeko kwa yule mume na nduguze.
        Turejee kwa mwenye mapenzi haoni. Anaona. Hebu jiulize. Ulipokuwa ukimtafuta au kutafutwa na mwenzako ni vitu gani ulikuwa unaangalia kwa vile ndivyo vilikuwa vigezo vyako vilivyokuvutia? Mwenye mapenzi anaona tena sana. Wakati mwingine anaona visivyoonekana. Vinginevyo wafitini wasingevunja au kuyumbisha uchumba hadi Waswahili wakaja na busara kuwa ficha uchumba na kutangaza ndoa kwa kuhofia mambo yanayoweza kuzushwa na wafitini na yakapewa umuhimu hata kama ni fitina na uzushi. Ndiyo maana tuna sifa na vitu vya kupatikana kwenye yule unayetaka kuoana naye. Ingekuwa hivyo basi kusingekuwapo na kuwahusisha jamaa kumuangalia na kumpima mtarajiwa wako. Unawaonyesha ili iweje kama siyo kutaka kusikia wanamuonaje? 
        Jamaa mmoja nchini Saudia aliona picha ya msichana mrembo wa kimisri aliyekuwa anatafuta mchumba mtandaoni. Alimpenda na kuridhika na sura yake kiasi cha kutoa mahari dola za kimarekani laki tano. Kitu ambacho msaudia hakujua kuwa kumbe yule msichana aliyekuwa ameweka picha yake kwenye mtandao alikuwa na dada yake mwenye makengeza ambaye hakuwa amebahatika kuolewa kutokana na mwonekano wake. Jamaa baada ya kulipa mahari ilifika siku ya kwenda Misri kuchukua jiko. 
        Alipofika akiwa na hamu ya kumuona mkewe, alionyeshwa dada mtu. Jamaa alipomuona, aliruka futi mia na kusema yule aliyeonyeshwa hakuwa yule aliyemuona na kumpenda. Kufupisha hadithi ndefu, jamaa alitaka arudishiwe fedha yake haraka. Wake walitia ngumu. Jambo hili lilifikishwa serikalini baada ya Saudia kutishia kuvunja uhusiano na Misri kama raia wake asingerudishiwa fedha yake. Je kama mwenye mapenzi haoni, si huyu Msaudia angebeba alichopewa?
        Mwisho, je mpaka hapa, bado unaamini mwenye mapenzi haoni au anaona sana tu? Kwa ufupi, mwenye mapenzi anaona sana tu. Siyo kila usemi unapaswa kuchukuliwa bila kufikiri hata kuhojiwa kama ilivyo dhana hii potofu kuwa mwenye mapenzi haoni wakati anaona sana.
Chanzo: Mwananchi leo.


Watufilisio wamefilisi, tumefilisika wamefilisika!

“Kufilisika kubaya. Jamanini kufilisika kubaya. Heri ufilisike mali kuliko akili. Heri ung’atwe na dogi kuliko kung’ata dogi.” Hayo ni maneno ya wimbo nilioutunga zamani nikakosa vifaa ukaishia kwenye makabrasha. Tuachane na mistari ya dhahabu ya zama za dhahabu. Naami mafyatu wote mnajua maana ya kufilisika. Niwasaidia wasiojua. Ni kuishiwa kitu chochote iwe akili au njuluku hata sera. Leo nitaongelea namna mafyatu wanavyofilisiwa na wanaowafilisi wanaopaswa kuwafilisi ili sote tufilisike na watufilisio wakiwamo ngoma droo ili kutenda haki.
Kunyaka mantiki ya somo, nitafudisha kupitia maswali kama ifuatavyo:
Mosi, je unapoteua cahawa kuwa mlongaji wa chata lako huligeuzi chata kuwa Chata cha Machawa (CcM)? Niliwaonya tusifanye mchezo na waharifu mafyatu wakadharau. Yako wapi sasa? Si tuliweka kikaragosi kikafyatufyatuka kikitaka kutubomoa eti kwa kujijenga baadaye eti kichukue ulaji wangu kama rahis wa mafyatu. Yametukuta mafyatu. Juzi katika kijiwe chetu cha uongozi si tukapendekeza fyatu mmoja aliyewahi kupatikana jinai ya kuteka na kuua mafyatu wenzake. Jamaa huyu chawa na changu kisiasa alijipenyeza, akapenya, na tukapenyeka tukamteua kuwa mlongaji wa Chama Cha Mafyatu (CCM). Naomba msichanganye CCM letu na nambari one ya twawala. Huko sipo. 
        Kufilisika nifundishao hauwahusu hao, kwani, walifilisika zamani machawa yalipowanyonya hadi wakaonda hata upstairs hadi wakawa wanalindwa na mbwa aliyekonda utadhani makondakonda sorry makandokando ya mikweche ya akina Daodi, Alubati, na Buushit.
Pili, unapofungulia mbwa, tena mwenye kichaa cha dog akawang’ate mafyatu usijue anaweza kukung’ata hata wewe, unategemea nini? Je hapa hujafilisika kisiasa? Je ulishajiuliza itakuwaje dogii akiamua kufilisika kama mwenyewe na kukung’ata wewe umfugaye? Hii huitwa mbwa kula mbwa kwani mbwai mbwai. Je unajua kuwa hizi ni baadhi ya dalili za kufilisika pale mwenye mbwa unapotegemea mbwa akulinde na kukuhakikishia usalama hata kukubalika kwako kwa mabavu wakati mbwa ni mbwa atabwabwaja na kufanya uumbwa? 
        Je unaambua nini kwenye ushauri huu wa bure toka kwa gwiji Dk, Profesa, Alhaji, Mhashamu, His Excellency, His Eminence, HH etc. Fyatu Mfyatuzi bin Mfyatuaji bin Mfyatukage wa Mfyatulizi mwana wa Mfyatukizi mjukuu wa Fyatuafyatua mwana wa Mfyatuizi? Naona yule anashangaa na kutikisa kichwa. Hujui naweza kutaja majina elfu na ushei ya kizazi changu kama kilivyoandikwa kwenye vitabu vitakatifu ingawa lilibadilishwa likawekwa la ka jamaa toka Mashariki ya nonihino? 
        Tatu, wewe unayeendelea kufanya makosa kuendekeza mbwa ukidhani atakuletea amani na usalama hata kwa kuwang’ata wachapakazi wako? Huku ndiko kufilisika kunakoongelewa hapa. 
        Nne, unapompa bangi mbwa mwenye kichaa tayari kung’ata wabaya au wapingaji wako  kwa sababu ana uzoefu wa kung’ata, kwanini nao wasijitoe akili wakamng’ata ikawa habari halafu wakakufyatua nawe na jibwa lako fyatu? Huku ndiko kufilisika kunakotufilisi kwa kufilisiwa na hawa waliofilisika wakatufilisi nasi.
        Tano, ili kuonyesha hawajafilisika, kwanini mafyatu wasinyongelee mbali hili jibwa ili wasing’atwe na kuendekeza madogiii? Huu si wakati wa madogii kutuchezea na kutung’ata kama kipindi kile walipokuwa wakibweka na kung’ata huku aliyewafuga akizidi kuchekelea na kuwanenepesha tena kwa njuluku na mamlaka ya mafyatu wafyatuliwa na kufilisiwa.
        Sita, mafyatu walipoona wanene tumempitisha huyu dogi, walisema wazi kuwa kipindi hiki ang’atwi fyatu hata mmoja. Badala yake mafyatu watang’ata hata mbwa mng’ataji. Hivi unapowaletea mafyatu mbwa, ina maana mafyatu wamekwisha au ni ile hali ya kuzidiwa na kunyonywa na chawa au kufilisika?
Saba, hivi inawezekanaje mbwa kuwazidi akili mafyatu tena wakubwa kiumri na kimaulaji? Je hapa mbwa na fyatu ni yupi au mmebalishana baada ya kufyatuka na kufilisika hadi mkaruhusu mbwa awafyatue na kuwafilisi? Je mfupa uliomshinda fisi nyinyi mtauweza?
Nane, inakuwaje mbwa anaendekezwa ili ang’ate mafyatu waliokwishafyatuka wakati tunao wanyama kibao na mabaki kibao kwa wale wanene wanaokula nyama? Kwanini wasimtupie mabaki ya milo yao badala ya kutaka awang’ate mafyatu wasio na noma na yeyote?
Baada ya kumaliza kuuliza maswali ambayo sitegemei kuletewa majibu ili yachapishwe kwa vile fyatu anayenihariri na kuruhusu hii kitu itoke hewani mafyatu wasome hataruhusu. Naye kuna siku nitamfyatua. We acha tu. Ukisoma hii, soma kimya asisikie akanifyatua nikashindwa kuwafyatua mafyatu wanaotufyatulia mimba itufyatue wasijue usawa huu, tutaifyatua kama mbaya, mbaya. Kwani mbwai mbwai kwa kimombo.
        Je tuko tayari kuendelea kung’atishwa majibwa tena yaliyochoka baada ya kujaribu hata kuwang’ata waliowakota majalalani? Inakuwaje mbwa koko anaendekezwa kiasi cha kuwazidi mafyatu wakati ananenepa kwa njuluku zao? Je kinachoendelea ni mbwa kugeuka chawa au chawa kula akanenepa na kugeuka mbwa?
Nimalizie. Kweli wametulifisi mali nao wakafilisika mawazo! Du! Kwani niko wapi?
Chanzo: Mwananchi Jumatano iliyopita.