Liberal Peace Conflict, Gender, and Peacebuilding

Liberal Peace Conflict, Gender, and Peacebuilding

Monday 29 July 2024

Mwenye mapenzi anaona tena sana


Kuna imani au tuseme usemi kuwa mwenye mapenzi haoni. Je kweli mwenye mapenzi haoni hata kama macho anayo? Je ukweli ni upi haoni au anaona tena sana? Ingawa “mwenye mapenzi haoni” ina tafsiri nyingi kutegemea na hali yaliyomo mapenzi, ukweli ni kinyume. Tutatoa sababu zifuatazo:
        Kwetu mwenye mapenzi lazima aone na aone kwelikweli. Utawezaje kuujua uzuri na mvuto wa mwenzako kama kweli mwenye mapenzi haoni? Ingekuwa hivyo, watu wengi wenye changamoto za aina mbalimbali za ulemavu ambazo ni kazi ya Mungu wasingenyanyapaliwa, kukataliwa, na wengine kutoolewa kabisa au kuachika tokana na changamoto ambazo siyo matokeo ya kazi wala utashi wao. Pia, ukitaka kujua mwenye mapenzi aone, jiulize ni visa vingapi wanandoa waliopeanda haswa walipoachana au kuuana baada ya mmojawapo kumtendea mwenzie mabaya? 
            Kuna kisa cha wanandoa wawili ambapo mke alikuwa si mzuri wa kuvutia ikilinganishwa na mumewe ambaye alimpenda mkewe vilivyo. Hata hivyo, kwa kujua anapendwa, mke alipata msukosuko wa ndoa akatembea na mganga wa kienyeji. Pamoja na mapenzi makubwa yaliyovutia wengi, mume alimuacha mkewe bila hata kumpa nafasi ya kujitetea. Kwa ufupi ni kwamba mwenye mapenzi anaona tena mambo mengine ambayo katika hali ya kawaida huwezi kuyaona wala kudhania yanaweza kuonekana. 
        Kisa kingine ni cha jamaa tunayemfahamu mwenye ulemavu wa macho. Ndugu zake walimtafutia mke toka nchini kwao kuja Kanada bila kumwambia ukweli kwa vile aliwahakikishia kuwa anampenda yule Bwana. Kufanya mambo kuwa magumu zaidi, walimuonyesha picha ya mdogo mtu badala ya muoaji mwenyewe wakiamini akifika Kanada, atazubazwa na uzuri na hali nzuri ya maisha. Pamoja na kuwaonya kuwa walipaswa kumueleza mchumba mtarajiwa kuwa ndugu yao alikuwa na changamoto ya kutoona, hawakufanya hivyo wakiamini mtarajiwa akifika asingeweza kumwacha mtu aliyemfadhiri kuja Kanada. Waliogopa kumwambia wakiogopa kuwa mtarajiwa angeweza kutumia fursa hii kujia Kanada kama ambavyo wengi wako tayari hata kuzama bahari au kudhalilishwa na wasafirishaji binadamu ilmradi wafike majuu. Na kweli, huyu bibie alipata fursa kuingia Kanada kama ilivyotokea. Jamaa akiwa amefurahi kuwa amepata jiko na ndugu zake kadhalika wakifurahi wamemhifadhi ndugu yao, mama alipofika, alilala siku mbili. Kwa sababu mwenye mapenzi anaona, yule mama alishangaa na kuchukia baada ya kugundua kuwa kumbe yule aliyeonyeshwa hakuwa mtarajiwa wake. Alikaa kimya ili lau ajipe muda wa kupokea hali ile iliyomfadhaisha sana.
         Siku ya tatu alisema bila aibu wala kumuogopa Mungu kuwa hawezi kuolewa na kipofu! Je hapa tatizo ni nini? Kuna matatizo mawili. Kwanza, yule mama alikuwa akitarajia mumewe angekuwa mwenye kuwa timamu kwa sababu hakuambiwa kuwa alikuwa na changamoto au tuseme ulemavu wa macho. Pili, yule mama alikuwa na matarajio tofauti na hali aliyoikuta. Alifichwa ukweli ili kuamua kama alikuwa tayari kuishi naye au la pamoja na mapungufu yake.
Kufupisha hadithi ndefu, tunapoandika, hatujui huyu bibie aliishia wapi zaidi ya kujua kuwa alikataa kuishi na mumewe licha ya kumdhanimi kwa matarajio kuwa wangeungana kupiga maisha majuu. Alichoacha ni sononeko kwa yule mume na nduguze.
Turejee kwa mwenye mapenzi haoni. Anaona. Hebu jiulize. Ulipokuwa ukimtafuta au kutafutwa na mwenzako ni vitu gani ulikuwa unaangalia kwa vile ndivyo vilikuwa vigezo vyako vilivyokuvutia? Mwenye mapenzi anaona tena sana. Wakati mwingine anaona visivyoonekana. Vinginevyo wafitini wasingevunja au kuyumbisha uchumba hadi Waswahili wakaja na busara kuwa ficha uchumba na kutangaza ndoa kwa kuhofia mambo yanayoweza kuzushwa na wafitini na yakapewa umuhimu hata kama ni fitina na uzushi. Ndiyo maana tuna sifa na vitu vya kupatikana kwenye yule unayetaka kuoana naye. Ingekuwa hivyo basi kusingekuwapo na kuwahusisha jamaa kumuangalia na kumpima mtarajiwa wako. Unawaonyesha ili iweje kama siyo kutaka kusikia wanamuonaje? 
J            amaa mmoja nchini Saudia aliona picha ya msichana mrembo wa kimisri aliyekuwa anatafuta mchumba mtandaoni. Alimpenda na kuridhika na sura yake kiasi cha kutoa mahari dola za kimarekani laki tano. Kitu ambacho msaudia hakujua kuwa kumbe yule msichana aliyekuwa ameweka picha yake kwenye mtandao alikuwa na dada yake mwenye makengeza ambaye hakuwa amebahatika kuolewa kutokana na mwonekano wake. Jamaa baada ya kulipa mahari ilifika siku ya kwenda Misri kuchukua jiko. Alipofika akiwa na hamu ya kumuona mkewe, alionyeshwa dada mtu. Jamaa alipomuona, aliruka futi mia na kusema yule aliyeonyeshwa hakuwa yule aliyemuona na kumpenda. Kufupisha hadithi ndefu, jamaa alitaka arudishiwe fedha yake haraka. Wake walitia ngumu. Jambo hili lilifikishwa serikalini baada ya Saudia kutishia kuvunja uhusiano na Misri kama raia wake asingerudishiwa fedha yake. Je kama mwenye mapenzi haoni, si huyu Msaudia angebeba alichopewa?
        Mwisho, je mpaka hapa, bado unaamini mwenye mapenzi haoni au anaona sana tu? Kwa ufupi, mwenye mapenzi anaona sana tu. Siyo kila usemi unapaswa kuchukuliwa bila kufikiri hata kuhojiwa kama ilivyo dhana hii potofu kuwa mwenye mapenzi haoni wakati anaona sana.
Chanzo: Mwananchi Alhamis iliyopita.

No comments: