Liberal Peace Conflict, Gender, and Peacebuilding

Liberal Peace Conflict, Gender, and Peacebuilding

Friday 12 July 2024

Mwapambana na ‘Machangu’ Wapi?

Kama mwanasharia na msomi, najua madhara ya kujadili jambo ambalo ni sub judice yaani lililoko mahakamani. Hivyo, nitaongelea kasheshe la baadhi ya mafyatu wanene kunyaka, kudhalilisha, na kuwapeleka kwa pilato dada wachovu eti kwa vile ni machangu. Pamoja na kutokuwa na ushahidi wala mashiko, niseme wazi. Uchangu si kosa kisheria bali aibu. Kama madada wanauza maungo yao, matatizo au mateso gani mafyatu tunaupata ikilinganishwa na wale wanaotuibia au kutuuza jumlajumla? Nani ananunua hizo laana zao? Naona yule anatikisa kichwa. Sitetei uchangudoa. Kinachogomba nikafyatuka kwa hasira na usongo ni kubaguana, kudanganyana, kudhalilishana na kuoneana.
Kamusi ya mafyatu inafasiri. Changudoa wako aina mbili, changu na changudoa (changu mwenye madoa) wapatikanao kwa wingi baharini kuliko wengine. Ni wa kike na wa kiume kama ngurumbili walio machangu. Tofauti, samaki si malaya wala wakware, wanyonyaji, wajinga, na wachafu kama chawa. Kosa lao ni upatikanaji wao kirahisi kama changu mafyatu.
Kwangu, changu ni fyatu yoyote asiyeaminika na mchumiatumbo ahiariye kutweza hata kuuza utu wake ilmradi apate tonge. Uchangu hauna unene, unono au unyonge. Hauna usomi wala ujinga. Ni fyatu aliyeishiwa akili hata ubunifu kiasi cha kujidhalilisha ili kujaza tumbo. Changu anaweza kuwa murume au jike. Anaweza kuuza mwili wake hata watu wake. Anaweza kuwa wa kijamii au hata wa kisiasa hata kiuchumi. Kimsingi, vyangu wote ni mafyatu wa kujidhalilisha kwa kushindwa kuheshimu utu wao. Machangu na machawa hawana tofauti. Tofauti iliyopo ni kwamba machawa ni machangu wa kisiasa na vyangu ni wa kijamii. Pia,wa kisiasa huwaonea wa kijamii.
Kwanini nafyatuka kwa hasira leo? Kama nilivyofyatua hapo juu, nilishika kichwa hadi tama, nilipoona mafyatu wazima, wanene, tena machawa, sorry, machangu, sorry, wenye ulaji wakiwakamata na kuwadhalilisha machangu wenzao wachovu. Wote, kifyatu, ni machangu. Tofauti yao ni waliposimama. Huwezi kumtofautisha changu wa kisiasa kama yule aliyetimika juzi na kwenda kuramba matapishi yake na hawa wakamatwao na kudhalilishwa. Nimesemaje? Nimesema Pita yule aliyemkana Tunda Lishe, sorry, Yesu? Message sent. Pita Msigwer ni shabiki wangu. Siwezi kumuita changu japo kwenye siasa kuna uchangu unaonekana kuhalalishwa na kuheshimika wakati ni uchangu kama uchangu wowote. Wala siwezi kusema ameramba, kubwia, na kupwakia marapishi yake. Si ndiye alisifika kuiponda Fisiemu akiwa Chakudema? Yethu na Maria. Nini hii la hawla wa la quwwata illa Billah.
Turejee dhana ya uchangu. Changu awezafanya chochote asijali madhara wala utu ilmradi apate atakalo. Anaweza kutoa mwili wake ale. Anaweza kuwaibia  wamtumiao, wakware au wanasiasa kama ambavyo mtashuhudia msimu huu wa usanii na uchawa kuelekea kwenye uchakachuaji. Mtawaona mafyatu wanene msiowezawadhania wakifanya uchangu kisiasa kwa vile ni halali kisheria. Kama nilivyofyatuka hapo juu, uchangu ni uchangu uwe wa kisiasa, kisanii, au kingoni. Changu avaaye vimini na avaaye suti au Tshirt za vyama wote vyangu. Changu atembea pekupeku na yule apandaye mashangingi na mashankupe wote vyangu. Nakazia. Changu ni changu awe mnene au mnyonge. Uchangu ni kama magonjwa mengine. Hayabagui. Tofauti ni kwamba uchangu ni ugonjwa wa kujitakia sawa na ujinga au imani kibubusa.
Uchangu ni kujiuza wewe na utu wako. Uchangu una sura nyingi tena mbaya. Unaweza kuunganisha uchangu na ukosefu wa maadili au upigaji madili. Wasomi wenzangu wanaoingia mikataba hatarishi kweli si machangu kimaadili na kiuchumi? Je hawa wanaotuibia kila uchao si machangu walio tayari hata kuumiza wenzao kama changu anavyoweza kumtilia mteja madawa ya usingizi kwenye kinywaji amfyatue uchache na rununu na kuishia? Hata wanaoahidi wasiyotekeleza na kupata kura ya kula ni machangu kisiasa. Wale wanaoruka viama kama daladala ni machangu tu. Heri uwe fyatu kuliko kuwa changu. Heri uwe fyatu kuliko kuwa chawa.
Natoa ujumbe mahsusi kwa wanaopoteza njuluku na muda vya mafyatu kuwinda na kukamata machangu. Waache uchangu. Kama watakamata basi wakamate machangu wote wa kimaadili na kisiasa. Uchangu ni uchangu. Unapaswa kushughulikiwa kwa namna na nguvu sawa bila kubagua wapi wa kukamata na wapi wa kukaribisha hata kuandalia halfa na kutangaza kwenye runinga wasijue nao ni uchangu tu. Nashauri, kuanzia leo, kuwe na usawa katika uchangu na ushughulikiwavyo. Mfano, penye machangu wa kike wapo wa kiume kwani wanafanya pekee. Dhana ya ukahaba vivyo hivyo. Kahaba ni wanawake na wanaume. Huko leo siendi japo ukahaba na uchangu ni mapacha. Tofauti ni matumizi yake hasa usawa huu wa kushitakiana hata kunyamazishana. 
Tumalizie kwa kuuliza. Mwapambana na changu wapi kulingana na mchanganuo huu? Woooi! Kumbe sijaenda baa sorry, ofisini, sorry, sokoni, sorry, Sinzer kuona vyangu!
Chanzo: Mwananchi Alhamis


No comments: